Umewahi kuhisi kana kwamba isingewezekana kwako kuponywa? Kweli, kuna visa vya watu wanaoshinda changamoto zilizoshindikana au kupata uponyaji wa kimiujiza wa afya zao. Lakini kwa nini inaonekana kama aina hiyo ya uponyaji bado ni jambo lisilowezekana au lililo mbali sana?
Kile unachohitaji zaidi ni matumaini kidogo au kutiwa moyo kidogo.
Biblia inatoa mifano isiyohesabika ya Mungu kuponya watu – baadhi yake katika nyakati zisizowezekana.
Mara nyingi tunafikiria juu ya Yesu akiwaponya watu aliokutana nao wakati wa huduma yake duniani. Lakini pia kuna visa kadhaa kadhaa kuhusu manabii na mitume wakiponya watu kwa nguvu ya Mungu.
Nakala hii itapitia kile Biblia inachosema kuhusu uponyaji na maana yake kwetu leo tunapoteseka. Pia utajifunza jinsi uponyaji unavyokusudiwa kuwa wa kina—ukihusisha mwili, akili, na roho.
Tutajadili:
- Kile Biblia inachosema kuhusu afya na uponyaji
- Mifano ya uponyaji katika Biblia
- Wakati Mungu haponyi
- Ahadi za Biblia kwa ajili ya uponyaji
- Uponyaji ambao Mungu anataka kwako
Kabla hatujajikita katika mada hii, tunatamani ujue kwamba makala hii haikusudiwi kuwa ushauri wa matibabu au afya ya akili. Haikusudiwi kuchukua mahali pa msaada wa matibabu au tiba ya kitaalamu.
Kwa kweli, Mungu mara nyingi hufanya kazi ya kutoa uponyaji kupitia wataalamu ambao wana ujuzi wa kukidhi mahitaji yetu maalum. Yeye hutumia njia nyingi tofauti kujaalia nguvu au uponyaji, hivyo kutafuta msaada sio kukosa imani.
Kwa kusema hivyo, hebu tuanze kwa muhtasari wa mada hii katika Biblia.
Ahadi za Biblia Kuhusu Uponyaji
- Mungu anaweza kutuponya (Kutoka 15:26; Kutoka 23:25)
- Mungu yuko tayari kumponya yeyote anayekuja kwake kwa imani (Mathayo 8:5-18)
- Mungu hutupatia uponyaji na faraja hata wakati ambapo matatizo yetu yanatokana na uamuzi mbaya wa kibinafsi (Zaburi 107:19-21)
- Mungu atarejesha afya yetu na kuponya majeraha yetu (Yeremia 30:17; Zaburi 41:3)
- Mungu yuko karibu na wale waliovunjika mioyo na huponya wale wenye roho iliyopondeka (Zaburi 34:17-22)
- Mungu anataka kukuponya, kukusamehe dhambi, na kukuvisha taji la upendo (Zaburi 103:2-4)
- Mungu anawapumzisha wale waliochoka (Mathayo 11:28-29)
- Tunaweza kumtumaini Mungu kutuponya na kutuinua (Zaburi 42:11)
- Tukiwa dhaifu, tunaweza kumtegemea Mungu ili kupata nguvu (Zaburi 73:26; Wafilipi 4:13)
- Ingawa mambo yanaweza kuwa ngumu, tunaweza kupata tumaini katika ukweli kwamba Mungu mwishowe atatuokoa kutoka matatizo yetu (Yohana 16:33)
- Mungu atatupa amani (Wafilipi 4:7)
- Watu wa Mungu watapewa miili isiyokufa ambayo kamwe haitasumbuliwa na magonjwa au uzee (1 Wakorintho 15:53-55)
- Watu wa Mungu siku moja wataishi katika ulimwengu usio na dhambi, maumivu, ugonjwa, wala kifo (Ufunuo 21:4)
Je, Biblia inasema nini kuhusu afya na uponyaji?
Mara nyingi tunauona uponyaji kama kuondolewa kabisa kwa ugonjwa au jeraha la kimwili. Lakini katika Maandiko, uponyaji unahusisha urejeshwaji wa afya ya kimwili, kiakili, na kiroho. Inajumuisha kila kitu kinachotufanya tuwe binadamu.
Sababu ya hili ni kwamba Biblia inatambua uhusiano kati ya miili yetu, akili zetu, na roho zetu, au hali yetu ya kiroho (1 Wakorintho 6:20; 1 Wathesalonike 5:23).
