Mungu alikusudia siku ya Sabato iwe kipindi cha saa 24 ambapo tunaweza kusimama na kufurahia wema wa uumbaji Wake. Tunafanya hivi kwa kuweka kando kazi zetu za kawaida ili tuweze kuelekeza mawazo yetu kwa Yeye na kuthamini kile alichoumba (Kutoka 20:8-11).
Hilo linaweza kuonekana rahisi vya kutosha. Lakini mambo yanakuwa magumu zaidi tunapofikiria jinsi mambo yalivyo leo.
Kazi zimekuwa nyingi na zimeendelea sana. Ratiba za kazi zinajaza saa zote za siku, na watu wengi huchukua kazi nyumbani au hata hufanya kazi wakiwa nyumbani. Mambo mengi yamekuwa ya kiotomatiki. Sio kazi zote zinahitaji nguvu za mwili. Na baadhi ya mambo ambayo zamani yalichukuliwa kuwa kazi (uvuvi, ushonaji, bustani, kutunza wanyama, matembezi marefu, kupika, n.k.) sasa ni mambo ambayo baadhi yetu hufanya kwa ajili ya kujifurahisha tunapopata muda kidogo wa kupumzika.
Basi tunawezaje kujua ni mambo gani yanahesabika (au hayahesabiki) kama “kazi” linapokuja swala la kuitunza Sabato ?
Naam, kuna sababu amri ya nne haikutoa orodha ya mambo ya kufanya au kutofanya. Njia ya kweli ya kujibu swali hili iko katika kuelewa kwa undani zaidi maana halisi ya kuitunza Sabato—ambayo Mungu aliiumba kwa ajili yetu (Marko 2:27).
Basi hebu tuangalie Maandiko na tuone tutakachoweza kupata.
Tutaangalia:
- Maana ya Biblia inaposema usifanye kazi siku ya Sabato
- Kwa nini baadhi ya watunza Sabato hufanya kazi siku ya Sabato
- Jinsi ya kutambua nini kinahesabiwa kama kazi
- Jinsi tafsiri ya “kazi” imebadilika katika historia
Tuanze kwa kuangalia Sabato ilianzishwa lini kwa mara ya kwanza, na jinsi ilivyokuwa desturi ya kawaida miongoni mwa Israeli wa kale.
Biblia inamaanisha nini inaposema usifanye kazi siku ya Sabato?

Photo by Cassidy Dickens on Unsplash
Ingawa siku ya Sabato inajadiliwa katika Kutoka 16, ni katika Kutoka 20 ambapo tunaisoma katika mfumo wa amri ya nne.
Kwa hiyo, kwanini jambo linaloonekana kuwa rahisi kama “kutofanya kazi” liwe sehemu ya amri ya milele?
Tunaambiwa tusifanye kazi siku ya Sabato kwa sababu tusingeweza kuipata kikamilifu ikiwa tutaendelea tu na shughuli zetu za kawaida. Ikiwa kitu ni maalum, unatengea muda. Ikiwa unataka kutambua kitu, kufurahia kitu, kujifunza zaidi kuhusu kitu… unapaswa kufanya nini ili mambo hayo yatokee?
Acha unachokifanya na uelekeze mawazo yako kwingine.
Mungu aliumba Sabato kama ruhusa yetu ya kusimama, kupumzika, na kubadilisha mtazamo wetu kutoka “kufanya kazi” hadi “kufurahia.”
Na hii inatupa fursa kamilifu ya kutumia muda zaidi kuwasiliana na Mungu (Kutoka 20:8-10; Isaya 58:13-14; Luka 14:6; Mathayo 11:28-30). Na sio sisi peke yetu tu, bali pia kumwabudu Mungu kama jamii ya waumini—“Sabato ya kustarehe kabisa, kusanyiko takatifu” (Mambo ya Walawi 23:3, SUV).
Kwa kuitakasa na kupumzika siku ya saba Mwenyewe, Mungu alitoa mfano wa jinsi tunavyoweza kusherehekea Sabato kwa kupumzika na kutumia muda pamoja Naye (Mwanzo 2:2-3).
