Watoto wanakufa kwa njaa. Raia wasio na hatia wakikumbwa na vita. Mpendwa akifa kwa saratani.
Ni wazi kwamba kuna kitu kibaya katika dunia yetu. Inaonekana kuna mgogoro wa kudumu kati ya mema na mabaya.
Ni mara ngapi tunajikuta tukifikiri, Hii si sawa! Hivi sivyo maisha yanavyopaswa kuwa!
Biblia inakubaliana na hili. Inatuonyesha jinsi hii haikuwa mpango wa awali wa Mungu. Badala yake, huu mgogoro ni matokeo ya vita ya siri kati ya Kristo na Shetani. Vita vilivyoanza mbinguni wakati Lusifa, malaika wa cheo cha juu, alipoamua kuasi dhidi ya Mungu. Waadventista wa Sabato wanaita vita hivi vya kiroho kuwa Pambano Kuu kati ya Kristo na Shetani.
Na kama viumbe vilivyoumbwa vyenye uhuru wa kuchagua, nasi pia tunahusika katika jambo hili.
Ili kuelewa vizuri zaidi, tutaangalia:
- Je, Pambano Kuu ni nini?
- Lusifa alikuwa nani?
- Lusifa alikuwaje Shetani?
- Shetani anapiganaje vita dhidi ya Mungu hapa duniani?
- Pambano kati ya Kristo na Shetani itakuwaje mwisho?
Hebu tuanze kwa kufafanua ile Pambano Kuu.
Je, mada ya Pambano Kuu ni nini?

Photo by Aleksandar Popovski on Unsplash
Pambano Kuu—ni neno kutoka katika maandishi ya Ellen White ambaye aliandika kitabu chenye jina hilo hilo—ni vita vya ulimwengu mzima kati ya Yesu Kristo na Shetani (Ufunuo 12:7-9). Vilianza mbinguni wakati malaika aitwaye Lusifa alipoasi dhidi ya sheria ya Mungu ya upendo na kujitoa, akachagua kuongozwa na dhambi, ambayo mizizi yake ni ubinafsi na kiburi (Isaya 14:12-14). Hata hivyo, hatakuwa na neno la mwisho, kwa sababu Kristo ndiye mshindi, akishinda ubinafsi kwa upendo wake wa kujitoa.
Wakati Lusifa alipoasi, Mungu hakuwa na budi ila kumtupa nje—pamoja na malaika aliowashawishi wamfuate—kutoka mbinguni. Kutoka hapo, Lusifa, ambaye sasa anajulikana kama Shetani, alikuja duniani na kuwadanganya wanadamu wa kwanza na amekuwa akifanya kazi kumuumiza Mungu kwa kuwaumiza watu kwa kila njia iwezekanayo—vita, majanga, mauaji, magonjwa, na zaidi (Yohana 8:44).
Lakini ingawa inaonekana kama Shetani anafanikiwa sasa hivi, haitakuwa hivyo daima.
Mungu anampa muda aonyeshe tabia yake halisi kwa ulimwengu mzima. Wakati huo huo, Mungu ameonyesha sheria yake ya upendo wa kujitoa kupitia maisha na kifo cha Kristo. Mwishowe, Kristo atashinda dhidi ya Shetani, akiharibu dhambi na uovu milele.
Lakini hebu tusimame kidogo na tupate historia ya pambano hili.
Yote yalianza na Lusifa…
Lusifa alikuwa nani?
Lusifa alikuwa malaika wa nuru aliyeishi mbinguni (Isaya 14:12). Katika Kiebrania cha asili, jina lake linamaanisha “mwenye kubeba nuru,” “mng’ao,” au “nyota ya asubuhi.” Alikuwa aina maalum ya malaika aitwaye kerubi afunikaye au “kerubi mlinzi.”
Angalia kile Ezekieli 28:12-13 inavyotuambia kuhusu uzuri wake na cheo chake cha juu:
“…..Wewe wakitia muhuri kipimo, umejaa hekima, na ukamilifu wa uzuri. Ulikuwa ndani ya Adeni, bustani ya Mungu; kila jiwe la thamani lilikuwa kifuniko chako, akiki, na yakuti manjano, na almasi, na zabarajadi, na shohamu, na yaspi, na yakuti samawi, na zumaridi, na baharamani, na dhahabu; kazi ya matari yako na filimbi zako ilikuwa ndani yako; katika siku ya kuumbwa kwako zilitengenezwa tayari” (SUV).
