Ninawezaje Kuanza Kutunza Sabato?
Sabato, inayokuja kila siku ya saba ya juma, ni siku maalum inayoheshimu amri ya nne na uumbaji wa Mungu.
Inaweza kuwa mbaraka kuanza kutunza Sabato. Lakini ikiwa hili ni jambo ambalo hujawahi kulifanya awali na umekuwa ukifanya kazi siku saba kwa juma, inaweza kuwa ngumu kufanya mabadiliko. Nitawezaje kukamilisha kila kitu?
Hivyo hebu tuzungumze kuhusu jinsi ya kufanya mabadiliko haya. Tutakupatia vidokezo kwa ajili ya kukusaidia kufanikisha kila kitu na bado utafurahia baraka ambayo Sabato ilikusudiwa kuwa.
Ingawa inaweza kuhitaji marekebisho fulani, tunataka kukutia moyo kwamba kutunza Sabato ni jambo linalowezekana, hata katika ulimwengu wa leo usio na mapumziko. Kwa kweli, kutunza
Sabato ni jambo la furaha – tunalopaswa kulitazamia kwa shauku.
Na pia sio lazima liwe jambo ngumu.
Tutakuongoza katika maana ya kutunza Sabato na kukusaidia kuendeleza desturi hii katika maisha yako.
Hivi ndivyo mazungumzo yetu yatakavyokuwa:
- Maana halisi ya kutunza Sabato
- Hatua za kivitendo za kuanza mazoezi ya kutunza Sabato
- Jinsi ya kujiandaa kwa ajili Sabato yako ya kwanza
- Jinsi ya kutumia Sabato
Tuanze kwa kupitia kidogo kuhusu utunzaji Sabato.
Maana halisi ya kutunza Sabato

Photo by Andrea Piacquadio
Mungu alikusudia Sabato itumiwe kama siku ya kupumzika kutoka katika kazi kawaida, kwa ajili yetu na kwa ajili ya wengine. Kwa sababu Aliipanga kwa ajili yetu, anatuagiza kuitakasa na kuifanya kuwa siku ya furaha.
Sabato ilitengwa kwanza kama kitu maalum mwanzoni mwa historia ya dunia, mara tu baada ya Mungu kumaliza kuumba ulimwengu (Mwanzo 2:2-3). Ilikuwa kumbukumbu ya Uumbaji.
Baadaye, alitupa mwongozo zaidi katika amri ya nne:
“Ikumbuke siku ya Sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni Sabato ya BWANA, Mungu wako, Siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako … wala mgeni aliye ndani ya malango yako” (Kutoka 20:8-10, NKJV).
Amri hii inatoa muhtasari wa kusudi kuu la Sabato:
1) Uitakase
2) Usifanye kazi
3) Usiwafanye wengine kufanya kazi
Na Isaya 58:13 inaongeza kwamba Sabato imekusudiwa kuwa ” siku ya furaha” (NKJV). Katika utafiti juu ya aya hii, Ed Christian, PhD, anaongeza kwamba Sabato ilipangwa kuwa “siku yenye kupendeza zaidi, yenye starehe na furaha katika juma!”1
Kuna mifano mingi katika Biblia inayoonyesha jinsi kanuni hizi zilivyotumika katika maisha ya kila siku.
Baada ya Wayahudi kurudi kutoka uhamishoni, nabii Nehemia aliwaagiza kuacha kufanya kazi siku ya Sabato. Walikuwa wamesahau wakiwa uhamishoni (Nehemia 13:15-22).
Watu katika Biblia walifanya Sabato kuwa takatifu kwa kukusanyika pamoja kuabudu (Walawi 23:3, Luka 4:16, Matendo 13:42).
Basi tunawezaje kutumia kanuni hizi za Kibiblia za utunzaji wa Sabato katika ulimwengu wa leo?