Aina hii ya pumziko ingekuwa na maana maalum kwa Waisraeli baada ya kutumia muda mrefu katika utumwa, ambapo walilazimika kufanya kazi mchana kutwa, kila siku. Hivyo Mungu alichukua tahadhari maalum kuwakumbusha kuhusu Sabato hiyo katika amri ya nne (Kutoka 20:8-11), akiwapa faraja na ruhusa waliyoihitaji ili kupata pumziko la kina walilonyimwa kwa miaka mingi.
Sabato ilikuwa—na bado ni—wakati wa kiroho. Iliumbwa ili kuelekeza mawazo yetu kwenye mambo ya kiroho ambapo tunaweza kupumzika kutoka kwa shughuli zetu za kila siku na kupata amani na kuungana tena na Mungu.
Hata hivyo, kama tulivyotaja awali, waashikao Sabato wanatambua kwamba kuna aina fulani za kazi ambazo lazima zifanywe kwa sababu ya ulazima.
Kwanini baadhi ya washika Sabato hufanya kazi siku ya Sabato?

Photo by CDC on Unsplash
Watunza Sabato wanaweza kufanya kazi siku ya Sabato ikiwa wanahisi kazi yao lazima ifanyike kwa ajili ya wengine (au kwa sababu tu kazi yao ni ya lazima na haiwezi kusimama siku yoyote ya wiki).
Hii mara nyingi hutokea kwa:
- Madaktari
- Wauguzi
- Walezi
- Wafanyakazi wa dharura
- Polisi
- Wazima moto
Kuna hata baadhi ya kazi ambazo watunza Sabato hufanya ambazo hufanyika siku ya Sabato kwa lengo la kuwasaidia wengine kuheshimu siku ya Sabato.
Ndio—tunazungumzia wachungaji na watumishi wa kanisa wanaowahudumia waumini watunza Sabato siku ya Sabato.
Hata katika nyakati za Biblia, Waisraeli walijua kulikuwa na aina fulani za kazi ambazo zililazimika kufanywa—hata siku ya Sabato.
Katika ulimwengu mkamilifu, kila mtu angeweza kufurahia kila Sabato kikamilifu. Lakini bila kujali ilikuwa siku gani, bado walihitaji kulisha wanyama wao, kuwalea watoto wao, na kuwahudumia wanajamii wagonjwa.
Hii ndiyo sababu Waisraeli walilazimika kutofautisha kati ya kazi ya lazima na isiyo ya lazima, au kazi ambayo ilihitaji kufanywa kila siku dhidi ya kazi ambayo haikuhitaji kufanywa siku ya Sabato.
Lakini kumbuka kwamba ufunguo halisi wa kuelewa nini kinachohesabiwa kama kazi siku ya Sabato sio swala la kuweka orodha na kugawa kazi fulani kama “fanya siku ya Sabato” au “usifanye siku ya Sabato.”
Kuelewa nini kinachohesabiwa kama kazi siku ya Sabato ni swala la kumjia Mungu na kumwomba akusaidie kutumia kanuni ya Sabato katika mambo yako binafsi.
Lakini kuna hali nyingi ambapo tunaweza kuona kwanini baadhi ya kazi lazima ziendelee kufanyika, bila kujali siku au saa.
Tunawezaje kubaini nini kinachohesabiwa kama kazi siku ya Sabato?

Photo by Tara Clark on Unsplash
Ingawa Biblia haitupatii orodha iliyopangwa kwa makundi, bado kuna njia tunazoweza kutumia kubaini jinsi “kazi” inavyofafanuliwa kuhusiana na Sabato. Hapa tutaangalia kile Mungu na manabii Wake waliwaagiza Waisraeli katika nyakati mbalimbali, na jinsi Waisraeli walivyoshika (au walivyoshindwa kushika) maagizo haya.
