Je, Ni Kawaida Wakristo Kuwa na Mashaka?
Ndio, ni kawaida kabisa kwa Wakristo kupitia vipindi vya mashaka katika maisha yao ya kiroho.
Kila mtu ameshawahi kuwa na mashaka wakati mmoja au mwingine, hata wachungaji, wanatheolojia, na watu muhimu katika Biblia. Mashaka hayaonekani kama jambo zuri, lakini sio ishara ya udhaifu. Sio kitu cha kutufanya tujisikie aibu.
Na sio dhambi.
Mashaka kimsingi yana kusudi. Inamaanisha haupokei imani kama kipofu – unazichunguza, kuzifikiria, na kuzikosoa, ambayo mwishowe inaweza kufanya imani yako kuwa imara zaidi.
Ni jinsi tunavyoshughulikia mashaka hiyo ndio muhimu.
Tutazungumzia mambo haya yote ili kuelewa zaidi kuhusu mashaka na mwitikio wetu unavyopaswa kuwa:
- Maana halisi ya “mashaka”
- Mashaka kama uzoefu wa kawaida
- Kile kinachoweza kusababisha mashaka
- Wakati mashaka yanapokuwa jambo la kuhofia
- Jinsi tunavyoweza kuitikia mashaka yetu
Hebu tuanze na ufafanuzi.
Maana halisi ya “mashaka”
Mashaka katika maana ya kiroho ni “kutetemeka au kutikisika katika maoni; kusita; kuwa kwenye hali ya sintofahamu; kuwa bila uhakika, kuhusu ukweli au uhalisia; kutokuwa na maamuzi.”1
Kimsingi, mashaka humaanisha kuwa tunasita. Ni ishara kwamba labda hatuko tayari kujitosa kabisa katika mafundisho, imani, au mtazamo tofauti. Tunataka kuyatathmini kwanza.
Hii inaweza kuonekana kama hali isiyoridhisha kuwemo, lakini sio sababu ya kujilaumu.
Kuwa na mashaka ni sehemu muhimu ya imani yetu. Roger W. Coon, PhD, anabainisha,
“Inaonekana wazi kwamba kama Mungu angeondoa kabisa fursa au sababu yoyote ya sisi kuwa na mashaka, Angeondoa pia, kwa wakati mmoja, fursa yote ya kutumia imani!” (msisitizo umeongezwa).2
Mashaka ni sehemu ya mchakato wa kujenga imani. Ikiwa hatuna shaka—au fursa ya kuhoji imani zetu—imani zetu zinakuwa dhaifu na zisizo na msingi imara. Hatuna msingi wa kuzitetea, hata kwetu wenyewe.
Yanaweza kutuonyesha ni wapi msingi unaweza kuwa unakosekana katika mfumo wetu wa imani.
Mashaka pia yanatambuliwa katika saikolojia. Carl Jung alisema, “mashaka na kutokuwa na uhakika ni sehemu muhimu ya maisha kamili.”3
Hivyo, mashaka sio adui. Na hatuhitaji kupingana na mashaka.
Pia ni muhimu kuelewa kwamba kuwa na mashaka haimaanishi kuwa tumepoteza imani yetu.
Tim Mackie, PhD, mwanzilishi wa Mradi wa Biblia, anatukumbusha kuwa mashaka ni “kukutana na kutathmini mifumo tofauti ya imani. Ni imani dhidi ya imani, sio imani dhidi ya kutokuamini.”4
Haimaanishi kupoteza imani yako; inamaanisha kuchunguza na kufurahia imani nyingine tofauti na kuzilinganisha na ukweli unaopatikana katika Biblia.
Kuwa na mashaka huku ukiwa na imani ni jambo linalowezekana. Mtu mmoja katika Biblia, aliyehitaji uponyaji kwa mtoto wake, alipaza sauti kwa Yesu, “Naamini, nisaidie kutokuamini kwangu.” (Marko 9:24, NKJV). Hakuwa akikata tamaa au hata kuruhusu mashaka yake kumzuia kuchukua hatua ya imani. Alikuwa akikiri kwa Yesu alipo katika imani yake. Hii ni aina ya mashaka na ni sawa kabisa.
Wakati mwingine tunaweza kuhitaji kuweka kando imani zetu ili kuona pale zinapohitaji kufanyiwa tathmini au kukuzwa zaidi.
Hapa ndipo mashaka yanajukumu na yana kazi.
Mashaka yana kusudi
Kuwa na mashaka kunaweza kutuonyesha wapi imani zetu zinaweza kuwa dhaifu au zisizo sahihi. Au, inaweza hata kutuonyesha jinsi imani ilivyo imara na muhimu kwetu.
