Ulikuwa unategemea simu kutoka kwa binti yako nusu saa iliyopita, na bado hajapiga simu. Pia hajibu simu zako. Unahisi moyo wako ukidunda huku mawazo yako yakikimbia: labda amepata ajali ya gari?, Vipi kama kitu kibaya kimetokea? Vipi kama…?
Aina hizi za mawazo ya wasiwasi ni za kawaida. Wakati mambo hayaendi kama ilivyopangwa, na hatujui kwa nini, ni rahisi sana kudhani kuwa yawezekana jambo baya zaidi limetokea.
Mara nyingi, hata hivyo, mambo haya huishia kuwa usumbufu usio na madhara au migogoro midogo.
Lakini tunawezaje kushughulikia wasiwasi huu unaoonekana kuwa mbaya sana? Tunawezaje kujikomboa kutoka katika kifungo chake?
Inaanza na mawazo yetu.
Ndiyo maana tunakusudia kujifunza namna ya kuyashughulikia. Tunayatuliza kwa kuyakabili moja kwa moja. Kisha tunaweza kubaini ikiwa hofu zetu ni halali au ikiwa ni matokeo ya sisi wenyewe kukuza mambo kuliko kawaida.
Hapa kuna muhtasari wa mambo tutakayojadili:
- Mawazo ya wasiwasi ni nini?
- Biblia inasema nini kuhusu mawazo ya wasiwasi
- Jinsi ya kushughulikia mawazo mabaya
- Kwa nini Waadventista wanajali afya ya akili
Ikiwa unatafuta suluhisho za kushughulikia mambo haya, anza kwa kutambua kwamba ni jambo linalowezekana. Tunapoelewa asili ya mawazo, tutakuwa na uwezo mzuri zaidi wa kuyashughulikia.
Fikira za wasiwasi ni nini?

Photo by Joice Kelly on Unsplash
Mawazo ya wasiwasi ni mawazo ambayo husababisha hisia za wasiwasi, mashaka, au hofu. Mara nyingi husababishwa na matukio au hali fulani. (Ingawa mara nyingine, yanaweza kusababishwa tu na fikra zetu nyingi.)
Chama cha Afya ya Akili cha Canada kinaeleza kuwa wasiwasi una vipengele vitatu:
1. Mawazo au matarajio kwamba kitu kibaya kitatokea
2. Dalili za kimwili, kama vile msongo, ongezeko la mapigo ya moyo, mikono inayonata, au tumbo lililokaza
3. Kitendo, kwa kawaida ni mwitikio wa kupigana au kukimbia (au kuduwaa).
Mambo haya matatu yanaendana na tiba ya tabia ya kisaikolojia (CBT), njia inayojulikana sana katika tiba ya akili leo. Kulingana na CBT, tukio la kuchochea hupelekea imani, ambayo kisha inasababisha matokeo. Matokeo ni hisia au tabia.
Mlolongo huu wa matukio ni ABC za CBT:
Tukio chochezi > Imani > Matokeo.
Wazo liko hivi:
Tunachochagua kuamini kuhusu hali fulani kinaamua jinsi tunavyojisikia na kuitikia hali hiyo.
Hivyo, tunapokuwa na mashaka au hofu, ni kwa sababu tumechagua kuona hali husika kwa njia ambayo ingepelekea hisia hizo. Mawazo yetu ndiyo mhusika mkuu.
Hebu tuongeze mtazamo wa Kibiblia kwenye ufahamu wetu.
Kile Biblia inachosema kuhusu mawazo ya wasiwasi
Biblia inatufundisha kwamba kile tunachofikiria kina uhusiano moja kwa moja na utambulisho wetu(Mithali 23:7). Kwa sababu hii, inatuhimiza tumwombe Mungu Achunguze mioyo yetu ikiwa ina mawazo ya wasiwasi ili kweli yake iwekwe kama mbadala wa mawazo hayo.
“Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu” (Wafilipi 4:6, NKJV).