Mark Finley, PhD, mchungaji na mhubiri, alielezea Sabato kama wakati wa “kukuza uhusiano wenye maana na Mungu na uhusiano mzuri na familia zetu na watu wanaotuzunguka”.2
Na katika ulimwengu wenye kasi wa leo, ambapo muda haupatikani kirahisi, tuna Sabato kama siku kuu kutoka kwenye machafuko na harakati za maisha yetu. Siku kuu maalum iliyoundwa kwa ajili ya kupumzika na kutumia muda pamoja na wale tunaowapenda. Kila kitu kingine kinawekwa kando ili tuweze kuzingatia hilo.
Fikiria Sabato kwa njia hii: Ikiwa ungekuwa na rafiki ambaye hujamwona kwa muda kidogo na wanakuja mjini kwa ziara, je, usingefanya kila uwezalo kutenga muda katika ratiba yako ili kutumia muda pamoja naye?
Ungeweka pembeni vitu vyote isipokuwa vile muhimu na vya lazima. Kwa njia hiyo, ungejikita katika muda wako na rafiki huyo. Unaweza kwenda kufanya kitu cha kufurahisha pamoja, au unaweza tu kupumzika na kufurahia kusikilizana.
Iko hivyo pia kwa Sabato. Mungu aliiumba kwa faida yetu (Marko 2:27), ambapo tunaweza kusahau vitu vyote visivyo muhimu.
Hapa inaangazia zaidi namna tunayoweza kufikiri.
John Mark Comer, katika kitabu chake cha The Ruthless Elimination of Hurry, anapendekeza kufikiria Sabato kwa njia hii: “Ningeweza kufanya nini kwa saa ishirini na nne ambacho kingeijaza roho yangu na furaha kuu? Hicho kingenifanya nilipuke kwa mshangao, heshima, shukrani, na sifa?”3
Huo ndio mtazamo tunaweza kuchukua tunapofikiria kuhusu kutunza Sabato.
Ikiwa una wasiwasi kuhusu kufuata orodha ya “fanya” na “usifanye” ya Sabato, hutaelewa lengo. Kwa kukumbuka kuwa ni mtazamo, shughuli zako zitabadilika na/au kugeuka kuakisi mtazamo huo. Sabato inaweza kuonekana tofauti kwa kila mtu kwa sababu uhusiano wa kila mtu na Mungu ni wa kipekee.
Kutunza Sabato kunaweza kuonekana kuwa rahisi, lakini inaweza kuwa ngumu na kulingana na mambo yanavyopangwa katika ulimwengu wa leo. Hapa tunaweza kutazama maana halisi ya kutunza Sabato leo.
Vidokezo halisi katika kuanza tabia ya kutunza Sabato
Kubadilika kuelekea katika mtazamo wa Sabato sio rahisi siku zote tunapozungukwa na mtazamo wa mbio kila wakati. Kama tabia mpya yoyote, ni mchakato ambao unaweza kuchukua muda fulani. Huenda usionekane rahisi mwanzoni, lakini hiyo ni sawa.
Kabla ya kujenga tabia mpya kama hii, unapaswa kuweka utaratibu.4 Unaweza kuanza na mambo machache yatakayo kusaidia kukumbuka kuwa ni Sabato. Unapozoea mfumo huo, unaweza kuongeza vipengele zaidi hadi itakapokuwa tabia.
Hatuwezi kukwambia jinsi ya kufanya hili kwa sababu hakuna njia ya kawaida ya kufanya hivyo. Ni mchakato wa maombi ambao utalazimika kuugundua mwenyewe.
Hata hivyo, tutajadili njia kadhaa za kutengeneza maamuzi yako ili yakusaidie katika mabadiliko haya. Hebu tuangalie vidokezo hivi.
Tenga Muda
Sabato huazimishwa siku ya Jumamosi. Lakini jambo la kushangaza zaidi ni kwamba, Biblia inaelezea kuwa Sabato inaanza jioni ya Ijumaa na kumalizika jioni ya Jumamosi.