Mashaka ni sehemu muhimu ya mfumo wetu wa imani. Inatusaidia kuonyesha ni sehemu zipi zinaweza kuwa dhaifu au zinahitaji msaada zaidi, na ni zipi zilizo imara na zenye msingi mzuri. Hivyo inatusaidia kujua jinsi ya kuendelea kukua, kujifunza, na kukomaa.
Lakini vipi kuhusu aya za Biblia zinazozungumzia kutokuwa na mashaka?5
Tuangalie mfano wa Petro alipotembea juu ya maji kwenda kwa Yesu na kuanza kuzama kwa sababu ya mashaka. Yesu akamwuliza: “Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka?” (Mathayo 14:31, NKJV).
Inaonekana kama Yesu anasema mashaka ni jambo baya. Ni kama anamkemea Petro kwa kupoteza imani yake.
Lakini Petro alionyesha imani kubwa katika aya chache zilizopita alipojitokeza juu ya maji. Mara tu Yesu alipomwambia aje kwake, Petro hakusita!
Hakupoteza imani yake lakini alisukumwa pembeni na dhoruba. Imani ya Petro katika uwezekano wa kuzama iliizidi imani yake katika kutembea na Yesu juu ya maji.
Yesu alipomuuliza kwa nini alikuwa na shaka, alikuwa anamuuliza Petro ni nini kilichosababisha kujisikia kushindwa na dhoruba.
Lakini angalia jinsi Yesu alivyokuwa pamoja na Petro katika mashaka yake. Petro alipozama na kulia akiomba msaada, Yesu alimshika mkono, akimwinua, na kutembea naye kurudi kwenye mashua.
Kisa hiki kinaonesha kwa uzuri jinsi Mungu anavyofanya kazi na sisi wakati mashaka yanapoipa changamoto imani yetu. Mara nyingine tunajisikia kushindwa, lakini Mungu hatuachi tumezwe. Badala yake, yeye hunyoosha mkono na anatamani kutusaidia kumwamini zaidi.
Ni muhimu pia kukumbuka kwamba imani ni mchakato. Katika visa vya Injili, Yesu anawaambia wanafunzi wake kwamba hata kuwa na imani ya mbegu ndogo ya haradali ingewawezesha kuhamisha milima (Mathayo 17:20). Imani ni yenye nguvu, hata kama sio kubwa. Na kama mbegu ya haradali, inaweza kukua na kuwa imara zaidi.
Jambo muhimu ni kwamba hauitaji kuwa na imani kamili kumtumikia Mungu au kumwakilisha au kumwakisi. Biblia imejaa “mashujaa” ambao walipambana na mashaka na kukata tamaa. Tutajifunza baadhi ya wazee, viongozi, na manabii ambao imani yao haikuwa kamili wakati wote, lakini walifanikiwa kufanya mambo ya kushangaza kwa nguvu ya Mungu.
Sisi sote hupatwa na mashaka. Kilicho muhimu ni kwamba hatuyashikilii mashaka badala ya Yesu. Hatuna haja ya kuyapa mashaka nguvu juu yetu.
Mashaka ni uzoefu wa kawaida—hata katika Biblia
Ikiwa kwa sasa una mashaka ya kiroho, uko katika sehemu nzuri. Utafiti wa Barna uligundua kuwa asilimia 65 ya watu wazima wa Marekani wanaojitambulisha kama Wakristo wanapitia kipindi cha mashaka wakati fulani.6
Hao ni watu wanne kati ya watu sita wanaoketi kwenye kiti cha mbele kanisani.
Haifanyi ujisikie mpweke tena, sivyo?
Kujua kuwa watu wengi wanapitia hisia na mawazo kama hayo kunaweza kuwa faraja.
Zaidi ya hayo, utafiti huo huo wa Barna uligundua kuwa kati ya wale wanaopitia mashaka, kati ya asilimia 81-95 yao (wana kawaida ya kuhudhuria ibada) walitoka katika kipindi hicho wakiwa na imani imara zaidi.7
Ni kwa sababu hiyo watu hao wanne bado wako kwenye kiti hicho cha kanisa.
Kwa kweli, baadhi ya watu wakubwa katika Maandiko walipitia vipindi vikubwa vya mashaka:
- Tomasi mtume, anayejulikana katika kisa maarufu kuhusu mashaka katika Biblia kama “Tomaso Mwenye Mashaka,” hakuamini kwamba Yesu alikuwa amefufuka kutoka kwa wafu hadi alipomwona Yesu uso kwa uso (Yohana 20:25). Hata hivyo, Yesu hakupuuza mashaka yake wala kumhukumu kwa hilo.