Aina za kazi zilizositishwa siku ya Sabato:
- Kazi za kawaida na biashara (Kutoka 20:8-10; Yeremia 17:20-22): Kazi nyingi au taaluma nyingi zinaangukia katika kundi hili. Hizi ni aina za kazi ambapo ikiwa kazi itafanywa siku sita tu kati ya saba kwa wiki, matokeo ya kazi hiyo yanapaswa kuwa ya kutosha kuitunza jamii.
- Kujihusisha na biashara/kununua au kuuza (Nehemia 13:15-22): Kuweka mkazo katika kupata faida au kupata mali ni kuhusu kukuza biashara au hadhi ya mtu binafsi, na ni kinyume na kusitisha biashara kwa ajili kumlenga Muumba, ambaye ndiye aliyefanya haya yote yawezekane. Zaidi ya hayo, mtu anaponunua kutoka kwa muuzaji, anamlazimisha muuzaji kufanya kazi, na hivyo kumzuia kupata pumziko la Sabato.
Hilo ndilo Mungu alimwagiza nabii Nehemia kulizungumza na Waisraeli walipoacha kulinda saa za Sabato na kuendelea na biashara zao au kufanya biashara na wafanyabiashara wasafiri.
- Kazi au shughuli zisizo za dharura (Kutoka 16:22-30; 35:3; Isaya 58:13-14): Hata kazi ambazo hazichukuliwi kama taaluma au biashara zilipaswa kusitishwa siku ya Sabato, kama vile kukusanya chakula, kuwasha moto, au hata “kuongea mambo ya biashara” (Isaya 58:13, SUV). Haya yote ni mambo ambayo yangeweza kufanywa kabla ya Sabato au kusubiri hadi baada yake.
Ingawa katika nyakati za Israeli ya kale kazi nyingi zilikuwa tofauti sana leo, kanuni bado zinatumika. Hakuna ubaya wowote katika kukuza biashara yako au kuongeza faida au kujadiliana kuhusu biashara au manunuzi. Mungu anataka tuwe mawakili wazuri na wafanyakazi wenye bidii (Mwanzo 2:15; Waefeso 6:6-8).
Sababu ya mambo haya kusitishwa siku ya Sabato, kwa mara nyingine, kwa ajili ya afya yetu ya kiakili na kiroho, na kwa ajili ya uhusiano wetu na Mungu.
Lakini vipi kuhusu aina za kazi ambazo zinaendelea saa zote za kila siku? Amri ya nne, na baraka za Sabato, zinawahusu vipi wale walio na kazi hizi?
Kabla hatujaingia zaidi katika maelezo, hebu tukumbuke kwamba kuomba uongozi wa Mungu katika hali zetu za kipekee ndilo hatua ya kwanza ya kuelewa na kufurahia Sabato kikamilifu.
Hata hivyo, kama unatafuta vidokezo vya kukusaidia kuamua mambo haya, hapa kuna maswali kadhaa ya kujisaidia unaweza kujiuliza:
- Je, hili ni jukumu ambalo ningeweza kulifanya kabla ya wakati?
- Je, hili ni jukumu linalopaswa kufanywa kila siku?
- Kwa kiasi kikubwa, nani anafaidika na kukamilika kwa jukumu hili?
- Je, kuna mtu atateseka nisipofanya hili leo?
- Je, kuna mtu atashindwa kufurahia Sabato ikiwa nitafanya (au sitafanya) hili leo?
Tunaweza pia kujiuliza kwanini tunafikiria kufanya kazi siku ya Sabato kwanza.
Jiulize:
- Je, natafuta kuridhika kwa kukamilisha kipengele cha mwisho kwenye orodha yangu ya mambo ya kufanya?
- Je, natamani kupata pesa zaidi au kupanda ngazi katika kazi yangu?
- Je, ninaogopa kupoteza kazi yangu ikiwa sitafanya kazi siku ya Sabato?
- Je, kweli ninatafuta kujua kama kazi hii au jukumu hili linaheshimu siku ya Sabato?
Wakati baadhi ya maswali haya ni rahisi kujibu, mengine yanaweza kuhitaji mawazo ya ziada na kujichunguza. Lakini tunaweza kuwa na imani kwamba Mungu atatuongoza kupata suluhisho.