Yohana pia anaonyesha hamu yake kwamba tuwe na afya katika mwili na roho anapoandika:
“Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo” (3 Yohana 1: 2, NKJV).
Hivyo zaidi ya kiroho, Biblia inazungumzia afya yetu ya kimwili kwa sababu ya jinsi inavyoathiri afya yetu ya kiroho na kiakili, na kinyume chake.
Yesu alisema kwamba sehemu ya lengo lake duniani ni kutusaidia kuwa na maisha kamili na yenye kuridhisha (Yohana 10:10).
Na maelezo mazuri ya maisha kamili ni kustawi kimwili, kiafya, na kiroho.
Tuanze na uponyaji wa kimwili.
Uponyaji wa kimwili
Uponyaji wa kimwili ni urejeshwaji wa sehemu tofauti za miili yetu katika utendaji wake wa kawaida. Inahusisha kupona kutokana na magonjwa yanayotuletea maumivu na mateso.
Visa vingi vya Biblia vinasimulia kuhusu watu walioponywa magonjwa na ulemavu.
Hapa kuna baadhi ya mifano:
- Vipofu kuona (Yohana 9:1-38)
- Viwete kutembea (Matendo 3:1-9)
- Viziwi kusikia (Marko 7:31-37)
- Bubu kuongea (Mathayo 9:32-33)
- Walemavu kupata afya kamili (Luka 13:10-17)
- Waliopooza kupona (Mathayo 9:1-8)
- Wenye ukoma kuponywa (2 Wafalme 5:1–27; Mathayo 8:2-4)
Tutajifunza kidogo baadhi ya visa hivi.
Uponyaji wa kiakili

Photo by Christian Erfurt on Unsplash
Inaweza kuwa ya kuvutia jinsi Biblia inavyosema mengi kuhusu afya ya akili.
Tunapata mfano wa msongo kwa Eliya alipokuwa akimkimbia Yezebeli.
Au kwa Yeremia, alipohisi msongo mkubwa kutokana na mvutano kati ya mipango ya Mungu na ukaidi wa watu wake mwenyewe.
Tunaona wasiwasi kwa Martha alipolemewa kwa kuwakaribisha wageni wake.
Tunaona msongo wa akili kwa Daudi, ambaye alikuwa amebeba majukumu ya uongozi na vitisho vya mara kwa mara kutoka kwa maadui zake.1
Na kama ilivyo katika uponyaji wa kimwili, tuna mifano mingi ya watu walioponywa kutokana na mizigo ya kiakili katika Biblia:
- Yesu alimtetea mwanamke ambaye alikuwa akipingwa na wanafunzi wake (Marko 14:3-9)
- Elisha aliwasaidia mjane na wanawe kulipa deni lao na kutoka katika hali ya kukata tamaa (2 Wafalme 4:1-7)
- Mungu alimsaidia Eliya kupata faraja kutokana na msongo wa mawazo ili aweze kusonga mbele (1 Wafalme 19:1-18)
- Yesu alimsaidia baba aliyelemewa na huzuni kwa kuponya mwana wake mwenye kifafa (Mathayo 17:14-18)
- Baada ya Petro kumkana Yesu, alijawa na hatia na aibu. Lakini Yesu alimkaribia baada ya kufufuka kwake, akathibitisha uhusiano wao, na kumtuma Petro kwa agizo lenye nguvu (Yohana 21:15-19).
Yesu anatupatia uponyaji wa kiakili kama huo leo.
Wengi wetu tunakabiliana na msongo wa mawazo, sonona, na wasiwasi. Lakini Mungu hatuachi kupigana vita hivi peke yetu.
Neno lake linatupatia kanuni kwa ajili ya faraja na uponyaji tunazoweza kufuata ili kuanza safari yenye afya zaidi. Pia anatupatia nguvu na kutupitisha katika hali ngumu kwa kutuimarisha na kututia moyo kwamba ameshinda ulimwengu, na siku moja atatupa uzima wa milele ambapo hatutakumbana tena na hofu, wasiwasi, huzuni, au maombolezo (Yohana 16:33; Ufunuo 21:4).
Zaidi ya yote, anatamani kutuvuta katika uwepo wake ambapo tunaweza kupata “furaha tele” na “mema ya milele” (Zaburi 16:11, NKJV).