Kwenye kitabu cha Mwanzo, Mungu aliumba kulingana na ratiba iliyohusisha asubuhi na jioni:
“Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya sita” (Mwanzo 1:31, NKJV).
Na Mambo ya Walawi 23:32 inaonyesha jinsi hilo linavyoathiri Sabato:
“Tangu jioni hadi jioni, mtaishika hiyo sabato yenu” (NKJV).
Hivyo Sabato ingeanza jioni ya usiku kabla—Ijumaa usiku.
Unaweza kufanya mambo tofauti yatakayokusaidia kukumbuka kuwa Sabato imeanza, kama vile:
- Andika katika kalenda ya familia au kalenda, kama unavyofanya kwenye miadi muhimu
- Tumia kikumbusha muda wakati wa machweo
- Tumia programu za hali ya hewa kukusaidia kufuatilia machweo
Kudhamiria5 kutenga muda ndiyo msingi wa kuanza desturi ya kutunza Sabato. Dirisha hili la masaa 24 ni miadi yako na Mungu. Unaweza kufanya nini ili kuufanya wakati huu kuwa maalum katika ratiba yako ya sasa?
Jambo kubwa linalopingana na masaa haya ni ratiba za kazi. Tutaliangalia baadaye.
Fanya makubaliano kazini

Photo by Christina @ wocintechchat.com on Unsplash
Kama tulivyosema hapo awali, Mungu anatuagiza kutofanya kazi siku ya Sabato.
Lakini sio kila kazi ni Jumatatu-Ijumaa, saa tatu hadi saa kumi na moja. Kazi nyingi zitapangwa Jumamosi au Ijumaa jioni au zitahitaji safari za mwisho wa wiki. Kusudi letu kubwa hapa ni kutafuta makubaliano.
Ili kufanya hivi, zungumza na meneja wako au bosi wako. Eleza imani yako mpya, na uliza ikiwa unaweza kufanya kazi Jumapili au siku nyingine badala yake, au kuja mapema Ijumaa ili uondoke kabla ya jua kuzama.
Baadhi ya mameneja wataelewa na kubadilisha ratiba yako ili kuruhusu Jumamosi iwe siku ya mapumziko.
Lakini wengine huenda wasikubali. Ikiwa unakabiliwa na changamoto hii, kuna nyenzo za kisheria zilizopo kwa ajili yako. Maswala ya Umma na Uhuru wa Kidini (PARL) ni idara ya kimataifa ya Kanisa la Waadventista Wa Sabato inayopigania uhuru wa kidini ulimwenguni kote. Kati ya mambo mengine, idara hii inasaidia watu wanaokumbana na ubaguzi kazini kwa sababu ya imani zao. Wasiliana nao ili upate msaada.
Kwa wengine, kazi mwishoni mwa wa wiki haijawahi kuwa sharti. Hata hivyo, unaweza kupokea barua pepe na simu nyingi za kazi nje ya masaa ya kazi. Hili linapotokea, unaweza kuzima taarifa hizo hadi baada ya Sabato.
Hata hivyo, hakikisha kuzungumza na wenzako kazini na/au meneja kabla ya kubadilisha upatikanaji wako kama hivyo. Hii inazuia mkanganyiko na kutokuelewana na kufanya mambo yaende vizuri.
Kwa nini ni muhimu sana kuacha kufanya kazi siku ya Sabato?
Sababu ya Mungu kutuagiza kufanya hivyo ni kwa sababu ya asili ya kazi. Kwa nini watu wengi wana kazi na taaluma? Ili kupata pesa na kufanikiwa kitaaluma.
Comer anaita sababu hizi mbili “kujilimbikizia na kufanikiwa”.6
Hakuna kitu kibaya kimsingi katika mambo hayo. Yanatusaidia kutunza familia zetu na kujifunza na kuboresha ujuzi wetu.
Tatizo ni kwamba Sabato haihusu mambo haya. Sabato inahusu kupumzika na kujiunganisha tena na Mungu na familia zetu.
