Kile Mfano wa Yesu Kinatufundisha Kuhusu Maombi na Kufunga

Maombi na kufunga vilikuwa sehemu muhimu ya maisha ya mashujaa wakubwa wa Biblia.1

Yesu hakuwa tofauti. Alifunga na kuomba ili kujiandaa kiroho, kuwabariki wengine, na kwa ajili ya uhusiano wake na Mungu.

Kufunga na kuomba vinaweza kutusaidia kufanya hivyo pia!

Hebu tuone jinsi mfano wa Yesu katika maombi na kufunga unavyoweza kutusaidia kujenga uhusiano wa kina zaidi na Mungu.

Fuatilia kwa umakini tunapojifunza:

Tuanze kwa kuelewa muktadha wa maombi na kufunga katika nyakati za Biblia.

Kuelewa Maombi na Kufunga

Maombi ni tendo la kuwasiliana na Mungu, na kufunga ni tendo la kujizuia kutoka kitu fulani (kawaida, chakula) kwa kipindi fulani cha muda.

Maombi yalifanywa kwa namna mbalimbali: wakati mwingine kwa makundi (Esta 4:16), wakati mwingine na watu binafsi (Danieli 6:10-13). Yalifanywa huku wakiwa wamesimama, wake piga magoti, na wakiwa wamelala kifulifuli.2 Maombi yalifanywa mara nyingi kwa siku, hasa asubuhi, adhuhuri, na jioni na kabla ya milo.3

Maombi haya kwa kawaida yalilenga kumsifu Mungu, kumwomba mambo fulani, na kuomba ufalme wa Mungu uje.4

Kufunga, kama ilivyo katika maombi, pia ilionyeshwa kwa njia tofauti. Baadhi ya watu walifunga kwa kutokula chakula, wengine kutokula chakula wala kunywa maji, wakati wengine walikula kidogo, na wengine walijizuia kwa kula chakula cha kawaida sana.

Katika nyakati nyingi, saumu zilikuwa fupi na iliruhusiwa kunywa maji.5 Kwa sababu wana Israeli walikuwa wanaishi katika hali ya hewa ya joto, kunywa maji ilikuwa sehemu muhimu ya kuepuka ukosefu wa maji mwilini.6 Wanachuo pia wanapendekeza kwamba vipindi vya kufunga vinaweza—katika nyakati nyingi—kuwa vya masaa ya mchana tu.7 Yaani, watu wangeweza kufunga bila kula wakati wa mchana na kuvunja saumu yao usiku.

Wengi wa Wayahudi wakati huo pia walikuwa wanakamilisha saumu zao kwa kuhudumia maskini, mara nyingine kwa kutoa chakula ambacho hawakukitumia wakati wa saumu kwa wale waliokuwa na uhitaji.8

Kufunga ulikuwa mwitikio kwa mahitaji makubwa— iwe mahitaji ya kimwili au ya kiroho.9 ilikuwa kwa ajili ya kuonyesha unyenyekevu (Zaburi 69:10); na kuomba wokovu na mwongozo wa Mungu (Ezra 8:23; Mathayo 17:21). Kulifanywa kwa ajili ya matukio maalum kama Siku ya Upatanisho na kwa sababu binafsi.10

Kwa ujumla, kufunga kuliwasaidia watu kuelekeza fikira zao kwa Mungu.

Hii ni kwa sababu kufunga kuliondoa kikwazo cha chakula, na kuwapa muda ambao wangeweza kuutumia kula ili wautumie kwa Mungu, kuungana naye kupitia sala. Pia iliwafanya watu wawe na shauku ya kumwelekea Mungu na kuwasaidia kumtegemea yeye kwa mahitaji yao.

Kufunga kuliwasaidia watu kugeuza fikira zao kutoka kwenye maswala ya kila siku ili wasikie na kufuata mpango wa Mungu.

Huenda sababu hii ndiyo iliyowapelekea watu wengi kufunga nyakati za Biblia wakati wa migogoro ya kiroho au kihisia – walipohitaji kutubu dhambi, walipohitaji majibu ya maswali magumu au maombi, au kama njia ya kukabiliana na huzuni.11

Kufunga ilikuwa njia yao ya kukabidhi matatizo hayo kwa Mungu na kuomba mwongozo wake.