Ni kupitia kujifunza kumwamini Mungu ndipo tunaweza kuhisi “furaha ya kuishi” ambayo inaimarisha hisia zetu za ustawi na kuwa na athari inayoenea kwa afya yetu kwa ujumla. Mtu mwenye hekima zaidi aliyeishi, Sulemani, alijua hili alipoandika:
“Moyo uliochangamka ni dawa nzuri; Bali roho iliyopondeka hukausha mifupa” (Methali 17:22, NKJV).
Wengi wetu tuna uzoefu huu—kadri tunavyokuwa na furaha, ndivyo tunavyokuwa na afya. Na kadhalika, kadri tunavyokuwa na huzuni ndivyo tunajisikia uchovu au hata kuugua.
Biblia inapozungumzia “moyo” hapa, haimaanishi moyo wetu wa nyama, bali utu wa ndani, akili, ufahamu, nafsi, kumbukumbu, mawazo, hisia, shauku, na kiti cha ujasiri.
Kwa hivyo tunapokuwa na “roho iliyopondeka,” inamaanisha kuwa msingi wetu wenyewe umepondeka.
Hata hivyo, moja ya sababu ambazo Yesu alikuja duniani ilikuwa “kuwaganga waliovunjika moyo” (Isaya 61:1; Luka 4:18, NKJV).
Mifano ya uponyaji tunayoona katika Biblia inaonyesha kwamba Mungu sio tu anajali afya yetu ya kimwili. Anajali afya yetu ya kiakili pia. Hataki kuponya miili yetu pekee – anataka kutengeneza mioyo yetu iliyovunjika na kutuletea furaha na amani.
Zaidi ya hayo, Anataka kuturejesha kiroho.
Uponyaji wa kiroho

Photo by Samuel Martins on Unsplash
Zaidi ya uponyaji wa mwili na moyo, Biblia inaelekeza kwenye hitaji kuu zaidi – uponyaji wa kiroho.
Kipawa hiki, kinachotoka kwa Kristo, kinatajwa katika Isaya 53. Akizungumzia kuhusu Kristo, inasema:
“Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona” (Isaya 53:5, NKJV).
Uponyaji ambao Yesu alitupatia kupitia maumivu yake ya kimwili kwanza kabisa ni uponyaji wa roho. Ni utakaso kutoka kwenye mambo ambayo ni kiini cha maumivu yetu yote.
Mambo kama hatia, aibu, na majuto kwa uasi dhidi ya sheria za Mungu. Na msongo na wasiwasi vinavyotokana na kuishi katika ulimwengu ulioharibika na wenye dhambi, uliojaa wasiwasi na uovu.
Yesu alilipa kwa uovu ulimwenguni na kwa mąkosa yetu na ubinafsi – mambo ambayo husababisha maradhi ya nafsi na hata kupelekea magonjwa ya akili na mwili.
Kupitia kafara ya Yesu, tunapokea msamaha na urejeshwaji wakati huo huo tukipata amani na raha ya kweli ambayo ulimwengu hauwezi kutupatia.
Na kama tutakavyoona katika mifano, kila wakati Yesu alipowaponya watu, alishughulikia upande huu wa afya.
Mifano ya uponyaji katika Biblia
Agano la Kale na Jipya katika Biblia kuna visa vingi vya watu walioponywa. Ingawa Yesu ndiye mponyaji wa mwisho, wanafunzi wake, na hata manabii wa Agano la Kale, waliponya wengine kwa nguvu ya Mungu pia.
Hapa kuna baadhi ya visa hivyo.
Miujiza ya Yesu ya uponyaji
Sehemu muhimu ya huduma ya Yesu ilikuwa uponyaji. Alipokuwa duniani, alikuwa tayari siku zote kuponya na kuhurumia wagonjwa na wenye maradhi—bila kujali hali zao.
Na alipowaponya watu, alijikita katika ustawi wa jumla: kimwili, kiakili, na kiroho.
1. Yesu anarudisha uwezo wa kuona kwa kipofu (Yohana 9:1-12)
Yesu alikutana na mtu aliyekuwa kipofu tangu kuzaliwa. Alimponya kwa kumpaka tope kwenye macho yake na kumwambia akanawe katika birika la Siloamu.
