Waadventista Wasabato Wanatafsiri Vipi Unabii wa Biblia?

Unabii wa Biblia unazua hisia tofauti kwa watu. Kwa baadhi, unaweza kuonekana kuwa wa kusisimua au wa kuvutia.

Kwa wengine, unaweza kuonekana kuwa wa kuchanganya, wa kuelemea.

Lakini ikiwa aya 8,352 katika Biblia ni unabii1—takribani 26% ya aya zake zote—je, hatupaswi kujaribu kuelewa baadhi yake? Ufunuo 1:3 hata unatangaza baraka kwa wale wanaosoma maneno ya unabii huo.

Ndiyo maana Waadventista Wa Sabato, tangu siku zao za mwanzo, wametumia muda mwingi kusoma na kushiriki kuhusu unabii. Hasa wale katika vitabu vya Danieli na Ufunuo.

Na kama vile tunavyoangazia Biblia ili kupata mafundisho yetu, tunataka ituongoze kuelewa unabii wake. Hii inamaanisha kuruhusu ituonyeshe jinsi ya kujitafsiri yenyewe.2
Yaani, watu wa wakati huo walielewa vipi unabii walioupokea? Na jinsi gani hilo linaweza kutusaidia leo?

Ili kuona jinsi hilo linavyoonekana katika vitendo, tutajibu yafuatayo:

Kanisa la Waadventista wa Sabato linatumia mfumo gani kutafsiri unabii?

Tunachambua Biblia kupitia mfumo wa kihistoria na kibiblia, au mfumo wa kihistoria. Mfumo huu unauona unabii ukianza wakati wa manabii walioupokea na kutimia kupitia historia hadi mwisho wa wakati.

Mfumo huu ni tofauti na preterism, ambao unaamini kwamba unabii wa Biblia tayari umetokea zamani na kuandikwa tu na waandishi. Au futurism, ambao unachambua zaidi unabii kama mambo yatakayofanyika baadaye sana katika siku za usoni.

Namna nyingine ambayo mfumo wa kihistoria unatofautiana na njia hizi mbili ni katika kutegemea Maandiko.

Richard Davidson, profesa wa tafsiri ya Agano la Kale, anasisitiza kwamba njia ya kihistoria na kibiblia ni “jaribio la kuelewa maana ya taarifa zinazotolewa na Biblia… kutoka katika Maandiko pekee.”3

Kwa maneno mengine, sisi…4

  • Tunaitazama Biblia kama Neno la Mungu na mamlaka na kipimo cha ukweli wote.
  • Tunatambua upatanifu uliopo katika Maandiko. Aya katika sehemu moja ya Biblia inaweza kutusaidia kuelewa aya katika sehemu nyingine.
  • Tunaona Biblia ikitumika katika nyakati na tamaduni zote.

Mtindo wa Kihistoria pia unahusu tunachokiona katika Maandiko yenyewe. Wakati malaika walipoonekana kwa manabii na kufafanua unabii kwao, walitumia njia hii.5

Kwa mfano, nabii Danieli aliona maono ya kondoo na mbuzi. Wakati malaika Gabrieli alipokuja kufafanua maono hayo kwake, alimwambia,

“Yule kondoo mume uliyemwona, mwenye pembe mbili, hizo ndizo wafalme wa Umedi na Uajemi. Na yule beberu, mwenye manyoya mengi, ni mfalme wa Uyunani; “ (Danieli 8:20-21, NKJV).

Danieli alikuwa Myahudi aliyeishi wakati wa uhamisho wa Waisraeli huko Babeli. Lakini hivi karibuni, Babeli ingeshindwa na Waamedi na Waajemi (Danieli 8:1; 5:30-31), hivyo unabii huu ulianza wakati wake na kuendelea kutoka hapo.

Unabii katika Danieli 2 ni mfano mwingine wa mtindo wa kihistoria.

Mfalme wa Babeli Nebukadreza alipokea maono ya sanamu yenye kichwa cha dhahabu, kifua na mikono ya fedha, kiuno cha shaba, miguu ya chuma, na nyayo zilizochanganyika chuma na udongo. Kisha jiwe dogo likaonekana, likaivunja sanamu nzima vipande vipande, na kukua kuwa mlima (Danieli 2:31-35).