Mwanachuo wa Biblia, Ángel Manuel Rodríguez, anaelezea hivi:

“Kwa kufunga, tunakabidhi maisha yetu kwa ukamilifu katika utunzaji wenye rehema wa Mungu. Huonyesha kujitoa kikamilifu, kusalimisha maisha yetu kwa upendo na imani kwa Mungu kama pekee anayeweza kutuokoa kutoka katika mateso ya dhambi”

Maombi na kufunga ni tabia binafsi. Ndiyo maana kulikuwa na namna nyingi za sala na kufunga, kama ilivyo leo. Hata hivyo, jambo linalobaki kuwa sawa ni kanuni za kudumu za sala na kufunga tunazopata kupitia mifano ya Biblia—hasa, kupitia mfano wa Yesu.

Kwanza, hebu tuzungumzie kwanini Yesu alikuwa na mazoea haya ya kiroho.

Kwa nini Yesu aliomba na kufunga

A man kneeling in prayer beside a foggy lake.

Image by Pexels from Pixabay

Yesu aliomba na kufunga ili kuwasiliana na kujenga uhusiano wa kina na Baba yake, Mungu.

Aliomba ili:12

  • Kumtukuza na kumsifu Mungu
  • Kuomba nguvu ya kupinga majaribu na kushinda uovu
  • Kumshukuru Mungu kwa baraka zake
  • Kuomba nguvu ya kufanya mapenzi ya Mungu

Kwake, sala ilikuwa ni zaidi ya kumwomba Mungu atimize maombi yake. Ilimpa fursa ya kukua na kudumisha uhusiano wake na Mungu.

Hata hivyo, Mahusiano hayajengwi tu katika vitu unavyomuomba mtu mwingine. Yanajengwa kwa upendo na imani inayojengwa baada ya kuzungumza na kutumia muda pamoja (Kutoka 33:11; Zaburi 28:7).

Biblia haituambii moja kwa moja kuhusu sababu ya Yesu kufunga. Lakini inawezekana kwamba tunaweza kuona kwa nini Yesu alifunga kwa kuangalia matokeo ya kufunga kwake – ilimsaidia kushinda majaribu na kutoa pepo (Mathayo 4:1-11; Mathayo 17:21). Mambo haya yanaweza kufanywa tu wakati mtu amejazwa na Roho Mtakatifu, ambae anaweza kupokelewa tu na wale walio katika uhusiano wa karibu na Mungu.13

Jinsi Yesu alivyoomba na kufunga

Biblia inatupa taarifa kadhaa kuhusu jinsi Yesu alivyokuwa akiomba na kufunga.

Yesu:

  • Aliomba mara kwa mara:14 Yesu aliomba alipokuwa peke yake, alipokuwa pamoja na watu wengine, alipokuwa akila, alipokuwa akifanya miujiza, moyo wake ulipojawa shukrani, na alipokuwa akijisikia kukata tamaa.
  • Aliomba kwa bidii:15 Yesu aliomba kwa moyo wake wote. Alipokuwa katika Bustani ya Gethsemane, alieleza waziwazi hofu na mateso yake kwa Mungu. Haikuwa kwa ajili ya kujionyesha—Aliomba kwa bidii na kwa moyo mnyofu kwa ajili ya uongozi wa Mungu.
  • Alitenga muda kwa ajili ya maombi binafsi:16 Yesu angeamka mapema au kuondoka katika maeneo yenye watu wengi ili kupata muda wa kipekee kwa ajili ya maombi binafsi. Angeenda katika maeneo ya faragha katika maumbile—kawaida mlimani.
  • Aliomba kwa ajili ya wengine:17 Yesu hakuomba tu kwa ajili Yake mwenyewe. Sehemu kubwa ya muda wake ulitumika kuomba kwa niaba ya wengine.
  • Alifunga ili kupata muunganiko:18 Yesu alifunga kwa siku 40 kabla ya kuanza huduma yake ili kujitoa kikamilifu na nia yake kwa Mungu.