Kwa maana, Yeye aliifanya Sabato kwa ajili yetu (Marko 2:27). Haipaswi kuwa jambo gumu sana kutunza Sabato. Na anaahidi kutupa hekima tunapohitaji (Yakobo 1:5).
Tunaweza pia kuangalia katika Maandiko ili kuona kama kuna matukio yoyote ambapo wafuasi wa Mungu walifanya kazi siku ya Sabato kwa namna fulani.
Mifano katika Biblia ya kazi iliyofanywa siku ya Sabato

Photo by Laura Ohlman on Unsplash
Biblia inaonyesha hali chache ambapo aina fulani za kazi zilihitajika kufanywa hata kama ilikuwa Sabato.
Makuhani walifanya kazi katika Hema au hekalu
Makuhani na watumishi wa patakatifu walifanya kazi siku ya Sabato ili kuendesha ibada za patakatifu (Mathayo 12:5; Mambo ya Walawi 23:1-3). Ingawa makuhani walifanya kazi siku ya Sabato, walifanya kazi kutimiza majukumu ambayo Mungu aliwapa. Walikuwa na jukumu la kudumisha kusanyiko takatifu siku ya Sabato. Pia walikuwa na jukumu la kutekeleza huduma za kila siku hekaluni.
Huduma ya kila siku kwa mifugo
Ingawa Waisraeli walifanya kila wawezalo kumaliza kazi zisizo za dharura kabla ya Sabato, daima kulikuwa na mambo machache ambayo yalilazimika kufanywa mara kwa mara. Kwa mfano, mifugo ilipaswa kunyweshwa kila siku (Luka 13:15; Mathayo 12:11-12).
Mwitikio wa dharura
Daima kulikuwa na uwezekano wa Mwisraeli kukutana na dharura ya kutishia maisha siku ya Sabato (Mathayo 12:11; Luka 14:5; Kutoka 23:4-5). Katika hali kama hizi, Waisraeli wangechukua hatua kuokoa maisha ya watu na wanyama, hata kama ingewalazimu kufanya kile ambacho kingeonekana kama kazi katika hali ya kawaida.
Walinzi walilinda malango ya Yerusalemu
Nehemia aliweka walinzi langoni mwa Yerusalemu ili kuwazuia wafanyabiashara kuingia mjini na kuwajaribu Waisraeli kushiriki katika biashara siku ya Sabato (Nehemia 13:15-22).
Hadithi hii inaonyesha tofauti kati ya kazi ya lazima na kazi ya biashara. Walinzi waliwekwa ili kulinda utakatifu wa Sabato kwa ajili ya jamii wakati wafanyabiashara walikuwa wakijaribu kupata faida.
Wanafunzi walichuma nafaka

Photo by Paz Arando on Unsplash
Biblia inatuambia kwamba wanafunzi 12 walichuma nafaka siku ya Sabato (Mathayo 12:1-2). Walifanya hivi kwa sababu walikuwa na njaa na hawakuwa na chakula pamoja nao.
Hakika hawakuwa wanafanya hivyo ili kuuza nafaka. Na haikuwa kana kwamba walikuwa wanavuna shamba lote, walichukua vipande vichache tu vya nafaka hapa na pale, vya kutosha kushibisha njaa yao.
Jambo la muhimu zaidi, kitendo chao cha kuchuma nafaka hakikuwazuia kutumia muda na Mungu. Kwa kweli, walikuwa wanapita kwenye shamba pamoja na Yesu Kristo Mwenyewe!
Na bado, kwa sababu kitendo cha kung’oa nafaka kutoka kwenye mashina yake kililingana na maelezo ya mojawapo ya sheria za Mafarisayo kuhusu kazi, viongozi wa Kiyahudi walisisitiza kwamba walikuwa wanavunja Sabato.
Lakini Mafarisayo walipowakosoa kwa kuchuma nafaka, Yesu alilinganisha na wakati ambapo Daudi alipewa mkate mtakatifu ale alipokuwa na uhitaji, ingawa sheria ilisema ni makuhani tu walioweza kula mkate huo mtakatifu.