- Ibrahimu alitilia shaka ahadi ya Mungu ya kumfanya kuwa baba wa mataifa kwa sababu yeye na Sara walikuwa wazee sana yakuwezekana kuwa na mtoto (Mwanzo 17:17).
- Musa alitilia shaka kufanikiwa kwake katika kumshawishi Farao aachilie wana Israeli. Kwa kweli, alikuwa na mashaka sana kiasi cha kutoa sababu tatu kwa nini asichaguliwe kwa ajili ya utume huo(Kutoka 3:11; 4:1, 10, 13).
- Gideoni alidai kwamba Mungu afanye ishara kadhaa kabla ya kuamini kwamba yeye ndiye aliyechaguliwa kuokoa Israeli kutoka kwa Wamedi (Waamuzi 6:15, 17, 36-40).
- Daudi alikuwa na wasiwasi sana alipoona Siklagi imechomwa. Pia aliandika Zaburi nyingi zikielezea nyakati za mashaka (1 Samweli 30:4; Zaburi 6, 13, na 38, kwa mfano).
- Eliya alikimbia kuokoa maisha yake kwa sababu alitilia shaka uwezo wa Mungu kumwokoa kutoka kwa Yezebeli. Hili linatokea, mara baada ya kushuhudia muujiza wa Mungu juu ya Mlima Karmeli! (1 Wafalme 18; 19:3-4)
Mifano hii inatuonyesha kwamba shaka hukumba hata wale ambao Mungu huwachagua kwa kazi yake. Lakini Mungu bado aliwatunza na hata kuwapa walichokiomba. Na hawa wote wenye shaka aliwatumia kwa madhumuni ya kushangaza. Hawakupoteza imani yao kama matokeo yao— bali walikuwa karibu zaidi na Mungu.
Basi, tuangalie kwa ukaribu zaidi kinachofunua mashaka kwetu.
Nini kinaweza kusababisha shaka?
Mashaka ya kiroho yanaweza kusababishwa na mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na:
- Hali ya maisha—Mambo yanayotokea nje ya udhibiti wako, na kuweka wazi maeneo ya imani yako ambayo hayajapata changamoto
- Uzoefu usiotarajiwa ambao usingwezekana kupangiwa
- Mahusiano mabaya yanayoweza kutikisa imani zetu
- Hofu pale mambo yanapoonekana tofauti na jinsi tunavyojisikia yanapaswa kuwa
- Mawazo mapya, kama kusoma makala inayoshawishi ambayo inapingana na moja ya imani zako
- Mtazamo mpya, kama kusikia sababu ya mtu mwingine kwa imani yake
- Uzoefu unaopingana, kama wakati mtu anapitia uzoefu kama wako lakini anakuwa na mwitikio tofauti sana
- Taarifa zinazokinzana, kama mtu akifikia hitimisho tofauti na wewe kuhusu dhana ileile, aya ya Biblia, mafundisho, kanuni, n.k.
- Kukutana na dhana katika Biblia ambayo bado hujaielewa, ambayo inaweza kutufanya tutilie shaka ufahamu wetu
- Vita vya kiroho, kwa sababu shetani anatamani tuwe na mashaka yoyote anayoweza kuyatumia kutukengeusha an kutukatisha tamaa.
Jambo lolote linalohitaji kurekebisha mfumo wetu wa kuelewa mambo lina uwezo wa kufunua mashaka.
Na ndio, mara nyingi ni mchakato usio rahisi.
Na ingawa moja ya sababu hizi inaweza kuwa kichocheo cha mashaka yako, mara nyingi ni mchanganyiko wa mambo ambao hatua kwa hatua huongezeka hadi kufikia kilele.
Mackie analinganisha mashaka na ziwa linalolishwa na mito mingi na vijito.8 Mchanganyiko wa mambo na hali, kubwa na ndogo, unalisha ziwa linalounda mashaka tuliyonayo.
Wakati mwingine, hata hivyo, mashaka yanaweza kwenda zaidi ya hili na kuwa na madhara. Tutajuaje wakati hili lishatokea?
Wakati mashaka yanapokuwa jambo la kusumbukia
Mashaka yanaweza kuwa tatizo tunapoyaangalia zaidi ya kusudi lake—ishara ya kujaribu na kuchunguza.
Kuinua mashaka akilini mwetu na kuyapa mamlaka zaidi kuliko imani yetu, kujikita katika hayo, au kukataa kuyakubali—kunaweza kudhoofisha imani yetu.
Na ikiwa yanatuzuia tusiendelee au kutufanya tuache imani bila uchunguzi zaidi…hapo ndipo yanapokuwa tatizo.