Mwandishi wa Zaburi Daudi aliona uhalisia wa hili alipokuwa akisali:
“Ee Mungu, unichunguze, uujue moyo wangu, Unijaribu, uyajue mawazo yangu” (Zaburi 139:23, NKJV).
Sisi pia tunaweza kusali na kumwomba Achunguze mioyo yetu na kutuonyesha mawazo yenye wasiwasi yanayosababisha mashaka na hofu zetu.
Mara nyingi, mawazo haya hayatakuwa ya kweli.
Hata hivyo, mara nyingine, yanaweza kuwa ya kweli lakini yasiyo muhimu.
Mungu anataka tuongee mawazo ya kweli na yanayotusaidia mioyoni mwetu (Zaburi 15:2) kwa sababu Anajua kwamba mawazo yetu yatajenga hisia na tabia zetu.
Anatualia kutafakari “yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema” (Wafilipi 4:8, NKJV).
Na jambo la kushukuru ni kwamba, hatulazimiki kuakisi kilicho kweli.
Biblia ni chanzo chetu cha ukweli (Yohana 17:17). Na huko, tunaona jinsi Yesu Alivyoishi ukweli huo (Yohana 14:6).
Mungu anataka tubadlishe mawazo mabaya kuwa mawazo sahihi na yenye manufaa. Katika sehemu inayofuata, tutajadili kwa undani jinsi ya kufanya hivyo.
Jinsi ya kushughulikia mawazo mabaya
Kushughulikia mawazo mabaya kunahusisha kutambua mifumo yetu ya kufikiri, kuikosoa, na kui badilisha na mawazo ya kweli na yenye manufaa.
Dk. Neil Nedley, daktari Mwadventista msabato na mzungumzaji maarufu duniani ambaye anaendesha programu ya kuponya sonona na wasiwasi, apigia debe njia hii katika kitabu chake The Lost Art of Thinking. Anasema:
“Lengo ni kuchunguza na kukosoa mawazo yako kwa mpangilio, kugundua kama ni sahihi, na kuhoji usahihi wake. Kwa kuchambua na kutafakari juu ya unachofikiri, utaweza kuona ikiwa unasikiliza ujumbe wa zamani na usiofaa akilini mwako.”1
Lakini kwa nini hatuwezi tu kupuuza wasiwasi na mashaka? Mara kwa mara inaonekana kana kwamba ingekuwa bora kuepuka kufikiria mambo yanayotusumbua au kutusababishia wasiwasi…
Tunagundua kwamba, tunapopuuza hisia hizi, tunajidhuru wenyewe lakini sio kisaikolojia tu. Kuzuia hisia huathiri miili yetu pia.
Watafiti kutoka Shule ya Afya ya Umma ya Harvard na Chuo Kikuu cha Rochester waligundua kwamba kwa zaidi ya miaka 12, watu waliokuwa wakipuuza hisia zao walikuwa na viwango vya juu vya vifo, ikiwa ni pamoja na vifo vilivyotokana na kansa.2
Na wale wetu ambao wamejaribu kupuuza wasiwasi wetu wanajua mara nyingi huzidisha tu hisia hizo. Mwishowe, hutufanya tujisikie vibaya zaidi!
Tunahitaji njia bora ya kushughulikia hisia za wasiwasi. Kwa nini usijaribu hatua hizi tatu?
1. Tambua wazo.
2. Kosoa wazo.
3. Badilisha wazo hilo na ukweli.
Ni hatua rahisi, ndiyo. Lakini zinahitaji uaminifu na uvumilivu ili tuweze kuendeleza tabia ya kuwa na fikira zenye afya.
Tafadhali kumbuka: Makala hii isichukuliwe kama ushauri wa kitabibu. Ikiwa wewe au mpendwa wako anakabiliana na ugonjwa wa akili, ikiwa ni pamoja na shida ya wasiwasi au hofu, tafadhali tafuta mtaalam wa afya ya akili. Kufanya hivyo sio kukosa imani.
