Pambano Kuu” ni msemo ambao Waadventista wa Sabato kawaida huutumia kuelezea mgogoro wa kiroho wa ulimwengu kati ya nguvu za mema (Mungu) na nguvu za uovu au dhambi (Shetani/iblis).
Ni sababu dunia yetu ina mabaya na mema ndani yake kwa wakati mmoja, yakipingana daima.
Hili ni fundisho muhimu katika Kanisa la Waadventista Wa Sabato linapokuja suala la kufafanua na kutafsiri Maandiko. Hivi ndivyo inavyoelezwa katika Imani Zetu za Msingi:
Mgogoro huu ulianzia mbinguni wakati kiumbe aliyepewa uhuru wa kuchagua, kwa kujitukuza mwenyewe alikuwa Shetani, adui wa Mungu, na kuongoza sehemu ya malaika katika uasi.
Aliingiza roho ya uasi katika ulimwengu huu alipowaongoza Adamu na Hawa katika dhambi. Dhambi hii ya binadamu ilisababisha upotoshaji wa sura ya Mungu kwa mwanadamu, kuchanganyikiwa kwa ulimwengu ulioumbwa, na uharibifu wake wa mwisho wakati wa gharika ya ulimwengu, kama ilivyoelezwa katika akaunti ya kihistoria ya Mwanzo 1-11.
Ulimwengu huu, ukiangaliwa na viumbe vyote, ukawa uwanja wa mzozo wa malimwengu, ambao katika huo Mungu wa upendo hatimaye atathibitishwa kuwa sahihi. Ili kuwasaidia watu Wake katika mzozo huu, Kristo anatuma Roho Mtakatifu na malaika waaminifu kuwaongoza, kuwalinda, na kuwategemeza katika njia ya wokovu.
Hivyo vita vya kiroho inayojumuisha kila kitu ndiyo iko nyuma ya kila kitu kibaya katika ulimwengu wetu. Tunakutana na pande zote za tofauti ya mema na mabaya, upendo na dhambi, ubinafsi na ukarimu. Na ni juu yetu kila siku kuamua tunavyoendelea katika ulimwengu ambapo “tunajua mema na mabaya”—yote yamechanganyika pamoja (Mwanzo 3:1-7, 22-24).
Lakini kwa nini mambo yako hivi? Na tunapaswa kuitikiaje ukweli kuhusu mgogoro tunaoishi ndani yake?
Hebu tuchambue mada hii.
Tutaangalia:
- Nini kinatokea katika mgogoro huu kati ya Mungu na Shetani
- Jinsi mambo yote yalivyoanza
- Jinsi ulivyoishia duniani
- Kwa nini Mungu hakumwangamiza Shetani mwanzoni
- Jinsi Pambano Kuu litakavyoisha
- Tunaweza kujifunza nini kuhusu Pambano Kuu kutoka katika huduma ya Yesu
- Kwa nini dhambi bado ni sehemu ya maisha, ingawa Yesu tayari alikufa msalabani
- Ikiwa tunapaswa kumogopa Shetani
Kwanza, hebu tupate wazo la jumla la kinachoendelea katika mgogoro huu kote katika historia—na hata leo.
Nini kinachotokea katika Pambano Kuu kati ya Mungu na Shetani?

Photo by Pixabay
Katika maisha yetu ya kila siku, tunakutana na mfululizo wa chaguzi.
Baadhi ni zia athari ndogo au hazina, kama vile ni kipi cha kula wakati wa kifungua kinywa. hata Hatufikirii mambo haya kama “maamuzi.
Lakini bila shaka tunahisi uzito wa maamuzi makubwa yanayotegemea maadili yetu. Je, tunadanganya kwenye kodi zetu ikiwa tunaweza kuepuka kwa urahisi? Tunawezaje kumtendea mwanafamilia mhitaji mwenye changamoto katika mipaka? Tunapaswa kuitikiaje vipi kwa kauli ya kashfa kutoka kwa msimamizi kazini? Je, tunapaswa kuripoti uhalifu tulioshuhudia, hata kama ulifanywa na rafiki mwema?