Kwa kutoa mfano huu, Yesu alionyesha kwamba huruma na mahitaji ya wanadamu vinapaswa kuwa kipaumbele. Sheria ipo ili kuwalinda wanadamu na kuwasaidia kustawi—sio kuwafanya maisha yao kuwa magumu zaidi.
Yesu aliponya watu siku ya Sabato
Yesu aliwaponya watu siku ya Sabato katika matukio mengi tofauti (Mathayo 12:10-14; Luka 13:10-17; Luka 14:1-6; Yohana 5:1-18; Yohana 9:1-16).
Ingawa Mafarisayo walimkosoa Yesu kwa kufanya kile walichokiona kama kazi siku ya Sabato, Yesu alisisitiza tena umuhimu wa kushughulikia mahitaji ya wengine kabla ya kutimiza matakwa ya sheria.
Alionyesha kwamba Mafarisayo wote walikuwa wakiwapa wanyama wao maji siku ya Sabato, jambo ambalo, ingawa ni aina ya kazi, bado lilifanywa ili kukidhi mahitaji ya wanyama wao.
Wayahudi walikuwa na wakati mgumu kuelewa maana halisi ya kuitunza Sabato. Badala ya kuishi kwa kanuni za Sabato, walikuwa wameanza kutegemea orodha ya masharti ya Sabato ambayo viongozi wao wa Kiyahudi, yaani Mafarisayo, walikuwa wameunda (Marko 7:5-13).
Kwa sababu hiyo, walijishughulisha sana na sheria na mapokeo yao kiasi kwamba walidhani Yesu Kristo Mwenyewe alikuwa anavunja Sabato alipokuwa Akiponya watu (Mathayo 12:10).
Lakini Yesu alieleza kwamba ni jambo jema kuponya siku ya Sabato, akisema:
“Ni mtu yupi miongoni mwenu mwenye kondoo mmoja, na yule kondoo ametumbukia shimoni siku ya sabato, asiyemshika akamwopoa? Je! Mtu ni bora kuliko kondoo mara ngapi? Basi ni halali kutenda mema siku ya sabato” (Mathayo 12:11-12, SUV).
Kwa namna hii, Yesu alieleza kwamba kuwahudumia wengine na kushughulikia mahitaji ya jirani zetu hakuvunji sheria. Kusudi zima la Sabato lilikuwa ni kwa ajili ya manufaa ya mwanadamu (Marko 2:27).
Hii ndiyo sababu ni muhimu sana tusipunguze utunzaji wa Sabato kuwa mkusanyiko wa sheria na orodha za makundi.
Hii inafanya iwe rahisi sana kupunguza Sabato kuwa ibada ya kutimiza tu, badala ya baraka ya kufurahia. Orodha ya jumla ya sheria pia inashindwa kushughulikia changamoto za hali mahususi tunazokutana nazo.
Badala yake, tunapaswa kuikaribia Sabato kwa kutegemea uongozi wa Roho Mtakatifu huku tukijifunza kanuni za Sabato alizotuachia katika Neno Lake.
Je, tafsiri ya “kazi” imebadilikaje katika historia?

Photo by Teona Swift
Watu wa karne ya 21 husherehekea Sabato kwa njia tofauti na wale tunaosoma kuwahusu katika Biblia. Tunakutana na hali tofauti na Waisraeli wa wakati wa Yesu.
Kwa mfano, kutokana na teknolojia ya kisasa, kile ambacho zamani kilichukuliwa kuwa kazi ngumu au inayochukua muda sasa ni rahisi kama kubonyeza kitufe.
Tunaweza kufikiria jinsi Waisraeli, walipokuwa watumwa huko Misri, hawakupata fursa ya kupumzika kutoka kwenye kazi zao. Lakini Mungu alipowaokoa kutoka utumwani Misri, aliwakomboa pia kutoka kwenye kazi walizokuwa wakifanya siku ya Sabato. Aliwapa siku ambayo wangeweza kupumzika, bila kuwa na wasiwasi kuhusu kupika, kulima, au kuwasha moto.