Kerubi afunikaye ni aina maalum ya malaika anayesimama karibu na kiti cha enzi cha Mungu. Tunajua hili kwa sababu Zaburi 99:1 inatuambia kwamba Mungu “Ameketi juu ya makerubi” (SUV).
Maskani iliyojengwa na Waisraeli inaonyesha jambo kama hilo kwa sababu ilionyesha chumba cha kiti cha enzi cha mbinguni (Waebrania 8:1-2, 5). Sanduku la agano—ambalo lilikuwa ni sanduku lililoshikilia Amri Kumi—lilikuwa na uwepo wa Mungu juu yake na lilikuwa linawakilisha kiti chake cha enzi. Juu yake kulikuwa na makerubi wawili wenye mabawa yao yakilifunika (Kutoka 25:8-22).
Kama vile Amri Kumi zilivyokuwa ndani ya sanduku la agano, ndivyo sheria ya upendo ya Mungu ilivyo msingi wa serikali yake. Na jukumu la kerubi afunikaye lilikuwa kulinda hiyo sheria.
Hivyo, Lusifa alikuwa na mojawapo ya nafasi za heshima kubwa mbinguni. Lakini Isaya 14:12 inatuambia kwamba alianguka kutoka mbinguni. Nini kilitokea?
Lusifa aligeukaje kuwa Shetani?

Photo by Jens Lindner on Unsplash
Lusifa alikuwa malaika mkamilifu, lakini aliruhusu kiburi kuingia moyoni mwake. Hii ndiyo asili ya uovu kama tunavyoijua. Alitaka kujikweza juu ya Mungu, na hatimaye, uasi huu ulimfanya awe Shetani (jina linalomaanisha “adui”). Yeye ni adui wa Mungu, ambayo ina maana ya kupigana dhidi ya sheria ya Mungu isiyobadilika ya upendo.
Na alipokuwa duniani, Shetani alimlenga Kristo kwa sababu Aliishika sheria hii na alikuwa na uhusiano wa karibu sana na Mungu Baba.
Kulingana na Ezekieli 28:15, Lusifa alikuwa “mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako” (SUV).
Kwa maana nyingine kutotii ni kuasi dhidi ya Mungu.1
Lusifa alianza kujifikiria sana kuhusu uzuri na cheo chake (Ezekieli 28:17). Hii ilimfanya kutoridhika na kile alichokuwa nacho na kuwa na wivu juu ya nafasi ya Mungu. Tamaa yake ilikuwa hii:
“…..Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, Katika pande za mwisho za kaskazini. Nitapaa kupita vimo vya mawingu, Nitafanana na yeye Aliye juu” (Isaya 14:13-14, SUV).
Kwanini malaika mkamilifu alianza kujisikia hivi?
Hivyo ndivyo Biblia inavyoiita “siri ya kuasi” (2 Wathesalonike 2:7, SUV). Ni jambo ambalo hatuwezi kulielezea.
Ellen G. White—mmoja wa waanzilishi wa Kanisa la Waadventista wa Sabato na mmoja wa waandishi wanawake walioandika sana katika wakati wake—anatoa maoni kuhusu hili katika kitabu chake: Pambano Kuu
“Dhambi ni mvamizi, ambaye hakuna sababu inayoweza kutolewa kwa kuwepo kwake. Ni ya ajabu, haiwezi kuelezeka; kutafutia sababu ni kuitetea. Kama sababu ya kuwepo kwake ingepatikana, au sababu ikaonyeshwa kwa kuwepo kwake, basi isingekuwa tena dhambi. Ufafanuzi wetu pekee wa dhambi ni ule uliotolewa katika neno la Mungu; ni ‘uvunjaji wa sheria’; ni matokeo ya kanuni inayopigana na sheria kuu ya upendo ambayo ndiyo msingi wa serikali ya Mungu.”2
Hivi ndivyo tunavyojua:
Mungu ni upendo—ikimaanisha upendo usio na ubinafsi ndio kiini cha asili Yake (1 Yohana 4:8; 1 Wakorintho 13:4-8). Na kila kipengele cha utawala Wake kimejengwa juu ya aina hii ya upendo. Sheria Yake—iliyodhihirishwa katika Amri Kumi—ina upendo kwa Mungu na upendo kwa wengine kama msingi wake (Kutoka 20:2-17; Mathayo 22:37-40). Hivyo basi, kwa kuwa tabia ya Mungu haibadiliki, sheria Yake ya upendo haiwezi kubadilika pia.