Watu wengi waliamini kwamba upofu wa mtu huyu ulikuwa adhabu kutoka kwa Mungu. Ilikuwa ni imani ya kawaida katika utamaduni wa Kiyahudi wakati huo. Hata wanafunzi wa Yesu na makuhani waliamini kwamba Mungu aliwapiga watu magonjwa kama adhabu kwa dhambi zao au dhambi za wazazi wao.
Lakini Yesu aliwakosoa na kuwaambia kwamba upofu haukutokana na dhambi zake au dhambi za wazazi wake. Aliweka wazi kwamba sio kila ugonjwa au ulemavu ni matokeo ya kitu ambacho mtu amefanya.
2. Yesu anamponya mtu aliyepooza kwenye Birika la Bethesda (Yohana 5:1-15)
Kwa miaka 38, mtu aliyepooza alilala karibu na bwawa lililoitwa Bethesda huko Yerusalemu, bila mtu yeyote kumsaidia. Yesu alimtembelea na kumuuliza ikiwa anataka kuponywa, na wakati mtu huyo aliposema ndiyo, Yesu akamponya.
Baadaye, Yesu alimkuta hekaluni na kumwambia:
“Angalia, umekuwa mzima; usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi” (Yohana 5:14, NKJV).
Yesu alitaka kumrejeshea afya yake kimwili na kiroho. Pia alimtaka aendelee na mtindo wa maisha unaoimarisha afya.
Yesu aliwatia moyo wale aliowaponya kufanya kila wawezalo kudumisha afya njema. Na kwa wale ambao walikuwa na magonjwa yaliyosababishwa na mtindo mbaya wa maisha, aliwataka kubadili njia zao na kuepuka vitu vilivyosababisha magonjwa hayo.
3. Mtu aliyepooza anaponywa (Luka 5:17-26)
Siku moja, Yesu alipokuwa akifundisha katika nyumba iliyokuwa imejaa watu, mtu mwenye kupooza aliletwa na kundi la rafiki zake mpaka katika nyumba hiyo.
Lakini marafiki hao hawakuweza kupenya kwenye umati mkubwa ili kumfikia Yesu, hivyo wakapanda juu ya paa na kutengeneza tundu moja juu ya mahali alipokuwa
Yesu. Kisha, kwa utulivu wakamshusha yule mwenye kupooza…moja kwa moja mbele ya Yesu.
Yesu alipoona imani ya marafiki hao, akamwambia yule mtu:
“…umesamehewa dhambi zako” (Luka 5:20, NKJV).
Viongozi wa kidini walianza kuhoji kwa nini alikuwa amemsamehe yule mtu (Luka 5:21), lakini Yesu aliwaambia kwamba ana mamlaka ya kusamehe dhambi.
Kisha akaendelea na kumwambia mtu huyo:
“Nakuambia, Ondoka, ujitwike kitanda chako, ukaende zako nyumbani kwako” (Luka 5:24, NKJV).
Hapa tena, Yesu alionyesha shauku yake ya urejeshwaji wa kiroho na kimwili. Kwanza alishughulikia mzigo mkubwa zaidi wa dhambi ya mtu na kisha akamrejeshea afya ya mwili wake.
4. Yesu anaponya mwenye ukoma (Mathayo 8:1-3)
Ukoma katika Biblia kwa ujumla uliwakilisha aina mbalimbali za magonjwa mabaya ya ngozi ambayo ilikuwa vigumu kuyatibu.3
Katika utamaduni wa Kiyahudi, mara nyingi ilikuwa kutumika kama ishara ya kuelezea dhambi kwa sababu ya njia ilivyopatikana na kuenea kwa urahisi. Ilikuwa ni ugonjwa mbaya na wa kuambukiza sana, unaosababisha kuharibika kwa mwili.
Kwa kweli, wale wenye ukoma walilazimika kuishi kama watu waliotengwa. Hawakuruhusiwa kuwakaribia watu wenye afya, na hakuna aliyeruhusiwa kuwagusa pia.
Lakini kinyume cha vizuizi hivyo, mtu huyu mwenye ukoma alimwendea Yesu—alijisikia kuwa hii ndiyo nafasi yake pekee. Yule mwenye ukoma “akamsujudia, akisema, Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa” (Mathayo 8:2, NKJV).
Yesu pia alienda kinyume cha “sheria” zilizowekwa na kumgusa kwa huruma ili kumponya.
