Shule ya Sabato ndio sehemu ya kujifunza Biblia ya programu za kanisa katika makanisa mengi ya Waadventista wa Sabato. Ni wakati wa kujifunza Biblia kuhusu mada au somo fulani. Badala ya kumsikiliza mhubiri, watu wanashirikiana na wenzao, hivyo kuwa nafasi nzuri ya kujenga urafiki.
Yawezekana rafiki au jamaa yako Mwadventista amewahi kukuambia kuhusu Shule ya Sabato. Au labda uliona bango la Shule ya Sabato nje ya Kanisa la Waadventista wa Sabato.
Una hamu ya kujua zaidi? Hebu twende pamoja katika kupata uzoefu huo. Mwishoni, utakuwa na kila kitu unachohitaji kujua ili ujaribu mwenyewe.
Tutajadili:
Shule ya Sabato ni nini?
Shule ya Sabato ni kama kikundi kidogo cha kujifunza Biblia kinachokutana asubuhi ya siku ya Sabato (Jumamosi) mbali na ibada kuu katika Kanisa la Waadventista Wa Sabato. Ni sawa na shule ya Jumapili kwa Wakristo wengine, na inapatikana kwa watu wa umri wote: kutoka kwa watoto wachanga hadi wazee.
Washiriki wa kanisa na wageni wanakaribishwa kushiriki, kujifunza, na kukua katika imani yao katika wakati huu.
Kwa hiyo Shule ya Sabato inajumuisha nini hasa?
Ina madhumuni matatu makuu:
1. Kujifunza Biblia
2. Ushirika
3. Utume
Kujifunza Biblia

Photo by Hannah Busing on Unsplash
Kauli mbiu ya Kanisa la Waadventista Wa Sabato katika Shule ya Sabato imekuwa “kanisa linalo jifunza.” Wakati huu tunachambua Biblia kwa undani, tukishiriki ufahamu na kukabiliana na mada zenye changamoto. Kipaumbele sio kuwa na majibu yote, bali kumtafuta Mungu na kutafuta majibu katika Neno lake huku Roho Mtakatifu akituongoza.
Kwa njia hii, tunakua katika safari zetu za imani tunaposhiriki na wengine na kujifunza kutoka kwao.
Unapohudhuria kwa mara ya kwanza, unaweza kutaka tu kutazama na kusikiliza, na hilo ni sawa kabisa! Lakini ikiwa unataka kuchangia, maswali yako na mawazo yako yataboresha wakati wa masomo ya Biblia. Kusikia uzoefu na ushuhuda wa wengine kutatuonyesha jinsi ambavyo Mungu bado anafanya kazi katika maisha ya watu leo.
Ushirika
Biblia inasema mengi kuhusu umuhimu wa jamii. Tunahitajiana. Na kusudi la pili la Shule ya Sabato ni kujenga hisia hiyo ya jamii. Ni wakati mzuri wa kuingiliana, kujuana, na kutiana moyo. Uwazi na uaminifu ni muhimu.
Tofauti na wakati wa ibada kuu ya kanisa, Shule ya Sabato inaruhusu washiriki wote kusimulia wanachohisi mioyoni mwao. Hatuketi tu na kumsikiliza mtu mmoja akiongea.
Vikundi vidogo hufanya hili liwezekane. Kulingana na kanisa, idadi ya washiriki inaweza kuwa watu 5-10 au 20-40. Makanisa katika maeneo makubwa mara nyingi hugawanya madarasa ili kuhakikisha yanabaki yakiwa madogo kiasi cha kutosha kwa mjadala.
Mazingira katika Shule ya Sabato ni ya kufurahisha zaidi hivyo watu hujisikia huru kutoa mawazo yao.
Utume

Photo by RDNE Stock project
Makanisa mara nyingi hutumia wakati wa Shule ya Sabato kusisitiza miradi ya uinjilisti ya ndani na ya kimataifa. Katika baadhi ya madarasa, washiriki wanaweza hata kuungana pamoja na kufikia jamii yao.
