Ellen White Alifundisha nini Kuhusu Matumizi ya Vyakula Vinavyotokana na Mimea?

Moja ya mambo ambayo unaweza kuwa umewahi kusikia kuhusu Waadventista wa Sabato ni msisitizo wao kwenye mtindo wa maisha wa kutumia vyakula vinavyotokana na mimea. Ikiwa unajiuliza kwa nini iko hivyo, inaanzia katika chanzo cha unyenyekevu cha kanisa letu:

Waadventista walipojifunza Biblia, walihisi jinsi wangeweza kumtukuza Mungu kwa kuitunza miili yao na akili zao. Kwa upande wake, Roho Mtakatifu alimwongoza Ellen G. White, kiongozi katika Kanisa la Waadventista Wa Sabato, kushiriki kanuni za kivitendo za afya, ikiwa ni pamoja na matumizi ya vyakula vinavyotokana na mimea.

Ingawa kamwe hajawahi kusema kuwa kula nyama ni dhambi, aliwahimiza watu kuchagua lishe inayotokana na mimea kwa kiasi kikubwa . Kwa njia hii, wangeweza kuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kupata afya bora kabisa na kumtumikia Mungu kwa uwezo wao wa juu zaidi.

Tuangalie kwa undani zaidi kile alichokuwa akisema kwa kuangalia:

Tukielewa safari yake binafsi ya kula vyakula vinavyotokana na mimea, tutauona uhusiano wake na mtazamo wenye usawa kuhusu mada hii.

Ni nini kilikuwa uzoefu wa Ellen White katika kuwa mtumiaji wa vyakula vinavyotokana na mimea?

Ellen White alibadilika kutoka kula nyama sana hadi kuwa mtumiaji wa maziwa na mayai kwa kipindi cha miaka takriban 31. Wakati huo huo, alipita kutoka katika udhaifu na maradhi akiwa kijana hadi kuwa na nguvu na afya njema katika miaka yake ya baadaye. Mungu alimwongoza hatua kwa hatua katika kuboresha lishe yake na kufurahia baraka zake.

Yote haya yalianza kwa maono aliyopokea mwaka 1863.

Maono ya Ellen White kuhusu afya

A drawing of Ellen White smiling and raising her arms as she experiences a vision.

Courtesy of the Ellen G. White Estate, Inc.

Mnamo Juni 6, 1863, Ellen White alipokea maono yake makubwa ya kwanza kuhusu matengezo ya afya kutoka kwa Mungu, na ilimpelekea kubadilisha namna aliyokuwa akila.

Hapa kuna baadhi ya dondoo ya lishe kuhusu kile alichojifunza kupitia maono hayo:

“Mungu aliwapa wazazi wetu wa kwanza chakula alichokusudia kizazi chetu kitumie. Ilikuwa kinyume na mpango wake kuua kiumbe chochote. Haikupaswa kuwe na kifo katika Edeni… [Yeye] hakumpa mwanadamu ruhusa ya kula chakula cha wanyama [nyama] hadi baada ya gharika. Kila kitu kilikuwa kimeharibiwa ambacho mwanadamu angeweza kuishi kwacho, na hivyo Bwana katika hali yao ya dharura alimpa Nuhu ruhusa ya kula wanyama safi alioingia nao ndani ya safina. Lakini chakula cha wanyama hakikuwa chakula bora zaidi kwa afya ya mwanadamu.”1

 

“Kuna wanyama wachache tu ambao hawana magonjwa.”2

Mpango wa awali wa Mungu kwa wanadamu ulikuwa lishe inayotokana na mimea. Lakini baada ya gharika, Aliwaruhusu watu kula nyama kwa kuwa mimea haikuwepo. Na watu wengi katika Biblia (ikiwa ni pamoja na Yesu) walikula nyama.

Hata hivyo, kutokana na kuongezeka kwa magonjwa kwa wanyama na mazoea mabaya ya usindikaji wa nyama, wakati wa Ellen White nyama iliendelea kupungua usalama kidogo kidogo kwa matumizi ya kiafya ya chakula.

