Hapana, Waadventista hakika hawaamini kwamba wao ndio pekee watakao kwenda mbinguni. Kwa kweli, hatuamini kwamba kupokelewa mbinguni kunategemea kanisa au madhehebu tunayohusiana nayo. Watu kutoka sehemu mbalimbali duniani kutoka madhehebu ya Kikristo tofauti, dini, na maisha watapokelewa na Yesu.
Hii ni kwa sababu Maandiko yanafafanua wazi kwamba wokovu hautegemei kutimiza orodha fulani ya mahitaji au kuwa sehemu ya klabu fulani. Ni kuhusu kumjua Yesu katika namna binafsi (Mathayo 7:22-23; Yohana 17:3).
Jiunge nasi tunapojibu:
Je, ni lazima kuwa Mwadventista wa Sabato ili kwenda mbinguni?

Photo by Igor Rodrigues on Unsplash
Ushirika kanisani, iwe katika Kanisa la Waadventista wa Sabato, Kanisa la Baptisti, au dhehebu lingine lolote, haituamulii ikiwa tutaishia mbinguni. Hii ni kwa sababu kuingia kwetu mbinguni kunategemea uhusiano wetu na Yesu Kristo. Tunamwamini na kupokea kutoka kwake zawadi ya uzima wa milele (Matendo 16:31).
Mtego ni kwamba sisi binadamu tunapenda kuweka mkazo mwingi katika kuwa sehemu ya kikundi fulani hivi kwamba tunasahau kuwa mshiriki katika jamii fulani ya imani wakati fulani haina maana yoyote. Tunaweza kuwa sehemu ya jamii lakini tukakosa kilicho muhimu zaidi—uhusiano binafsi na Mungu.
Tunaweza kuamini kila fundisho la kanisa fulani na kufuata Amri Kumi neno kwa neno lakini tusiwe na imani katika Yesu, Mwana wa Mungu—ambayo ndiyo njia pekee ya kuokolewa (Waefeso 2:8-9).
Sasa, unaweza kujiuliza, Je, ni nini kuhusu kuwa sehemu ya masalio? Unaweza kusikia Waadventista wakizungumzia hili, na unajiuliza jinsi linavyohusiana na wokovu.
Hebu tuangalie hiyo.
Je, lazima niwe sehemu ya masalio ili niende mbinguni?

Image by Gerd Altmann from Pixabay
Waadventista wanafahamu kwamba katika historia yote, daima kumekuwepo na Masalio-kundi dogo la watu ambao huchagua kuwa waaminifu kwa Mungu wakati jamii inapowashinikiza kufanya vinginevyo. Kundi hilo sio kikundi au kanisa tunachojiunga nacho bali ni maelezo ya watu waaminifu kwa Yesu. Ufunuo 14:12 unaelezea kundi dogo katika nyakati za mwisho ambao watasaidia kuonya dunia kuhusu mpambano lake la mwisho.
Moja ya Imani za Msingi 28, au mafundisho ya msingi ya Uadventista wa Sabato, inaelezea somo hili kama ifuatavyo:
“Kanisa la ulimwengu linajumuisha wote wanaoamini kweli kweli katika Kristo, lakini katika siku za mwisho, wakati wa uasi utakaoenea kote [kuacha kweli ya Mungu], kundi dogo limeitwa kudumisha amri za Mungu na imani ya Yesu. Kundi hili linatangaza kuja kwa saa ya hukumu, linatangaza wokovu kupitia Kristo, na inatangaza ujio wake wa mara ya pili wa hivi karibuni. Tangazo hili limewakilishwa na malaika watatu wa Ufunuo 14; linakwenda sambamba na kazi ya hukumu mbinguni na kusababisha kazi ya toba na matengenzo duniani. Kila anayeamini ameitwa kuwa na sehemu binafsi katika ushuhuda huu wa ulimwengu wote.”1
Masalio katika siku za mwisho
Wazo hili la masalio katika siku za mwisho linatokana na imani yetu kwamba wakati huo, pambano kuu (vita kati ya wema na uovu, Mungu na Shetani) itafikia kilele chake katika mgogoro wa ibada. Mgogoro huu utatenga kila mtu duniani katika makundi mawili—wale wanaobaki waaminifu kwa Mungu na wale wanaochagua kufuata sheria zilizotengenezwa na wanadamu.
