Je, Waadventista Wasabato Wana “Sheria”?

Hapana, Waadventista Wasabato hatuna “sheria” tunazopaswa kufuata.

Hii ni kwa sababu hatuamini kwamba tunaokolewa kwa matendo au kufuata sheria. Badala yake, tunaamini kwamba tunaokolewa kwa neema kwa njia ya imani katika Yesu Kristo (Waefeso 2:8-9).

Na kwa sababu tuna utambulisho huu na hakikisho katika Kristo, Waadventista (kama wakristo wengi) wana jitahidi kuishi kanuni zisizobadilika zilizo elezwa katika Biblia. Ili kutusaidia kufanya hivyo, Kanisa la Waadventista lina seti ya mafundisho ya Kibiblia ambayo hutusaidia kutafsiri Maandiko na kutumia kanuni hizi.

Kuwa Mwadventista kunamaanisha kwamba mtu binafsi anakubaliana na kujisalimisha kwa mafundisho haya, akiwa na lengo la kufunua tabia kama ya Kristo katika maisha yake ya kila siku. Hata hivyo, utekelezaji wa vitendo wa kanuni hizi unaweza kuonekana tofauti kidogo kwa kila mshiriki wa kanisa, kulingana na imani binafsi, utamaduni, wakati, na hali.

Hapo ndipo uzuri wa Ukristo wa Waadventista unapoonekana—sio kuhusu tunachopaswa kufanya bali tunachochagua kufanya kama matokeo ya uhusiano wetu binafsi na Mungu na utafiti wa Neno lake.

Hebu tuchunguze mada hii kidogo zaidi ili kuondoa ufahamu wowote usio sahihi. Tutajadili:

Kwanza, tutazame zaidi kuhusu msingi wa haya yote.

Kiini cha swala lenyewe: kumfuata Yesu

Shauku kuu ya Waadventista wa Sabato ni kuwa wafuasi wa Yesu.

Kwa hivyo, hilo lina maana gani, haswa?

Yesu alipowaita wanafunzi kumi na wawili, walikuwa wanaishi naye na kujifunza kutoka kwake kwa miaka mitatu na nusu. Aina hii ya ufuasi haikuwa jambo lisilo la kawaida kwani marabi wa wakati huo mara nyingi walikuwa wanawaita wanafunzi kuwafuata. Wanafunzi hawa walikuwa na malengo matatu makuu:1

1. Kuwa pamoja na mwalimu wao
2. Kuwa kama mwalimu wao
3. Kufanya kama mwalimu wao alivyofanya

Ingawa hatuwezi kumwona Yesu kimwili leo, bado tunaweza kuwa wanafunzi wake, kwa makusudi kubaki katika uwepo wake kupitia sala na Neno lake. Kwa njia hii, tunajifunza kutoka kwake na kufuata mwongozo wake.

Inaanza kwa kumpokea Yeye kama Mwokozi wetu.

Hii inamaanisha tunatambua utambulisho wetu halisi—ya kwamba kila binadamu ni mtoto wa pekee na mpendwa wa Mungu. Na tunachagua kuishi kwa njia inayoonyesha utambulisho huu. Wakati huo huo, Roho Mtakatifu hutuongoza na kutubadilisha tabia yetu (Warumi 12:2). Hivyo mabadiliko haya ya ndani yanapelekea mabadiliko ya nje kiasili.

Misingi tunayofuata na mabadiliko yanayotokea katika tabia yetu sio kuhusu kupata wokovu. Yanatokana na tayari kuwa watoto na wanafunzi wake. Na kama vile wanafunzi wa karne ya kwanza, Tunataka:

1. Kuwa pamoja na Yesu
2. Kuwa kama Yesu
3. Kufanya kama Yesu alivyofanya

Mafundisho yetu yote, imani zetu zote, na kanuni zetu zote za maisha zinatokana na tamanio hili.