Kwa sababu hiyo, aliwahimiza watu warudi kwenye “lishe ya kawaida na yenye afya” ili waweze kuweka mwili katika “hali yenye afya kadri iwezekanavyo.”3

Maono haya yalikuwa mwanzo wa safari ya Ellen White kuelekea afya bora.

Safari ya kuwa mtumiaji wa Vyakula vinavyotokana na mimea

Baada ya maono mwaka wa 1863, Ellen White alianza kufanya mabadiliko kwenye mazoea yake ya maisha, ikiwa ni pamoja na lishe yake. Aliamua kuepuka nyama—iliyokuwa changamoto kubwa kwake.

Wakati ambapo vyakula safi vilikuwa havipatikani kila wakati, alikuwa akitegemea nyama. (Huenda alikuwa mchaguzi wa chakula kidogo, pia.) Hivyo, kwa kusita kidogo, alianza kula mkate wa nafaka nzima, matunda, na mboga. Hivi ndivyo anavyoelezea:

“Kwa muda fulani ilikuwa ngumu kidogo kupata hamu ya kula mkate, ambao, hapo awali, sikuwa na hamu sana. Lakini kwa kuvumilia, nimefanikiwa kufanya hivi. Nimeishi kwa karibu mwaka mmoja bila nyama.”4

Na matokeo yakamshangaza.

Alijua alihitaji nyama ili kupata nguvu, lakini aligundua kuwa kizunguzungu na udhaifu wake ulipotea alipoacha kula nyama.5

Na hivyo, aliendelea kufanya hivyo.6

Lakini Ellen White alikuwa na usawa. Kamwe hakuchukulia kula nyama kama dhambi na alifanya mabadiliko katika hali kama ifuatavyo:

  • Wakati mboga zilikuwa ghali sana. Mwaka wa 1878, alikula nyama ya paa katika kifungua kinywa cha Krismasi alichoshiriki na familia iliyokuwa maskini sana.7
  • Alipokuwa safarini na hakuweza kupata chakula kinachotokana na mimea. Mwaka wa 1890, alisema, “Niliposhindwa kupata chakula nilichohitaji, mara nyingine nilikula kiasi kidogo cha nyama.”8
  • Wakati wapishi wake walipokuwa bado wanajifunza kupika chakula kinachotokana na mimea. Kwa sababu ya jinsi huduma ya Ellen White ilivyomshughulisha, aliajiri wapishi nyumbani kwake. Lakini kila wakati wapishi wapya walipofika, hawakuwa na uzoefu wa kupika chakula kinachotokana na mimea. Hii ilimaanisha kwamba wangeweza kupika nyama hadi alipokuwa na muda wa kuwafundisha mapishi ya chakula kinachotokana na mimea.9

Mwaka wa 1894, alifanya uamuzi wa kuacha kula nyama katika hali zote. Mbali na wasiwasi wake kuhusu magonjwa, pia alikuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu ukatili ambao wanyama walipitia katika viwanda vya usindikaji wa nyama.

Aliendelea kula samaki kwa miaka michache zaidi, lakini alianza kuwa na wasiwasi zaidi kuhusu usalama wake wa kiafya pia:

“Katika maeneo mengi samaki wameathiriwa sana na uchafu wanaolishwa hivyo kuwa chanzo cha magonjwa.”10

Ellen White alipofikia mwisho wa maisha yake, alitazama jinsi afya yake ilivyo badilika katika miaka iliyopita:

“Nina afya bora leo, ingawa nina miaka sabini na sita, kuliko nilivyo kuwa katika siku zangu za ujana. Namshukuru Mungu kwa kanuni za matengenezo ya afya.”11

Aliishi yale aliyofundisha na kuonyesha faida zake. Hebu tutazame mafundisho hayo sasa.

Ellen White alisema nini kuhusu matumizi ya chakula kinachotokana na mimea?