Lakini ili aweze kukubalika na jamii yote, Yesu alimwomba afanye “uchunguzi.” Makuhani wangemchunguza na kuthibitisha kwamba amepona kabisa na ni salama kuwa karibu naye (Mathayo 8:4).
Kwa kumwomba afuate taratibu hizi, Yesu alisaidia kumrejesha mtu huyo katika nafasi ya kukubalika katika jamii—jambo muhimu kwa uponyaji wa kijamii pia.
5. Yesu anamponya mwanamke aliyetokwa na damu kwa miaka 12 (Marko 5:25-34)
Mwanamke asiyejulikana alikuwa amekuwa akisumbuliwa na kutokwa na damu kwa miaka 12 bila kukoma. Katika jamii ya Kiyahudi, alikuwa mtu aliyetengwa. Alikuwa ameitumia pesa yake yote kwenda kwa madaktari na kujaribu kupata msaada, lakini hakuna kilichofanya kazi.
Yesu alikuwa tumaini lake la mwisho. Licha ya hadhi yake kijamii, alipenya katikati ya umati, akiwa na azimio la kumfikia Yesu. Alijiambia mwenyewe, “Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona” (Marko 5:28, NKJV).
Na alipofanya hivyo, aliponywa papo hapo.
Lakini alipojaribu kuondoka kimya kimya, Yesu aliuliza ni nani aliyemgusa. Hivyo mwanamke akaja mbele na kueleza kisa chake. Yesu akamthibitishia:
“Binti, imani yako imekuponya, enenda zako kwa amani, uwe mzima, usiwe na msiba wako tena” (Marko 5:34, NKJV).
Ni Mponyaji mwenye upendo kiasi gani!
Tunaweza kutiwa moyo kwamba tunapomwendea Mungu kwa imani na mahitaji yetu, Atatuhurumia, akituhakikishia amani yake pia.
6. Yesu aponya mtu aliyepagawa na pepo (Marko 5:1-20)
Katika nchi ya Wagerasi, Yesu alikutana na mtu mkali mwenye “pepo mchafu.” Alikuwa anaishi makaburini, na hakuna mtu aliyeweza kumfunga hata kwa minyororo. Alipiga kelele mchana na usiku na kujikata na mawe.
Yesu alipomkaribia, jeshi la pepo ndani yake likasema na kumtambulisha Yesu kama Mwana wa Mungu. Yesu kisha aliwaamuru waondoke na kuingia kwenye nguruwe waliokuwa wanachungwa karibu.
Baada ya pepo kutolewa, mtu huyo alikuwa “ameketi, amevaa nguo, na akili zake “ tena (Marko 5:15, NKJV).
Kisa hiki ni mfano wa mtu ambaye aliponywa kutokana na ugonjwa wa akili na kiroho wa kina. Yesu alimrejesha kabisa, akionyesha mamlaka yake kamili juu ya nguvu za mapepo.
Uponyaji wa wanafunzi wa Yesu na mitume wengine wa Agano Jipya
Wanafunzi wa Yesu pia walifanya miujiza ya uponyaji—wakati Yesu alipokuwa duniani na baada ya yeye kurudi mbinguni.
Hebu tuangalie baadhi ya mifano.
1. Wanafunzi wakiponya wakati Yesu alipokuwa nao.
Kulikuwa na nyakati mbili ambapo Yesu aliwatuma wanafunzi wake kuponya na kutoa pepo kwa jina lake. Matukio haya yapo katika Marko 6:7-13 na Luka 10:1-23.
Katika Marko 6:7-13, Yesu aliwatuma wanafunzi 12. Kama sehemu ya utume wao ilikuwa “wakatoa pepo wengi, wakapaka mafuta watu wengi waliokuwa wagonjwa, na wakawapoza” (Marko 6:13, NKJV).
Katika Luka 10:1-23, Yesu aliwatuma wanafunzi 70 kama wamishonari kwenda katika miji jirani. Waliporudi kutoka kwenye utume, waliripoti kwa furaha kwamba “hata pepo wanatutii kwa jina lako” (Luka 10:17, NKJV).
Visa hivi viwili ni ushahidi wa uponyaji usio wa kawaida unaweza kutokea kwa jina la Yesu. Kwa njia hii, Mungu anaweza kufanya kazi kupitia binadamu wengine kutuletea uponyaji.