1. Tambua wazo.

Photo by Rebe Pascual on Unsplash
Hatua ya kwanza katika kukabiliana na mawazo ya wasiwasi ni kugundua mawazo hayo. Wakati tumbo lako linapojikaza na joto linapoongezeka usoni mwako, unafikiria nini wakati huo?
Je, unaweza kuwa unajisalimisha kwa mfumo wa mawazo mabaya?
Katika kitabu cha The Lost Art of Thinking, Dkt. Nedley anajadili vikwazo kumi vya mawazo vinavyojitokeza mara kwa mara katika ushauri na saikolojia.
Angalia kama wazo lako baya linaweza kuwa katika moja ya makundi haya:
- Fikira za kupata vyote au kukosa vyote—Kila kitu kiko wazi; hakuna nafasi ya kati. Unaweza kufikiri, Kama sitafanya kazi hii kikamilifu, mimi ni bure kabisa.
- Kujumlisha—Unafikia hitimisho kutoka uzoefu mmoja mbaya, ukitegemea uzoefu wote ujao utakuwa huo huo. Kwa mfano, Sijapata kazi. Siwezi kupata kazi yoyote.
- Vichujio vya kiakili—Unazingatia mambo mabaya huku ukichuja mambo mema. Unaweza kuchagua kitu kimoja kilichokwenda vibaya kati ya mambo mengi yaliyo kuendea vizuri.
- Kupuuza mambo mazuri—Unajitafutia sababu za kufanya jambo zuri lisiwe na uzuri wowote. Mtu akikusifu kwa hotuba nzuri uliyotoa, unajibu, “ni bahati tu,” au unafikiri moyoni, wanajaribu tu kuwa wema.
- Kusoma mawazo—Unadhani unajua mtu anafikiria nini kukuhusu au hali fulani. Kwa mfano, wakati jirani yako aliposhindwa kukusalimia, ulifikiri, huenda hanipendi.
- Kutabiri mustakabali—Unatabiri matokeo mabaya kabla hayajatokea. Unaweza kudhani kitu kibaya kimetokea kwa binti yako kwa sababu tu hajapokea simu zako.
- Kukuza mambo—Unazidisha matatizo na makosa. Mtindo huu wa mawazo mara nyingi unakwenda sambamba na kupunguza sifa njema.
- Mantiki ya kihisia—Unaamini kwamba jinsi unavyojisikia inaakisi ukweli. Unaweza kufikiri, Najiona siwezi, hivyo kwa kweli siwezi.
- Kuweka lebo—Unajibandika sifa mbaya au kwa wengine kulingana na makosa na mapungufu yanayoonekana. Unaweza kujiambia, Mimi siwezi chochote au Mimi sivutii, hivyo ninafaa kuwa peke yangu.
- Ubinafsishaji—Unajiwajibisha mwenyewe kwa mambo yasiyo katika udhibiti wako. Kwa mfano, mzazi anaweza kufikiri, Ni kosa langu mwanangu kupata ajali. Nilipaswa kumwonya aendeshe kwa uangalifu kwenye mvua.
2. Pinga mawazo.
Sasa baada ya kutambua mfumo wako wa mawazo mabaya, ni wakati wa kuupinga. Kujiuliza maswali ni njia yenye ufanisi ya kufanya hivyo.
Hapa kuna baadhi ya maswali ya kuanza nayo3:
- Je, wazo hili ni la kweli? Kuna ushahidi gani kwa hilo?
- Ni kwa njia gani nyingine ninaweza kuitazama hali hiyo?
- Ni kwa namna gani hofu yangu itatokea? Nini kinachoweza kutokea zaidi?
- Je, wazo hili linanisaidia au kunidhuru? Kwa namna gani?
- Ningemwambia nini rafiki mwenye wasiwasi kama huo?