Lakini kumbuka baadhi ya kazi ambazo zina ratiba ya kawaida siku ya Sabato ni muhimu. Kwa sababu hazihusu kukusanya mali na mafanikio kama ilivyo kutumikia wengine.
Baadhi ya kazi hizi ni pamoja na madaktari, wauguzi, na wahudumu wa dharura. Wanawasaidia na kuwaokoa wengine, ambayo hata Yesu alishiriki mara kwa mara siku ya Sabato (Mathayo 12:10-14, Luka 13:10-17, Yohana 5:1-18). Fikiria—ikiwa hospitali zingefungwa siku ya Sabato, watu wengi wangekufa!
Hivyo kuna baadhi ya matakwa ya kipekee kuhusu wazo kuu la kuacha kufanya kazi.
Lakini zaidi ya mazoea ya kawaida ya kuacha kufanya kazi kwa ajili ya Sabato, je! Biblia inaeleza chochote kuhusu shughuli nyingine?
Hamisha kazi na majukumu yasiyo muhimu kwenda siku nyingine

Photo by Blake Wisz on Unsplash
Kwa sababu Sabato ni wakati uliotengwa kwa ajili ya kupumzika na kujiunganisha upya na Mungu, tunaweza kupunguza vikwazo vyetu kwa kuhamisha vitu visivyo vya lazima katika maisha yetu kwenda siku nyingine.
Tena, hii labda itaonekana tofauti kidogo kwa kila mtu. Vitu vinavyotusumbua vinaweza kutokuwa tatizo kwa mtu mwingine.
Na kumbuka pia kwamba mchakato huu unaweza kuwa wa hatua ndogo, au tabia ndogo ndogo.7 Anza kwa vitu vichache vikuu, na kadri tabia inavyokolea zaidi, ongeza vitu vingine.
Kufuta ghafla majukumu yote ya Sabato uliyokuwa umeahidi kunaweza kuonekana kuwa ni ukosefu wa heshima. Inaweza kuchukua muda kufanya kazi kupitia ratiba yako na kupanga mambo upya
Basi, unachaguaje nini cha kuhamisha?
Unapofikiria kuhusu shughuli unazofanya siku ya Jumamosi, unaweza kujiuliza maswali kadhaa ili kukusaidia kufanya maamuzi.
Ni shughuli zipi zingeweza kukufanya usijihisi kama ni Sabato? Labda mambo kama kusafisha nyumba au kufanya kazi shambani inaonekana kama kazi ngumu. Ikiwa ndivyo, unaweza kuahirisha kazi hizi na kuzifanya siku nyingine.
Ni mambo gani ungetaka kupanga upya ili uweze kufurahia Sabato? Ikiwa mradi wa kurembesha bafu au miadi na daktari wa meno ni vitu visivyopendeza kwenye orodha ya mambo ya kufanya Jumamosi, badilisha kwenda siku nyingine. Kisha, Sabato inaweza kuwa ya kufurahia na ya pekee zaidi (kwa hakika, piga simu mapema ili kupanga upya miadi).
Ni vyema kuhamisha shughuli za biashara kwenda siku nyingine, ikiwezekana. Kununua na kuuza visivyokuwa vya lazima kunafanya watu wengine wafanye kazi ya kutuhudumia, hivyo kukiuka lengo la Sabato.
Hii haimaanishi kwamba tunapaswa kupuuza dharura kwa sababu ni Sabato. Kwa mfano mradi wa nyumbani kwetu. Kurekebisha bafu lako huenda hakuhitaji kuendelea siku ya Sabato. Lakini ikiwa bomba linapasuka bafuni siku ya Sabato mchana, na kumwaga maji kwenye sakafu yote, kwa vyovyote vile, Badilisha!
Na ikiwa mtu ameanguka na kuvunja mkono wake siku ya Sabato, usisubiri kutafuta msaada wa matibabu jua litakapotua.