Kuwasha moto katika Israeli ya kale ilikuwa kazi ngumu sana. Ilihusisha kugawanya, kubeba, na kuwasha kuni mbichi. Ilikuwa ni afueni kubwa kuachiliwa kutoka kwenye kazi hii ya kuchosha siku ya Sabato (Kutoka 35:3)!
Lakini hiyo ilikuwa zamani.
Leo, tunaweza kuwasha hita zetu au kuwasha majiko ya gesi kwa kuzungusha tu kitufe.
Kugeuza kitufe sio jambo ambalo Waadventista wengi wangeliona kuwa ni kazi ngumu. Muhimu zaidi, hatuoni kwamba kugeuza kitufe ni jambo litakalotuzuia kufurahia utimilifu wa Sabato au kututenga na ushirika na Mungu.
Shughuli nyingi ambazo hapo awali zilikuwa ngumu sasa zinaweza kufanywa bila hata kufikiria sana kuzihusu. Baadhi tunazifanya bila hata kujitambua.
Hata hivyo, tunatambua kwamba kile kinachochukuliwa kuwa “kazi” kinaweza kutofautiana kutoka utamaduni mmoja hadi mwingine kama vile kinavyoweza kutofautiana kutoka karne moja hadi nyingine. Wazo la kazi linaweza kuonekana tofauti kwa tamaduni mbalimbali kulingana na maana, thamani, na teknolojia iliyopo.
Hii ni sababu nyingine tena ya kuwa waangalifu kuhusu kupunguza utunzaji wa Sabato kuwa orodha ya sheria.
Sheria mara nyingi hutegemea muktadha.
Wakati muktadha wa hali yetu unabadilika, inaweza kuathiri jinsi baadhi ya kanuni zinavyotumika.
Wakati kanuni ni za milele, jinsi tunavyotumia kanuni hizo katika maisha yetu itabadilika kadri muda unavyopita au katika mazingira tofauti.
Ni muhimu pia kufahamu kwamba sheria zinaweza kufuatwa bila kufikiri sana, ilhali kuzingatia kanuni kunatufanya tutumie akili zetu, tuombe kwa Mungu, na kuziuliza Biblia zetu.
Zaidi ya hayo, orodha ndefu ya mambo ya kuacha au kuepuka inaweza kutuzuia kwa urahisi tusiione Sabato kama furaha (Isaya 58:13-14).
Zaidi ya hayo, kuchukua hatua nyingi kupita kiasi ili kuepuka kazi kunaweza kuwa aina ya kazi pia!
Joe A. Webb, DMin, aliyekuwa mchungaji mkuu wa Kanisa la Waadventista wa Sabato la Caboolture, alieleza kwamba:
“Jinsi tunavyoshika Sabato vizuri haitegemei jinsi tunavyozijua sheria vizuri au jinsi tunavyojitahidi, au hata jinsi tunavyowakaripia wengine tunaowachukulia kuwa wavunjaji wa Sabato, bali inategemea jinsi tunavyomjua Bwana wa Sabato na kuungana naye, hasa siku ya Sabato.”1
Hii ndiyo sababu hatuwezi kutegemea sheria zilizotungwa na wanadamu. Tunapaswa kukubali kanuni zisizopitwa na wakati ambazo Mungu alitupa ili kupokea baraka ya siku ya Bwana kwa kweli.2
John Brunt, Ph.D., aliyekuwa makamu wa rais wa utawala wa masomo katika Chuo Kikuu cha Walla Walla, anaongeza:
“Hii haimaanishi kwamba uzembe na ukosefu wa kujali kuhusu utunzaji wa Sabato unapaswa kutawala. Inamaanisha kwamba jamii inayomfuata Yesu itakuwa jamii ya aina maalum. Itakuwa jamii inayofikiria kuhusu maana ya Sabato. Itakuwa jamii inayotafakari pamoja jinsi Sabato inavyoweza kutunzwa vyema ili kuchangia maana yake na kuwanufaisha watu ambao Mungu amewapa kama zawadi.”3
Mwishowe, kutunza Sabato kunahusu mambo yafuatayo:
- Kuelekeza mawazo yetu kwa Mungu kama Muumba wetu
- Kuzingatia kanuni alizotupa
- Kumuomba Mungu atuonyeshe jinsi ya kuitunza Sabato kwa namna itakayotukaribisha zaidi kwake
Mungu anataka kila mmoja wetu afurahie amani na furaha inayokuja na kusherehekea Sabato. Anataka tuone jinsi tunavyoweza kuitumia kutumia muda zaidi na familia au katika ushirika na waamini wenzetu.