Misingi ya imani na kanuni, sio sheria

Kama tulivyosema, Uadventista wa Sabato hauna sheria. Tunayo misingi ya imani 28, mkusanyiko wa kauli zinazoeleza jinsi tunavyotafsiri na kutumia Maandiko. Kwa njia hii, zinasaidia kufafanua na kueleza Uadventista wa Siku ya Sabato badala ya kulazimisha tunachofanya.

Mtu anapojiunga na Kanisa la Waadventista wa Sabato, anakubaliana na mafundisho haya. Ahadi za ubatizo wa Mwadventista zinajumuisha kukubali imani katika mafundisho ya Kibiblia yafuatayo:2

Lakini mbali na mafundisho yetu, Biblia pia hutupatia “kanuni.”

Hizi ni kweli ambazo hubaki kuwa vile vile hata wakati muda, utamaduni, na hali zinapo badilika. Baadhi ya mifano inaweza kuwa kuwapenda jirani yetu (Luka 10:25-37), kutunza miili yetu kama mahekalu ya Roho Mtakatifu (1 Wakorintho 6:19-20), au kuonyesha unyenyekevu (Wafilipi 2:3-4).

Lakini, kinacho badilika ni jinsi kanuni hizi zinavyotekelezwa. Utekelezaji unaweza kuonekana tofauti kulingana na mtu, hali, na utamaduni. Hii inamaanisha kuna nafasi kwa ajili ya kujifunza Biblia na kufikia hitimisho binafsi. Mara nyingine, inamaanisha tofauti za imani (huku bado tukikubaliana juu ya mafundisho ya msingi).

Basi, hii inaonekanaje?

Hebu tuchukue mahusiano kama mfano.

Biblia inazungumzia sana kanuni za mahusiano yenye afya—upendo wa kujitolea, uaminifu, heshima, na uvumilivu, kwa kutoa mifano michache. Hizi zote ni za kudumu na hazina wakati—hakutakuja wakati ambapo hazitakuwa za kweli tena. Zinaendelea kuwa muhimu kwa mahusiano bila kujali hali au tamaduni.

Lakini jinsi zinavyotumika inaweza kutofautiana.

Kwa mfano, njia za uchumba katika nyakati za Agano la Kale zilikuwa tofauti sana na za leo (fikiria Ibrahimu kutuma mtumishi wake kumchagua mke kwa Isaka au Yakobo kulazimika kufanya kazi miaka saba kwa baba mkwe wake ili aweze kumuoa Raheli). Hata hivyo, kanuni ya heshima ilikuwa msingi wa hali hizi.

Leo, huenda usitumie njia kama hiyo.

Huenda usioe mtu ambaye hujawahi kukutana naye. Na ni vigumu kufikiria hali ambapo mtu yeyote angehitajika kufanya kazi miaka saba ili kuthibitisha kuwa wanastahili kuoa mtu fulani. Tunakaa katika wakati na utamaduni tofauti sana— lakini kanuni ya heshima bado inatumika. Unapokuwa katika uhusiano na mtu, unaweza kutafuta njia za kujenga uhusiano wa heshima na wazazi wake. Au unaweza kutafuta ushauri kutoka kwa wazazi wako au watu unaowaamini unapofikiria ndoa. Na zaidi ya yote, unahitaji kuheshimu mahitaji na shauku ya yule unayemchumbia.

Hii ni njia ya kutumia kanuni za Biblia kwa njia inayofaa kitamaduni.

Na Waadventista wanafanya vivyo hivyo wanapojifunza Biblia.

Kwa bahati mbaya, kwa sababu baadhi hawawezi kutofautisha kati ya kanuni na utekelezaji wa kanuni hizo, wanaweza kuwaelewa vibaya Waadventista wa Sabato, wakiona kanuni zetu za maisha kama “sheria.” Kwa hiyo, hebu tuangalie kwa karibu kanuni hizi na jinsi zinavyolingana na maisha yetu.