Ellen White alihamasisha lishe itokanayo na mimea kupitia mafundisho yake na maandishi. Ingawa kamwe hakusisitiza mambo ya kupindukia wala hakufanya iwe swala la wokovu au ushirika wa kanisa, alionyesha jinsi lishe inayozingatia vyakula vinavyotokana na mimea inavyoweza kuboresha maisha yetu.

“[Vyakula vya mimea] huleta nguvu, uwezo wa kustahimili, na nguvu ya akili, ambayo haipatikani kwa lishe tata na inayosisimua zaidi,” alisema.12

Tafsiri ya Ellen White juu ya Matumizi ya vyakula vinavyotokana na Mimea

Watu wengi wanafikiri kuwa mtumiaji wa vyakula vinavyotokana na mimea kunamaanisha kuondoa kabisa nyama yote katika lishe. Na leo, hiyo inaweza kuwa kweli. Lakini Ellen White alitumia neno hilo kwa upana zaidi akimaanisha kutumia kwa kiasi kikubwa zaidi lishe inayotokana na mimea. Ni matumizi ya chakula kinachotokana na mimea kwa sababu vyakula hivyo vinakuwa kiini cha lishe, badala ya lishe yenye nyama zaidi (ambayo ilikuwa imezoeleka zaidi wakati huo).

Katika barua kuhusu mtazamo wa Kanisa la Waadventista Wa Sabato kuhusu mada mbalimbali, aliandika, “Wote ni watumiaji wa vyakula vinavyotokana na mimea, wengi wakiepuka kabisa matumizi ya nyama, wakati wengine wakitumia kwa kiwango cha chini kabisa.”13

Kwake, kuwa mtumiaji wa vyakula vinavyotokana na mimea kunaweza maanisha kutokula nyama kabisa au kula nyama mara chache tu. Lakini kwa njia yoyote ile, ilikuwa ni uamuzi wa kwenda kuelekea chakula cha awali:

“Nafaka, matunda, karanga, na mboga zinaunda chakula kilichochaguliwa kwa ajili yetu na Muumba wetu. Vyakula hivi, vikitayarishwa kwa njia rahisi na asilia iwezekanavyo, ni vyakula bora zaidi kwa afya na ustawi.”14

Mamlaka nyingi za afya leo zinakubaliana na hilo. Dkt. Michael Greger—mhitimu wa Chuo Kikuu cha Cornell, daktari, mzungumzaji, na mwandishi—ni mmoja wao. Aliulizwa katika mahojiano, “Ni lishe ipi bora kwa kuishi maisha marefu na yenye afya?”

Jibu lake:

“Chakula kilichojikita katika mimea nzima, ikiwa ni pamoja na aina mbalimbali za nafaka nzima, maharage, matunda, karanga, na mboga nyingi tunazoweza kujaza vinywa vyetu.”15

Mwandishi habari wa New York Times na mwandishi Michael Pollan anahitimisha hivi:

“Kula chakula. Sio kingi. Hasa mimea.”16

Athari za nyama kwa afya

Moja ya sababu muhimu ya Ellen White kukataza lishe nzito ya nyama ni kwamba wanyama wamekuwa wagonjwa zaidi karne hizi. Alikuwa na wasiwasi kuhusu magonjwa kwa wanyama na jinsi yanavyoweza kuathiri binadamu.17

Mwaka wa 1905, aliandika:

“Saratani, uvimbe, na magonjwa yote ya kuvimba kwa kiasi kikubwa husababishwa na kula nyama.”18

 

“Nyama kamwe haijawahi kuwa chakula bora; lakini matumizi yake sasa ni hatari zaidi, kwa sababu magonjwa kwa wanyama yanazidi kuongezeka haraka.”19

Na zaidi ya miaka 100 baadaye, ulimwengu wa matibabu unakubaliana na hilo. Kliniki ya Mayo inasema kwamba nyama nyekundu na iliyosindikwa inaongeza “hatari ya vifo vinavyotokana na ugonjwa wa moyo, kiharusi, au kisukari”—magonjwa yote ya kuvimba yanayoweza kuathiriwa na mtindo wa maisha.

