Waadventista Wa Sabato wanaamini nini kuhusu Ubatizo?

Kama Wakristo wengi wa Kiprotestanti ulimwenguni kote na katika historia, Kanisa la Waadventista wa Sabato linaamini katika ubatizo, sherehe ambapo watu huzamishwa ndani ya maji kudhihirisha hadharani “kufa kwa maisha ya zamani” na “kuanza kwa maisha mapya katika Kristo”.

Wazo la “kufa kwa maisha ya zamani“ linahusu kukubali na kuheshimu kifo cha Yesu kwa dhambi na ufufuo wake kwa haki. Kwa kuzamisha na kuibuka tena kutoka kwenye maji, tunatangaza kuwa tutakuwa tunaishi tukiwa na akili zetu zimeelekezwa kwa Yesu, badala ya ulimwengu uliovunjika unaotuzunguka. (Warumi 6:1-5; Wagalatia 2:20; Wakolosai 2:12).

Aina hii ya ubatizo inaonyeshwa na kuthibitishwa mara kwa mara katika Maandiko.1

Ukurasa huu utakuelekeza kuhusu kile Biblia inachofundisha kuhusu ubatizo na jinsi Waadventista wanavyoufanya leo. Utajifunza:

Kwa kuanza, huu hapa ni Msingi ya Imani ya Waadventista kuhusu ubatizo:

“Kwa ubatizo tunakiri imani yetu katika kifo na ufufuo wa Yesu Kristo, na kushuhudia kuhusu kifo chetu kwa dhambi na kusudi letu la kutembea katika uzima mpya.

Hivyo tunamkiri Kristo kama Bwana na Mwokozi, kuwa watu wake, na kupokelewa kama washiriki wa kanisa lake.

Ubatizo ni ishara ya umoja wetu na Kristo, msamaha wa dhambi zetu, na kupokea Roho Mtakatifu.

Unafanywa kwa kuzamishwa katika maji na unategemea kuthibitisha imani katika Yesu na uthibitisho wa toba ya dhambi. Unafuata mafundisho katika Maandiko Matakatifu na kukubali mafundisho yake.”

Endelea kusoma kwa maelezo zaidi!

Ubatizo ni nini?

Ubatizo ni desturi ya kidini, kawaida ikijumuisha kuzamishwa katika maji, ambayo inatangaza uamuzi wa mtu wa kufuata Yesu Kristo au kuwa “kuzaliwa mara ya pili.” Ni moja ya “maagizo” ya Biblia ya zamani zaidi na muhimu, au desturi za kidini, zilizofanywa katika kanisa la Kikristo kwa miaka elfu kadhaa iliyopita.

Tunaweza kuelewa ubatizo vizuri kwa kuuliza:

Tuanze na swali la kwanza.

Maana ya ubatizo ni nini?

Ubatizo ni kielelezo cha kuadhimisha kifo na ufufuo wa Yesu. Kama vile Yesu alikufa na kuzikwa kaburini, Mkristo mpya anazikwa katika maji ya ubatizo. Kisha, kama vile Yesu alivyofufuka kutoka kaburini, mtu binafsi anainuka kutoka majini—ishara ya maisha mapya katika Kristo.

Mtume Paulo katika Agano Jipya anaelezea hivi:

“Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake? Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima” (Warumi 6:3–4, NKJV).

Aya hii nafupisha ni nini maana ya wokovu.

Wakati wa ubatizo, tunazamishwa chini ya maji, ambayo inaashiria kifo chetu katika Kristo. Kifo cha maisha yetu ya awali ya dhambi, uasi, na kumkataa Mungu na sheria yake.

Pia inaashiria kukubali kwetu zawadi ya Mungu na kupokewa katika familia yake, licha ya maisha yetu ya awali ya dhambi.

Maisha yaliyopita ya dhambi yamekufa na kuzikwa chini ya maji. Tunawekwa huru dhidi yake.

