Baada ya Yesu kupaa: Alichofanya katika Agano Jipya

Tunapata kumjua Yesu, Mwana wa Mungu na Masihi wetu, kwanza kwa kusoma habari za Injili kuhusu huduma yake duniani. Na baada ya kufa kwa ajili ya dhambi zetu na kufufuka, alirudi mbinguni. Hii inajulikana kama “Kupaa kwa Yesu Kristo,” na imeelezwa katika Marko 16:19, Luka 24:50-51, na Matendo 1:9-11).

Lakini baada ya hapo? Yesu alikuwa akifanya nini katika sehemu iliyobaki ya Agano Jipya?

Katika aya hizo tatu kuhusu kupaa kwake, kinachosemwa mara moja ni kwamba “Aliketi mkono wa kuume wa Mungu” (Marko 16:19).

Nini maana yake?

“Kuketi mkono wa kuume” maana yake ni kuwa katika nafasi ya heshima na nguvu.1 Hivyo, kupaa kwa Yesu kurudi mbinguni pia kulikuwa ni kupaa kwenda katika nafasi maalum ya mamlaka kuhusiana na mwanadamu (Waebrania 1:2-4).

Yeye hufanya kazi kwa mamlaka haya kuwatunza na kuwaongoza wale wanaomkubali kama Mwokozi wao (Waebrania 2:9-11), na kukamilisha kazi aliyoianza maishani mwetu (Wafilipi 1:6).

Hivyo ingawa kimwili aliondoka duniani, hakuliacha kamwe Kanisa lake (jamii ya waamini ulimwenguni) kufanya kazi nzito – amekuwa akifanya kazi ndani ya watu wake kusambaza Injili na kufunua tabia ya Mungu.

Pia amekuwa akiandaa siku ambapo ataungana nasi milele.

Waandishi wa Agano Jipya walifunua kile alichokifanya na anaendelea kukifanya.

Tutachunguza njia ambazo Yesu amekuwa akifanya kazi na wanadamu baada ya kupaa:

Moja ya viashiria vya kwanza ambavyo Yesu alitoa kuhusu jukumu lake baada ya kupaa lilikuwa kuhusiana na mustakabali wetu pamoja kama waamini.

Kuandaa makao kwa ajili ya watu wake

A little girl in a white dress picks flowers in a field, giving a picture of a peaceful life in heaven and on the New Earth.

Photo by Emma Bauso

Yesu aliwaahidi wanafunzi wake kwamba atarudi kwa ajili yao kwa sababu Alikuwa “akiandaa mahali” kwa ajili yao.

“Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo” (Yohana 14:2-3, NKJV).

Ingawa hii inaweza au isingemaanisha kujenga majengo tutakayoyaita nyumbani siku moja, inaonyesha kwamba yeye mwenyewe anataka kuifanya milele iwe uzoefu wa furaha kwetu. Katika Mbingu mpya na Nchi mpya, tutakuwa tukipata ufalme wa Mungu kikamilifu. Tutakuwa mahali ambapo tunaweza kutembea na kuzungumza naye kama tunavyofanya na yeyote mpendwa wetu (Ufunuo 7:15-17; 21:3).

Kristo alipoondoka duniani, haikuwa kwaheri ya kuonana. Zaidi ilikuwa kama anasema, “Ningojeeni. Nitakuja na kuwachukua wakati utakapowadia.”

Tunaweza kuichukulia kama uhusiano thabiti kati ya watu walio mbali.

Lakini haimaanishi kwamba tunakaa tu tukitazama angani. Yesu aliwafundisha wanafunzi wake kujiandaa kwa ujio kwake.

Yesu alitoa mfano kuhusu jinsi alivyotarajia wafuasi wake kujishughulisha na kujiandaa kwa ujio wake (Mathayo 25:14-30; Luka 19:11-27). Akifundisha hilo, aliwaelezea wafuasi wake kama watumishi wanaofanya “biashara ya bwana wao” mpaka bwana wao ataporudi (Luka 19:13). Watumishi waaminifu walingoja kwa kutumia rasilimali za bwana wao kwa kazi yake (Mathayo 25:14-28; Luka 19:11-27).

Mfano huu unatufundisha kutumia kile ambacho Mungu ametubariki nacho ili kazi yake duniani isonge mbele- kusambaza Injili na kuwahudumia wengine – huku yeye akiendelea na kazi yake mbinguni.

Lakini anajua hatuwezi peke yetu, hivyo alimtuma Roho wake kutusaidia kuwa tayari.