Unabii wa Biblia unawakilisha makundi haya mawili kama kanisa lenye imani la Mungu na kanisa lililo asi la Babeli.
Lakini kumbuka:
Kanisa katika Biblia haimaanishi jengo au madhehebu. Inahusiana na mwili wa waamini katika Kristo.
Agano Jipya linaelezea kanisa hili kwa ishara ya mwanamke safi, anayelindwa na Mungu (Ufunuo 12:1, 6). Wakati huo huo, Ufunuo unatumia mwanamke asiye mwaminifu, mzinzi aitwaye Babeli kuwakilisha machafuko ya kidini ambayo Shetani anauongoza ulimwengu kwa upotofu (Ufunuo 17:2-6).
Kabla Yesu arudi, kilichosalia cha kanisa la kweli la Mungu huitwa masalio katika Toleo la New King James la Biblia (Ufunuo 12:17).
Kulingana na Ufunuo 12:17 na 14:12, watu hawa:
- Wanashika amri za Mungu
- Wana ushuhuda wa Yesu
Watakuwa kikundi kidogo cha wafuasi waaminifu wa Mungu ambao wanapinga mafundisho ya uwongo ya dini bandia ya Shetani kwa kufuata sheria ya Mungu na kushikilia ushuhuda na imani ya Yesu.
Ili kuwa wazi, hata hivyo, wafuasi hawa hawashiki amri ili kupata wokovu. Kulingana na mafundisho mengine ya Neno la Mungu (Waefeso 2:8-10; Warumi 3:24), aya hii inaeleza tu wanavyofanya kama matokeo ya kupokea wokovu wa Yesu.
Ingawa Biblia inaeleza wazi kwamba masalio watakuwa na jukumu maalum mwishoni mwa nyakati, dhana ya masalio sio mpya kabisa.
Masalio katika Biblia

Baadhi ya visa vya mwanzo kabisa katika Biblia zinazungumzia vikundi vidogo vya watu ambao walibaki wakiwa waaminifu kwa Mungu na kuwaongoza wengine kwenye kweli yake.
Mmoja ya mifano katika Agano la Kale ni kisa cha Nuhu na familia yake.
Walikuwa watu pekee waliobaki waaminifu kwa Mungu katika ulimwengu muovu. Na walikuwa na kazi—kuwaonya watu duniani kuhusu gharika inayokuja (Mwanzo 6:5–7).
Vivyo hivyo, masalio watakao kuwepo kabla ya Yesu kurudi watakuwa na onyo maalum linaloitwa ujumbe wa malaika watatu (Ufunuo 14:6–12, 14). Ni wito kwa watu kutoka katika machafuko ya kidini na kumtukuza Mungu kama Muumba wetu. Pia ni onyo kuhusu mifumo ya ibada ya uwongo.
Waadventista wa Sabato wanatafuta kuwa sehemu ya kundi hili la watu, lakini wanafahamu kwamba Biblia haiwachukulii kundi hili kuwa la pekee. Wote wanaomfuata Yesu kwa uaminifu watakuwa sehemu yake katika nyakati za mwisho.
Biblia inasema nini kuhusu wale watakao kwenda mbinguni?
Moja ya aya zinazojulikana zaidi katika Biblia inasisitiza ukweli kuhusu wokovu ambao tunapata katika kurasa zake—”kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele” (Yohana 3:16, NKJV). Imani katika Yesu Kristo ni sharti la kwenda mbinguni (Warumi 10:9–13).