Sasa tumeona “jinsi” hebu tujadili “lini” Yesu alifunga na kuomba katika Agano Jipya.

Nyakati ambazo Yesu alifunga na kuomba

Ingawa Biblia haijataja nyakati zote ambazo yesu alifunga na kuomba, inatuonyesha kwa uzuri namna maombi na kufunga yalivyoathiri huduma yake:

Yesu alifunga na kuomba:

  • Kwa siku 40 jangwani (Mathayo 4:1-2)
  • Ili kutoa mapepo (Mathayo 17:21)

Yesu aliomba:

Kabla ya ubatizo wake (Luka 3:21)

  • Kabla ya kwenda Galilaya (Marko 1:35, 36)
  • Alipokuwa peke yake (Luka 5:16)
  • Kabla ya kuchagua wanafunzi 12 (Luka 6: 12-13)
  • Kabla ya kulisha watu 5,000 (Yohana 6:11) na 4,000 (Mathayo 15:36)
  • Kabla ya kutembea juu ya maji (Mathayo 14:23)
  • Alipomponya mtu aliyekuwa kiziwi na bubu (Marko 7: 31-37)
  • Kabla ya kuwauliza wanafunzi Yeye ni nani (Luka 9:18-20)
  • Alipobadilika sura (Luka 9: 28-29)
  • Baada ya kikundi cha wanafunzi 72 kurudi na mafanikio (Luka 20:21)
  • Kabla ya kuwafundisha wanafunzi jinsi ya kuomba (Luka 11:1)
  • Kabla ya kumfufua Lazaro (Yohana 11: 42-44)
  • Kwa ajili ya watoto (Mathayo 19:13-15)
  • Kumtukuza Mungu (Yohana 12: 27-28)
  • Kwenye Meza ya Bwana (Mathayo 26:26)
  • Kwa ajili ya Petro (Luka 22:31-32)
  • Kabla na alipokuwa katika Bustani ya Gethsemane (Yohana 17:1-26; Mathayo 26:26-46. Luka 22:40-45)
  • Msalabani (Mathayo 27:46; Luka 23:46)
  • Alipobariki chakula baada ya kupaa kwake (Luka 24:30)
  • Alipobariki juhudi za wanafunzi wake katika kupeleka Injili (Luka 24:50-53)

Hebu tuangalie baadhi ya aya za Biblia zilizoorodheshwa hapa.

Alifunga kwa siku 40 (Mathayo 4:1-2)

Yesu aliongozwa na Roho Mtakatifu kufunga kwa siku 40 za kimwili jangwani.

Kisa kinaonyesha kuwa kufunga kwa hali ya juu haikuwa tendo la ibada au onyesho la nguvu za kiungu, bali, njia ya Yesu ya kuweka imani yake kwa Mungu.

Yesu alijaribiwa na Shetani atumie nguvu zake mwenyewe kujiokoa, badala ya kumtegemea Mungu, lakini Yesu alikataa (Mathayo 4:3-11). Kila mara Shetani alipomjaribu, alikiri imani yake kwa Mungu na Neno Lake.

Alipokuwa jangwani, alikuwa peke yake, huru dhidi ya vikengeusha fikra, na huru kuwa na muda wa faragha na Baba. Na tendo la kufunga lilikuwa njia nyingine ya kuweka kando masumbuko yake kujifunza imani kamilifu na kumtegemea Mungu kabisa (Yeremia 29: 13-14; Methali 3: 5-6).

Ingawa Maandiko hayaelezi sana kuhusu wakati Yesu alipofunga isipokuwa kisa hiki, tunaweza kuona nafasi ya jambo hili katika huduma ya Yesu na imani yake katika uhusiano wake na Mungu Baba.

Ukweli kwamba Alifanya hivi mapema kabla ya kuanza Huduma yake hutupatia ushahidi zaidi kwamba hii ilikuwa ni hatua ya maandalizi ya kiroho.

Aliomba akiwa peke yake (Luka 5:16)

Yesu alitumia muda mwingi wa maisha yake kuwasaidia watu wengine, na hata hivyo, kulikuwa na nyakati ambapo alilazimika kujitenga na umati na kutumia muda wa faragha katika sala.