Mungu Mwenyewe alimpa Danieli tafsiri katika Danieli 2:36-45. Kichwa cha dhahabu kilikuwa kinawakilisha Babeli, na kila sehemu ya sanamu baada ya hiyo iliwakilisha falme za dunia zilizofuata: Umedi-Uajemi, Ugiriki, na Rumi. Nyayo za chuma na udongo ziliwakilisha mataifa yaliyogawanyika ya Ulaya, na jiwe lilikuwa linawakilisha ufalme wa Mungu.

Hivyo, unabii huu unatoa historia nzima kutoka wakati wa Danieli hadi mwisho wa dunia.

Na hatukulazimika kutafsiri chochote sisi wenyewe kwa sababu Biblia ilituambia tafsiri yake. Inaashiria jinsi tunavyopaswa kuelewa unabii mwingine wa Biblia pia.

Ni kanuni zipi zinazo-ongoza Kanisa la Waadventista wa Sabato katika kutafsiri unabii?

Kama tulivyo-onyesha hapo juu, Waadventista wa Sabato wanaamini kwamba Neno la Mungu ndio mwongozo wetu katika kutafsiri unabii. Imani hii imetuongoza kwenye kanuni nyingi:

  • Hitaji la Roho Mtakatifu
  • Kristo kama mada kuu na ya msingi
  • Biblia kama mtafsiri wake mwenyewe
  • Aina mbili za unabii
  • Maana ya moja kwa moja kwanza
  • Umuhimu wa muktadha
  • Mifano ya Agano la Kale katika Ufunuo
  • Kanuni ya siku kwa mwaka
  • Kurudia na kukuza
  • Jukumu la nyenzo nyingine nje ya Biblia

Kanuni nyingi hizi zinatumika kila tunapojifunza Biblia, lakini tutachunguza kwa undani jinsi zinavyohusiana na tafsiri ya unabii.

Bila shaka, kumbuka kwamba hata pamoja na kanuni na mwongozo huu, Waadventista mara nyingine wanaweza kuwa na maoni tofauti kuhusu unabii fulani.

Na hilo ni sawa.

Baada ya yote, sisi ni kundi la watu —na hilo linamaanisha umoja badala ya mfanano. Tunakubaliana kuhusu sehemu muhimu za imani yetu na mafundisho lakini pia tunaruhusu nafasi kwa mitazamo tofauti linapokuja swala la maelezo.

Hitaji la Roho Mtakatifu

Unabii haikuwa matokeo ya mawazo ya kibinadamu ya kufikirika. Manabii walipokea ujumbe huu kupitia Roho Mtakatifu na kuandika kwa faida yetu (2 Petro 1:21).

Hii inamaanisha Roho Mtakatifu pia anaweza kutusaidia kuelewa ujumbe huu. Hasa unapoonekana kuwa ni wenye kuleta mkanganyiko.

Katika 1 Wakorintho 2:12, mtume Paulo aliandika:

“Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu” (NKJV).

Tunahitaji utambuzi huu wa kiroho ili kuelewa kile Mungu anachojaribu kutuambia (1 Wakorintho 2:14).

Waadventista wanaamini kwamba, kwa sababu hii, maombi yanapaswa kuanzisha kila utafiti wa Biblia. Kwa njia hii, tunaweza kupokea ahadi ya Roho Mtakatifu kutuongoza “katika kweli yote” (Yohana 16:13, NKJV).

Kristo kama mada kuu na ya msingi

Yesu aliwaambia viongozi wa kidini wa wakati wake kwamba Maandiko (Agano la Kale wakati huo) “hayo ndiyo yanayonishuhudia” (Yohana 5:39, NKJV).

Na Waadventista wanajifunza unabii kutoka mtazamo huu – kwamba kila sehemu ya Neno la Mungu linamzungumzia Yesu.

Ufunuo wenyewe unaanza na kauli hii:

“Ufunuo wa Yesu Kristo” (Ufunuo 1:1, NKJV).

Ufunuo unamfunua Yeye, na ni ujumbe ambao Yesu anao kwa ajili yetu, wafuasi wake.

Mwana-kondoo – ishara ya Yesu (Yohana 1:29) – inatajwa mara 27 katika Ufunuo. Ujumbe mkuu ni kwamba Yeye ni mshindi (Ufunuo 5:12; 12:11; 17:14).

Tunatambua kwamba tafsiri zote za kibiblia za unabii zitamweka Yesu kuwa kiini.

Biblia kama mtafsiri wake mwenyewe

Kanuni hii inatambua kwamba Maandiko yenyewe yanaweza kutusaidia kuelewa maana yake. Kwa sababu ya upatanifu kati ya vitabu vya Biblia, tunaweza kulinganisha aya za Maandiko ndani ya muktadha na kuona kile Biblia nzima inachosema kuhusu mada fulani.