Kwa mfano, wanaweza kuamua kutembelea wagonjwa au kujitolea kuandaa supu mchana wa Sabato. Au wanaweza kukusanya pesa pamoja kumfadhili mtoto. Kuna mambo mengi yanayoweza kufanyika.
Kwa ufupi, Shule ya Sabato huturuhusu kukusanyika pamoja, kujifunza Neno la Mungu kwa kina, na kuhudumia ulimwengu wetu na jamii yetu. Inafuata mfano wa kanisa la Kikristo la awali, ambalo lilikusanyika katika vikundi vidogo kwa ajili ya kujifunza Biblia na ushirika:
“Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali” (Matendo 2:42; pia aya 46–47, NKJV).
Yesu Mwenyewe aliwafundisha wanafunzi wake katika vikundi vidogo (Mathayo 24:3; Marko 9:28), na aliahidi hivi:
“Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao” (Mathayo 18:20, NKJV).
Kinachofanyika wakati wa Shule ya Sabato ni nini?
Shule ya Sabato kawaida huanza asubuhi, kati ya saa 3 na saa 5 asubuhi kulingana na kanisa, na inaendelea kwa takribani saa moja na dakika 20. Katika wakati huu Muda mwingi ni kwa ajili ya kujifunza Biblia. Lakini katika makanisa mengi, huanza na shughuli nyingine kama huduma ya nyimbo, ripoti ya utume, na maombi.
Hebu tupate uzoefu kamili.
Shule ya Sabato inaanza
Makanisa mengi huanza na Shule ya Sabato ili kuruhusu programu ya awali na watu wote waliokusanyika pamoja. Lakini mara chache, ibada kuu hufanyika kwanza, ikiwa mchungaji ana makanisa mengi ya kuhubiri kila Sabato.
Na katika baadhi ya makanisa makubwa kuna ibada mbili tofauti ili waweze kujumuisha washiriki wote. Kisha kuna wakati wa Shule ya Sabato kati yake. Kwa njia hiyo haijalishi ibada ipi unahudhuria, Shule ya Sabato bado inaweza kuingizwa kwa urahisi katika ratiba yako ya asubuhi.
Lakini kwa mfano huu, tutawasili saa tatu unusu asubuhi—wakati wa kawaida wa kuanza Shule ya Sabato.
Tutaelekea kwenye hekalu—ukumbi mkuu wa kanisa—ambapo programu ya awali inaendelea. Watu kawaida hukutana hapa kwanza.
Tunapoingia, tunaweza kusikia sauti ya nyimbo tayari. Nyimbo kadhaa zaidi huimbwa kabla ya mratibu wa asubuhi (anayejulikana kama mkuu wa Shule ya Sabato) kusimama kuwakaribisha kila mtu na kuomba. Mtu huyu anatangaza kwamba ripoti ya utume itatolewa baadaye.
Ripoti ya utume inaweza kutokea kwa njia kadhaa tofauti.
Idara ya Ujumbe wa Waadventista wa Sabato hutoa video ya “Mission Spotlight” kila mwezi, ambayo inasisitiza kazi ya utume ya kanisa katika eneo fulani duniani. Video hiyo ina urefu wa dakika 5 hadi 10.
Siku nyingine za Sabato, mtu anaweza kusoma kisa cha utume cha wiki kutoka kwenye kitabu cha Utume wa Vijana na Watu Wazima.
Baadaye, mkuu wa Shule ya Sabato hutoa baadhi ya matangazo, husoma aya ya Biblia, au kusoma wazo la kiroho kabla ya kuwaruhusu watu kwenda kwenye madarasa yao.
Muda wa vikundi vidogo

Photo by Israel Torres
Sehemu muhimu zaidi ya Shule ya Sabato hufanyika wakati vikundi vidogo vinakusanyika kujifunza Neno la Mungu kwa undani.