Wakati mmoja, watu waliokuwa wakitafuta uponyaji walipoanza kumzingira Yesu, Yesu alijitenga ili asali peke yake.

Maombi binafsi yalimpa Yesu nafasi ya kuzungumza na Baba moja kwa moja na kushiriki hisia zake na mapambano, pamoja na kuomba nguvu. Katika matukio mengine ya maombi binafsi ya Yesu, kama vile katika Bustani ya Gethsemane, tunamuona akimimina moyo wake kwa Mungu (Yohana 17:1-26; Mathayo 26:26-46).

Muda wa kawaida katika maombi binafsi labda ulimpa Yesu nafasi ya kupumzika kutoka mahitaji makubwa ya huduma yake na kujisikia uwepo wa Bwana Mungu wa kutia moyo na kufariji (Isaya 40:31).

Aliomba kabla ya kuchagua Wanafunzi 12 (Luka 6: 12-13)

Yesu pia alitumia muda zaidi katika sala kabla ya kuanza utume muhimu.

Yesu aliomba usiku kabla ya kuchagua wanaume ambao wangekuwa wanafunzi wake.

Alikwenda mlimani, labda ili kutafuta mahali pa faragha ambapo angeweza kujikita katika amani na faragha ya uwepo wa Mungu.

Na hakukaa tu huko kwa saa chache. La, aliomba usiku kucha.

Inawezekana wakati huu ulimuandaa kwa kazi ya kuchagua wanafunzi, kuhakikisha mapenzi yake yalilingana na ya Mungu katika kuchagua viongozi ambao wangeliongoza Kanisa la kwanza baada ya Yesu kupaa.

Aliomba kabla ya kulisha watu 5,000 na 4,000 (Yohana 6:11; Mathayo 15:36)

Yesu aliomba kabla ya kulisha watu 5,000 na 4,000..

Alikuwa na desturi ya kuomba kabla ya chakula (Mathayo 26:26; Luka 24:30). Hii ilifanywa ili kumshukuru Mungu kwa chakula na kuomba baraka za Mungu ili chakula kiweze kuhuisha mwili.

Alifanya hivi kwa milo ya kawaida na wakati wa muujiza wa chakula watu 5,000 na 4,000.

Kama vile mtu anaweza kuomba na kumshukuru rafiki kwa ajili ya chakula, Yesu alikumbuka kumshukuru Baba kwa riziki na huduma yake. Na ni kupitia uhusiano wa Yesu na Mungu, ndipo Yesu angeweza kumuomba Mungu amsaidie kuwalisha umati.

Aliomba wakati Alipobadilika sura (Luka 9: 28-29)

Kwa mara nyingine, Yesu aliondoka kwenda mlimani kusali. Lakini safari hii aliwachukua baadhi ya wanafunzi wake wa karibu—Petro, Yakobo, na Yohane—pamoja naye.

Tayari tumeshazungumzia kuhusu milima kuwa eneo la kujitenga na faragha. Lakini ni nini maana ya Yesu kuwaleta wanafunzi wake kusali pamoja naye?

Biblia inatuambia kuna kitu cha kipekee kuhusu kuomba pamoja na wengine.

“Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni. Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, mimi nipo papo hapo katikati yao.” (Mathayo 18:19-20, NKJV).

Hilo ni kweli katika mambo mengi, sivyo? Watu ni imara zaidi pamoja kuliko wanapokuwa peke yao.

Kwa kweli, Mungu kamwe hakukusudia yeyote kukabili safari ya Kikristo peke yake. Alituita kujiunga na kikundi cha waamini kama sisi, Kanisa, ambapo tunaweza kusaidiana, kutiana nguvu, na kutiana moyo (1 Wathesalonike 5:11).

Yesu alitambua nguvu iliyo katika kuungana na wengine katika maombi. Na yalikuwa maombi haya yaliyomwezesha Yesu kukutana na Musa na Eliya wakati alipobadilika sura.

Aliomba kabla ya ufufuo wa Lazaro (Yohana 11: 42-44)

Ilikuwa kwa njia ya sala kwamba Yesu alidumisha uhusiano wake na Mungu.