Paulo, katika sura hiyo hiyo, baadaye anaeleza:

“Kwa maana kama mlivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika mtaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake; mkijua neno hili, ya kuwa utu wetu wa kale ulisulubishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena; kwa kuwa yeye aliyekufa amehesabiwa haki mbali na dhambi” (Warumi 6:5–6, NKJV).

Tambua, mtu wa kale ni sisi tulivyokuwa kabla hatujazaliwa “upya” (Yohana 3:3). Na sasa “tumesulubiwa” pamoja naye, maana yake tumekufa pamoja naye kwa nafsi yetu ya kale na njia zetu za kale (Wagalatia 2:20).

Lakini ubatizo sio tu kuzamishwa ndani ya maji.

Kuibuka toka kwenye maji inawakilisha kusafishwa na kuanza maisha mapya katika Kristo.

Sio tu kwamba utu wetu wa zamani umekufa, bali sisi pia ni watu wapya katika Yesu (2 Wakorintho 5:17).

Kitabu cha Mafundisho ya Kanisa la Waadventista wa Sabato kinaeleza dhana hii:

“Wakristo wanakufa kwa dhambi na kufufuliwa katika ubatizo wao; kwa njia hii wanadhihirisha kukubali kwao kwa kusamehewa kupitia Yesu Kristo. Kupitia Yeye, Wakristo wanapokea uwezo wa kufa kwa dhambi kila siku na kufufuka kwa upya wa maisha kwa kumtii Mungu.”2

Lakini unaweza kujiuliza, ibada hii ilianzia wapi?

Ubatizo utoka wapi?

Ubatizo umekita mizizi katika Agano Jipya. Yesu alionyesha kielelezo kwanza wakati Alipoanza huduma yake (Marko 1:9).

Alienda mpaka Mto Yordani ili abatizwe na Yohana Mbatizaji, mtu ambaye alikuwa ameandaa njia kwa ajili ya kuja kwa Yesu (Mathayo 3:3).

Yohana alikataa kumbatiza Yesu kwa sababu aliamini kwamba Yesu ndiye alipaswa kumbatiza yeye. Lakini Yesu alijibu:

“Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote” (Mathayo 3:15, NKJV).

Ilikuwa na maana gani kwa Yesu “kutimiza haki yote”?

Yesu alikuja duniani ili awe dhabihu yetu na kuishi maisha kamili yasiyo na dhambi kama kielelezo chetu.

Ubatizo wake ulikuwa ni onyesho la hadharani la imani yake kwa Baba yake na pia kifo chake na ufufuo. Kwa kuwa alikuwa akituwekea mfano, alipitia ubatizo ambao sisi pia tunapaswa kupitia.

Wakati Yohana alipombatiza Yesu, Roho Mtakatifu alishuka kutoka mbinguni kwa mfano wa njiwa. Na sauti ya Mungu ilifuatana nae:

“Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye” (Mathayo 3:17, NKJV).

Watu wote watatu katika Utatu wa Mungu walikuwepo wakati wa ubatizo wa Yesu.

Na ukweli huu ni muhimu sana hivi kwamba baadaye katika maisha Yake, Yesu alipowapa wafuasi wake amri inayoitwa Agizo Kuu, Alisema:

“Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari” (Mathayo 28:18–20, NKJV).

Kama wanafunzi wake—wafuasi—walivyohubiri Injili kwa ulimwengu wote, walipaswa kubatiza waamini wapya kwa jina la Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Yesu alitenga ibada hii kama kitu muhimu katika mianzo ya maisha ya Kikristo.

Jinsi Biblia inavyoagiza Wakristo kufanya ubatizo?

Agano Jipya inafundisha kwamba ibada muhimu ya Kibiblia inahusisha kuzamishwa katika maji.

Neno la Kigiriki linalotafsiriwa kama “kubatiza” linatokana na mzizi wa neno bapto, ambao maana yake ni “kutosa au kuzamishwa chini.” Neno hili linaonesha wazo la mtu kuzamishwa kabisa chini ya maji.