Kumtuma Roho Mtakatifu

Baada ya Yesu kupaa, Aliitimiza ahadi Yake ya kumtuma Roho Wake Mtakatifu. Wakristo wengi hurejelea hili kama “kumwagwa kwa Roho Mtakatifu,” na lilikuwa mwanzo wa kanisa la awali. Kwa karne nyingi, Roho Mtakatifu amewaunganisha watu na Yesu, kuwawezesha kushinda changamoto wanazokumbana nazo.

Hivi ndivyo inavyotokea:

Ahadi kabla ya kusulubiwa

Yesu alitangaza kabla ya kifo chake kwamba atamtuma “Msaidizi mwingine,” “Roho wa kweli.” Haya ni majina mengine ya Roho Mtakatifu ambaye angemfunua Yesu na kuwaongoza wafuasi wake (Yohana 15:26-27; 16:13-14).

Wanafunzi walipambana awali na ahadi hii kwa sababu ilimaanisha kwamba alikuwa anaondoka. Na hiyo inaeleweka. Ni ngumu kumuaga mtu wako wa karibu, hasa mtu ambaye umekuwa ukiongea naye kila siku.

“Lakini sasa mimi naenda kwake yeye aliyenipeleka, wala hakuna mmoja wenu aniulizaye , Unakwendapi? Ila kwa sababu hayo huzuni imejaa mioyoni mwenu. Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke; kwa maana nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu” (Yohana 16:5-7, NKJV).

Hawakuelewa bado kwamba Yesu angeweza kuwa nao daima kupitia Roho Mtakatifu.

Akiwa kimwili duniani, angeweza kuwa mahali pamoja kwa wakati mmoja.

Lakini kupitia Roho Mtakatifu, Yeye anaweza kuwepo kila mahali kwa kuishi mioyoni mwetu (Yohana 16:13-15). Kupitia Roho, tunaweza kubaki tukiwa na uhusiano naye kama chanzo chetu, kama vile matawi yanavyostawi kutoka kwenye mzabibu kama chanzo cha uzima na nguvu zao (Yohana 15:4-5).

Hapa kuna njia kadhaa ambazo Roho hutuunganisha na Yesu:

  • Yeye “anaishi ndani” yetu (Yohana 14:14-16). Hii inamaanisha kwamba tunaweza kufikia Yesu wakati wote na moja kwa moja. Tunaweza kumuomba wakati
  • wowote, na Yeye daima atatuongoza (Warumi 8:14, 16).
  • Kutufundisha “vitu vyote” na kutukumbusha yale ambayo Yesu alisema (Yohana 14:26, NKJV).
  • Kutuongoza katika kweli yote (Yohana 16:13).
  • Kumfunua Yesu na anachotaka tujue (Yohana 15:26; 16:14).
  • Kutupa maneno ya kusema tunapohitaji (Marko 13:11).
  • Yeye anatuombea sisi, anachunguza mawazo yetu, na kutafsiri sala zetu (Warumi 8:26-27).

Injili zinamtaja Roho Mtakatifu kama “Msaidizi” (“Mshauri” katika Biblia ya Kiwango cha Kikristo ).2 Ni faraja kujua kwamba Roho wa Kristo anafanya kazi ya kutusaidia na yupo kwa ajili yetu wakati tunapopitia changamoto za maisha haya.

Wanafunzi 12 hawakuelewa kabisa lengo halisi la utume na kifo cha Kristo. Hii ilikuwa dhana kubwa na mpya kwao. Lakini Bwana alijua hili na aliwaahidi Roho Mtakatifu angeweka wazi mafundisho Yake (Yohana 16:13).

Kweli, wakati Yesu alipofufuka kutoka kwa wafu, Roho Mtakatifu aliwafungua macho yao (Yohana 20:21; Luka 24:44-45) na hatimaye wakaelewa kwamba “ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu” (Luka 24:46-47, NKJV).

Sasa, walihitaji tu nguvu na faraja ya kutangaza hilo.

Ahadi baada ya kufufuka

A tomb with the stone rolled away, illustrating the resurrection of Jesus Christ.

Photo by Jonny Gios on Unsplash

Roho Mtakatifu aliwawezesha kuhubiri Injili kama mashahidi wake. Kabla ya kupaa, Yesu aliwaagiza wanafunzi wake kukaa Yerusalemu mpaka atakapomtuma Roho Mtakatifu (Luka 24:49).

“Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi” (Matendo 1:8, NKJV).