Na sehemu mbaya zaidi ya baadhi ya maamuzi haya ni kwamba mara nyingine inaonekana hakuna jibu “sahihi”. Daima kuna mabadilishano, daima kuna hasara kadhaa kwa faida, daima kuna hatari kwamba mambo yanaweza kuwa mabaya bila kujali unachofanya.
Lakini msukumo huu wa mara kwa mara tunaoijisikia katika dhamiri zetu unahusiana na kuishi katika ulimwengu ambapo mema na mabaya yapo pamoja, yote yakiwa yamechanganyikana.
Na nyuma ya pazia, nguvu mbili zinazopingana zinataka kuathiri maamuzi yetu.
Mungu anataka kutuongoza. Shetani anataka kutudanganya.
Mungu daima atatukubali na kutupatia ukweli. Lakini kamwe hatatulazimisha kufuata mwongozo wake. Upendo hauwezi kutokea kwa kutumia nguvu.
Lakini Shetani anatumia fursa hii na kutushawishi kufanya maamuzi na tabia zinazojali masilahi yetu binafsi ambazo mwishowe zinatupeleka kuelekea uharibifu.
Vurugu iliyoje.
Ndio sababu, hata bila kuzingatia dini na hali ya kiroho, kuna hadithi, nadharia, mashairi marefu, hadithi za kishujaa, na hadithi za maajabu kuhusu mapambano ya daima ya wema dhidi ya uovu. Haijalishi ni nini watu wanaita jema au baya, ni wazi kwamba mapambano hayo ni halisi.
Vita ilianza muda mrefu uliopita, katika sehemu nyingine ya Uumbaji, sasa inachezwa hapa duniani kwa sababu Mungu alituumba kama viumbe wenye uhuru wa kuchagua – uwezo wa kuchagua wenyewe.
Wengine wanasema mapambano haya yanatokana na nguvu za asili na za kihistoria, au matokeo ya nguvu mbalimbali za kisiasa, kiuchumi, na kijamii zinazoendelea. Wengine wanachukulia kama kuendelea kwa mchakato wa uibukaji ambapo maisha yanapambana kwa ajili ya kuwepo.
Na wengine wanachukulia mapambano kati ya mema na mabaya kuwa ni ya kisaikolojia tu. Wanayaona kama mgogoro wa ndani unaotokana na akili ya binadamu, ambao kisha unachezwa katika maigizo ya uwepo wa binadamu.
Kwa njia moja au nyingine, sote tunakiri kwamba nguvu za maadili zinazopingana zipo kazini.
Huo huenda ndio sababu mshairi T.S. Eliot aliandika:
Dunia inageuka na dunia inabadilika,
Lakini kitu kimoja hakibadiliki.
Katika miaka yangu yote, kitu kimoja hakibadiliki.
Hata ujifiche vipi, kitu hiki hakibadiliki:
Mapambano ya milele kati ya Mema na Mabaya.1
Hata mtu asiyeamini kuwa kuna Mungu kama Mjerumani Frederick Nietzsche aliona hili:
“Hebu tuhitimishe. Thamani mbili zinazopingana ‘nzuri na mbaya,’ ‘nzuri na ovu’ zimekuwa zikipigana vita vikali duniani kwa maelfu ya miaka; na ingawa thamani ya pili imekuwa juu kwa muda mrefu, bado kuna maeneo ambapo vita bado haijaamuliwa.”2
Na Biblia ina mengi ya kusema kuhusu ulimwengu uliojaa dhambi tunaoishi ndani yake.
Mtume Paulo anaelezea hali ya mkanganyiko wa kutaka kufanya mambo yote sahihi na kufuata Sheria ya Mungu kikamilifu lakini kukosa nguvu ya kufanya hivyo kwa ukawaida.
“Maana sijui nifanyalo, kwa sababu lile nilipendalo, silitendi; bali lile nilichukialo ndilo ninalolitenda…Basi nimeona sheria hii, ya kuwa kwangu mimi nitakaye kutenda lililo jema, lipo lililo baya. Kwa maana naifurahia sheria ya Mungu kwa utu wa ndani, lakini katika viungo vyangu naona sheria iliyo mbali, inapiga vita na ile sheria ya akili zangu, na kunifanya mateka ya ile sheria ya dhambi iliyo katika viungo vyangu” (Warumi 7:15, 21-23, SUV).