Kwa mfano, Biblia inasema kwamba Yohana Mbatizaji alibatiza katika Mto Yordani (Mathayo 3:6; Marko 1:5) na katika “Ainoni, karibu na Salimu, kwa sababu huko kulikuwa na maji tele” (Yohana 3:23, NKJV).

Kwa nini Yohana alihitaji mahali penye “maji mengi”?

Bila shaka kwa sababu alikuwa anawabatiza watu kwa kuzamisha kabisa katika maji.

Pia tazama kile Marko alichokiandika kuhusu ubatizo wa Yesu:

“Ikawa siku zile, Yesu alikuja kutoka Nazareti ya Galilaya, akabatizwa na Yohana katika Yordani. Mara alipopanda kutoka majini, akaona mbingu zinapasuka, na Roho, kama hua, akishuka juu yake” (Marko 1:9–10, NKJV).

Maandiko yanasema Yesu “alipopanda kutoka majini,” maana yake alikuwa chini ya maji.

Kitabu cha Matendo kinatoa mfano mwingine wa ubatizo kwa kuzamishwa.

Kinasimulia hadithi ya mtume Filipo kukutana na mtu wa Kushi, towashi aliyekuwa akipenda imani ya Kiyahudi (Matendo 8:27) na alikuwa amekubali kuwa Yesu alikuwa Masihi.

“Wakawa wakiendelea njiani, wakafika mahali penye maji; yule towashi akasema, Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe? [Filipo akasema, Ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana. Akajibu, akanena, Naamini ya kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu.] Akaamuru lile gari lisimame; wakatelemka wawili majini, Filipo na yule towashi; naye akambatiza. Kisha, walipopanda kutoka majini, Roho wa Bwana akamnyakua Filipo….” (Matendo 8:36–39, NKJV).

Wote wawili “walitelemka ndani ya maji” na “wakapanda kutoka majini” – tena ikimaanisha ubatizo wa kuzamisha.

Lakini kwa kuwa Biblia inasema waziwazi kuhusu njia hii ya ubatizo, kwa nini baadhi ya makanisa hutumia kunyunyizia badala yake?

Wazo la ubatizo wa watoto (kunyunyiza maji) lilitoka wapi?

Wakati mazoea ya kupendeza yaliyolenga kujali roho za watoto wetu wapendwa, “kunyunyiza,” au kuweka matone ya maji kwa mfumo wa ibada kichwani mwa mtoto mchanga, hayakuanza wakati wa Biblia bali katika desturi za kanisa la mapema katika karne ya pili na ya tatu.

Wakati huo, viwango vya vifo vya watoto wachanga vilikuwa vya juu. Kwa hofu ya watoto wao kufa na kwenda kuzimu kabla ya ubatizo, wazazi wangewabatiza muda mfupi baada ya kuzaliwa, wakiamini kuwa ibada hiyo iliondosha dhambi zao.

Kuzamisha kichwa cha mtoto mchanga chini ya maji kulikuwa na hatari, ingawa baadhi wangefanya hivyo kwa uangalifu kwa kutumia “sehemu ya kubatizia” iliyokuwa kina cha kutosha kwa kuzamisha haraka.

Vikundi vingine vilikuwa vinatumia desturi ya kuwanyunyizia watoto maji matakatifu kichwani.

Ikiwa mtoto alikufa na hajabatizwa, watu walikuwa na wasiwasi kwamba roho ya mtoto ingeenda Jehanamu au kuzimu.

Lakini mtazamo huu unakinzana na kile Biblia inachofundisha kuhusu ubatizo na umuhimu wake kwa wokovu.

Ubatizo sio unaomwokoa mtu. Ni kitendo ambacho mtu aliyeokolewa hufanya ili kuifanya imani yake iwe wazi.

Ubatizo unakuja baada ya mtu kukubali kwamba Yesu Kristo alikufa ili kutupatia zawadi ya wokovu.

Hii inatupeleka kwenye swali letu linalofuata.

Waadventista Wanafundisha nini kuhusu umuhimu wa ubatizo?

Waadventista hawaamini wokovu kwa matendo wala wokovu kwa ubatizo.