Kanuni za mtindo wa maisha ambazo Waadventista wanazishikilia

Mada zifuatazo ni kanuni katika Uadventista ambazo mara nyingi huchanganywa na “sheria.” Ifahamike kuwa, kanuni hizi hazihusu mambo ambayo Waadventista wanaweza au hawawezi kufanya. Badala yake, zinaakisi jinsi Waadventista wanavyochagua kuishi kwa kuzingatia Biblia—sio ili kuokolewa, bali kwa sababu tayari wana uhusiano wa upendo na Yesu.

Tunatambua kwamba Mungu alitoa kanuni hizi ili kutusaidia kuishi maisha yenye kuridhisha zaidi.

Twende kwa undani.

Chakula bora na mtindo wa maisha

A healthy meal consisting of toasts with different toppings including avocado, tomatoes, and bananas.

Photo by Ella Olsson on Unsplash

Tunachukulia miili yetu kama mahekalu ya Roho Mtakatifu, maana ndio njia ambayo Mungu hutumia kuongea na mioyo na akili zetu (1 Wakorintho 6:19-20). Kwa sababu hii, tunafuata kanuni ya kumtukuza Mungu katika kila tunachokula au kunywa—na katika jinsi tunavyojali afya zetu (1 Wakorintho 10:31).

Mungu alipompa Adamu na Hawa mlo wao Bustanini Edeni, aliwapa wingi wa matunda, karanga, na nafaka (Mwanzo 1:29). Kufuatia Gharika, hata hivyo, sehemu kubwa ya mimea iliondolewa, hivyo aliwaruhusu kula nyama (Mwanzo 9:3).

Wakati huo, Mungu alitaja kula nyama “safi”—kama njia ya kuwalinda watu wasile nyama zisizo na afya au nyama “chafu” kutoka kwa wanyama wanaokula nyama, kama vile nguruwe, wanaokula chini ya maji, au ndege wanaokula mizoga.

Alitoa mwongozo huu kwa undani zaidi katika Mambo ya Walawi 11.

Kwa sababu hiyo, Waadventista huchagua kuepuka nyama ya nguruwe, kamba, kaa, na nyama nyingine zilizoorodheshwa kama najisi—siyo kwa sababu ya “sheria” ya kibinadamu bali kwa sababu wanatamani kutunza miili yao.

Baadhi hata hujiepusha na kafeini au kuchagua lishe ya mboga au mimea pekee, ingawa hii itatofautiana kulingana na imani binafsi, hali, au upatikanaji wa chakula.

Kutokana na kanuni hizi za kutunza afya na kumtukuza Mungu, Waadventista pia hujiepusha na vinywaji vyenye kilevi na tumbaku kwa sababu tunatambua vinaweza kudhuru afya yetu na kuathiri wengine kwa njia mbaya.

Namna ya kutunza Sabato

Waadventista wanashika Sabato ya siku ya saba kwa sababu Mungu aliianzisha kama kumbukumbu ya Uumbaji na wokovu (Mwanzo 2:2-3; Kumbukumbu la Torati 5:12-15) na kutuagiza kuishika katika Amri Kumi (Kutoka 20:8-11). Tunachagua kutii amri hii kwa upendo kwake na kutambua kwamba kufanya hivyo kutatusaidia kufanikiwa.

Katika ulimwengu wenye harakati ambapo thamani yetu mara nyingi hutokana na kile tunachofanya, Mungu alitupa siku hii ya mapumziko kama baraka (Marko 2:28). Inahusu kile Mungu amefanya kwetu, sio kile tunachofanya sisi. Na inatupa fursa ya kuunganisha na Mungu na kuwabariki wengine.

Kanuni za utunzaji wa Sabato ni pamoja na kupumzika kutoka kazi (Kutoka 20:8-11), kutenda mema kwa wengine (Mathayo 12:12), na kufurahia Mungu na kile alichotupatia (Isaya 58:13-14).