Uwezo huu ulianza siku ya Pentekoste. Pia inaitwa Sikukuu ya Majuma, Pentekoste ilikuwa sikukuu ya Kiyahudi iliyofuata baada ya Sikukuu ya malimbuko ya kwanza (Walawi 23:9-22; Kutoka 34:22).

Sikukuu ya malimbuko ya Kwanza ilielekeza katika ufufuo wa Yesu (1 Wakorintho 15:20),3 na Sikukuu ya Majuma ilimaanisha “mavuno” ya kiroho ambapo maelfu walimkubali Kristo baada ya kujazwa Roho Mtakatifu.4

Yesu alitumia Roho Mtakatifu kujenga Kanisa lake, kuwasiliana na watu wake, na kufanya kazi kupitia kwao. Hii ilionekana katika namna tofauti tofauti:

  • Aliwapa wafuasi wake ujasiri wa kuhubiri Injili (Matendo 4:8-13, 31, 33).
  • Aliwaponya watu kupitia wanafunzi wake (Matendo 3:1-8; 9:32-35; 16:16-18; 19:11-17).
  • Aliwasaidia wafuasi wake katika nyakati ngumu, ama kwa kuwaondoa au kuwapa neema ya kustahimili (Matendo 6:54-60; 18:9-11; 2 Timotheo 4:16-18).
  • Alizungumza kupitia maono na unabii (Matendo 9:10-17; 11:5-15, 27-28; 18:9-11; 21:10-11). Hata alimwonyesha Yohana, ambaye alikuwa “katika Roho siku ya Bwana,” maono ambayo yangekuwa Kitabu cha Ufunuo (Ufunuo 1:9-11, NKJV)!
  • Aliwaongoza nani aende wapi(Matendo 8:26-35; 13:2-3; 16:6-10).
  • Na aliwapa karama mbalimbali za Roho (1 Wakorintho 12:4-11).

Na Yesu yule yule ambaye aliliongoza kanisa la kwanza kwa Roho Wake anaendelea kufanya hivyo leo! Injili bado inahubiriwa. Miujiza bado inatokea. Mungu bado anaweza kuwa na uhusiano wa kina na binafsi nasi.

Njia nyingine ambayo Yesu anaitumia kutuwezesha ni kazi yake kama mwombezi wetu.

Kutuombea

Mpatanishi au mwombezi ni mtu ambaye “anasimama katika nafasi” kwa ajili ya mtu mwingine. Kazi yao kuu ni kupatanisha mahusiano yaliyoharibika na kutekeleza majukumu kwa niaba ya watu ambayo hawawezi kuifanya. Uombezi unahusisha pia kusimama kwa niaba ya watu wakati kukabiliana moja kwa moja au upatanisho unaposhindikana .

Katika Agano la Kale, makuhani walitumika kama wapatanishi na waombezi kati ya Mungu na watu wake (Waebrania 7:27). Majukumu yao duniani yalitoa mfano wa kile ambacho Yesu anafanya kwa ajili yetu sasa.

Yesu aliporudi mbinguni, alibadilika kutoka kuwa dhabihu yetu msalabani na kuingia hekaluni mbinguni kama Kuhani wetu Mkuu (Waebrania 8:24-26).

Biblia inasema hekalu la duniani lilikuwa mfano wa lile la mbinguni. Vitu vyote vya ndani vilielekeza kwa Kristo atakavyofanya kazi kama mpatanishi wetu katika agano jipya (Waebrania 8:5; 9:9; 10:1).

Kama kuhani mkuu, Yesu anatuombea sisi katika namna kadhaa:

  • Kusamehe dhambi zetu
  • Kutusafisha kutoka katika unajisi wa dhambi zetu
  • Kuwa wakili wetu
  • Kutusaidia kushinda majaribu
  • Kutupa mwongozo wakati wa mahitaji, kupitia Roho Wake Mtakatifu.

Hebu tuyaangalie mambo haya.

Kusamehe dhambi

Yohana aliandika kwamba Kristo alikuja ulimwenguni “aziondoe dhambi na dhambi haimo ndani yake” (1 Yohana 3:5, NKJV).

Hii inamaanisha kwamba Alibeba matokeo ya mwisho ya dhambi – mauti na kutengwa milele na Mungu. Anatangaza kwamba tumesamehewa dhambi na kuponya uhusiano wetu uliovunjika naye (Waebrania 10:11-23). Alibeba adhabu ya kifo kwa niaba yetu na sasa anasimama mahali petu kama wakili wetu (Waebrania 9:11-12).