Kwa kukuza uhusiano wa karibu na Baba, Yesu alikuwa na uwezo wa kutambua na kufanya mapenzi Yake. Yeye na Baba walikuwa na nia na kusudi moja.

Alipokuwa akiomba kabla ya ufufuo wa Lazaro, alikiri kwamba alielewa mapenzi ya Mungu katika kumfufua Lazaro. Pia alikiri imani kamili na ya dhati katika uhusiano wake na Mungu: “Baba, nakushukuru kwa kuwa umenisikia. Nami nalijua ya kuwa wewe wanisikia sikuzote…” (Yohana 11:41-42, NKJV).

Yesu alitumia mfano wa hadithi za ujumbe kuhusu kuwa na imani kama mbegu ya haradali, na kuomba kwa imani, akiwa na hakika kwamba angeweza kutegemea Mungu kujibu ombi lake la kumfufua Lazaro (Mathayo 17: 20-21; Marko 11:24).

Aliomba kwa ajili ya Petro (Luka 22: 31-32)

Yesu hakuomba tu kwa ajili yake mwenyewe. Pia likuwa na tabia ya kuomba kwa ajili ya wengine.

Katika kisa hiki, Yesu aliomba kwa ajili ya rafiki yake na mwanafunzi, Simoni Petro, ili aweze kumrudia hata baada ya kumkana mara tatu.19

Kwa njia hii, Yesu alitambua nguvu ya maombi ya kuombea wengine (Waefeso 6:18).

Aliomba Gethsemane (Yohana 17:1-26; Mathayo 26:26-46, Luka 22:40-45)

Ni muhimu kufahamu kwamba yote ambayo Yesu alifanya akijua kuwa atakamatwa na kusulubiwa ilikuwa kuomba.

Alienda tena kwenye eneo lililojitenga, Bustani ya Gethsemane, pamoja na wanafunzi kadhaa ambao aliwaomba waombe pamoja naye.

Katika ombi lake, alijisalimisha kwa Mungu, akimwomba Mungu atende mapenzi yake kuliko yake mwenyewe.

Kisha akaanza kutoa jasho la damu. Hii ilikuwa ni ishara ya kimwili ya mapambano ya kiroho na kiakili aliyokuwa akipitia.

Alizungumza kwa uaminifu kuhusu hofu yake, akimwomba Mungu amwongoze na kumthibitisha kupitia hatima yenye maumivu ambayo angeipitia Msalabani.

Katika nyakati za udhaifu na mashaka, alijua angeweza kupata nguvu kwa kuzungumza na Baba (Zaburi 118:14).

Lakini katika sala hii, Yeye anafanya zaidi ya kujiombea kuhusu kusulubiwa kwake. Kwa bidii Anaomba kwa ajili ya wanafunzi wake.

Na anaomba kwa ajili yetu. Ndiyo! Anaomba kwa ajili ya wote wanaomwamini:

“Wala si hao tu ninaowaombea; lakini ya wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao. Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi” (Yohana 17: 20-23, NIV).

Hata katika uso wa mateso makubwa na maumivu ya kimwili na kihisia, Yesu anatufikiria na kutuinua kwa Baba yake. Upendo usio na kikomo!

Kile Yesu anachofundisha kuhusu maombi na kufunga

Yesu alifundisha kwamba maombi na kufunga ni kuhusu kujenga uhusiano wetu na Mungu.

Sio kwa ajili ya kuonyesha haki yetu au kufanya kazi ili kupata upendeleo wa Mungu kama Mafarisayo walivyoamini.

Kwa kweli, Yesu alizungumza dhidi ya wale wanaofanya sala kuwa maonyesho ya haki yao mbele za watu:

“Tena msalipo, msiwe kama wanafiki; kwa maana wao wapenda kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia, ili waonekane na watu. Amin, nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao” (Mathayo 6:5, NKJV).

Badala yake, Yesu anatuita tuombe kwa bidii na unyenyekevu:

“Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye siri atakujazi. Nanyi mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke, kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi. Basi msifanane na hao; maana Baba yenu anajua mnayohitaji kabla ninyi hamjamwomba” (Mathayo 6:6-8, NKJV).