Imani hii sio tu imani katika uwepo wa Mungu, hata hivyo (Yakobo 2:19). Ni kuhusu kumtumaini Yeye na nguvu Yake kutuokoa kupitia uhusiano binafsi na Yeye. Ndiyo maana Yohana 17:3 inatuambia kwamba kumjua Yesu Kristo ndio kiini cha uzima wa milele.
Ni aina ya imani na upendo kwake ambao hutuchochea kufuata nyayo za Yesu—sio kwa sababu tunahitaji kupata upendeleo wake bali kwa sababu tayari tunao upendeleo wake. Na imani hii na upendo hufunuliwa kupitia utii (Yohana 14:15).
Hivyo, kuwa tayari kwa ajili ya mbingu kunahusiana na mchakato wa kuhesabiwa haki na utakatifu.
Tunahesabiwa haki (kusamehewa na kusafishwa) tunapokubali kafara ya Yesu kwa ajili ya dhambi zetu (Warumi 3:38; 1 Yohana 1:9). Hapo ndipo mchakato wa utakatifu—au ukuaji—unapoanza tunapojisalimisha kila siku mioyo yetu kwa Mungu. Hatua hizi zote mbili sio kwa ajili ya kujipatia mbingu. Badala yake, zote zinahusisha uamuzi wa makusudi wa kukubali malipo ya Yesu kwa mshahara wa dhambi na kujisalimisha kufuata mapenzi Yake.
Mungu anataka kila mtu awepo mbinguni
Mungu anatoa zawadi ya uzima wa milele kwa kila mtu—bila kujali madhehebu. Shauku yake kuu ni kwamba sote tuokolewe (1 Timotheo 2:4–6), na inamuumiza watu wanapochagua kugeuka mbali na zawadi yake (Ezekieli 33:11).
Anamuona kila mmoja wetu kama mtu binafsi. Anaona hali ya mioyo yetu na tulipo katika safari zetu za kiroho. Na akizingatia hilo, anatuongoza kuelekea ufahamu wa kina wa ukweli.
Tunaweza tusiwe wote katika sehemu moja katika safari zetu.
Hatufikii hitimisho moja katika kila mada.
Lakini Mungu anatuona kama tulivyo, anakutana nasi pale tulipo, na anahidi kutusaidia kukua kuwa watu aliotuumba kuwa.
Je Unataka kuelewa vizuri imani ya Waadventista Wa Sabato kuhusu wokovu?
Kurasa Zinazohusiana
- “What Adventists Believe About the Remnant in the Bible,” Seventh-day Adventist World Church, https://www.adventist.org/remnant-and-its-mission/. [↵]
Majibu Zaidi
Waadventista Wa Sabato wanaamini nini kuhusu Ubatizo?
Kama Wakristo wengi wa Kiprotestanti ulimwenguni kote na katika historia, Kanisa la Waadventista wa Sabato linaamini katika ubatizo, sherehe ambapo watu huzamishwa ndani ya maji kudhihirisha hadharani “kufa kwa maisha ya zamani” na “kuanza kwa maisha mapya katika Kristo”.
Waadventista Wasabato wanaamini nini kuhusu Biblia?
Biblia ndiyo msingi wa kila kanuni na mafundisho ya Waadventista wa Sabato.
Waadventista Wa Sabato Wanaamini Nini Kuhusu Mamlaka ya Biblia?
Jifunze jinsi kitabu kimoja cha zamani sana (Biblia) kilivyo msingi pekee wa imani zote za Waadventista wa Sabato.
Je, Waadventista Wa Sabato Wanaamini Nini Kuhusu Uumbaji Katika Biblia?
Waadventista Wa Sabato wanaamini kwamba Mungu ndiye Muumbaji wa ulimwengu. Wanafikia hitimisho hili kutoka kitabu cha kwanza cha Biblia—Mwanzo.
Namna Waadventista Walivyojifunza Fundisho la Patakatifu na Maana Yake
Wakati Waadventista wanapozungumzia “fundisho la Patakatifu,” wanarejelea dhana kwamba hekalu la mbinguni linafunua mpango wa wokovu