Sasa ni karibu saa 4 asubuhi, maana yake vikundi vitakuwa na muda wa takribani dakika 45 hadi 50 pamoja.
Baadhi ya madarasa ya watu wazima hukutana katika eneo la kanisa, wakati wengine wana vyumba tofauti. Tunaelekea kwenye mduara wa viti na kukaa chini na kikundi cha watu kama 10 hivi.
Mtu anayeongoza darasa la shule ya Sabato atamsalimia kila mtu, labda atazungumza kidogo, na kuuliza ikiwa kuna ombi la kushiriki kwa pamoja. Dakika hizi chache za mazungumzo husaidia kuvunja ukimya na kuunganisha washiriki.
Kisha mwalimu anaomba, akiomba Roho Mtakatifu aongoze, na tunajitosa katika somo la wiki hii.
Tunajifunza nini?
Darasa linaweza kujifunza mada fulani au kitabu cha Biblia, au hata kusoma Biblia pamoja. Lakini katika makanisa mengi ya Waadventista, mwalimu ataongoza mjadala kupitia mwongozo wa kujifunza Biblia wa darasa la shule ya Sabato.
Hebu tujifunze kuhusu hilo baadaye.
Miongozo ya kujifunza Biblia ya Shule ya Sabato ni nini?
Kanisa la Waadventista wa Sabato linazalisha Mwongozo Rasmi wa kujifunza Biblia kwa Watu Wazima ili utumike wakati wa Shule ya Sabato. Mara nyingi huitwa “Lesoni” au “Mwongozo wa Robo,” jina ambalo linatokana na neno robo kwa sababu inalenga robo moja ya mwaka (miezi 3 au wiki 13). Katika kipindi hicho, somo la kila wiki linajikita katika sehemu tofauti za mada iliyochaguliwa au kitabu cha Biblia.
Kwa mfano, somo moja kamili la mwongozo katika robo linaweza kujikita katika kitabu cha Mathayo. Lingine linaweza kuwa kuhusu mada ya mwili wa Kristo, mahusiano ya familia, Tunda la Roho, n.k..
Mwongozo wa Shule ya Sabato una ukurasa mmoja kwa kila siku. Ukurasa huo hutoa mafungu ya Biblia ya kuchunguza na maswali ya kujibu pamoja na maelezo fulani.
Madarasa mengi hupitia somo la wiki iliyopita siku baada ya siku na kujadili walichojifunza.
Lakini usiwe na wasiwasi – hata kama hukufanikiwa kusoma somo la wiki, bado utaweza kufuatilia na kufurahia mjadala.
Naweza leta nini kwenye Shule ya Sabato?
Unahitaji kuja wewe mwenyewe na nia ya kujifunza—kweli, ni rahisi kama hivyo. Lakini wengine pia hupenda kuja na Biblia zao na nakala ya lesoni zao.
Mwongozo wa kujifunza Biblia wa Shule ya Sabato kwa kawaida hukabidhiwa Sabato kabla ya kuanza kwa robo mpya. (Robo huanza mwezi wa Januari, Aprili, Julai, na Oktoba.)
Ikiwa hukuwepo ili kuupata, kuna uwezekano kwamba kuna miongozo ya ziada iliyobaki kwenye meza katika mlango wa kanisa. Na ikiwa sivyo, unaweza kupata somo la Shule ya Sabato mtandaoni au kwenye programu ya Shule ya Sabato kwenye simu yako ya mkononi.
Sadaka ya Shule ya Sabato
Wakati wa kujifunza Biblia, mwalimu anaweza kusitisha somo ili kupitisha bahasha chache kwa ajili ya sadaka ya Shule ya Sabato. “Sadaka” ni zawadi ya hiari ya pesa ili kusaidia kusaidia mambo mbalimbali katika kanisa. Sadaka hii inakusanywa katika madarasa yote, pamoja na yale ya watoto.
Unaweza kugundua kuwa kuna bahasha mbili. Moja ni kwa ajili ya matumizi ya Shule ya Sabato, kama vile ununuzi wa mwongozo wa masomo ya Biblia.