Lakini upendo hauwezi kuwepo bila uchaguzi.
Na pamoja na uchaguzi pia kunakuja uhuru wa kutopenda, kufanya maovu.
Kwa sababu Mungu anajali sana kuhusu uhuru wa kumpenda au kutompenda, aliwapa viumbe Wake wote huo uchaguzi. Kwa bahati mbaya, Lusifa alichagua kutopenda. Alikata shauri kutaka kufanya mambo tofauti na Mungu—kujikuza mwenyewe badala ya kuwa mnyenyekevu.
Na ilikuwa ni uchaguzi huu uliosababisha Lusifa kuwa Shetani—adui wa Mungu na wa njia Yake ya upendo.3 Alimshambulia Mungu kwa kushambulia tabia Yake na sheria ya upendo.
Kwanini Shetani na malaika zake walitupwa kutoka mbinguni?

Photo by Felix Mittermeier on Unsplash
Ingawa uasi wa Lusifa ulianzia moyoni mwake, baada ya muda ukageuka kuwa uasi wa wazi. Alieneza mawazo yake kiasi kwamba malaika wengine walijiunga naye. Biblia inatuambia kwamba “kulikuwa na vita mbinguni” wakati Mikaeli malaika mkuu na malaika zake walipigana na Shetani na malaika zake (Ufunuo 12:7). Kwa sababu kanuni ya kiburi ya Shetani ilikuwa kinyume na roho ya kujitoa ya mbinguni, Mungu alimfukuza yeye na malaika zake.
Yesu Mwenyewe baadaye alisema, “Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme” (Luka 10:18, SUV).
Basi, vita hivi vilikuwa vya aina gani?
Tunapofikiria vita, tunafikiria mapigano kati ya watu wenye silaha wakiwa na AK-47.
Lakini vita vya mbinguni vilikuwa tofauti.
Katika Ufunuo 12, neno la Kigiriki linalotumika kwa ajili ya vita ni polemos (ambapo tunapata neno la Kiingereza polemic). Neno hili linaweza kumaanisha vita vya kimwili, lakini pia linaweza kurejelea mabishano au vita vya maneno na mawazo. Iwapo vita vya mbinguni vilikuwa vya kimwili, hatujui. Lakini tunaweza kuelewa kwamba vilikuwa vita kati ya kanuni zinazopingana—wema dhidi ya uovu, na upendo dhidi ya ubinafsi.
Kwa sababu Shetani na malaika zake walikuwa wakiishi kwa kanuni za uovu, ubinafsi, na kiburi, hawakuweza tena kukaa katika mazingira ambapo thamani kuu zilikuwa wema, upendo, na unyenyekevu. “mahali pao hapakuonekana tena mbinguni” (Ufunuo 12:8, SUV).
Kwa nini Mungu hakumuangamiza Shetani na malaika zake mara moja?
Kwanini Mungu hakumuangamiza Shetani na malaika zake mara moja?
Kama Shetani na malaika zake walikuwa wanaharibu mazingira ya mbinguni, tungefikiri suluhisho rahisi lingekuwa kuwaangamiza kabisa. Lakini kufanya hivyo kungemwonyesha Mungu kama mkatili anayeharibu yeyote anayethubutu kumpinga; kungepingana na tabia Yake ya upendo. Hivyo, Mungu alimpa Shetani muda wa kuonyesha jinsi alivyo kweli. Malaika na watu walihitaji kuona tabia ya Mungu dhidi ya tabia ya Shetani ili waweze kuchagua nani wa kumfuata.
Ili kuelewa kwanini, fikiria kile ambacho kingekuwa kinatokea katika akili za malaika wengine.
Walimpenda na kumheshimu Lusifa kama mmoja wa malaika wa juu kabisa katika ufalme wa Mungu. Alipoanza kueneza uasi wake, angekuwa mjanja, akifanya ionekane kana kwamba anataka mema kwa ajili ya malaika.
Hivyo, kama Mungu angemwangamiza Lusifa mara moja, malaika wengine wangejiuliza, Labda Lusifa alikuwa sahihi baada ya yote!
Wangeweza kuasi pia. Au kama wangeendelea kumtumikia Mungu, wangefanya hivyo kwa hofu badala ya upendo.
Na kumbuka, Mungu anataka ufalme Wake ufanye kazi kwa upendo!