Paul pia anasisitiza ukweli kwamba hili si pambano la nguvu au azimio. Tuko katikati ya vita kati ya nguvu za kiroho. Ndio maana tunahitaji msaada wa kiroho kutoka kwa Mungu.
“Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho” (Waefeso 6:12, SUV).
Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze. Nanyi mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kuwa mateso yale yale yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani” (1 Petro 5:8-9, SUV).
Maelezo yote haya yanaweza kuonekana kuwa ya kutisha. Lakini hata tunapoendelea kupitia maelezo haya kuhusu mada ya Pambano Kuu, kumbuka kwamba Mungu yuko upande wetu. Anataka tuweze kushinda nguvu za kiroho za Shetani ambazo hazitutakii mema. Ndiyo maana anatupatia ahadi nyingi katika Maandiko na kutuambia tuombe daima ili tuweze kushinda juhudi za Shetani na kusimama “imara katika imani.
Sasa tugeuke nyuma kuangalia jinsi mambo yalivyogeuka kuwa yalivyo.
Pambano Kuu lilianzia wapi?

Pambano Kuu kati ya Yesu Kristo na Shetani lilianzia mbinguni.
Yohana alielezea mwanzo wa vita hii katika kitabu cha Ufunuo aliposema:
“Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake” (Ufunuo 12:7, SUV).
Vita mbinguni kati ya viumbe vya mbinguni?
Ndio, Biblia inafundisha kwamba maisha duniani siyo maisha pekee katika ulimwengu. Kwa mfano, mtume Paulo alizungumzia akili nyingine zisizo za duniani:
“ili sasa, kwa njia ya kanisa, hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ijulikane na falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho” (Waefeso 3:10, SUV).
(Aya nyingine zinazozungumzia ukweli wa maisha mengine katika ulimwengu ni pamoja na: 1 Wakorintho 4:9; Mathayo 18:10; Wakolosai 1:16,17; Ayubu 1:6, 7; 38:7).
Na maisha yote haya—siyo tu duniani bali pia katika ulimwengu mzima—yaliumbwa na Mungu mwenye upendo. Lakini kwa nini ni muhimu kwetu kujua kwamba Mungu ni Mungu wa upendo?
Kwa sababu kuelewa upendo wa Mungu ni muhimu katika kumwelewa Mungu Mwenyewe, mwanadamu, na kuzaliwa kwa pa,mbano hili.3
Upendo ni kanuni kuu inayoongoza jinsi Mungu anavyohusiana na viumbe vyake. Hili linaonekana katika aya maarufu, Yohana 3:16:
“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee” (SUV).
Na kama matokeo ya moja kwa moja ya Upendo wake, Aliwaumba viumbe wake wote wakiwa wenye akili na uwezo wa kupenda pia.
Lakini ili upendo uwe upendo wa kweli, hauwezi kulazimishwa. Lazima utolewe kwa hiari. Hivyo, uhuru huu wa kimaadili tulionao ni kanuni msingi ambayo Mungu amewapa viumbe wote wenye akili, iwe mbinguni au duniani.
Mwanazuoni wa Kiadventista Frank Holbrook aliandika:
Mungu aliumba viumbe vyote vyenye akili kama mawakala huru wa maadili wenye uwezo wa kumpa Mwumbaji utiifu wa upendo au kukataa mamlaka yake.4
Biblia inaeleza matukio ya kwanza ya kutumia vibaya uhuru huu na malaika anayeitwa Lusifa. Labda andiko linalofunua zaidi kuhusu Lusifar linapatikana katika kitabu cha Agano la Kale cha Ezekiel:
“Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; nami nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, umetembea huko na huko kati ya mawe ya moto. Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako” (Ezekieli 28:14-15, SUV).
Huyu alikuwa kiumbe wa mbinguni, malaika aliyeumbwa na Mungu. Na alikuwa mkamilifu. Mungu hangeweza kuumba kitu ambacho si kamili.
Lakini ukamilifu huu haukudumu. Lusifa, au Shetani kama alivyoitwa baadaye, alikuwa mkamilifu mpaka “uovu,” au tabia iliyopinda kuelekea dhambini,5 ilipoonekana ndani yake.