Haihusu orodha ya sheria, au kufanya na kutofanya mambo fulani.

Kweli, Waadventista wengi hawataki kwenda kununua, kula nje au kuhudhuria michezo siku ya saba ya wiki. Lakini haya sio “sheria” zinazotakiwa kufuata. Badala yake, tunafanya maamuzi haya tukiwa na lengo letu kuu akilini: kuacha kando shughuli za kila siku ili tujikite kwa makusudi katika kile Mungu ametufanyia, kutumia muda pamoja naye, na kuungana na wapendwa wetu.

Kudumisha heshima

A girl reading a devotional and praying

Photo by Ben White on Unsplash

Mavazi na uchaguzi wa mapambo unatofautiana kati ya Mwadventista na Mwadventista. Hii ni kwa sababu kila mshiriki wa kanisa anaweza kuwa na imani tofauti kidogo kulingana na namna anavyojifunza Biblia, utamaduni, historia, na uzoefu au uzoefu uliopita.

Lakini kanuni kuu ni staha ama heshima – unyenyekevu na utiifu kwa sisi wenyewe na wengine katika kila eneo la maisha yetu.

Msingi wetu wa imani kuhusu tabia ya Kikristo inasema yafuatayo kuhusu kanuni hii:

“Kwa kutambua tofauti za kitamaduni, mavazi yetu yanapaswa kuwa rahisi, yenye unyenyekevu, na safi, yanayostahili wale ambao uzuri wao wa kweli hauko katika mapambo ya nje bali katika mapambo yasiyoharibika ya roho ya upole na utulivu.”3

“Inahusiana na 1 Petro 3:3-4:

“Kujipamba kwenu, kusiwe kujipamba kwa nje, yaani, kusuka nywele, na kujitia dhahabu na kuvalia mavazi; bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika; yaani, roho ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu” (NKJV).

Mungu huangalia moyo (1 Samweli 16:7). Kwa hivyo, linapokuja swala la mavazi, kila mtu lazima ajichunguze moyo wake mwenyewe. Mwishowe, tunatafuta kuvaa na kutenda kwa njia itakayodhihirisha uwakili bora, unyenyekevu, kuridhika, na heshima kwa Mungu (Luka 12:15; 1 Wakorintho 10:31; 1 Timotheo 6:7-8).

Uaminifu katika mahusiano ya dhati

Mungu ni Mungu wa mahusiano anayeakisi kujitoa na uadilifu anayetamani tuudhihirishe katika mahusiano yetu. Kwa sababu hii, Waadventista wanachukulia mahusiano, hasa ndoa, kuwa ni matakatifu na mazuri. Ndoa inakusudiwa kuakisi upendo mzuri wa kujitoa mhanga ambao Kristo anao kwa watu wake (Waefeso 5:25-26).

Sasa, huenda umesikia kwamba Waadventista kwa kawaida hawaoi wasio Waadventista au kwamba wameshauriwa dhidi ya kufanya hivyo.

Ni kweli kwamba Waadventista kwa kawaida hutafuta kuolewa na Waadventista wengine-lakini sio kwa sababu ya “kanuni” ya madhehebu yetu. Badala yake, ni kutokana na shauku ya kweli ya kuunganisha maisha yetu na mtu ambaye ana imani na maadili sawa na sisi, na ambaye anakubaliana nasi kumweka Mungu kwanza (2 Wakorintho 6:14).