Yesu Kristo anatoa mfano katika kitabu cha Luka wa dharura kama hizi zinazoweza kutokea. Akizungumza na kikundi cha wanasheria na Mafarisayo, Yesu alibainisha,
“Akawaambia, Ni nani miongoni mwenu, ikiwa Ng’ombe wake au punda wake ametumbukia kisimani, asiyemwopoa mara hiyo siku ya Sabato?” (Luka 14:5, NKJV)
Ni kanuni ya kuacha mambo ambayo hatuhitaji kufanya Jumamosi ndiyo muhimu.
Baadhi ya mambo ya kawaida yanahitaji kufanywa, bila kujali ni Jumamosi. Kulisha na kutunza wanyama na kupika chakula cha kawaida, kwa mfano, bado ni lazima kufanyika (Luka 13:15). Hizo sio kazi ambazo Mungu alikuwa anazungumzia katika amri (Kutoka 20:8-11). Hayo hayahusu kufanya kazi ili kupata pesa au kutimiza tamaa zetu.
Tumezungumzia baadhi ya shughuli zinazofanana na biashara. Je, vipi kuhusu shughuli zingine za hiari, kama matukio ya michezo, kukutana pamoja, au sherehe za watoto na za kuzaliwa?
Hili nalo ni jambo la kuliangalia wewe mwenyewe. Fikiria kama shughuli husika itakukosesha utakatifu wa Sabato au itakusaidia kufanya hivyo vizuri zaidi.
Sasa, labda umechagua baadhi ya mambo unayotaka kuyahamisha kwa siku nyingine lakini hujui jinsi ya kupata muda kwa ajili yake katika ratiba yako iliyosheheni tayari. Utafanyaje?
Hapa ndipo kanuni za usimamizi wa muda zinapoweza kuwa na manufaa.8 Angalia ratiba yako na jiulize mambo gani ni muhimu zaidi. Hakikisha yanapewa kipaumbele kwenye ratiba yako ya kila wiki.
Kisha jaza na shughuli zisizo muhimu, ondoa baadhi ambazo hautakuwa na muda wa kufanya – kujaribu kujaza shughuli zaidi ya uhalisia sio wazo nzuri pia. Hii itakusaidia kupanga mapema. Utakuwa na msongo wa mawazo kidogo na utaweza kuandaa ratiba yako kwa ufanisi ili kupata nafasi kwa ajili ya Sabato.
Ratiba yako mpya inaweza kuwa ngumu kidogo mwanzoni. Itachukua muda kusawazisha shughuli. Lakini baada ya muda mfupi, utazoea zaidi na Sabato itakuwa furaha unayoingojea.
Shiriki/eleza jitihada yako mpya kwa marafiki na familia
Unapofikia uamuzi wa kutaka kutunza Sabato, ni wazo zuri kuwajulisha familia na marafiki mapema. Kisha mnaweza kushirikiana nao imani yako mpya na uamuzi na kuwaweka wote katika ukurasa mmoja wa matarajio.
Kutunza Sabato ni mabadiliko kwako na wale walio karibu nawe. Wale ambao hawaelewi Sabato hawatapata maana ya kila kitu unachofanya, hivyo unaweza kulazimika kuwaeleza.
Familia yako wanaweza kujiuliza kwa nini hufanyi baadhi ya shughuli tena.
Kwa kuwaeleza, kwa upole, matarajio na mipaka yako mipya, unaweza kuepuka mkanganyiko, kutokuelewana, au hisia za kuumiza. Unaweza kuonyesha heshima yako kwao na shauku yako ya kuitikia dhamira yako mwenyewe.
Hata kama bado hawaelewi, au wanajaribu kukushinikiza ufanye kitu siku ya Sabato ambacho hujisikii vizuri nacho, fahamu kwamba ni sawa kusema hapana kwa heshima. Tafuta njia ya kufanya hivyo bila kuwafanya wajisikie kuwa unawatenga.
Je, vipi kuhusu ikiwa unaishi na mtu ambaye hatunzi Sabato?