2. Petro na Paulo wakiponya baada ya Yesu kupaa mbinguni
Waamini, kama vile Petro na Paulo, waliponya watu hata baada ya Yesu kupaa mbinguni.
Katika Matendo 3:1-10, Petro na Yohana walikutana na kilema ambaye hajawahi tembea kabla. Lakini Petro akamwambia, “kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende” (Matendo 3:6, NKJV). Na kwa mshangao wa kila mtu, yule mtu alisimama, “akaingia ndani ya hekalu pamoja nao, akienda, akiruka-ruka, na kumsifu Mungu” (Matendo 3:8, NKJV).
Mungu aliwaponya watu kupitia Paulo pia. “Mungu akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida, hata wagonjwa wakaletewa leso na nguo zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao yakawaondokea, pepo wachafu wakawatoka” (Matendo 19:11-12, NKJV).
Visa vyote viwili vinaonyesha uwezo wa Mungu wa kuponya usio na kikomo – kupitia watu wengine (au hata vitu ambavyo watu wengine wanagusa!).
Mbali na kuonekana katika Agano Jipya, hadithi za uponyaji pia zimeandikwa katika Agano la Kale.
Visa vya uponyaji vya manabii katika Agano la Kale
Uponyaji haukuanza wakati wa Yesu. Kabla ya hapo, Mungu alifanya kazi kupitia manabii ambao walifanya miujiza ya kushangaza, hata kuwafufua wafu.
Tutaangalia baadhi ya visa hivi:
1. Nabii Eliya anamponya mtoto wa mjane wa Sarepta (1 Wafalme 17:17-24)
Wakati wa njaa katika Israeli, nabii Eliya aliishi na mjane na mwanae katika eneo linaloitwa Sarepta. Mungu aliwapatia chakula ili wasife njaa.
Alipokuwa huko, mtoto wa mjane akawa mgonjwa na kufa, hivyo Eliya akamlilia Mungu, naye akamfufua mtoto wa mjane.
Kupitia muujiza huo, Mungu alieneza upendo na huduma yake kwa mwanamke huyu asiye Mwisraeli. Alijifunza kuhusu Mungu wa Israeli na akachagua kumwamini.
2. Nabii Elisha amponya mwana wa mwanamke wa Shunemu (2 Wafalme 4:8-37)

Photo by Zach Lucero on Unsplash
Wakati wa safari zake, nabii Elisha alikaribishwa na mwanamke tajiri huko Shunemu. Na kwa kuwa alikuwa tasa, Elisha aliomba kwa ajili yake apate mimba. Mungu alikubali ombi lake na kumpa mwanamke mtoto wa kiume.
Hata hivyo, mtoto alipokuwa akikua, alikufa ghafla akiwa kazini shambani wakati wa joto. Mama aliyejawa na huzuni alipanda punda na kukimbilia kumtafuta Eliya, ambaye alikuja na kumuombea mwanae afufuliwe.
Kama ilivyokuwa kwa mjane wa Sarepta, mwanamke wa Shunemu alipata upendo na huduma ya Mungu kupitia muujiza huo.
3. Nabii Isaya anamponya Mfalme Hezekia (2 Wafalme 20; Isaya 38)
Hezekia, mfalme wa Yuda, alipatwa na ugonjwa mbaya wa ngozi na alikuwa amekaribia kufa. Hata nabii Isaya alimjia na kumwambia ajitayarishe kwa kifo.
Lakini Hezekia alimgeukia Mungu na kuomba apewe neema. Mungu, kwa rehema yake ya uvumilivu, alimpa miaka 15 zaidi ya uhai. Kupitia Isaya, alimwagiza mfalme kuweka mkate wa tini kwenye jipu, kuponya ugonjwa.
4. Nabii Elisha akimponya jenerali wa Shamu, Naamani (2 Wafalme 5)
Jenerali wa Shamu aliyeitwa Naamani alisafiri hadi Israeli ili Elisha amponye ukoma wake.
Nabii Elisha, akimtukuza Mungu, alimwambia aende akoge katika Mto Yordani mara saba. Na alipofanya hivyo, aliponywa. Kwa kweli, ngozi yake ilikuwa afya hata zaidi kuliko ilivyokuwa kabla ya kuugua ukoma!
Kutoka katika kisa hiki, tunajifunza kwamba Mungu mara nyingine anaweza kutumia vitu vya kawaida sana kurejesha afya.