Bahasha nyingine ni kwa ajili ya sadaka ya utume na inasaidia eneo la kanisa la ulimwengu lililochaguliwa kwa robo (eneo lile lile lililoangaziwa katika “Mission Spotlight”).
Lakini hakuna shinikizo—hulazimishwi kutoa.
Kutoa sadaka ni uamuzi wako na kile Mungu anaweka moyoni mwako (Kutoka 35:22); ni tofauti na zaka (Malaki 3:10), ambayo inahusisha kurudisha asilimia kumi ya mapato yetu kwa Mungu.
Sadaka ya Sabato ya 13 ni nini?
Sadaka ya Sabato 13 huwa ni neno linalotumika kwa ajili ya ukusanyaji maalum wa pesa siku ya mwisho ya robo—Sabato ya 13. Siku hiyo, makanisa ulimwenguni kote huchangia mradi maalum wa uinjilisti uliochaguliwa na Idara ya Uinjilisti ya Kanisa la Waadventista wa Sabato Konferensi Kuu.
Mbali na ukusanyaji wa sadaka, madarasa ya watoto yanaweza kuandaa programu maalum ya awali. Wanaweza kuimba wimbo au kufanya igizo linalohusiana na eneo la dunia ambapo mradi wa uinjilisti unafanyika.
Shule ya Sabato imeisha kwa asubuhi
Mara nyingi utasikia ishara fulani mwishoni mwa Shule ya Sabato saa 4:50 asubuhi. Ibada kuu ya kanisa itaanza hivi karibuni.
Mwalimu wetu hutoa maoni ya mwisho kabla ya kumaliza kwa maombi. Tunatumia muda mfupi kuzungumza na watu huku tukikusanya vitu vyetu na kwenda kutafuta kiti kwa ajili ya ibada kuu.
Tumemaliza uzoefu wetu wa Shule ya Sabato kwa watu wazima, lakini unaweza kujiuliza kuhusu madarasa kwa watoto.
Hebu tuangalie chaguzi tofauti katika kanisa la kawaida.
Ni chaguzi gani zipo katika Shule ya Sabato kwa makundi tofauti ya umri?
Makanisa mengi ya Waadventista wana madarasa ya Shule ya Sabato kwa watu wazima na watoto. Madarasa haya hugawanywa kulingana na umri au hatua ya maisha ili kutoa yaliyo sahihi na fursa ya ushirika. Kuna makundi matatu makuu: watoto, vijana/vijana wazima, na watu wazima.
Lakini makanisa makubwa huchukua makundi haya na kuyagawa zaidi.
Mara nyingi, kuna madarasa maalum zaidi kwa watu wazima: darasa kwa wanawake, darasa kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, au darasa kwa watu wanaotaka kujiandaa kwa ubatizo.
Madarasa ya watoto pia yamegawanywa zaidi kama ifuatavyo:
- Awali (kuzaliwa–umri wa miaka 2)
- Chekechea (umri wa miaka 3–4)
- Msingi (umri wa miaka 5–9)
- Vijana wadogo (umri wa miaka 10–12)
- Imani hai (umri wa miaka 13–14)
- Vijana/ Uhusiano na Yesu (umri wa miaka 15–18)
Kwa hiyo nini hufanyika katika madarasa ya watoto?
Kanisa la Waadventista wa Sabato hutoa vifaa vya kujifunzia Biblia kwa kila darasa. Walimu wanaweza kuchagua kutumia vifaa hivi kama muhtasari wa msingi kwa madarasa yao.
Darasa la Awali ndiyo darasa lenye ushirikiano kuliko yote. Kawaida, darasa litakuwa na mapambo na vitu vya kufanana na mandhari, kama vile mbingu au Uumbaji. Katika programu nzima, mwalimu husoma maelezo mafupi, yaliyochanganywa na nyimbo na shughuli kwa ajili ya watoto kufanya.