Hivyo, Alijua kwamba ulimwengu ungehitaji muda kuona tofauti kati Yake na Shetani, upendo na ubinafsi. Kila mtu alihitaji kushawishika moyoni mwake. Pia walihitaji nafasi ya kuchagua wenyewe kama watamfuata Mungu au watamfuata Shetani.
Ndiyo maana bado tunaona vita kati ya mema na mabaya vikiendelea leo.
Ellen White anafupisha wazo hili la kibiblia kwa maneno yafuatayo:
“Uovu lazima uruhusiwe kukomaa. Kwa ajili ya mema ya ulimwengu mzima katika enzi zisizo na mwisho, Shetani lazima aendelee kuonyesha kanuni zake, ili mashtaka yake dhidi ya serikali ya Mungu yaonekane katika mwanga wake wa kweli na viumbe vyote vilivyoumbwa, ili haki na rehema ya Mungu na kutobadilika [hali ya kutobadilika] kwa sheria Yake viwekwe milele mbali na mashaka yote.”4
Shetani anapiganaje vita dhidi ya Kristo hapa duniani?

Photo by RDNE Stock project
Wakati Shetani alipotupwa kutoka mbinguni, alitafuta njia nyingine za kumshambulia Kristo. Alianza kwa kuwajaribu Adamu na Hawa na kumchora Mungu kama mwongo Asiyejali (Mwanzo 3:1-5). Kristo alipokuja duniani, alikabiliwa kila mara na mashambulizi na majaribu ya Shetani. Na kwa sababu Shetani alishindwa kumshusha Kristo, anaendelea kujaribu kumuumiza Kristo kwa kuwaumiza watu Wake.
Si ajabu Ufunuo 12:12 inasema, “Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu” (SUV).
Andiko lingine linatuambia kwamba “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze” (1 Petro 5:8, SUV).
Katika Bustani ya Edeni, Shetani (kupitia nyoka) alijaribu kupanda mashaka juu ya tabia ya Mungu katika akili ya Hawa. Alimchora Mungu kama mwongo asiyejali kwa kuwazuia kula tunda la mti wa ujuzi wa mema na mabaya (Mwanzo 3:1-7).
Naye ameendelea kutumia udanganyifu na uongo kuhusu tabia ya Mungu ili kuwageuza watu wamwache Yeye (Yohana 8:44).
Pia amewatesa watu wa Mungu (Ufunuo 12:17) na kusababisha aina zote za maafa—mateso, kifo, na magonjwa (Ayubu 1-3).
Hapa kuna mifano michache ya jinsi ambavyo mambo haya yamejitokeza katika historia:
- Shetani aliwaongoza watu kabla ya gharika kuingia katika giza na uovu (Mwanzo 6:5-6).
- Katika wakati wa waamuzi na wafalme wa Israeli, Shetani alijaribu kuwageuza watu wa Mungu wamwache Yeye na waabudu sanamu (Waamuzi 2:11-19).
- Shetani alimlenga Yesu alipokuwa duniani lakini alishindwa kumfanya aanguke. (Tazama sehemu inayofuata kwa maelezo zaidi kuhusu hili.)
- Katika kipindi cha kanisa la kwanza la Kikristo, Shetani alitumia mateso kujaribu kudhoofisha ushawishi wa wafuasi wa Mungu (Matendo 7:59; 8:1).
- Mateso yalipungua wakati wa Zama za Giza, lakini Shetani aliwaongoza wengi kanisani kushusha viwango vya imani yao badala yake. Wengi walipoteza mtazamo wa kanuni zisizopitwa na wakati za Biblia, na ni kundi dogo tu la watu lilibaki waaminifu kwa Mungu.
- Wakati wa Matengenezo ya Kiprotestanti, wanamatengenezo wakuu—kama vile John Wycliffe, Huss na Jerome, na Martin Luther—walifichua kweli zilizokuwa zimesahaulika kupitia kujifunza Biblia. Hili lilipotokea, Shetani alifufua mateso dhidi ya watu wa Mungu.5
- Katika nyakati za mwisho, Shetani atapigana vita dhidi ya wale “wazishikao amri za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa Yesu” (Ufunuo 12:17, SUV).
Kama Mungu angezuia mambo mabaya ambayo Shetani anatamani kufanya, Shetani angesema “sio haki” na kudai kwamba Mungu anaogopa kumruhusu atekeleze namna yake ya utawala.
Hivyo, kwa kiwango fulani, Mungu lazima amruhusu Shetani aonyeshe njia yake ya kutawala. Matokeo yake ni huzuni na maumivu duniani leo.