Maombi ambayo Yesu anawapa wanafunzi ni mfano mzuri sana wa hili.

Ni rahisi na moja kwa moja. Na yote ni kuhusu kuwa mkweli mbele za Mungu.

Linatangaza utukufu wa Mungu na ukweli kuhusu udhaifu wetu wa kibinadamu, likieleza hitaji na shauku ya kuwa na tabia kama ya Kristo na kufanya mapenzi ya Mungu:

“Baba yetu uliye mbinguni,
Jina lako litukuzwe,
Ufalme wako uje,
Mapenzi yako yatimizwe,
hapa duniani kama huko mbinguni.
Utupe leo riziki yetu.
Utusamehe deni zetu,
kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu.
Na usitutie majaribuni,
lakini utuokoe na yule mwovu.
[Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amina.]” (Mathayo 6:9-13, NKJV).

(Kujifunza zaidi kuhusu jinsi Sala ya Bwana ilivyo ya ajabu na ya makusudi, angalia makala yetu yote kuhusu sala baadaye).

Yesu pia aliwaonya watu dhidi ya kufanya kufunga kuwa onyesho la haki.

Tena mfungapo, msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao, ili waonekane na watu kuwa wanafunga. Amin, nawaambia, wamekwisha kupata thawabu yao” (Mathayo 6:16, NKJV).

Badala yake, Yesu anatuita kufanya saumu kuwa siri —kati yetu na Mungu, “Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso; ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi” (Mathayo 6:17-18, NKJV).

Sasa tunajua jinsi Yesu anavyotaka tufunge na kuomba, lakini tunawezaje kutumia hekima hii katika maisha yetu kwa vitendo?

Hebu tuzungumze kuhusu hilo.

Tunawezaje kutumia mfano wa Yesu katika maisha yetu?

Huku tukifuata ushauri wa Yesu kuhusu maombi na kufunga, tunaweza pia kufanya vema kufuata mfano wake.

Bila shaka, kuna baadhi ya tofauti—hasa kuhusu kitendo chake cha kufunga kwa siku 40.

Hii ni kwa sababu kufunga kwa muda mrefu inaweza kuwa hatari.20 Kwa kweli, wataalamu wa afya wanapendekeza kushauriana na daktari kabla ya kuanza kufunga kwa zaidi ya masaa 24.21

Tunajua Yesu na Musa walifunga kwa siku 40 (Kutoka 34:28-25), lakini huku walikuwa wakiongozwa na Roho na kuwezeshwa na Roho kufanya hivyo, sio jambo ambalo Mungu kawaida anawauliza wafuasi wake kulifanya.

Anathamini afya na usalama wetu na anapinga mazoea yoyote yanayoweza kuhatarisha afya yetu, kama vile saumu iliyopitiliza (1 Wakorintho 6:19-20; Mathayo 6: 31-34). Hivyo japokuwa hatuwezi kufunga kwa siku 40 kama Yesu alivyofanya, mfano wake unatupatia kanuni nzuri, ambazo kwa kiasi kikubwa tunaweza kuzitumia katika safari yetu ya kiroho.

Kama ilivyokuwa kwa Yesu, tunaweza kufanya juhudi ya kutenga nyakati maalum kwa ajili ya maombi binafsi na ya pamoja ili kuimarisha uhusiano wetu na Mungu. Tunaweza pia kuomba na kufunga kwa bidii, tukiwa na imani kamili kwamba Mungu atatusikia tunapomwendea.

Mwishowe, maombi na kufunga ni fursa nzuri ya kumkaribia Mungu. Katika utulivu wa maombi na kufunga, tunaweza kupunguza mwendo na kujikita katika kumjua Mungu na kumruhusu yeye atujue. Kupitia uzoefu huu, tunaweza kujifunza kumtegemea Mungu na kukubali uongozi wake katika maisha yetu.

Uhusiano huu ndio unaotubadilisha na kutufanya kuwa wafuasi Yesu.

Je, unatamani kujifunza zaidi kuhusu maombi na kile yanachoweza kukufanyia?