Kanuni hii inaelezwa kwa mtindo wa kishairi katika Isaya 28:9-10; 13:

“Atamfundisha nani maarifa? Atamfahamisha nani habari hii?… Kwa maana ni amri juu ya amri, amri juu ya amri, kanuni juu ya kanuni, kanuni juu ya kanuni, huku kidogo na huku kidogo” (NKJV).

Yesu Mwenyewe alieleza Maandiko kwa njia hii.
Alipoonekana kwa wanafunzi wawili kwenye Barabara ya Emau, aliwaeleza unabii kuhusu yeye mwenyewe katika Agano la Kale:

“Akaanza kutoka Musa na Manabii wote, akawaeleza katika maandiko yote mambo yanayomhusu yeye mwenyewe” (Luka 24:27, NKJV).

Ili ieleweke, hata hivyo, kanuni hii haimaanishi Biblia inatuambia kila kitu kwa mtazamo wa juu na hivyo hatuhitaji kujitahidi kujifunza sisi wenyewe. Na haimaanishi tunaweza kutumia aya mmoja tu, bila muktadha, kwa urahisi kuthibitisha hoja zetu. Lakini kama Profesa Davidson anavyosema,

“Kwa kuwa Maandiko mwishowe yana Mwandishi mmoja wa kimungu, ni muhimu kukusanya yote yaliyoandikwa kuhusu mada fulani ili uweze kuzingatia aya zote za mada hiyo.”6

Mfano rahisi wa hili ni maono ya Danieli ya wanyama wanne wakubwa katika Danieli 7. Ukisoma maono hayo, unaweza kujiuliza hawa wanyama wanawakilisha nini. Lakini ukienda kidogo zaidi, tunapata tafsiri katika sura hiyo hiyo: “Wanyama hao wakubwa walio wanne ni wafalme watakaotokea duniani” (Danieli 7:17, 23, NKJV).

Kisha, wakati Ufunuo unapotumia alama hiyo hiyo ya wanyama, tunaweza kuhitimisha kwamba pia inazungumzia kuhusu wafalme au falme (Ufunuo 13).

Aina mbili za unabii

Manabii wa Biblia wanagawanyika katika makundi mawili makuu:

1. Jumla
2. Wa mambo yajayo

Unabii wa jumla unahusiana na watu wa Mungu, hasa taifa la Israeli. Kawaida hauna vielelezo. Unahusika na “matukio ya eneo husika, mataifa, na hali,”7 lakini pia unaruka kutoka “mgogoro wa eneo fulani hadi siku ya mwisho ya Bwana.”8

Unabii katika Isaya, Yeremia, na ule wa manabii wadogo wanangukia katika kundi hili. Ulikuwa hasa kuhusu watu wa Israeli na mji wao, Yerusalemu. Lakini pia ulikuwa na matumizi ya pili kuhusiana na matukio yanayohusiana na Kurudi kwa Pili kwa Yesu, hukumu, milenia (kipindi cha miaka 1,000 baada ya Yesu kurudi), na dunia mpya.

Mathayo 24, na dalili za kurudi kwake mara ya pili, pia ni unabii wa jumla.

Kutoka kwa neno la Kigiriki lenye maana ya “kufunua” au “ufunuo.”9 Unabii huu, tofauti na unabii mwingine, huwa na matumizi ya ulimwengu mzima na mara nyingi ni wa mafumbo.

Gerhard Pfandl, hapo awali mkurugenzi msaidizi wa Taasisi ya Utafiti wa Kibiblia, anataja sifa za aina hizi za unabii. Anajumuisha yafuatayo:10

  • Unabii huu mara nyingi huja katika maono na ufunuo.
  • Kwa kawaida ni ya mafumbo.
  • Hujikita kwenye Pambano kuu, vita kati ya Mungu na Shetani, mema na mabaya (Ufunuo 12-14).
  • Zinahusiana na kuja kwa Yesu, hukumu, na ufufuo katika siku za mwisho.
  • Mara nyingi hufafanuliwa na kuelezewa na malaika.

Maana halisi kwanza

Baadhi ya unabii umejaa mfumbo ambayo hayawezi kuwa ya moja kwa moja -majoka, wanyama, mwanamke amevikwa jua, na vitasa vya ghadhabu, kwa kuyataja machache. Lakini sio unabii wote ni wa mafumbo, hivyo tunapaswa kuweza kutofautisha kilichomaanishwa kwa uhalisia na kilichomaanishwa kwa mfano.