Lakini kwa neema ya Mungu, hatamruhusu Shetani kufanya kazi yake chafu milele.
Je, vita kati ya Kristo na Shetani itakuwaje mwisho wake?

Photo by Ricardo Gomez Angel on Unsplash
Ingawa Shetani amefanya bidii kusababisha uovu na mateso katika dunia yetu, hajafanikiwa katika vita yake dhidi ya Kristo. Kristo alipokuwa duniani, alishinda, akitupatia uhakika kwamba Shetani atapata mwisho wake katika ziwa la moto.
Kristo alipokuja duniani, lengo lake lilikuwa kuharibu nguvu za Shetani (Waebrania 2:14; 1 Yohana 3:8) na kuwaweka huru wale “walioonewa na Ibilisi” (Matendo 10:38, SUV). Shetani alikuwa ameshambulia tabia isiyobadilika ya Mungu na sheria ya upendo, lakini Yesu alikuja kuthibitisha na kuishi sheria hiyo (Mathayo 5:17-18). Aliishi maisha kamilifu—bila dhambi—kisha akafa msalabani, akichukua adhabu ya wanadamu kwa kuvunja sheria ya Mungu.
Ilikuwa ni mapambano ya uchungu kwa Kristo kwa sababu Shetani alimshambulia na kumjaribu katika kila jambo tunalojaribiwa sisi (Waebrania 4:15). Lakini Yesu alishinda kwa sababu alikataa kuachana na Baba yake wa mbinguni (Mathayo 4:1-11).
Angalia jinsi 1 Petro 2:21-24 inavyoelezea:
“Kwa sababu ndio mlioitiwa; maana Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akawaachia kielelezo, mfuate nyayo zake. Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake. Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa, hakuogofya; bali alijikabidhi kwake yeye ahukumuye kwa haki. Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa” (SUV, msisitizo umeongezwa).
Msalabani, Alitoa onyesho kuu la upendo wa Mungu kwa kujitoa maisha Yake. Alipopaza sauti, “Imekwisha” (Yohana 19:30, SUV), ushindi dhidi ya Shetani ulikuwa umekamilika.
Ushindi wa Yesu unatupatia sisi pia ushindi dhidi ya Shetani.
Ufunuo 12:10-11 unaeleza hivi:
“Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku. Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa” (SUV).
Yesu, kwa kifo chake, aliharibu nguvu za ibilisi na kutabiri mwisho wake hatimaye.
Mwisho wa dunia hii, wakati wote watakaposhawishika juu ya wema wa utawala wa Mungu, Shetani mwenyewe atakufa katika ziwa la moto lililoandaliwa kwa ajili yake na malaika zake (Mathayo 25:41, Ufunuo 20:10).
Uovu, mateso, na kifo vitaondoka milele, na tutaishi katika dunia mpya itakayokuwa chini ya sheria ya upendo ya Mungu.
Ufalme wa upendo utashinda

Photo by Emmanuel Phaeton on Unsplash
Tangu Shetani alipoanguka duniani, dunia yetu imezidi kuwa mbaya zaidi. Kwenye habari, tunasikia hadithi za mauaji, unyanyasaji, na vita. Maumivu na uovu pia vinatusumbua: saratani isiyotibika, talaka mbaya, kifo cha mtoto…
Sasa tunaelewa mahali vita hii kati ya mema na mabaya—Kristo na Shetani—ilipoanzia. Shetani, adui wa Mungu, hataki kitu kingine zaidi ya kuleta uharibifu.
Na pia tunajua jinsi itakavyomalizika.
Ingawa hatuelewi kikamilifu kwanini Lusifa alichagua njia ya uasi aliyoichukua, bado tunaweza kuona jinsi Mungu alivyo upendo, na jinsi upendo huo ulivyo, kwa asili yake, hauna masharti. Amefuata mpango bora kabisa wa kuhifadhi uhuru wa kuchagua na kumaliza dhambi—mpango uliomhusisha Yesu Kristo kufa ili achukue dhambi zetu juu Yake na kutuonyesha jinsi upendo wa kujitoa unaweza kwenda mbali kiasi gani.
Na kwa sababu ya dhabihu Yake, haitachukua muda mrefu kabla Shetani hajakutana na mwisho wake.
Kisha, baada ya Pambano Kuu kuisha, tutaweza kuishi milele katika ufalme mkamilifu wa upendo, mbele za Mungu, hatimaye tukipata kile ambacho tumekuwa tukikitamani sana ndani kabisa ya mioyo yetu.