Kiumbe kamili, kilichoumbwa na Mungu kamili, katika mbingu kamilifu? Kwa nini uovu uonekane ndani yake?
Yote inarejea kwa upendo na uhuru ambao Mungu anatupatia katika upendo.
Lusifa kama kiumbe kamili pia alilazimika kuwa kiumbe huru, kiumbe mwenye uwezo wa kupenda. Kuwa kamili kunahitaji kuwa huru. Hivyo kwa sababu alikuwa huru, uhuru huo ulimruhusu kuwa na uwezo wa kutunza mawazo yaliyompelekea kuasi dhidi ya Mungu.
C.S. Lewis anaelezea kwa nini aina hii ya uhuru ni muhimu:
Ikiwa kitu ni huru kinapaswa kuwa chema, pia kiko huru kuwa kibaya. Na nia huru ndiyo iliyowezesha uovu.
Kwa nini basi Mungu aliwapa nia huru? Kwa sababu nia huru, ingawa inawezesha uovu, pia ndiyo kitu pekee kinachowezesha upendo au wema au furaha yenye thamani ya kuwa nayo.
Dunia ya automata—ya viumbe ambao wanafanya kazi kama mashine—ingekuwa haina thamani ya kuumbwa. Furaha ambayo Mungu anapanga kwa viumbe wake wa juu ni furaha ya kuwa huru, kwa hiari, wakiungana naye na kati yao katika unyakuo wa upendo na furaha ambao ukilinganishwa na upendo wa kipekee kati ya mwanaume na mwanamke duniani hapa ni maji na maziwa tu. Na kwa hilo wanapaswa kuwa huru.6
Kwa kutumia uhuru huu, Lusifa alikosa kuridhika na nafasi yake ya juu kama kerubi mlinzi, na alitaka zaidi. Hivyo akapinga nafasi ya Mungu, na bado hajakoma katika hili, hata leo. Amejizatiti, na hataki kusalimu amri.
Katika taswira ya kishairi ya wafalme wa kidunia, Biblia inatuambia kile kilichotokea na Lusifa mbinguni na jinsi alivyoasi:
“Moyo wako uliinuka kwa sababu ya uzuri wako; umeiharibu hekima yako kwa sababu ya mwangaza wako” (Ezekiel 28:17, SUV).
Inasema pia haya kuhusu Lucifer:
“Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, Katika pande za mwisho za kaskazini. Nitapaa kupita vimo vya mawingu, Nitafanana na yeye Aliye juu.” (Isaya 14:13, 14, SUV).
Kwa namna fulani, katikati ya kina cha akili yake, Lusifa alitamani kuwa Mungu Mwenyewe. Na kadri mawazo hayo yalivyomtawala, ndivyo ilivyoanza hadithi ya dhambi na Pambano Kuu.
Ikiwa Pambano Kuu lilianzia mbinguni, liliishiaje duniani?

Photo by Georgia de Lotz on Unsplash
Mgogoro huu wa kipekee ulihamia duniani kwa sababu wanadamu walikuwa huru pia kuchagua matendo na uaminifu wao. Kwa kuwa Shetani aliwakilisha upinzani dhidi ya Mungu, alimshawishi Adamu na Hawa katika Bustani ya Edeni kwa kutumia “ujuzi wa mema na mabaya,” nao wakakubali (Mwanzo 3).
Ufunuo 12:7-9 unasimulia jinsi Shetani alivyofika duniani mara ya kwanza baada ya uasi wake mbinguni.
Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake; nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni. Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye” (SUV).
Kisha, Mwanzo 3 inaeleza kisa cha jinsi Adamu na Hawa, walioumbwa kama malaika kama mawakala huru wa maadili, walitumia uhuru huo kwa masilahi yao ya ubinafsi kwa ushawishi wa Shetani (ona pia Ufunuo 12:9; 20:2-3).
Na kama vile Lucifer mbinguni alivyoanguka kwa sababu alitaka kuwa kama Mungu, alitumia kilichomtokea mbinguni kumjaribu na kumdanganya binadamu wa kwanza duniani.