Moja ya kanuni ni kwenda na maana ya kwanza inayomaanishwa, maana halisi. Davidson anaeleza:

“Mfano thabiti wa waandishi wa Biblia ni kwamba Maandiko yanapaswa kuchukuliwa kwa maana yake ya wazi, inayomaanishwa, isipokuwa ikiwa inaonekana wazi na dhahiri kwamba fumbo linamaanishwa.”11

Kanuni hii inatuzuia kutoa maana za mafumbo kwa hadithi yoyote tu ya Biblia.

Davidson anatoa mfano wa wanafunzi wa Yesu, ambao walitambua tofauti kati ya lugha ya uhalisia na ya mafumbo wakati Yesu alipowaambia. Walikuwa wanaweza kutofautisha kati ya mifano na mafumbo, na mafundisho ya moja kwa moja (Yohana 16:25-29).

Umuhimu wa muktadha

Muktadha ni muhimu katika kuelewa aya yoyote katika Biblia. Aina zote zifuatazo za muktadha zinapaswa kuzingatiwa:

  • Muktadha wa Kimaandiko—muktadha wa aya zinazozunguka, sura, vitabu, maandishi mengine ya mwandishi huyo, na mafundisho ya Biblia kwa ujumla
  • Muktadha wa Lugha—maana ya maneno katika lugha zake za awali
  • Muktadha wa Kitamaduni
  • Muktadha wa Kihistoria/Akiolojia

Waadventista wanachukua vipengele hivi kwa uzito hasa wanapotafsiri mafumbo. Inaweza kuwa rahisi kutafsiri unabii kulingana na mfumo wa kisasa, lakini tunapaswa kukumbuka kutazama muktadha halisi wa Biblia.

Mfano mmoja ni maono ya Danieli ya simba mwenye mabawa ya tai (Danieli 7:4).

Muktadha wa Maandiko hutusaidia kuelewa kwamba mnyama huyo ni mwakilishi wa ufalme (Danieli 7:17, 23).

Lakini, baadhi wamefikiria kuwa ni ishara ya Marekani—kwa kuwa tai ni ishara ya nchi hii leo.

Hata hivyo, hii inapuuza muktadha wa kitamaduni na kihistoria wa aya hiyo, ikiwa ni pamoja na ukweli kwamba Marekani haikuwepo wakati huo.

Tukichunguza wakati wa Danieli zaidi, tunagundua kwamba simba na mabawa ya tai yalitumiwa kawaida kurejelea Babeli (Yeremia 4:7, 13; Habakuki 1:6). Zaidi ya hayo, “wachimbuaji wa vitu vya kale wamegundua idadi kubwa ya sanamu za simba wenye mabawa miongoni mwa vifusi vya Babeli ya kale.”12

Vielelezo vya Agano la Kale katika Ufunuo

A page from the book of Revelation written by the apostle John

Matukio na watu halisi katika Agano la Kale mara nyingi huwa na matumizi ya kiroho, Kiulimwengu katika Agano Jipya au wakati wa mwisho.

Kwa mfano, Agano la Kale linazungumzia sana kuhusu taifa halisi la Israeli, huku Agano Jipya likizungumzia Wakristo wote kama watu maalum wa Mungu (1 Petro 2:9). Au, katika Agano la Kale, watu wa Mungu walikwenda utumwani kwa kweli Babeli (Danieli 1), huku Ufunuo ikizungumzia watu wa Mungu wakiwa utumwa wa kiroho wa Babeli (Ufunuo 14:8).

Kielelezo kingine kikubwa kutoka katika Agano la Kale ni patakatifu, ambapo palikuwa ni mfano wa mpango wa wokovu.

Lugha ya patakatifu hutumiwa kote katika Ufunuo kutusaidia kuelewa kwamba patakatifu halisi ni chumba cha enzi cha Mungu mbinguni. Tunakuta:

  • Vinara saba vya dhahabu (Ufunuo 1:12; 2:1)
  • Chetezo cha uvumba na madhabahu ya uvumba (Ufunuo 5:8; 8:3-5)
  • Sanduku la agano (Ufunuo 11:19)
  • Mwana-Kondoo aliyechinjwa (Ufunuo 5:6, 12; 12:11)

Kanuni ya Siku kwa Mwaka

Katika unabii wa ufunuo, vipindi vya muda pia ni fumbo na vinaweza kueleweka kwa kanuni ya siku-kwa-mwaka: siku moja ya unabii = mwaka mmoja halisi.13

Biblia yenyewe inatoa mifano mingi kuhusu hili.