Darasa pia litakuwa na wakati wa visa hadithi, kutumia vifaa vya kujifunzia vinavyovutia usikivu wa watoto. Kitamaduni, madarasa mengi ya Sabato ya Watoto wa Waadventista walitumia ubao—ambao vipande vilivyokatwa vya kitambaa vya wahusika na vitu viliwekwa ili kusimulia hadithi.
Madarasa ya Shule ya Sabato ya Kidato cha Awali na Msingi pia hutumia michezo na vitu kuingiliana na watoto, ingawa kufikia umri huu, wanaweza kuelewa na kushiriki zaidi. Mwalimu anaweza kuwapa picha za kupaka rangi au vitu vya kutengeneza, pia.
Wanafunzi wanapokuwa wakubwa, madarasa yanabadilika kutoka shughuli za vitendo hadi kuzungumza na kushirikiana kwa kiwango kikubwa zaidi. Cha kuzingatia ni kutumia kanuni na visa vya Biblia katika maisha ya watoto na vijana katika kila kundi la umri.
Kwa kila darasa—kutoka kwa watoto wadogo hadi vijana—kanisa la Waadventista limeandaa vifaa vya kujifunzia nyumbani vinavyo jumuisha hadithi za Biblia zinazofaa kwa umri na masomo ya kujenga tabia.
Jinsi ya kupata Shule ya Sabato karibu nawe
Sasa unajua zaidi kuhusu Shule ya Sabato, kilichobaki ni kupata uzoefu wa moja kwa moja! Tovuti ya Kanisa la Waadventista Wasabato ina chombo kinachoweza kukuwezesha kupata kanisa katika eneo lako. Mara unapopata moja, angalia tovuti yake au ukurasa wa Facebook ili kujua muda wa ibada.
Pia unaweza kuleta Shule ya Sabato nyumbani kwako. Pakua somo la Shule ya Sabato kwenye tovuti ya Mwongozo wa Kujifunza Biblia kwa Watu Wazima. Kwa njia hii, unaweza kufuata kile ambacho makanisa ulimwenguni kote wanajifunza. Huenda hata ukaweza kutazama moja kwa moja ibada za kanisa lako la karibu.
Programu nyingi mtandaoni zinafuata mwongozo huo huo wa kujifunza, zikitoa ufahamu na mjadala kuhusu somo la wiki. Hapa kuna baadhi ya vipindi maarufu zaidi:
Haijalishi uko wapi, unaweza kufurahia baraka za kujifunza Neno la Mungu!
Shule ya Sabato ni kwa ajili ya kila mtu.

Photo by Erika Giraud on Unsplash
Shule ya Sabato hutoa mazingira ambayo watu wa umri wote wanaweza kuungana, kujifunza Biblia, na kutimiza utume wa kanisa la ulimwengu.
Miongozo ya kujifunza Biblia husaidia kuwaunganisha watu duniani kote wanapojikita katika somo moja.
Na muundo wa Shule ya Sabato huwaruhusu watu kumfahamu Yesu na wenzao vizuri zaidi wanapokuja na maswali na mawazo yao. Wakati huu, urafiki unaweza kuchanua na ukuaji wa kiroho unaweza kutokea.
Iwe wewe ni kijana au mama mdogo au mtu aliyezeeka, kuna mahali kwako!
Hivyo ndivyo ilivyo:
Kuungana na wengine kuchambua ukweli wa Biblia ambao ni muhimu kwa maisha yetu na utume wa kumshiriki Yesu Kristo kwa wengine.
Tayari kuona mambo wewe mwenyewe?
Tafuta Kanisa
If you’re interested in finding a local Adventist church near you, you can use the Adventist Locator provided by the General Conference of Seventh-day Adventists.
Majibu Zaidi
Ninawezaje Kuanza Kutunza Sabato?
Sabato, inayokuja kila siku ya saba ya juma, ni siku maalum inayoheshimu amri ya nne na uumbaji wa Mungu.