Kanuni ya Kanisa la Waadventista Wa Sabato inasisitiza hili:

“Ndoa zina uwezekano mkubwa zaidi wa kudumu, na maisha ya familia kutimiza mpango wa kimungu, ikiwa mume na mke wako pamoja na wameungana na kufungwa pamoja na maadili ya kiroho na mitindo ya maisha. Kwa sababu hizi, Kanisa linakataza ndoa kati ya Mwadventista wa Sabato na mshiriki wa dini nyingine na linawahimiza wachungaji wake kutofunga ndoa kama hizo.”4

Tambua ufafanuzi muhimu huu, hata hivyo:

“Kanisa linatambua kwamba ni haki ya kila mshiriki kufanya uamuzi wa mwisho kuhusiana na uchaguzi wa mwenzi wa ndoa.”5

Kwa ufupi, kila Mwadventista anafanya uamuzi wao wenyewe kuhusu nani wa kuoa au kuolewa—kulingana na imani yao binafsi inayotokana na kanuni za Biblia.

Tabia ya Kiungu na burudani

A hand pointing a T.V. remote at a T.V. screen to pull up the latest Netflix shows.

Photo by freestocks on Unsplash

Vipi kuhusu kuchagua sinema, muziki, shughuli, burudani, au watu tunaohusiana nao au sehemu tunazotembelea?

Tena, Waadventista hawana sheria zinazo sema tunaweza au hatuwezi kufanya nini katika muda wetu wa ziada. Lakini hapa kuna kanuni za msingi tunazozingatia tunapofanya maamuzi.

Tunatambua kwamba Biblia inatuita kumweka Yesu kipaumbele katika maisha yetu, tukitafuta ufalme Wake kuliko vitu vyote. Chaguo letu la burudani mara nyingi linajenga msingi huu (Mathayo 6:21, 33). Kwa hivyo, swali kubwa tunauliza tunapofikiria shughuli za kufanya ni hili:

Je, naweza kumtukuza Mungu kupitia shughuli hii (1 Wakorintho 10:31)?

Wafilipi 4:8 pia hutoa vigezo rahisi vya kutathmini burudani. Aya hii inatuhimiza kutafakari mambo ambayo ni ya kweli, yenye heshima, ya haki, safi, yenye kupendeza, yenye sifa njema, ya maadili bora, na yenye sifa njema.

Wakati huo huo, Waadventista wanatambua kwamba “furaha” ni neno binafsi, hivyo hata wakati wanazingatia mwongozo wa Wafilipi 4:8, shughuli na chaguo la burudani litatofautiana kiasili kutoka kwa mtu hadi mtu, au hata kutoka kwa jamii moja hadi nyingine.

Lakini tunajua kwa hakika kwamba furaha ni tunda la Roho Mtakatifu (Wagalatia 5:22-23), na Yesu anataka hili liwe sehemu ya maisha yetu (Yohana 15:11). Alipokuwa duniani, alipata muda wa ushirika na furaha kwa kwenda kwenye mikusanyiko ya kijamii na harusi (Yohana 2:1-11) na kuzungumza na wale waliokuwa karibu naye (Yohana 21:9-14).

Ingawa Waadventista wanaweza wasishiriki katika shughuli zote ambazo jamii inachukulia kuwa “furaha,” tunapata njia nyingi za kuleta furaha inayomheshimu Mungu na kicheko katika maisha yetu.

Kujifunza kutoka katika ushauri wa Ellen White

A black and white photograph of Ellen G. White sitting at a desk writing a manuscript.

Waadventista wengi husoma na kuyatekeleza mashauri kutoka maandishi ya Ellen G. White, mmoja wa waanzilishi wa Uadventista aliyeishi katika karne ya 19. Tunaamini kwamba alikuwa na karama ya unabii, karama ya Roho iliyotajwa katika Agano Jipya (1 Wakorintho 12:4-11).

Pia anakidhi vigezo vya manabii tunavyopata katika Biblia, kama vile uaminifu kwa Biblia, kumtukuza Yesu, na kuakisi tabia ya Kristo.

Mtume Paulo hutukumbusha kwamba manabii wangekuwepo duniani hadi mwisho wa nyakati, “kuujenga mwili wa Kristo” na kusaidia kuwaongoza watu mbali na udanganyifu (Waefeso 4:11-16). Kanuni hii inawaongoza Waadventista kuzingatia kwa uangalifu mashauri katika maandishi ya Ellen White kwa sababu tunaamini alikuwa na karama ya unabii kama ilivyoandikwa katika Biblia.