Kwa kujiuliza maswali haya, ni rahisi kugundua sababu zisizo za lazima za wasiwasi. Na pia yanatuandaa kwa hatua ya mwisho…
3. Badilisha wazo hilo na ukweli.
Tunapobaini fikira mbaya kama ilivyo, tuko tayari kuibadilisha na ukweli wa Biblia na ukweli wa hali halisi.
Biblia inaita mchakato huu “tukiteka nyara kila fikra ipate kumtii Kristo” (2 Wakorintho 10:5, NKJV).
Tunapoleta fikira zetu kwa Mungu na kuzibadilisha, Yeye hutuweka huru (Yohana 8:32).
Hivyo hapa kuna baadhi ya mifano ya ukweli—Aya za Biblia na uhalisia—zinazoweza kuchukua nafasi ya fikira zetu za wasiwasi:
| Fikra hasi | Upotoshaji | Ukweli |
| Siwezi kufanya makosa | Fikira za kupata vyote au kukosa vyote | Sisi sote tunafanya makosa, lakini Mungu hutupatia neema na msamaha (1 Yohana 1:9). |
| Mama yangu aliniacha tangu utotoni, hivyo nitabaki mpweke maisha yangu yote | Kujumlisha | Mungu asema, “Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa” (Waebrania 13:5, NKJV). |
| Siwezi kujisamehe kwa maneno yanayoumiza niliyomwambia dada yangu. (Ingawa lilikuwa dogo lilikilinganishwa na nyakati nyingi nzuri ambazo mmekuwa nazo pamoja.) | Vichujio vya kiakili | Dada yako anakumbuka nyakati zote nzuri pamoja nawe—hafikirii tu kuhusu wakati ule uliposema kitu kilichomuumiza. |
| Walikuwa wakisema tu kwamba wanatamani hotuba yangu ieleweke vizuri. Kwa kweli, mimi sifai kwa jukumu hili. | Kupuuza mambo mazuri | Unaweza kuwa na ujasiri katika kile Mungu alichokufanya uwe. Yeye hukupa nguvu na hekima unapojisikia hautoshi (Wafilipi 4:13; Yakobo 1:5). |
| Jirani yangu hakunipungia mkono. Hanipendi | Kusoma mawazo | Jirani wako huenda hakukuona ukimpungia mkono. Huenda alikuwa amejikita katika mambo mengine. Na hata kama jirani yako hakupendi, thamani yako inatokana na upendo wa Mungu kwako (Yeremia 31:3). |
| Naogopa kuna jambo baya litatokea | Kuamua mustakabali |
Mungu anakuwazia “mawazo ya amani wala si ya mabaya” (Yeremia 29:11, NKJV). na “Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami” (Zaburi 23:4, NKJV). |
| Siwezi kushughulikia hali hii, ni ngumu sana kwangu | Kukuza mambo | Mungu anasema unaweza kufanya mambo yote kupitia Kristo (Wafilipi 4:13). |
| Naogopa, labda sina imani kabisa | Mantiki ya kihisia |
Mungu amewapa kila mtu “kiasi cha imani” (Warumi 12:3, NKJV). na “…Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali, mtauambia mlima huu, ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwepo neno lisilowezekana kwenu” (Mathayo 17:20, NKJV). |
| Mimi ni mtu niliyekataliwa na sio chochote | Kujiweka lebo | Mungu anakwambia kwamba wewe ni “ametuneemesha katika huyo Mpendwa” (Waefeso 1:6, NKJV). |
| Nashangaa hili linanipata, Mungu ananiadhibu | Ubinafsishaji | Mungu anaelewa udhaifu wetu na ni mwenye rehema kwetu. Hatutendei kama tunavyostahili (Zaburi 103:10–14). Na mambo yanayo tupata yanaweza kuwa sehemu tu ya changamoto za ulimwengu wetu uliochanganyika (Mathayo 5:45). |
Habari njema ni kwamba kwa kila uongo tunaojiambia, Mungu ana kitu katika Neno lake cha kukabiliana nao. Yeye hutuweka huru ili kufurahia wakati wetu sasa kama baraka kutoka kwake.