Katika Ezekieli 4:5-6, Mungu alimwambia Ezekieli aigize mfano wa unabii ambapo kila siku ya mfano iliwakilisha mwaka mmoja:

“Maana nimekuagizia miaka ya uovu wao iwe kwako hesabu ya siku, yaani, siku mia tatu na tisini, ndivyo utakavyouchukua uovu wa nyumba ya Israeli. Tena utakapozitimiza hizo, utalala kwa ubavu wako wa kuume, nawe utauchukua uovu wa nyumba ya Yuda; siku arobaini, siku moja kwa mwaka mmoja, nimekuagiza.” (NKJV)

Hesabu 14:34 pia inazungumzia jinsi siku 40 zilivyo wakilisha miaka 40 Waisraeli wangekuwa jangwani.

Kihistoria, wasomi Wayahudi, wachambuzi wa Biblia, na wanamatengenezo wa Kiprotestanti wameitumia kanuni hii kuelewa unabii unaohusisha vipindi vya wakati.14

Na ina mantiki kwa sababu unabii mwingi katika Danieli na Ufunuo ni kwa ajili ya siku za mwisho (Danieli 8:17). Kama idadi ya siku ingekuwa halisi, badala ya kuwakilisha miaka, unabii huo ungeisha muda mrefu kabla ya siku za mwisho.15

Kwa hivyo, tunajuaje wakati namba zinapokuwa za mafumbo?

Kwanza, zitakuwa katika muktadha wa mafumbo mengine, na, pili, zitakuwa katika maono ya unabii au kifungu cha Biblia badala ya kile kinachoelezea tu tukio la kihistoria. Tatu, kawaida hutajwa kama masaa, siku, wiki, miezi, au mwaka badala ya vipindi virefu.16

Kuongeza na kurudia

Unabii wa Biblia mara nyingi hurudia dhana, ikiongeza maelezo zaidi kila wakati.

Unabii wa Danieli ni mfano mzuri wa hili.

Danieli 2 hutoa muhtasari wa falme za ulimwengu kutoka wakati wa Babeli hadi mwisho wa dunia.

Danieli 7 na 8 zote zinafuata mfuatano huu lakini zinaongeza habari kuhusu falme fulani na hukumu mbinguni.

Danieli 11 inajumuisha maelezo maalum sana kuhusu mataifa yaliyotajwa katika nabii tatu za kwanza.

Ufunuo pia inafuata kanuni hii. Inataja makanisa saba, kisha mihuri saba, kisha tarumbeta saba, na kisha mfuatano wa kihistoria katika Ufunuo 12-14—yote ambayo yanatabiri matukio kutoka wakati wa Yohana wa Ufunuo hadi siku za mwisho na Ujio wa Pili wa Kristo.17

Nafasi ya nyenzo nyingine nje ya Biblia

Waadventista hawapingi kutumia nyenzo nyingine kusaidia katika kujifunza unabii wa Biblia—tangu kwenye kamusi za Biblia hadi vitabu vya marejeo na maelezo. Hata hivyo, sisi daima hujaribu kile tunachokipata katika Biblia ili kuhakikisha kuwa ni thabiti katika mafundisho yake kwa ujumla.

Tunaamini kwamba Ellen G. White, kiongozi wa awali katika Kanisa la Waadventista, alikuwa na Karama ya unabii (au roho ya unabii) na alipokea ujumbe kutoka kwa Mungu. Lakini hii haimaanishi kwamba tunamfuata yeye kuliko Biblia.

Badala yake, tunakubali maandishi yake kwa sababu, kupitia kujifunza, tumebaini kuwa yanalingana na Biblia na husaidia kuthibitisha kile inachosema.

Na tena, Biblia ndiyo mamlaka ya mwisho kwa kila tunachohitimisha.

Kwa nini tunatafsiri unabii kwa namna hii?

Close-up of the definition for prophecy in dictionary. This illustrates how people have tried to make sense of what prophecy is and how to interpret it.