Alimwambia Hawa kwamba kama angekula matunda ya mti uliokatazwa, angekuwa kama Mungu, akijua mema na mabaya (Mwanzo 2:17; 3:5).
Kile kinachofanya hili kuwa la kusikitisha zaidi ni kwamba Adamu na Hawa tayari walikuwa wameumbwa “kwa mfano wa Mungu” (Mwanzo 1:27, SUV).
Hivyo, kwa namna fulani, tayari walikuwa kama Mungu.
Lakini tunaelezwa kwamba Shetani alikuwa “mwerevu” hata akichagua kuchukua umbo la nyoka mwenye uzuri, mng’ao (sana tofauti na nyoka wa leo). Lakini tabia yake ilikuwa bila shaka kama ile ya nyoka. Alichanganya ukweli na kosa—aina ya uongo ambao ni rahisi zaidi kuangukia.
Alianza kwa kunukuu vibaya amri ya Mungu, akijua kwamba Hawa angekuwa na uwezo wa kumrekebisha (linganisha Mwanzo 2:16-18 na Mwanzo 3:1-3).
Hivyo akawafanya wanadamu wa kwanza wadhani kwamba wana udhibiti wa mazungumzo.
Kisha aliwaambia sehemu ya kile ambacho kingetokea kweli ikiwa wangekula matunda kutoka kwa mti uliokatazwa. Aliwaahidi kwamba ikiwa wangekula tunda, wangekuwa “kama Mungu” kwa namna maalum sana – “kujua mema na mabaya” (Mwanzo 3:4-5, SUV).
Na hii ilikuwa matokeo halisi na jina kamili la mti. Kwa hivyo hakuwa hata akidanganya kuhusu sehemu hiyo. Hakuwa na haja ya kufanya hivyo.
Adamu na Hawa huenda walivutwa na upya wa wazo lenyewe. Hakukuwa na kitu kama hicho kilichowahi kuwapata hapo awali. Na hawakuwa wamepitia uzoefu wa “mabaya” ambayo sasa yanazungumziwa.
Ongeza kujaribiwa kuwa “kama Mungu,” ambayo pia ilikuwa wazo jipya na lenye kuvutia.
Na kwa vipande hivi vichache vya mazungumzo vilivyotolewa kwa njia iliyopangwa kwa uangalifu, Shetani aliweka shaka akilini mwa wanadamu wa kwanza. Aliashiria kwamba Mungu alikuwa akijionyesha kuwa mwenye ubinafsi, asiyeaminika, na anazuia kitu kutoka kwa wanadamu ambao alidai kuwapenda.
Hivyo hapa tunaweza kuona kwamba Vita Kuu ilianza kwanza mbinguni na Lucifer, lakini alileta uasi huu duniani baada ya kufukuzwa mbinguni na kuitwa “Shetani.
Kwa nini Mungu hakumwangamiza Shetani mara tu alipoasi?
Mfano unaweza kusaidia kujibu swali hili la haki.
Tuseme ungekuwa kiongozi mwema unayeipenda nchi yako. Kwa sababu isiyo ya haki na isiyo ya kweli, mtu fulani alianzisha uasi na kukushutumu kuwa mkatili, asiye na haki, na mwonevu.
Je, utajibu mashtaka haya kwa kuangamiza tu waasi?
Ndio, huenda umemaliza uasi, lakini vipi kuhusu mashtaka yaliyowasilishwa dhidi yako?
Kwa kuua waasi, ungekuwa umethibitisha tu mashtaka yao. Unaweza kuitwa mkatili, asiye na haki, na mwonevu.
Lakini kama tulivyoona, Maandiko yanafundisha kwamba Mungu ni Mungu wa upendo, wala halazimishi viumbe vyake kumfuata.
Badala yake, kwa haki, Mungu anaruhusu kanuni za Shetani na uasi kufanyika mbele ya macho ya ulimwengu (Waefeso 3:10; 1 Wakorintho 4:9; Ufunuo 15:3).
Kwa njia hiyo, tutajua kwa kweli kinachotokea tukichagua njia nyingine. Vinginevyo hakuna mtu yeyote ambaye angeweza kusema hivyo.
Pambano Kuu litaishaje?