Kama msisitizo wa hili, kuhani mkuu wa Israeli alivaa kilemba na kifuko cha kifuani kilicho wakilisha makabila ya Israeli. Kuvaa hivi kulimaanisha yeye kubeba uzito wa hatia yao (Kutoka 28:29-30, 37-38).

Vivyo hivyo, Yesu amechukua dhambi zetu, hatia yetu, juu yake mwenyewe. “Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti; ili kwamba, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa” (1 Petro 2:24, NKJV).

Kwa kufanya hivi, Alidhihirisha kilele cha upendo usio na masharti: Alijitoa kufa kwa ajili ya kila mtu, hata akijua kwamba baadhi walikuwa dhidi Yake na hata walitaka kumuua.

“Kwa maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu. Kwa kuwa ni shida mtu kufa kwa ajili ya mtu aliye mwema. Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi” (Warumi 5:6-8, NKJV).

Kile kinachomfanya Yesu kuwa tofauti na makuhani wa Kiyahudi ni kwamba kazi yake inatosha kutuokoa. Makuhani walitumika kama wapatanishi kwa ishara, hawakuwa na uwezo halisi wa kutoa wokovu—kwa sababu wao pia walikuwa wanauhitaji!

Yesu, kwa upande mwingine, alifanya iwezekane kuokolewa kwa kukubali kile alichofanya kwa ajili yetu.

Sasa anatutakasa kutoka dhambini na kutusaidia kukua katika ukomavu wa kiroho.

Kututakasa kutoka katika dhambi zetu

Wakati Kristo anapoondoa nguvu ya dhambi katika maisha yetu, Yeye kwa upole hubadilisha mioyo yetu ili iwe kama Yeye (2 Wakorintho 3:18).

Paulo anaeleza kwamba Kristo alijitoa kwa ajili ya watu wake “ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, wale walio na juhudi katika matendo mema” (Tito 2:14, NKJV).

Uzoefu huu endelevu mara nyingi huitwa “utakaso.” Na mfano mzuri wa mchakato huu ni maisha ya Paulo.

Mtume anakumbuka badiliko lake kutoka kulitesa kanisa hadi kuwa mmoja wa wawakilishi wake wenye shauku zaidi. Ilikuwa kwa neema ya Mungu kwamba anajulikana kama mtume ambaye alibadilisha kazi yake kwenda katika kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya kanisa badala ya kuwa dhidi yake (1 Wakorintho 15:9-10, NKJV).

Kwa bahati mbaya, mara nyingi tunakosea katika mchakato huu. Lakini Mungu hatuachi.

Kuwa wakili wetu

Lakini tunapokosea, hatuhitaji kujiadhibu. Sio mapenzi ya Mungu tutende dhambi, lakini Hajitengi nasi tunapofanya hivyo.

“Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki” (1 Yohana 2:1, NKJV).

Mungu ni kama baba anayetakia mema watoto wake. Kama wazazi wengi, ameweka mipaka na matarajio iliyoundwa kwa ajili yetu kuwa na uhusiano bora naye na kupata uzoefu wa maisha katika namna bora kabisa kadri inavyowezekana.

Na kwa sehemu kubwa, mara nyingi sisi ni kama watoto wenye bidii ambao huvunja mipaka hiyo au hata kuivuka wakati mwingine. Lakini kama mzazi mwenye upendo hawaachi mtoto wake tu kwa sababu wanafanya kitu kibaya au kufanya maamuzi mabaya, Mungu hatukatai au kuacha kutupenda hata tunapomkosea.

Kama baba katika mfano wa “mwana mpotevu”, Yeye hutukumbatia. Na jambo bora zaidi ni kwamba Yeye hubadilisha makosa yetu kuwa uzoefu wa kujifunza na fursa ya kuelewa huruma zake kwa kina zaidi.

Wazazi mara nyingi huwa mawakili kwa ajili ya watoto wao kwa kuwawakilisha kama walezi wa kisheria. Wanafanya hivi wakati ambapo watoto wao hawawezi kufanya maamuzi kama watu wazima wanavyoweza. Kama watoto waliokubaliwa na Mungu, tunaye Kristo kama mwakilishi wetu. Anafanya hivi kwa sababu nguvu yetu ya kibinadamu peke yake haiwezi kutosha kutuwezesha kuishi mapenzi Yake kikamilifu.

Na Yesu sio tu anasimama katika nafasi yetu na kuwasiliana moja kwa moja na Mungu Baba, bali pia anachukua hatua wakati ibilisi, “mshtaki wa ndugu zetu,” anapojaribu kutukumbusha maisha yetu ya zamani ili kutukatisha tamaa (Ufunuo 12:10-11, NKJV).