Lakini zaidi ya yote, anataka tukumbuke kwamba Sabato inahusu kukua katika uhusiano wetu naye.
Unataka mawazo ya jinsi unavyoweza kutumia siku ambayo Mungu aliitenga kuwa pamoja nawe? Angalia “Pumziko na Muunganiko: Maana Halisi ya Kutunza Sabato” kwa orodha ya shughuli 55 unazoweza kufurahia siku ya Sabato.
Kurasa Zinazohusiana
- Webb, A., Joe, “The Sabbath experience,” Ministry Magazine, Seventh-day Adventist World Church [↵]
- Mark 7:7-8; Matthew 23: 1-4; 2 Corinthians 3:5-6; Romans 2: 28-29. [↵]
- Brunt, John, “How shall we keep the sabbath?” Ministry Magazine, Seventh-day Adventist World Church, [↵]
Majibu Zaidi
Kwa Nini Waadventista wa Sabato Huabudu Siku ya Jumamosi?
Waadventista huabudu siku ya saba ya juma kwa sababu Mungu aliifanya Jumamosi kuwa siku takatifu wakati wa uumbaji. Jifunze ni nini kinachofanya siku hii kuwa maalum kwa Waadventista.
Kila Kitu Unachohitaji Kujua Kuhusu Chakula cha Siku ya Sabato
Kwa Waadventista Wa Sabato, kushiriki chakula cha Siku ya Sabato pamoja na marafiki na familia ni moja ya sehemu muhimu na ya kumbukumbu ya Sabato.
Je! Tunaweza Kuitunza Siku Yoyote ya Wiki Kama Sabato?
Katika sura za kwanza kabisa za Biblia, tunamwona Mungu akianzisha kumbukumbu ya kila wiki na siku ya mapumziko, inayoitwa Sabato (Mwanzo 2:2-3).
Pumziko na Kuunganishwa Tena: Maana Halisi ya Kutunza Sabato
Biblia inatuambia kwamba tunatunza Sabato kwa kuepuka kazi. Mungu alitoa sheria hii kwa sababu alijua itatuimarisha na kutuletea furaha, pamoja na kutupa muda wa kuungana naye na kujipatia nguvu kutokana na maisha yetu yenye shughuli nyingi.
Nani Aliyebadilisha Sabato kwenda Jumapili?
Nani Aliyebadilisha Sabato kwenda Jumapili?Ikiwa Biblia haijawahi kutaja mabadiliko ya Sabato, kwa nini leo wengi wanaenda kanisani Jumapili? Nani alibadilisha siku hiyo? Lakini hilo sio swali sahihi la kuuliza. Sabato haijabadilika. Kilichobadilika ni uamuzi wa...
Kila kitu unachohitaji kujua kuhusu Shule ya Sabato
Kila kitu unachohitaji kujua kuhusu Shule ya SabatoShule ya Sabato ndio sehemu ya kujifunza Biblia ya programu za kanisa katika makanisa mengi ya Waadventista wa Sabato. Ni wakati wa kujifunza Biblia kuhusu mada au somo fulani. Badala ya kumsikiliza mhubiri, watu...
Ninawezaje Kuanza Kutunza Sabato?
Sabato, inayokuja kila siku ya saba ya juma, ni siku maalum inayoheshimu amri ya nne na uumbaji wa Mungu.