Photo by Alicia Quan on Unsplash
Waadventista wanaamini kwamba sehemu kuu ya Pambano Kuu ni maisha na huduma ya Yesu, na kilele chake kilikuwa msalabani.
Yesu alipouawa kikatili akiwa hana hatia kabisa, hatima ya dhambi iliamuliwa mara moja na kwa wote.
Turudi nyuma kwenye mfano wa kiongozi ambaye alishtakiwa na waasi kuwa mkali, asiye na haki, na dhalimu
Je, ikiwa, ili kujibu mashtaka, kiongozi huyu alishuka kwa hiari hadi kwenye kiwango cha watu wake wote? Je, ikiwa aliishi kati yao, akateseka kati yao, na hata akatoa maisha yake kwa ajili yao?
Hii ingesemaje kuhusu mashtaka dhidi yake?
Hili lingefuta mashtaka yote
Na ikiwa yule aliyemtuhumu kiongozi kuwa mkatili ndiye aliyemuua kwa njia isiyo ya haki?
Je, hilo halitamfanya mpinzani kuwa asiye haki badala yake?
Ingawa ni mfano tu, hii inaonyesha jinsi Yesu alivyojibu mashtaka ya Shetani dhidi yake.
Tunawezaje kuona Pambano Kuuu katika huduma ya Yesu?
Vita kati ya Kristo na Shetani inafunuliwa katika maisha na kifo cha Yesu.
Kama mfano, tunaona kwamba mara baada ya ubatizo wake, Pambano Kuu lilionekana wakati Shetani alipomjaribu Yesu jangwani (Mathayo 3:13-17; 4:1-11).
Shetani, ambaye ni kiumbe wa kiroho, alijaribu kumjaribu Yesu mara tatu. Shetani alijaribu kumfanya Yesuatilie mashaka utambulisho wake, alimshawishi kwa mahitaji yake ya kidunia, na kumkengeusha kutoka kwenye utume wake.
Lakini mara zote tatu, Kristo alimshinda Shetani, ambayo ilikuwa ishara ya kushindwa kwa Shetani mwishoni mwa wakati (Ufunuo 20:10).
Katika huduma yake yote duniani, Yesu mara nyingi alirejelea kwa Shetani—au kukabiliana na kushinda nguvu za kishetani—katika muktadha wa Pambano Kuu (Mathayo 12:26; Marko 4:15; Luka 10:18; 22:3, 31).
Wakati mmoja, Yesu alipokutana na mtu aliyekuwa ameshikwa na mapepo, mapepo yalilia:
“Tuna nini nawe, Mwana wa Mungu? Je! Umekuja kututesa kabla ya muhula wetu?” (Mathayo 8:29, SUV).
Wazi kabisa, Yalielewa kuwa hayakuwa na uwezo dhidi ya Yesu.
Kisha, kitabu cha Matendo kinazungumzia “jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye” (Matendo 10:38, SUV).
Kabla tu ya Msalaba, Yesu alisema kwamba kifo chake mwenyewe kingepelekea ushindi dhidi ya Shetani.
“Sasa hukumu ya ulimwengu huu ipo; sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje” (Yohana 12:31, SUV).
Ni pale Msalabani ambapo Shetani alishindwa milele. Pia, alifunuliwa mbele ya ulimwengu kwa kile alichokuwa kweli:
Msalabani, Shetani (ikiwa ni pamoja na malaika wengine walioanguka) alionekana wazi katika mwanga wake halisi kama mpinga Kristo na muuaji. Tunaweza kudokeza kwamba uhusiano wowote wa huruma bado ukiwepo akilini mwa viumbe wa mbinguni kwa ajili ya kusudi la Shetani ulivunjwa milele.7
Ikiwa Shetani alishindwa msalabani, kwa nini dhambi bado ipo leo?

Photo by Kindel Media
Hata baada ya kushindwa kwa Shetani msalabani, ambayo ilihakikisha uharibifu wake wa mwisho, hadithi ya mwanadamu bado inaendelea. Yapo mengi zaidi ya kuonyesha kuhusu tabia ya Mungu, na ukombozi wa wetu pamoja bado haujakamilika.
Uhuru wetu wa kuchagua bado upo. Na kusitisha mgogoro huu haraka kutatuzuia sote tusiokolewe, au hata tusiweze kusamehewa.