Ubatizo ni ishara tu ya nje mbele ya wanadamu na Mungu. Inaonyesha imani yetu kwa Yesu, ambaye tayari ametuokoa—hata kabla ya ubatizo.

Maji hayana kitu cha kichawi au cha kimuujiza ambacho kinatuosha kwa kweli.

Kwa mfano wa kulinganisha, fikiria sherehe ya mahafali ya elimu ya juu ya sekondari au chuo kikuu.

Sherehe hiyo inatambua kukamilika kwa mahitaji ya kozi ya mtu. Lakini sherehe hiyo sio iliyosababisha mafanikio hayo. Ni ishara yake.

Tunapomkubali Kristo kwa imani—na kuanza maisha mapya naye—ubatizo wetu ni kielelezo cha kile ambacho tayari tuna uzoefu wake.

Ndiyo maana kuwanyunyizia watoto maji hakuungwi mkono na Maandiko. Mtoto bado hajafanya uamuzi wa kumfuata Mungu. Biblia inafundisha kwamba ubatizo unapaswa kufanyika mtu anapokuwa mzima wa kuelewa kweli za Biblia na kufanya uamuzi wa dhati kwa Kristo (Mathayo 28:19–20).

Kipi cha kutarajia katika sherehe ya ubatizo wa Waadventista wa Sabato

Katika kanisa la Waadventista wa Sabato, ubatizo huanza kwa mchungaji kusoma viapo vya ubatizo vya Kanisa la Waadventista wa Sabato. Viapo hivi ni kukubali mafundisho ya msingi ya Biblia kama yalivyoainishwa katika Kanuni Kuu 28 za Kanisa la Waadventista wa Sabato.

Hapa kuna mifano michache tu ya viapo vya ubatizo vilivyoorodheshwa katika Kitabu cha Mwongozo wa Kanisa la Waadventista wa Sabato:

  • Je, unaamini kuna Mungu mmoja: Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu, umoja wa nafsi tatu za milele?
  • Je! Unamkubali Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wako binafsi, ukiamini kwamba Mungu, katika Kristo, amesamehe dhambi zako na kukupa moyo mpya, na je! unazikataa njia za dhambi za ulimwengu?
  • Je! Unajua na kuelewa kanuni kuu za Biblia kama zinavyofundishwa na Kanisa la Waadventista Wa Sabato? Je! Unaazimia, kwa neema ya Mungu, kutimiza mapenzi Yake kwa kuishi kulingana na kanuni hizi?

Imani za Biblia zilizotajwa tayari zitakuwa zinafahamika kwa mhusika wa ubatizo kwani Kanisa la Waadventista Wa Sabato linahimiza watu kukamilisha mfululizo wa masomo ya Biblia kabla ya ubatizo (Mathayo 28:19–20).

Mchungaji ataisoma swali na kumwomba mtu athibitishe imani yake kwa kuinua mkono wake wa kulia au kusema “amen” au “ndiyo” kwa nguvu.

Kisha, mchungaji na anayekwenda kubatizwa watabadilisha nguo zao kwa maandalizi ya ubatizo (kama hawajafanya hivyo tayari). Katika baadhi ya makanisa, huvaa mavazi ya ubatizo.

Wakiwa tayari, wote wataingia ndani ya maji – ama katika tanki la ubatizo kanisani au nje katika bwawa, ziwa, au mto.

Mchungaji anaweza kutoa maoni au kumpa anayebatizwa fursa ya kusema maneno machache. Baadaye, mchungaji atatangaza, “Nakubatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu.”

Kisha mchungaji ataweka mkono kwenye mgongo wa mtu huku akifunika pua ya mtu kwa taulo (ili kuzuia maji kuingia puani mwake). Mtu huyo anashushwa ndani ya maji, na mara moja kuletwa juu tena.

Mara ngapi mtu anapaswa kubatizwa?

Ubatizo kawaida hufanyika mara moja mwanzoni mwa safari ya mtu na Mungu. Mtu huyo hubatizwa katika mwili wa Kristo na kupokea ushirika wa kanisa (1 Wakorintho 12:13).