Na ndio maana hili somo ni muhimu sana kwetu kama Waadventista.
Kwa nini Waadventista wanajali afya ya akili
Waadventista wanajali afya ya akili kwa sababu Mungu anajali pia. Anataka tuweze kufurahia uhuru unaotokana na kufikiri na kuishi ukweli. Anajua akili zetu zina uhusiano na miili yetu na kwamba kimoja huathiri kingine.
Na ni kwa sababu alituumba hivyo. Sisi ni “jinsi ya ajabu ya kutisha” (Zaburi 139:14, NKJV).
Biblia inatuita “nawe umpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote” (Marko 12:30, NKJV). Hii inajumuisha kila sehemu ya maisha yetu – hisia zetu, hali ya kiroho, mawazo, na miili yetu.
Tunapojali akili zetu kwa kufikiria mawazo yenye afya, tunamuonyesha upendo Muumba wetu. Na afya ya akili zetu inaathiri afya ya miili yetu. Kwa upande mwingine, kujali ustawi wetu kimwili ni njia ya kusaidia akili yenye afya. Haya yote ni sehemu muhimu za kanuni za afya za Waadventista.
Unaweza kuwa huru dhidi ya mawazo ya wasiwasi.
Zaidi ya kitu kingine chochote, Mungu anataka uwe huru kutoka katika wasiwasi na hofu, ukipata furaha kamili katika maisha yako ya kila siku (Yohana 10:10; 15:11, NKJV).
Na aina hiyo ya maisha inatokana na kuamini na kuishi ukweli.
Ikiwa umekuwa ukisumbuliwa na mawazo ya wasiwasi, tambua kwamba Mungu anataka kukufanya uwe huru kutoka huko. Yeye yupo hapa kukusaidia kutambua, kukabiliana, na kuyabadilisha na mawazo yenye manufaa na sahihi.
Ukifanya hivyo, utakuwa kwenye njia kuelekea akili yenye afya ambayo inaweza kumpenda Yeye kikamilifu.
Chagua Masomo ya Biblia Mtandaoni
Unataka kuendelea kujifunza? Pata habari zaidi kuhusu Yesu, mwanadamu, mpango wa wokovu, na jinsi Mungu anavyokupenda kiasi cha kutosha kujitolea kila kitu, ili tu kukupatia nafasi ya kumchagua.
Wakati mwingine inaweza kuwa ngumu kujua pa kuanzia, ndio maana tunatoa chaguo za masomo ya Biblia mtandaoni bure, rahisi kutumia, unaweza kufanya wakati wowote, mahali popote, na kwa kasi yako mwenyewe.
Shule hii ya Biblia mtandaoni itakuelekeza kupitia mada kuu za Maandiko, ikivunja dhana ngumu za Biblia katika vipande vidogo, ambavyo vinaweza kukusaidia kupata majibu ya maswali magumu zaidi ya maisha.
- Nedley, Neil, The Lost Art of Thinking (Nedley Publishing, 2011), p. 20. [↵]
- Chapman, et al., “Emotion Suppression and Mortality Risk Over a 12-Year Follow-Up,” Journal of Psychosomatic Research, vol. 75(4), 2013, pp. 381–385. [↵]
- “Are Your Thoughts Holding You Back?” Alice Stapleton Career Coaching, Feb. 23, 2014. [↵]
Majibu Zaidi
Njia 12 Halisi za Kukabiliana na Wasiwasi
Njia 12 Halisi za Kukabiliana na WasiwasiTAHADHARI: Maudhui haya ni kwa madhumuni ya taarifa tu. Hayawakilishi ushauri wa kitaalamu wa matibabu, na haikusudiwi kama mbadala wa matibabu ya kitaalamu ya afya ya akili. Ni rahisi kushikwa katika mzunguko wa wasiwasi. Hasa...