Mifano hii ya uponyaji inaweza kututia moyo kwamba Mungu bado anaponya watu hata katika hali ngumu. Lakini swali linaweza kuwa limejitokeza akilini mwako:
Vipi kuhusu wakati Mungu haponyi?
Wakati ambapo Mungu Haponyi
Wakati mwingine, tunaweza kujisikia kana kwamba Mungu hatuponyi sisi au mtu tunayempenda tunapomhitaji. Lakini tunaweza kuwa na imani kwamba Mungu ana maslahi yetu bora kabisa moyoni mwake; na tunaweza kuwa na hakika kwamba uponyaji utakuja—ingawa, kwa sababu mbalimbali, huenda usitokee kwa wakati wetu.
Tazama aya hii katika kitabu cha Yakobo kuhusu maombi ya uponyaji:
“Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kupaka mafuta kwa jina la Bwana. Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa” (Yakobo 5:14-15, NKJV).
Tunahakikishiwa kwamba “kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule.” Shauku kuu ya Mungu ni kutuokoa na kutupa uzima wa milele.
Lakini kwa sasa, tunaishi katika ulimwengu wenye dhambi – ulimwengu ambapo kuna wema na uovu. Ugonjwa na maradhi ni sehemu ya ukweli huo wa kusikitisha.
Mara nyingi, hatutaelewa kwanini hatuponywi. Na hilo ni jambo gumu!
Lakini kuna jambo moja ambalo tunaweza kuwa na uhakika nalo: Mungu anaweza kuchukua hali ngumu zaidi na kuzitumia kwa mema (Warumi 8:28). Hatakuacha upitie maumivu au ugonjwa peke yako (Waebrania 13:5-6).
Hata katika Biblia, tunakuta nyakati ambazo watu waliomba uponyaji – na kutamani huo uponyaji – lakini hawakuponywa. Au uponyaji ulichukua muda mrefu kuliko ulivyotarajiwa.
Paulo alikuwa mmoja wao.
Alikuwa na tatizo – aliloliita “mwiba katika mwili” (2 Wakorintho 12:7, NKJV) – ambacho baadhi ya wanachuo wanadhani kilikuwa kinahusiana na kuona kwake. Aliomba kwa Mungu mara tatu ili akiondoe (aya ya 8).
Lakini Mungu hakukiondoa.
Badala yake, Mungu alimwambia Paulo kwamba hata alipokuwa akihangaika na udhaifu huo, neema ya Mungu ingetosha kwake. Kupitia udhaifu, Paulo angegundua nguvu ya Mungu ikidhihirishwa kwa ukamilifu zaidi ndani yake (2 Wakorintho 12:9).
Vivyo hivyo, wakati maombi yetu ya uponyaji hayajibiwi, sio lazima iwe kwa sababu ya yale tuliyoyafanya au hatukuyafanya. Inaweza kuwa ni jambo ambalo Mungu analitumia kutufanya tuwe na nguvu zaidi ndani Yake.
Kisha, kuna kisa cha Lazaro.
Lazaro, rafiki wa karibu wa Yesu, alikuwa na ugonjwa hatari wa kufisha. Dada zake walituma ujumbe kwa Yesu wakimwomba aje, bila shaka wakitarajia angemponya ndugu yao.
Lakini Yesu hakwenda kwa siku nyingine nne. Na wakati huu, Lazaro alikuwa amekufa.
Yesu alipofika, aliwaonyesha dada waliokuwa wanahuzunika kwamba alikuwa na mpango mkubwa zaidi kwa kumfufua Lazaro.
Alitumia tukio hili kutekeleza muujiza wake wa kushangaza zaidi na kufundisha somo muhimu kuhusu ufufuo.
Kwa hivyo, mara nyingine uponyaji unachukua muda mrefu. Lakini hata hivyo, Mungu bado ana mpango unaofunua utukufu wake (Yohana 11:4) na kuleta matokeo mazuri.
Kwa hivyo, unapoomba kwa ajili ya uponyaji, faraja, na amani, dai ahadi zake kwa ajili yako na marafiki zako ambao ni wagonjwa. Kwa njia moja au nyingine,
Ataponya, atarejesha, na kuimarisha!
Ahadi za Biblia kwa ajili ya uponyaji

Photo by Marc-Olivier Jodoin on Unsplash
Biblia ina ahadi nyingi za urejeshwaji wa kiafya—kimwili, kiakili, na kiroho.