Katika kufafanua hili, nabii Zakaria aliona maono ambapo Shetani alimhukumu na kumshitaki Yoshua kuhani mkuu mbele za Bwana, lakini akakemewa na kunyamazishwa. Mbele za Mungu, Yoshua alikuwa amesamehewa, na ibilisi hakuwa na mamlaka ya kusema vinginevyo (Zakaria 3:1-10).

Mtu pekee mwenye haki ya kutuhukumu alijitoa Mwenyewe na sasa anatufanyia upatanishi (Warumi 8:34). Ni kama kuwa na wakili na jaji upande wetu!
Kwa hivyo kupitia kazi ya Kristo ya kubadilisha maisha, Anaingia ili kunyamazisha dai lolote ambalo Ibilisi angeweza kuzua.

Simoni Petro alipokea uzoefu huu mapema. Yesu alimwambia Petro kwamba alikuwa akimwombea kwa sababu alijua kwamba Shetani anataka kumkwaza (Luka 22:31-32).

Na hili kweli lilitokea. Petro alikuwa mmoja wa wafuasi wa karibu zaidi wa Yesu, lakini alikana uhusiano wao mara tatu (Luka 22:54-62).

Baada ya kufufuka, Yesu alimrejesha Petro kwa kumpa nafasi ya kumuonyesha upendo wake mara tatu (Yohana 21:15-17).

Huruma ya Kristo ilibadilisha mvuvi huyu jeuri na shaghala baghala na kumfanya kuwa mmoja wa wahubiri hodari zaidi katika Agano Jipya (Matendo 2:14-38; 3:12-17; 4:8-12).

Kutupatia neema wakati wa mahitaji.

Yesu anawapa kanisa lake kila kitu wanachohitaji kushinda mapambano.

Chochote unachopambana nacho – iwe ni mapambano ya kifedha, ugonjwa wa muda mrefu, majeraha, au mgogoro wa kiimani – Yesu anaelewa, na anataka kukupa ushindi.

“Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu, bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupate rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji” (Waebrania 4:15-16, NKJV).

Paulo alipoandika kuhusu “mwiba katika mwili” wake (2 Wakorintho 12:7, NKJV), alikumbuka kwamba Mungu aliahidi neema yake ingekuwa ya kutosha kumwezesha kuendelea mbele. Hii ilimaanisha kuwa udhaifu wa Paulo usingemzuia, na badala yake nguvu na uwezo wa Yesu ungeangaza. Hivyo Paulo alikaribisha changamoto na upinzani. Alijua kwamba uzoefu wake mgumu ungempa nafasi ya kupata uzoefu na kudhihirisha uwezo wa Kristo wa kuokoa (aya ya 9-10).

Aina hii ya neema tayari ipo wakati tunapopambana na mwelekeo na tabia za dhambi.

Kutusaidia Kushinda Majaribu

Kristo anaweza kutusaidia kushinda majaribu kwa sababu anajua jinsi ilivyo kupambana na dhambi. Ingawa kamwe hakutenda dhambi, alikabiliana na majaribu yote tunayokutana nayo. Lakini pia alishinda yote. Ana uwezo wa kushinda dhambi, na ni furaha Yake kutupatia nguvu ya kushinda pia.

“Hivyo ilimpasa kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote, apate kuwa kuhani mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili afanye suluhu kwa dhambi za watu wake. Na kwa kuwa mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wao wanaojaribiwa” (Waebrania 2:17-18, NKJV).

Maandiko yanasema hakuna jaribu lenye nguvu sana ambalo Yesu hawezi kutusaidia kulishinda. Pamoja na Yesu kama mwombezi wetu, daima kuna njia ya Kutokea (1 Wakorintho 10:13).

Wakati mwingine njia ya kutokea ni kwa kuondoa kitu fulani katika maisha yetu.

Jifunze kwa waumini wapya wa Efeso, kwa mfano. Walikuwa wakijihusisha na mizimu, lakini baada ya kuona Yesu akifanya miujiza kupitia Paulo, waliharibu “vitabu vyao vya uganga” (Matendo 19:11-20). Hii ilikata uhusiano wao na mazoea ya mizimu na ingefanya iwe rahisi kushinda majaribu ya kurudi nyuma.