Nyakati Yesu Aliomba na Kufunga:

Yesu alifunga:

  • Kwa siku 40 nyikani (Mathayo 4:1-2)
  • Kutoa pepo (Mathayo 17:21)

Yesu aliomba:

  • Wakati wa ubatizo wake (Luka 3:21)
  • Kabla ya kwenda Galilaya ( Marko 1:35, 36 )
  • Akiwa peke yake (Luka 5:16)
  • Kabla ya kuchagua wanafunzi 12 (Luka 6:12-13)
  • Kabla ya kulisha 5,000 (Yohana 6:11) na 4,000 (Mathayo 15:36)
  • Kabla ya kutembea juu ya maji (Mathayo 14:23)
  • Alipokuwa akimponya mtu aliyekuwa kiziwi na bubu (Marko 7:31-37).
  • Kabla ya kuwauliza wanafunzi yeye ni nani (Luka 9:18-20)
  • Wakati wa kugeuka sura (Luka 9:28-29)
  • Baada ya kundi la wanafunzi 72 kurudi kwa mafanikio ( Luka 20:21 )
  • Kabla ya kuwafundisha wanafunzi jinsi ya kuomba (Luka 11:1)
  • Kabla ya kumfufua Lazaro (Yohana 11:42-44)
  • Kwa watoto ( Mathayo 19:13-15 )
  • Kumtukuza Mungu (Yohana 12:27-28)
  • Katika Meza ya Bwana (Mathayo 26:26)
  • Kwa Petro (Luka 22:31-32)
  • Kabla na wakati wake katika bustani ya Gethsemane (Yohana 17:1-26; Mathayo 26:26-46)
  • Msalabani (Mathayo 27:46; Luka 23:46)
  • Kubariki mkate baada ya kupaa kwake (Luka 24:30)
  • Kubariki juhudi za Wafuasi wake katika kueneza Injili (Luka 24:50-53)
  1. Esther 4:16; Daniel 6:10-13; Ezra 8:21-22. []
  2. Ephesians 3:14; Judges 20:26; Luke 18:10-13. []
  3. Psalm 5:3; Psalm 92:2; Psalm 88:1; Psalm 55:17; Daniel 6:10; Psalm 119:55, 62; Matthew 14:19. []
  4. Ostberg, René, “Lord’s Prayer,” Britannica, July 29, 2024. []
  5. Rodríguez, Ángel Manuel, “What is the purpose of religious fasting?” Biblical Research Institute, Sept. 13, 2001. []
  6. Ibid. []
  7. Ibid. []
  8. Johnston, Madeline S., “Fasting with Balance,” Ministry Magazine, Jan., 1995. []
  9. Leviticus 16:29; Acts 13: 2-3; Esther 4:16; Jonah 3:9. []
  10. Leviticus 16:29; Daniel 10:2-3. []
  11. Jonah 3:1-10; Esther 4:16; Nehemiah 1:4. []
  12. Matthew 6:9-13. []
  13. 1 Chronicles 16:11; Romans 8:13; Matthew 12:28. []
  14. Luke 9:18; Mark 6:41; Hebrews 5:7; Luke 6:12. []
  15. Matthew 26:36-39; Mark 14:32-36; Luke 22:39-44. []
  16. Matthew 14:23; Luke 5:16; Mark 1:35; Mark 6:46. []
  17. John 17:9,15, 20-23; Luke 22:31-32. []
  18. Matthew 4:1-2; Matthew 17:21. []
  19. Nichol, F. D., Seventh-day Adventist Bible Commentary, vol.5, p.868. []
  20. To Fast or Not To Fast?National Institutes of Health. []
  21. Sissons, Claire, and Mandy French, “All You Need to Know About Water Fasting,Medical News Today, Oct. 18, 2023. []

Je, Una swali kuhusu Waadventista? Uliza hapa!

Pata majibu kwa maswali yako kuhusu Waadventista Wasabato

Majibu Zaidi

Je, Ni Kawaida Wakristo Kuwa na Mashaka?

Ndio, ni kawaida kabisa kwa Wakristo kupitia vipindi vya mashaka katika maisha yao ya kiroho. Kila mtu ameshawahi kuwa na mashaka wakati mmoja au mwingine, hata wachungaji, wanatheolojia, na watu muhimu katika Biblia.