Tunapofikia hatua hii, ni muhimu kutambua kwamba mashaka yetu sio ya kawaida. Yamekuwa mchakato wa mawazo yenye madhara. Inaweza kusababisha hali ya kutokuwa na imani, kutufanya tuhoji nia na uaminifu wa watu, kudhania hatia kabla ya kutokuwa na hatia, nk. Ikiachwa bila kudhibitiwa, njia hii inaweza kusababisha kukata tamaa mara kwa mara, ukosoaji, au msongo.
Hali hizi zenye madhara kisaikolojia zinaweza kusababisha matatizo ya afya ya kimwili na kiakili.9
Mashaka yanaweza pia kumfanya mtu akatae ukweli kabisa au kujikita kwenye maelezo ambayo yanaweza kufanya taswira kuu kuwa ya kutatanisha. Hili lilitokea kwa viongozi wengi wa kidini katika siku za Yesu. Walikuwa na wasiwasi zaidi kuhusu kutoa zaka ya viungo kuliko “mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani” (Mathayo 23:23, NKJV).
Yaani, walielekeza fikira zao kwenye vitu vya kimaumbile, vinavyoweza kupimika…sio kwa sababu vilikuwa muhimu zaidi, bali kwa sababu vilikuwa rahisi kufuatilia na kuthibitisha.
Wakati mashaka yetu yanapotusumbua kama hivi, hapo ndipo maombi yanapochukua nafasi yake. Tunaweza kujisikia kama Petro—tunaweza kujisikia kama tunazama katika mashaka yetu na hakuna matumaini. Hapo ndipo tunaweza kunyoosha mkono wetu na kuomba, na Yesu atakuwepo kwa ajili yetu kutuinua juu.
Usiwe na wasiwasi ikiwa huwezi kuondoa mashaka yako mara moja. Mashaka ya kiroho makubwa na yanayojumuisha mambo mengi yanaweza kuchukua muda mrefu kutatuliwa, na hakuna aibu katika hilo. Inachukua muda kadri inavyohitajika.
Muhimu ni kutokata tamaa katika kutafuta ukweli kwa sababu ya mashaka.
Omba kwa Mungu ili kupata mwongozo na tafuta msaada. Kujikita katika Yeye na Neno lake kutakusaidia kuepuka kupoteza mwelekeo.
Wakati mashaka yetu yanapofanya kazi yake ipasavyo, basi tunaweza kuendelea na uchunguzi na ukuaji wetu.
Jinsi tunavyoweza kuitikia mashaka yetu
Njia bora ya kushinda mashaka yetu ni kuchukua hatua – usiache yakizurura akilini mwako bila kupingwa!
Tena, hili linaweza kuchukua muda mrefu, hata miaka. Inaweza kuwa ngumu kufanya hivyo, lakini hakuna ubaya wowote katika hilo. Ni muhimu kuyazingatia na kujifunza kwa maombi.
Biblia kimsingi inatuhimiza kujaribu imani zetu.
“Jijaribuni wenyewe kwamba mmekuwa katika imani; jithibitisheni wenyewe” (2 Wakorintho 13:5, NKJV).
“Jaribuni mambo yote; lishikeni lililo jema” (1 Wathesalonike 5:21, NKJV).
Aya hizi huthibitisha haja yetu ya kupima habari mpya dhidi ya vile tunavyoamini tayari.
Ikiwa hatufanyi chochote kuhusu mashaka yetu, yanaweza kukua akilini mwetu kama uvimbe, na kushindwa kudhibitiwa na kuanza kuathiri sehemu zingine za maisha yetu. Badala yake, Mackie anasisitiza kwamba lazima tuwe “wenye mashaka kuhusu mashaka yetu.”10 Wakati mashaka yetu yanapozipa changamoto imani zetu, hiyo ni ishara ya kuyapa changamoto mashaka yetu!
Hivyo jambo la kwanza tunaloweza kufanya ni kuchunguza mashaka yetu. Yaombee na omba Roho Mtakatifu akusaidie. Tafakari kwa nini ulianza kuyapata. Ni mambo gani yaliyo changia kutokea kwa mashaka? Je, ni hofu? Je, umekuwa ukizidiwa na majukumu mapya? Je, mtu au kitu fulani kimekukosea? Je, jambo fulani baya lilitokea kwako au kwa mpendwa wako?