Lakini kuondoa kitu kuna maana ya kuhitaji pia kuchukua kitu bora badala yake. Na sio kila mtu lazima aondoe kitu kabisa ili kushinda majaribu. Inaweza kuwa swala la kuweka mipaka au kubadilisha mtazamo. Kwa hivyo, kuna njia nyingi ambazo Mungu husaidia watu kushinda mapambano yao.

Hivyo ingawa hatuwezi kumwona na kumsikia Yesu kama watu walivyoweza wakati wa huduma yake duniani, kuna njia nyingi zinazoweza kutusaidia kuona anavyofanya kazi katika maisha yetu. Kupitia Roho Mtakatifu wake, anafanya huduma yake ya kikuhani, ya utakaso.

Yesu anafanya nini sasa?

Kazi ya Yesu haijabadilika hata leo, hata baada ya muda wote huu. Yeye bado anaendelea kushiriki kikamilifu katika kila wakati wa maisha yetu. Anatafuta kutuokoa kutoka vifungo na dhambi wakati tunapojifunza zaidi na zaidi kuhusu upendo wake, tabia yake, na utume wake. Wakati Akikamilisha makao yetu ya milele, anaendelea kutusaidia kupitia Roho Mtakatifu:

  • Anatuwezesha kumshinda shetani na majaribu (1 Petro 5:8-10)
  • Anatia nguvu maombi yetu (Warumi 8:26-27)
  • Anatusaidia kukua katika imani yetu na ukuaji wa kiroho (2 Petro 1:5-10)
  • Anasafisha mioyo yetu na tabia zetu, na mwishowe tunagundua jinsi shauku zetu za kweli, safi, na za kina zinavyolingana na zake (Wafilipi 2:12-13)

Na bila shaka, mchakato huu utaonekana tofauti kwa kila mtu. Sisi sote tuna uzoefu tofauti, mwelekeo, mitazamo, n.k. Kwa namna moja au nyingine, sote tunajaribiwa na tamaa ya uchoyo, wivu, kiburi, n.k. Lakini tunaweza kuwa na hakika kwamba Yesu, Muumba wetu, Mwokozi wetu, na Kuhani wetu Mkuu, anaungana nasi katika safari. Na Yeye anajua kabisa tunachohitaji kushinda kila changamoto tunayokabiliana nayo.

“Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe” (2 Petro 1:3, NKJV).

Hata wakati kazi ya upatanishi ya Yesu ikiwa inaendelea leo, kitu kimoja cha kuvutia kimebadilika katika patakatifu pa mbinguni la Mungu.

Agano la Kale linazungumzia wakati kuhani mkuu wa Israeli alipoingia mahali patakatifu zaidi katika patakatifu ili kukamilisha upatanisho na watu wa Mungu (Walawi 16). Hii ilikuwa tukio la ishara, likitabiri kitu kingine ambacho Yesu alifanya (na anaendelea kufanya) kwa ajili yetu.

Ikiwa una nia ya kujifunza kuhusu tukio hili na jinsi linavyoelekeza zaidi kwa Yesu kama mwombezi wetu, tazama kurasa hizi kuhusu upatanisho au

  1. Nichols, Francis D., https://archive.org/details/SdaBibleCommentary1980/SdaBc-6%20%2845%29%20Romans/page/n125/mode/2up []
  2. John 14:16; 15:26; 16:13 []
  3. Commentary on Leviticus 23:11, NKJV Andrews Study Bible []
  4. Commentary on Leviticus 23:16, NKJV Andrews Study Bible []

Je, Una swali kuhusu Waadventista? Uliza hapa!

Pata majibu kwa maswali yako kuhusu Waadventista Wasabato

Majibu Zaidi

Je, Tunaweza Kumpata Yesu Kristo Katika Agano la Kale?

Je, Tunaweza Kumpata Yesu Kristo Katika Agano la Kale?

Je, Tunaweza Kumpata Yesu Kristo Katika Agano la Kale?Ndio, unaweza kushangaa kujua kwamba kuna mamia ya aya katika Agano la Kale kuhusu Yesu. Ingawa hazimtaji Yesu kwa jina, zinataja majina mengine tunayoyahusisha naye kama Masihi, Mwana wa Mungu, na Mwana wa Adamu....

Ni Lini Yesu Atarudi Tena?

Ni Lini Yesu Atarudi Tena?

Biblia inasema kwamba hakuna mtu anayeweza kujua, hata malaika (Mathayo 24:36)! Ndio maana Biblia inatushauri tusijaribu kuweka tarehe ya kurudi kwake. Kwa sasa, tunahimizwa kuwa tayari.