Na ahadi hizi ni kwa kila mtu, hata kama wewe sio Mkristo. Mungu yuko tayari kumponya yeyote anayekuja kwake kwa imani (Mathayo 8:5–13).
Kama vile Mungu alivyowaambia Waisraeli, Anakuambia, “Mimi ndimi BWANA nikuponyaye” (Kutoka 15:26, NKJV).
Aliahidi kwamba kama wangebaki waaminifu kwake, “nami nitakuondolea ugonjwa kati yako” (Kutoka 23:25, NKJV).
Na hii ni ahadi yake kwetu pia.
Ikiwa unapambana na ugonjwa, jua kwamba “Bwana atamtegemeza alipo mgonjwa kitandani. Katika ugonjwa wake umemtandikia” (Zaburi 41:3, NKJV).
Ikiwa moyo wako umevunjika, unaweza kufarijiwa kwamba “Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, Na waliopondeka roho huwaokoa” (Zaburi 34:18, NKJV).
Na ikiwa unapambana na majuto na hatia, unaweza kumsifu Bwana “akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote, Aukomboa uhai wako na kaburi, Akutia taji ya fadhili na rehema” (Zaburi 103:3–4, NKJV).
Katika hali yoyote unayopitia, Anasema:
“Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu” (Mathayo 11:28–29, NKJV).
Mungu anataka upate uponyaji
Maradhi—iwe ni ugonjwa wa kinga ya mwili usioeleweka, mapambano ya mara kwa mara ya saratani, au ulemavu wa muda mrefu—kamwe sio rahisi. Na Mungu anaelewa hilo. Yeye yupo hapo kutembea pamoja nawe, kukutia moyo, na kukutia nguvu.
Unaweza kumwamini Mungu hata katika nyakati hizi ngumu kwa sababu siku moja, Mungu atatimiza ahadi yake ya mwisho kwetu—ahadi ya kutuokoa kutoka ulimwengu huu wa dhambi na mateso. Na ahadi ya kutupa mwili ambao kamwe hautakuwa mgonjwa tena au kuzeeka (1 Wakorintho 15:53–55).
Na wakati Mungu atakapokomesha dhambi yote, atatufariji milele kwa yote tuliyopitia:
“Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita” (Ufunuo 21:4, NKJV).
Biblia inaonyesha picha ya Mungu ambaye anataka uponyaji wako zaidi kuliko wewe mwenyewe.
Zaidi ya kutuponya, Yeye hutupa ahadi za kututia moyo. Pia Hutupatia hekima ya kutafuta aina sahihi ya huduma na kuishi kulingana kanuni za msingi kwa mtindo wa maisha wenye afya.
Ili kujifunza zaidi kuhusu kanuni hizi zilizojikita katika kanuni,
Chagua Masomo ya Biblia Mtandaoni
Unataka kuendelea kujifunza? Pata habari zaidi kuhusu Yesu, mwanadamu, mpango wa wokovu, na jinsi Mungu anavyokupenda kiasi cha kutosha kujitolea kila kitu, ili tu kukupatia nafasi ya kumchagua.
Wakati mwingine inaweza kuwa ngumu kujua pa kuanzia, ndio maana tunatoa chaguo za masomo ya Biblia mtandaoni bure, rahisi kutumia, unaweza kufanya wakati wowote, mahali popote, na kwa kasi yako mwenyewe.
Shule hii ya Biblia mtandaoni itakuelekeza kupitia mada kuu za Maandiko, ikivunja dhana ngumu za Biblia katika vipande vidogo, ambavyo vinaweza kukusaidia kupata majibu ya maswali magumu zaidi ya maisha.
- 1 Kings 19; Luke 10:38–42; Psalm 35; 86; Jeremiah 20:14-18 and Lamentations 3:1-8 [↵]
- “Heart,” Strong’s Expanded Exhaustive Concordance of the Bible (Nashville: Thomas Nelson, 2009). [↵]
- Francis D. Nichol, The Seventh-Day Adventist Bible Commentary, Volume 1, pp. 758-763 (Washington, DC: Review and Herald Publishing Association, 1953). [↵]
Majibu Zaidi
Biblia Inasema Nini Kuhusu Deni?
Kuwa na wasiwasi kuhusu deni la kifedha kunaweza kutufanya tuamke tukiwa na kijasho chembamba.