Waefeso 3:10 inasema kwamba “ili sasa, kwa njia ya kanisa, hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ijulikane na falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho” (SUV).
Kutokana na uasi wa awali wa Shetani, viumbe vingine vya mbinguni vinaweza bado kuwa na shaka kuhusu tabia ya Mungu. Na wanadamu pia. Kwa hivyo, ili kumaliza mashaka ghayo, kila mtu lazima aone mwisho wa dhambi na hekima na ushindi wa Mungu kutoka katika mtazamo wa ubinadamu.
Ili kurahisisha hilo, bado tuna chaguzi za kufanya. Hata baada ya kujua kuhusu huduma ya Yesu duniani, bado tunaweza kufanya chaguo la mwisho la mahali tunapoweka uaminifu wetu. Ni kwa Mungu, Muumba wetu? Au mahali pengine?
Mwishoni mwa wakati, baada ya hukumu za Mungu kutolewa, viumbe wa mbinguni huimba:
“Naam, Bwana Mungu Mwenyezi, ni za kweli, na za haki, hukumu zako” (Ufunuo 16:7; 19:2, SUV).
Hivyo, hata baada ya Msalaba, kuna zaidi kwa wanadamu na ulimwengu kuona na kuelewa kuhusu Pambano Kuu, ikiwa ni pamoja na jinsi Mungu anavyohukumu. Hafichi chochote —Anataka sisi sote tujue na kuelewa.
Agano Jipya, lililoandikwa baada ya Msalaba, linafunua ukweli unaendelea wa Pambano Kuu
“Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu” (Ufunuo 12:12, SUV).
Uovu wote, mateso, na vurugu duniani yatafunua hasira ya Shetani, na kwamba yeye hataanguka bila kupigana.
Baada ya yote, wanadamu walichagua “kujua mema na mabaya.” Sasa bila shaka tunashuhudia na kujifunza kuhusu maana halisi ya kuchagua kati ya hayo mawili kila siku.
Kumbuka onyo la Petro:
“Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze” (1 Petro 5:8, SUV).
Hata baada ya Msalaba, Shetani anaendelea kufanya kazi, akitafuta kumwongoza mbali yule anayeweza kabla ya siku za mwisho.
Je, tunapaswa kumwogopa Shetani?

Photo by Nik Shuliahin 💛💙 on Unsplash
Jambo la kushukuru, la! Mungu hataki tuishi kwa hofu—Anataka tuishi kwa imani.
Waadventista wanashikilia wazo la Kibiblia kwamba Shetani ni adui aliyeshindwa na yeyote anayechagua kumfuata Yesu atapata msaada na ulinzi dhidi ya Shetani. Mkristo anahimizwa kuwa mwangalifu kuhusu nia na njia za shetani, lakini asidhoofishwe na hofu wakati anapoendelea na maisha ya kila siku.
Paul anatutia moyo katika Waefeso:
“Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho” (Waefeso 6:11-12, SUV).
Hoja ya Paulo hapa ni kwamba kupitia Kristo, tunaweza kupata ushindi dhidi ya shetani. Kwa nguvu zetu wenyewe, hatuna ulinzi, lakini tunapomwita Mungu, Yeye hutupatia nguvu inayohitajika kwa hali hiyo (1 Wakorintho 10:13).
“Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia” (Yakobo 4:7, SUV).
Ndio, uovu bado unatokea, na ugonjwa na kifo bado ni sehemu ya uuhalisia wa maisha yetu ya sasa, lakini mwishowe, wote waliomo katika Kristo wana uhakika wa ushindi sasa. Tunaweza kusema kama Paulo:
“Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu” (Wafilipi 4:13, SUV).
Na tunaahidiwa umilele pamoja na Yesu katika mbingu mpya na nchi mpya (Isaya 66:22; 2 Petro 3:13; Ufunuo 21:1).
Kwa sasa, tunaishi tukiwa tunajua kwamba Pambano Kuu ni halisi. Lakini haijalishi tunachukia uovu kiasi gani, hatupaswi kuchanganyikiwa na uwepo wake unaotisha.