Ni bayana, kwamba, Waadventista hawaweki maandishi yake juu ya Biblia. Badala yake, tunatumia Biblia kama mfumo na kipimo kwa kila kitu tunachojifunza nje ya Maandiko. Na kwa kufanya hivyo, tunagundua kwamba mambo mengi aliyoyaandika yanaweza kuwa na manufaa sana katika kutuonyesha jinsi ya kutumia kanuni za Biblia katika maisha yetu ya kila siku na katika mwingiliano wetu na wengine.

Ellen White mwenyewe alikuwa makini katika kutofautisha maneno yake na Neno la Mungu. Tangu alipoona kwamba katika siku zake, “Biblia haikuzingatiwa sana,” hivyo alitumika katika jukumu la “mwanga mdogo kuwaongoza wanaume na wanawake kwenye mwanga mkubwa,” au Biblia yenyewe.6

Na kuhusu utunzaji wa afya ya mtu binafsi, mwishowe aliwahimiza watu kutafuta Mungu kwa hekima juu ya jinsi ya kujitunza:

“Nataka uwe unasimama katika hadhi yako binafsi na katika kutakaswa kwako binafsi mbele za Mungu, mwili wako wote ukiwa umetolewa kwake.”7

Hakutaka mtu yeyote kutegemea ushauri wake, bali mwongozo wa Roho Mtakatifu katika maisha yao kila mmoja.

Uadventista wa Sabato unahusu kutafuta kumfuata Yesu

Waadventista wa Sabato wanathamini uhuru wa kuchagua uliotolewa na Mungu. Ndani ya kanuni za Kibiblia, mara nyingine tunaweza kufanya maamuzi tofauti linapokuja swala la afya, mavazi, burudani, na kadhalika.

Na hiyo ni sawa!

Tunatofautiana, na tunatumia kanuni tofauti kulingana na mazingira, wakati, na mahali. Hakuna mtu katika Kanisa la Waadventista anapaswa kuhisi kwamba ni jukumu lao kulazimisha wengine kutumia kanuni fulani kwa namna fulani. Roho Mtakatifu hufanya kazi na kila mmoja wetu kwa njia tofauti, na mtume Paulo kutuhimiza tuchukue hatua kulingana na dhamiri yetu halisi (Warumi 14:5), na pia kuheshimu imani za wengine (Warumi 8:4-13).

Zaidi ya yote, tunatamani kuweka mkazo kwenye mambo muhimu yanayotuunganisha—misingi ya imani kutoka katika Neno la Mungu na shauku ya kuwa kama Kristo na kushiriki upendo wake. Kwa hivyo ni muhimu siku zote kuzingatia, kama wafuasi wa Yesu, jinsi maamuzi yetu ya mtindo wa maisha yanavyotuathiri sisi wenyewe na wengine.

Ikiwa unatafuta kuelewa vizuri maana ya kumfuata Yesu,

Kurasa zinazohusiana

  1. Comer, John Mark, Practicing the Way (Waterbrook, 2024), p. 9. []
  2. Seventh-day Adventist Church Manual, 20th ed., p. 51-52. []
  3. “What Adventists Believe About Christian Behavior,” Seventh-day Adventist Church. []
  4. Seventh-day Adventist Church Manual, p. 160. []
  5. Ibid. []
  6. White, Ellen G., The Review and Herald (January 20, 1903), par. 9. []
  7. White, Ellen G., Manuscript Releases, vol. 13 (Ellen G. White Estate, Silver Spring, MD, 1990), p. 202. []

Je, Una swali kuhusu Waadventista? Uliza hapa!

Pata majibu kwa maswali yako kuhusu Waadventista Wasabato

Majibu Zaidi