Shirika la Afya Duniani pia limetangaza kwamba nyama nyekundu na zilizosindikwa ni visababishi vya saratani. Zinaweza kusababisha saratani ya tumbo na utumbo mpana, na labda saratani ya kongosho na tezi dume.

Katika wakati ambapo watu hawakujua mengi kuhusu saratani, maandishi ya Ellen White yalikuwa sahihi.

Umuhimu wa lishe yenye virutubisho vya kutosha

Hata Ellen White alipendeleza lishe inayotokana na mimea, aliona ni mchakato badala ya uamuzi wa mara moja. Watu wako tofauti na wanapaswa kubuni lishe zao ili kuhakikisha wanapata lishe sahihi. Lishe yetu ni “kwa ajili ya kujenga mwili…kutunza kila uwezo katika hali bora kwa huduma ya juu kwa Mungu na mwanadamu.”20

Akizingatia hili, alisisitiza umuhimu wa kupata mbadala sahihi wa nyama kabla ya kuacha kabisa. Alisisitiza hasa kubadilisha nyama na nafaka nyingi, matunda, karanga, na mboga. Kufanya hivyo kutazuia mapungufu ya lishe.21 Leo, tungeongeza pia thamani ya kula mikunde (maharage, dengu) ili kupata protini tunayoweza kupata kwenye nyama.

Mtazamo wake ulio na usawa

Ellen White alikuwa na mtazamo wa usawa sana kuhusu afya, akiwatia moyo watu kufanya wanavyoweza katika hali walizo kuwemo. Kamwe hakufanya maisha yake kuwa kigezo kwa wengine kuiga.22 Badala yake, aliwashauri kuepuka upande mmoja, kusoma mapenzi ya Mungu, na kugundua kilichokuwa bora kwa afya yao.23

Pia hajawahi kusema kwamba ili mtu awe mwadventista au aokolewe sharti awe mtumiaji wa chakula kinachotokana na mimea.24

“Sijawahi kuhisi kwamba ilikuwa wajibu wangu kusema kwamba mtu hapaswi kula nyama katika hali yoyote. Kusema hivi wakati watu wameelimishwa kuishi kwa kutegemea nyama kwa kiasi kikubwa ingekuwa kukuza mambo kwa kiasi kikubwa. Sijawahi kuhisi kwamba ilikuwa wajibu wangu kufanya madai makubwa. Nilichosema nimesema chini ya hisia ya wajibu, lakini nimekuwa mwangalifu katika kauli zangu, kwa sababu sikutaka kutoa sababu kwa yeyote kuwa dhamiri kwa mwingine.”25

Katika hali ambapo watu hawangeweza kumudu kubadilisha nyama kwenye meza zao au hawakupata chakula mbadala, aliandika:

“Haikuwa wajibu wangu, wala sikufikiria ilikuwa wajibu wa mtu mwingine yeyote, kuwapa mihadhara kuhusu madhara ya kula nyama…. Kuna wakati wa kusema na wakati wa kukaa kimya.”26

Mafundisho ya Ellen White kuhusu chakula kinachotokana na mimea yanavyo hamasisha Kanisa la Waadventista wa Sabato

Mafundisho ya Ellen White kuhusu matumizi ya chakula kinachotokana na mimea yalikuwa na athari kubwa katika Kanisa la Waadventista wa Sabato. Idadi kubwa ya Waadventista wanatumia lishe inayotegemea mimea na kiasi kidogo cha nyama, na wengi hawatumii nyama nyekundu au kuku kabisa. Waadventista pia wamechapisha machapisho mengi kuhusu matumizi ya chakula kinachotokana na mimea, kujaribu mapishi yasiyo na nyama, na kutengeneza na kuuza mbadala wa nyama.

Kukubalika kwa lishe inayotokana na mimea

A doctor takes a woman's blood pressure, illustrating how lower blood pressure is one of the benefits of the vegetarian diet.