Kuchunguza chanzo husaidia kutambua jinsi ya kukabiliana na mashaka. Kwa mfano, tunaweza:
- Kujifunza kile Biblia inachosema kuhusu mada tunayopambana nayo (Mithali 30:5). Tafakari jinsi ulivyofikia imani au dhana unayoipinga. Je, ilitegemea kifungu kuwa halisi au ni ishara? Je, ulidanganywa au kuchanganyikiwa na uvumi au tafsiri za watu wengine? Je, kuna njia kadhaa za kutumia dhana ya Kibiblia kuliko ulivyofahamu awali?
- Zungumza na mshauri au mlezi anayeaminika, kama mchungaji, mwana familia Mkristo, au Mkristo mwingine unayemheshimu. Kuzungumza nao husaidia kupangilia mawazo yako na wanaweza kukupa ushauri wa kukusaidia kukabiliana na shaka.
- Tuliza akili. Sikiliza muziki wa kuelimisha, podcast ya Biblia, au mahubiri; enda utembee nje, n.k. Shughuli kama hizi zinaweza kukusaidia kusafisha akili yako na kuzingatia mawazo yenye kujenga ambayo mara nyingi hufunikwa na vikwazo.
Ikiwa una jamii iliyojikita katika ibada, maombi, kujifunza, na imani, jitumbukize ndani yake. Hii inaweza kuwa kanisa lako, kikundi cha marafiki, au familia. Watu hawa wanaweza kukutia moyo na kukusaidia, wakikuelekeza kwa Yesu unapochunguza, kurekebisha, na kuboresha imani yako.
Utafiti wa Barna uligundua kwamba kubaki katika jamii hii ilikuwa moja ya mambo muhimu katika kushinda mashaka.11
Mashaka hutokea kwa karibu kila mtu, bila kujali ni nani.
Ni sehemu muhimu ya imani, kutupa changamoto ya kuchimba kwa kina zaidi katika imani yetu ili tuweze kutoka katika mashaka yetu tukiwa na imani yenye nguvu zaidi kuliko hapo awali.
Unapopitia mashaka, kumbuka kuomba kuhusu jambo hilo. Mungu daima husikiliza tunapomwomba (Luka 11:9; Wafilipi 4:6). Atatusaidia katika mapambano yetu, na daima atakuwa upande wetu.
Aya muhimu za Biblia (NKJV) unapopambana na mashaka:
- Methali 3:5-6. “Mtumaini BWANA kwa moyo wako wote, Wala usitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.”
- Yuda 1:22. “Wahurumieni wengine walio na shaka.”
- 2 Wakorintho 13:5. “Jijaribuni wenyewe kwamba mmekuwa katika imani; jithibitisheni wenyewe.”
- 1 Wathesalonike 5:21. “Jaribuni mambo yote; lishikeni lililo jema.”
- Zaburi 50:15. “Ukaniite siku ya mateso; Nitakuokoa, na wewe utanitukuza.”
- Yohana 16:13. “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote;”
- 1 Petro 5:6-7. “…huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.”
- Mathayo 19:26. “….bali kwa Mungu mambo yote yawezekana.”
Kurasa zinazohusiana
- “Doubt,” KJV Dictionary. [↵]
- Coon, Roger W, PhD. “The Danger of Doubt and the Nature of Faith,” Andrews University. [↵]
- Beattie, Geoffrey. Doubt: A Psychological Exploration, Routledge, 2023. p.2. [↵]
- Mackie, Tim. “Doubt,” Psalms Study, Exploring My Strange Bible, Bible Project, October 26, 2017. [↵]
- Mathayo 21:21; Marko 11:23; Mathayo 14:31; Luka 24:38; Warumi 14:23; Yakobo 1:5-821:21 [↵]
- “Two-Thirds of Christians Face Doubt,” Barna, July 25, 2017. [↵]
- Ibid. [↵]
- Mackie, “Doubt.” [↵]
- https://www.psychologytoday.com/us/blog/emotions-dont-think/202302/cynicism-is-lethal-toxic-and-sometimes-fatal [↵]
- ibid. [↵]
- “Two-Thirds of Christians Face Doubt.” [↵]
Majibu Zaidi
Kile Mfano wa Yesu Kinatufundisha Kuhusu Maombi na Kufunga
Kufunga na kuomba vilikuwa sehemu muhimu ya huduma ya Yesu Duniani. Hebu tujifunze jinsi mfano wa Yesu unavyoweza kutufundisha jinsi ya kuwa na uhusiano wa karibu zaidi na Mungu. Kufunga na kuomba vilichukua sehemu kubwa ya huduma ya Yesu Duniani.
Aya za Biblia Wakati Unapojisikia Kukata Tamaa
Maisha kamwe sio rahisi, lakini mara kwa mara mambo huwa magumu zaidi, yenye maumivu, au yanayo vunja moyo.