Hata hivyo, Kanisa la Waadventista Wa Sabato huruhusu ubatizo wa pili katika hali fulani:

  • Wakati mtu amegeuka mbali na Mungu na anarudi kwake
  • Wakati mtu anapojifunza mafundisho mapya muhimu katika Biblia na anataka kueleza upya ahadi yake kwa Mungu

Njia ya pili inapata msingi wake katika kisa cha Matendo 19:1–5.

Mtume Paulo alikutana na kikundi cha watu ambao walikuwa wafuasi wa Yesu lakini hawakuwahi kusikia kuhusu Roho Mtakatifu.

Paulo alipowafundisha, waliamua kubatizwa tena, wakionyesha ufahamu wao ulioongezeka kuhusu ukweli.

Kanisa la Waadventista Wa Sabato halisemi mtu anaweza kubatizwa mara ngapi. Lakini kwa sababu ubatizo ni uamuzi wa maana, tunahimiza watu kuchukua hatua hiyo baada ya kufikiria kwa uangalifu na maombi.

Kanuni ya Kanisa inasema hivi:

“Kubatizwa tena inapaswa kutokea tu katika mazingira maalum na inapaswa kuwa nadra. Kutoa ubatizo mara kwa mara au kwa msingi wa kihisia kunapunguza maana yake na inawakilisha kutokuelewa uzito na umuhimu ambao Maandiko huupa.”

Lakini kwa mtu anayetaka kuchukua hatua hiyo kwa moyo wa kweli, hivi ndivyo unavyoweza kufanya.

Jinsi gani mtu anachukua hatua ya ubatizo?

Sehemu muhimu zaidi ya ubatizo inaanza kwa kumwamini Mungu, ambayo inapelekea kubatizwa. Neno la Mungu linafanya sehemu hiyo iwe wazi:

“Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini atahukumiwa” (Marko 16:16, NKJV).

 

“Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako” (Matendo 16:31, NKJV).

Tazama jinsi aya hizi zinavyosema kwamba imani inakuja kwanza, kisha ubatizo.

Imani, sio ubatizo, ndio inayokoa.

Ingawa Biblia inafundisha kwamba ubatizo ni muhimu, sio njia ya wokovu. Wokovu ni kwa imani pekee.

Kisha, tunapompenda Mungu sana hivi kwamba tunatamani kumfuata popote anapotuongoza, ina maana tu kuadhimisha uamuzi huu kwa sherehe yenye maana.

Kama vile harusi zinavyo adhimisha muungano wa watu wanaojitoa maisha yao kwa mwingine, au jinsi sherehe za kuzaliwa zinavyoadhimisha mwaka mwingine wa maisha ya mwanadamu, ubatizo unaadhimisha moja ya furaha kuu tunayoweza kufikiria—kwamba Yesu alikufa kwa ajili yetu, alitusafi kutokana na dhambi zetu, na kufufuka tena ili tuweze kuwa na uzima wa milele pamoja naye.

Je! Ungependa kuchukua hatua ya ubatizo wewe mwenyewe?

Yesu aliwahimiza wafuasi wake kuwafanya wengine wanafunzi na kuwafundisha. Vivyo hivyo, Kanisa la Waadventista wa Sabato linahimiza watu kusoma Biblia na kuelewa uamuzi wanayofanya kabla ya kubatizwa.

Kurasa zinazohusiana

  1. Matthew 3:6, 13; 28:19-20; Mark 1:5, 9; Luke 3:21; John 3:23; Acts 2:38; 8:12-13, 8:35-38; 9:18; 19:4-5; Romans 6:1-11; Galatians 3:27; 1 Peter 3:21 []
  2. Handbook of Seventh-day Adventist Theology (Review and Herald Publishing Association, 2000), p. 586. []

Je, Una swali kuhusu Waadventista? Uliza hapa!

Pata majibu kwa maswali yako kuhusu Waadventista Wasabato

Majibu Zaidi