Photo by Gustavo Fring

Namna Waadventista wanavyokula leo ni kwa njia nyingi matokeo ya matumizi kanuni ya kibiblia ya kumtukuza Mungu kwa miili yetu katika maisha ya Ellen White (1 Wakorintho 6:19–20; 1 Wakorintho 10:31). Alifundisha kwamba chakula na hali ya kiroho mara nyingi zinaweza kuwa na uhusiano—kile tunachokula kinaweza kuathiri uwezo wetu wa kuishi kwa ajili ya Mungu.

Hivyo, bado tunafuata kanuni hizi za kula kiafya.

Na leo, Utafiti wa kiadventista Kuhusu Afya -2 uliofanywa na Chuo Kikuu cha Loma Linda unathibitisha faida nyingi za kutumia chakula kinachotokana na mimea. Wale wanaokula njia hii kwa kawaida hupata faida zifuatazo ikilinganishwa na wale wanaokula nyama:

  • Kiwango cha chini cha cholesterol
  • Kiwango cha chini ya shinikizo la damu
  • Hatari ndogo ya kisukari na syndrome ya kimetaboliki
  • Hatari ndogo ya aina za saratani
  • Kiwango cha chini ya BMI

Kama ilivyokuwa katika safari ya Ellen White mwenyewe, mabadiliko katika Kanisa yalikuwa mchakato uliotokea polepole. Kila mtu lazima apitie mchakato wanapofanya mabadiliko ya lishe pia. Hivyo, utumiaji wa chakula kinachotokana na mimea ni uamuzi binafsi badala ya kipimo cha kuwa Mwadventista.

Ikiwa ungependa kujifunza jinsi ya kula chakula kinachotokana na mimea, angalia nyenzo zifuatazo:

Vitabu

Ellen White aliandika mengi kuhusu lishe na mtindo wa maisha. Konferensi Kuu ya Kanisa la Waadventista wa Sabato ilisambaza maandishi haya kwa washiriki wa kanisa.27

Vipeperushi na vitabu alivyoandika ni pamoja na:

  • Wito kwa Mama (1864)
  • “Afya,” Karama za Roho, kitabu cha 4a (1864)
  • “Ugonjwa na Sababu Zake” katika kitabu Afya, au Jinsi ya Kuishi (1865)
  • Kiasi katika Ukristo na Afya ya Biblia (1890)
  • Huduma Uponyaji (1905)

Watu wengine pia walianza kuandika kuhusu uzoefu wao katika kubadilisha chakula. Ushuhuda huu katika machapisho ya Kanisa uliwahamasisha watu zaidi kuwa watumiaji wa vyakula vinavyotokana na mimea.28

Mapishi mapya na tasnia ya chakula kinachotokana na mimea.

A portrait of John Harvey Kellog, whose efforts played a key role in diet during the health reform.

Courtesy of the Ellen G. White Estate, Inc.

Kadiri ya Waadventista walivyoacha nyama, waliona haja ya kufundisha watu jinsi ya kupika bila nyama. Katika karne ya kumi na tisa, Waadventista walikuwa waanzilishi katika tasnia ya vyakula vya afya walipokuja na mapishi yanayochukua nafasi ya nyama.29

John Harvey Kellogg, ambaye alikuwa akisimamia kituo cha afya cha Waadventista kilichoitwa Battle Creek Sanitarium, alizingatia ushauri wa lishe wa Ellen White. Yeye na ndugu yake William walianza kutumia chakula kinachotokana na mimea katika sanitariamu na kutengeneza na kuuza bidhaa za chakula.

Kwa kweli, wawili hao walikuja na zaidi ya mapishi 80 ya chakula kinachotokana na mimea. Pia walitengenza nafaka za kifungua kinywa ili kuchukua nafasi ya kifungua kinywa cha kawaida cha mayai na nyama kinacholiwa na Wamarekani wengi.30

Jaribio lao liliwapelekea kufungua Kampuni ya Chakula ya Sanitas. Kutoka hapo, walitayarisha chakula kwa wagonjwa katika Sanitarium ya Battle Creek. Mmoja wa ndugu wa Kellogg pia alitengeneza baadhi ya mbadala wa nyama kutoka kwa njugu.