Tunaweza kuwa macho na waangalifu (1 Petro 4:7) huku tukitambua kwamba Yesu ameshinda ushindi muhimu kwa ajili yetu msalabani.
Na mwishowe, baada ya siku za mwisho, Yesu atawaita wafuasi wake wapendwa ili wakutane naye katika mawingu ili waende mbinguni, tunaweza kuwa na hakika tutarejeshwa katika ukamilifu (1 Wathesalonike 4:17; 1 Wakorintho 15:35-58).
Na baada ya hayo, hatutatenda dhambi tena—kwa maana tutakuwa tumeona uhalisia wa maana ya kujua mema na mabaya.
Jifunze zaidi kuhusu mgogoro huu wa kiroho wa kipekee na athari zake kote katika historia na muhtasari wa kitabu cha Ellen G. White, Pambano Kuu.
Unataka kujifunza zaidi kuhusu jinsi Mungu atakavyoharibu dhambi milele?
Chagua Masomo ya Biblia Mtandaoni
Unataka kuendelea kujifunza? Pata habari zaidi kuhusu Yesu, mwanadamu, mpango wa wokovu, na jinsi Mungu anavyokupenda kiasi cha kutosha kujitolea kila kitu, ili tu kukupatia nafasi ya kumchagua.
Wakati mwingine inaweza kuwa ngumu kujua pa kuanzia, ndio maana tunatoa chaguo za masomo ya Biblia mtandaoni bure, rahisi kutumia, unaweza kufanya wakati wowote, mahali popote, na kwa kasi yako mwenyewe.
Shule hii ya Biblia mtandaoni itakuelekeza kupitia mada kuu za Maandiko, ikivunja dhana ngumu za Biblia katika vipande vidogo, ambavyo vinaweza kukusaidia kupata majibu ya maswali magumu zaidi ya maisha.
Kurasa zinazohusiana
- Eliot, T.S., excerpt from “The Rock.” [↵]
- Frederick Nietzsche, The Genealogy of Morals, 1887, p. 16. [↵]
- Also see 1 John 4:8, 16. [↵]
- Handbook of Seventh-day Adventist Theology, p. 970. [↵]
- Orr, James, M.A., D.D. General Editor. “Iniquity,” International Standard Bible Encyclopedia. [↵]
- Lewis, C.S., Mere Christianity. [↵]
- Holbrook, p. 986. [↵]
Majibu Zaidi
Waadventista Wa Sabato wanaamini nini kuhusu Ubatizo?
Kama Wakristo wengi wa Kiprotestanti ulimwenguni kote na katika historia, Kanisa la Waadventista wa Sabato linaamini katika ubatizo, sherehe ambapo watu huzamishwa ndani ya maji kudhihirisha hadharani “kufa kwa maisha ya zamani” na “kuanza kwa maisha mapya katika Kristo”.
Waadventista Wasabato wanaamini nini kuhusu Biblia?
Biblia ndiyo msingi wa kila kanuni na mafundisho ya Waadventista wa Sabato.
Waadventista Wa Sabato Wanaamini Nini Kuhusu Mamlaka ya Biblia?
Jifunze jinsi kitabu kimoja cha zamani sana (Biblia) kilivyo msingi pekee wa imani zote za Waadventista wa Sabato.
Je, Waadventista Wasabato Wanaamini Wao Pekee Ndiyo Watakao Kwenda Mbinguni?
Hapana, Waadventista hakika hawaamini kwamba wao ndio pekee watakao kwenda mbinguni. Kwa kweli, hatuamini kwamba kupokelewa mbinguni kunategemea kanisa au madhehebu tunayohusiana nayo.
Je, Waadventista Wa Sabato Wanaamini Nini Kuhusu Uumbaji Katika Biblia?
Waadventista Wa Sabato wanaamini kwamba Mungu ndiye Muumbaji wa ulimwengu. Wanafikia hitimisho hili kutoka kitabu cha kwanza cha Biblia—Mwanzo.
Namna Waadventista Walivyojifunza Fundisho la Patakatifu na Maana Yake
Wakati Waadventista wanapozungumzia “fundisho la Patakatifu,” wanarejelea dhana kwamba hekalu la mbinguni linafunua mpango wa wokovu