Chagua Masomo ya Biblia Mtandaoni
Unataka kuendelea kujifunza? Pata habari zaidi kuhusu Yesu, mwanadamu, mpango wa wokovu, na jinsi Mungu anavyokupenda kiasi cha kutosha kujitolea kila kitu, ili tu kukupatia nafasi ya kumchagua.
Wakati mwingine inaweza kuwa ngumu kujua pa kuanzia, ndio maana tunatoa chaguo za masomo ya Biblia mtandaoni bure, rahisi kutumia, unaweza kufanya wakati wowote, mahali popote, na kwa kasi yako mwenyewe.
Shule hii ya Biblia mtandaoni itakuelekeza kupitia mada kuu za Maandiko, ikivunja dhana ngumu za Biblia katika vipande vidogo, ambavyo vinaweza kukusaidia kupata majibu ya maswali magumu zaidi ya maisha.
Makala Zinazohusiana
- “Iniquity,” Gesenius’ Hebrew-Chaldee Lexicon. [↵]
- White, Ellen, The Great Controversy (Pacific Press, Mountain View, CA, 1911), p. 492. [↵]
- Strong’s Concordance[↵]
- White, The Great Controversy, p. 498. [↵]
- The History of Protestantism, volumes 1-4, by James Wylie, is an in-depth look at the Protestant Reformation and the persecution that happened during that time. [↵]
Majibu Zaidi
Je, Yesu Ndiye Njia Pekee ya Kwenda Mbinguni?
Biblia inaposema Yesu ndiye njia pekee ya kwenda mbinguni, inamaanisha nini? Ukurasa huu unachunguza vifungu muhimu vya Biblia ili kupata picha iliyo wazi ya tamanio la Mungu kutuokoa.
Dhambi ni Nini?
Dhambi ni Nini?Ingawa hili linaweza kuonekana kama swali gumu, kuna njia rahisi ya kulielewa. Dhambi ni kushindwa kumpenda Mungu na kuwapenda wengine. Ni kinyume cha upendo. Hii ndiyo maana Biblia inafafanua dhambi kama uasi wa sheria, au kuvunja sheria ya Mungu (1...
“Nenda Usitende Dhambi Tena”—Yesu Alimaanisha Nini?
“Nenda Usitende Dhambi Tena”—Yesu Alimaanisha Nini?Maneno haya yanayojulikana ya Yesu Kristo yanatoka katika hadithi mbili za Agano Jipya katika kitabu cha Yohana—mtu aliyeponywa kwenye birika la Bethesda (Yohana 5) na mwanamke aliyekamatwa katika uzinzi (Yohana 8)....
Kwa Nini kuna Wema na Uovu Duniani?
Kwa Nini kuna Wema na Uovu Duniani?Asili ya binadamu inaweza kufanya matendo ya kujitoa mhanga na ya shujaa zaidi—askari akitoa maisha yake kwa ajili ya nchi yake, mama kulinda watoto wake dhidi ya madhara, mtu kuruka ndani ya maji mengi yaendayo kasi kwa ajili...
Imani na Matendo – Je! Yote Ni Muhimu katika Maisha ya Mkristo?
Katika dini nyingi katika nyakati zote, watu hufanya kazi kuelekea ufahamu, wokovu, au kibali kutoka kwa mungu.
Kile Unachohitaji Kujua Kuhusu Majaribu na Jinsi ya Kuyapinga
Unajiuliza jinsi ya kupinga majaribu na kutoka kwenye mzunguko wa kushindwa? Yesu hutupa tumaini na kielelezo cha kukabiliana na majaribu ya shetani. Soma zaidi hapa!
Uhalisi wa Kisheria katika Biblia: Maana, Hatari, na Mifano
Gundua kile Biblia inachosema kuhusu uhalisi wa kisheria, kwanini ni hatari na namna tunavyoweza kuepuka leo.
Kila Kitu Kuhusu Agano la Kale na Jipya katika Biblia
Kila Kitu Kuhusu Agano la Kale na Jipya katika Biblia“Agano" ni mada iliyoenea kote katika Biblia. Wakristo mara nyingi hutofautisha agano la kale na jipya wanapoyazungumzia, lakini kwa kweli, Maandiko yanarejelea hatua au kufanywa upya tofauti wa agano moja. Ndiyo...