Mbadala huu wa nyama ulipata umaarufu sana ndani ya taasisi za Kanisa la Waadventista —kama vile Worthington Foods na Loma Linda ya Atlantic Natural Foods.

Kanisa la Waadventista hatimaye liliachana na Kellogg kutokana na mabadiliko yake ya kuelekea upande wa itikadi kali katika maeneo kadhaa. Lakini mchango wake katika juhudi za mageuzi ya afya ya Waadventista ulikuwa wa kipekee na uliweka msingi kwa maendeleo mengi zaidi katika maeneo ya lishe na chakula kinachotokana na mimea.

Mafundisho ya Ellen White kuhusu chakula kinachotokana na mimea yanaendelea kuishi.

Mafundisho ya Ellen White kuhusu chakula kinachotokana na mimea labda yalionekana kuwa ya ajabu wakati nyama ilipokuwa ni sehemu muhimu ya chakula. Lakini Mungu alipompa hekima, alishiriki kanuni zilizokuwa zimejengwa katika kanuni za Biblia na kuepuka matatizo na matumizi yaliyo kithiri ya wakati wake.

Leo, Waadventista bado wanathamini sana ushauri wake katika eneo hili. Mafunuo yake ya kiroho na mwongozo wa kawaida uliowasilishwa kuhusu matumizi ya chakula kinachotokana na mimea kama baraka kwa afya na njia ya kumtumikia Mungu na wengine.

Unataka kujifunza zaidi kuhusu jinsi Waadventista wanavyokula?

Kurasa Zinazohusiana

  1. White, Ellen, Spiritual Gifts, vol. 4a (Seventh-day Adventist Publishing Association, Battle Creek, MI, 1864), p. 120. []
  2. Ibid, p. 146. []
  3. Ibid., pp. 132, 148. []
  4. Ibid., p. 153. []
  5. Ibid., p. 153. []
  6. White, Ellen, Counsels of Diet and Foods (Review and Herald, Washington, D.C., 1938), pp. 484, 486. []
  7. White, Ellen, Letter 63, 1878. []
  8.  White, Counsels of Diet and Foods, p. 394. []
  9. Ibid., p. 487. []
  10.  White, Letter 128, 1896. []
  11. White, Ellen, The Ministry of Healing (Pacific Press, Mountain View, CA, 1905), pp. 314, 315. []
  12. White, Counsels of Diet and Foods, p. 482. []
  13. White, The Ministry of Healing, p. 296. []
  14. White, Letter 99, 1894. []
  15. White, The Ministry of Healing, p. 296. []
  16. How Not to Die: 9 Questions for Michael Greger, MD,” Blue Zones. []
  17. Pollan, Michael, In Defense of Food (The Penguin Press, New York, 2008), p. 1. []
  18. White, Ellen, Selected Messages, book 2 (Review and Herald: Washington D.C., 1958), p. 418. []
  19. White, Counsels on Diet and Foods, p. 388. []
  20. White, The Ministry of Healing, p. 313. []
  21. Ibid., p. 319. []
  22. White, Counsels on Diet and Foods, p. 398. []
  23. White, The Ministry of Healing, p. 319. []
  24. White, Ellen, Testimonies for the Church, vol. 9 (Pacific Press, Mountain View, CA, 1909), p. 159. []
  25. White, Letter 76, 1895. []
  26.  Ibid. []
  27. Robinson, Doris, The Story of Our Health Message (Southern Publishing Association, Nashville, TN, 1965), p. 90. []
  28. Ibid., p. 96. []
  29. Ibid., p. 108. []
  30. Banta, et al., “The Global Influence of the Seventh-day Adventist Church on Diet,” Religions, 9(9), August 22, 2018. []

Je, Una swali kuhusu Waadventista? Uliza hapa!

Pata majibu kwa maswali yako kuhusu Waadventista Wasabato

Majibu Zaidi