Photo by Mick Haupt on Unsplash

Mfumo wa kihistoria umekuwepo kwa muda mrefu. Kama tulivyoona, ulikuwa mfumo “mkuu” wa kutafsiri unabii wa Biblia nyakati za Danieli na Yesu.18

Pfandl pia anabainisha kwamba ulitumiwa na mababa wa kanisa wa karne za awali MK na katika kipindi cha Kati.19 Na waanzilishi wa matengenezo ya Kiprotestanti pia walikuwa wafuasi wa mfumo wa kihistoria.20

Ni hadi karne ya 16 ndipo mifumo mingine mikuu, kama futurism na preterism, ilipoanza kujitokeza katika Kanisa la Kikristo. Na hata wakati huo, mfumo wa kihistoria kilikuwa mfumo wa kawaida zaidi hadi karne ya 19.21

Mfumo wa Kihistoria pia umekuwa msingi wa Kanisa la Waadventista wa Sabato tangu mwanzo.

Baada ya yote, sisi ni vuguvugu lililojengwa katika kujifunza unabii.

Katika miaka ya awali ya 1800, William Miller alijifunza kwa bidii unabii wa Biblia, hasa unabii wa siku 2,300. Utafiti wake ulimfanya aamini kwamba kipindi hiki cha muda kingeishia mwaka wa 1844. Ugunduzi huu ulichochea vuguvugu la wafuasi wa Miller, ambalo lilifundisha kwamba Yesu angekuja mwaka huo.

Ingawa William Miller alikosea kuhusu tukio lililotokea mwaka wa 1844, utafiti wake kuhusu wakati wa unabii ulikuwa sahihi.

Waadventista waliendelea kutumia kanuni zake za tafsiri walipojifunza Biblia. Walitambua kwamba Miller alikuwa amekosea kuweka tarehe ya kuja kwa Yesu (Mathayo 24:36), lakini walipata ufahamu mwingi muhimu kutoka katika utafiti wake.

Waadventista wanapata tumaini kupitia kujifunza unabii

Unabii wa Biblia umekuwa sehemu muhimu ya uzoefu wa Mwadventista tangu mwanzo. Umetusaidia kuanzisha imani zetu nyingi za msingi na kupata mada kuu za Neno la Mungu. Pia umetupa ujasiri kuhusu nyakati za mwisho.

Lakini zaidi ya chochote kingine, kujifunza unabii kumetujenga imani yetu kwa Mungu. Tunauona jinsi unabii ambao tayari umetimia. Na hilo hututia moyo kwamba hata ule unaokuja utatimia pia.

Katika ulimwengu wa kutokuwa na uhakika, mkanganyiko, na maumivu mengi, unabii unatupa sababu ya kuwa na matumaini.

Kurasa zinazohusiana

  1. Jackson, Wayne, “How Many Prophecies Are in the Bible?” Christian Courier. []
  2. Davidson, Richard, “Interpreting Scripture According to the Scriptures,” Biblical Research Institute, p. 1.  []
  3. Ibid, p. 10.  []
  4. Ibid. []
  5. Pfandl, Gerhard, “Understanding Biblical Apocalyptic,” Biblical Hermeneutics: An Adventist Approach, p. 275. []
  6. Davidson, p. 6. []
  7. Pfandl, p. 267.[]
  8. Methods of Bible Study,” Seventh-day Adventist Church. []
  9. Pfandl, p. 269. []
  10. Ibid. []
  11. Davidson, p. 7. []
  12. Anderson, Roy Allen, Unfolding Daniel’s Prophecies, p. 89. []
  13. Pfandl, Gerhard, “In Defense of the Year-Day Principle,” Journal of the Adventist Theological Society, pp. 3-17. []
  14. Ibid. []
  15. Goldstein, Clifford, “The Day-Year Principle,” Ministry. []
  16. “20 Reasons to Apply the Year/Day Principle,” Secrets Unsealed. []
  17. Pfandl, p. 283.[]
  18. Ibid. []
  19. Ibid. []
  20. Shea, William, “Making Sense of Bible Prophecy,” Adventist Review. []
  21. Pfandl, p. 274-275.[]

Je, Una swali kuhusu Waadventista? Uliza hapa!

Pata majibu kwa maswali yako kuhusu Waadventista Wasabato

Majibu Zaidi

Muhtasari wa Elimu ya Juu ya WaAdventista wa Sabato

Muhtasari wa Elimu ya Juu ya WaAdventista wa Sabato

Muhtasari wa Elimu ya Juu ya WaAdventista wa SabatoKanisa la WaAdventista Wasabato lina takribani shule za sekondari 118 ulimwenguni kote.1 Ingawa nyingi zipo ndani ya Amerika Kaskazini, pia utapata vyuo vikuu vya WaAdventista katika nchi mbalimbali duniani—mahali...