Ingawa hii inaweza kufanya mambo kuwa magumu, hakikisha unadumisha heshima wakati mnaposhughulikia tofauti zenu. Jadilini kile kilicho muhimu kwa kila mmoja wenu na kile ambacho kila mmoja anaweza kufanya kuheshimu imani binafsi za mwenzake.9
Hali hio huenda isitatulike kabisa—mtu mwingine huenda asichague kutunza Sabato kamwe. Lakini kwa uwazi na kuheshimiana, mnaweza kupata suluhisho linalotekelezeka.
Kidokezo kingine muhimu, unapoanza kutunza Sabato, ni kutafuta watu utakaotumia muda wa Sabato pamoja nao.
Tafuta jamii mtakayoshiriki Sabato pamoja
Kupata kikundi cha watu wenye mawazo kama yako kuwa pamoja nao katika Sabato ni muhimu ili kudumisha Sabato na inaweza kuifanya iwe ya kufurahisha. Pia inaweza kukusaidia kujisikia kukubalika ikiwa wewe ndiye pekee katika kijamii yako anayetunza Sabato.
Maandiko yanatuambia kwamba watu walitunza Sabato kwa kukusanyika pamoja kujifunza Biblia.
Katika Agano la Kale, Waisraeli wa kale walitumia Sabato kwa “kusanyiko takatifu” (Mambo ya Walawi 23:3, NKJV), au mkutano mtakatifu.
Hii huenda ilifanyika katika hekalu (ikiwa wanaishi karibu) au katika nyumba binafsi.
Katika Agano Jipya, Wayahudi walihudhuria kwenye sinagogi kila Sabato (Luka 4:16).
Na barua za mtume Paulo zinaonyesha kwamba makanisa ya Wakristo wa awali yalijitokeza muda mfupi tu baada ya Yesu kusulubiwa na kufufuka tena (Waefeso 4:11-12, Ufunuo 1:4)! Walitambua umuhimu wa jamii.
Leo, unaweza kufanya vivyo hivyo. Unaweza kuhudhuria kanisani siku ya Sabato, au kujiunga na kikundi cha kujifunza Biblia. Sio tu kwamba utakutane na watu wapya wanaoshiriki imani yako, bali pia unaweza kuimarisha uhusiano wako na Mungu kutoka mtazamo tofauti.
Baada ya kuzingatia vidokezo vyote hivi, ni kawaida kujiuliza jinsi unavyoweza kujiandaa kwa Sabato. Hebu tuangalie hilo sasa.
Jinsi ya kujiandaa kwa Sabato yako ya kwanza

Photo by MART PRODUCTION
“Kujiandaa” kwa ajili ya Sabato hakuhusu sana kazi kama inavyoonekana. Kunahusu zaidi kutafakari yajayo ili uweze kuwa tayari kwa siku hiyo na kupunguza vikwazo.
Kulingana na hali yako, hapa kuna mambo ambayo unaweza kujaribu kufanya ili ujiandae kwa Sabato:
- Fanya usafi wa nyumba siku ya Ijumaa
- Nunua vyakula mapema ndani ya wiki
- Panga chakula cha Sabato kisichohusisha kazi nyingi, au andaa chakula cha Sabato siku ya Ijumaa ili ukipashe moto tu
- Jaza gari lako mafuta kabla ya Sabato
Tafadhali kumbuka kwamba hauhitaji kufanya mambo haya maalum. Ni mambo ya kawaida tu ambayo watu wamechagua kufanya ili Sabato iwe ya furaha zaidi.
Na usihangaike kufanya kila kitu kinacho wezekana kabla ya Sabato – lengo sio kusisitiza kufanya kila kitu kwa usahihi kamili.
Kanuni ya kujiandaa kwa Sabato ndio jambo muhimu—kufanya mambo mapema ambayo yataifanya Sabato iwe yenye pumziko.
Sasa hebu tuzungumze kuhusu utunzaji wa Sabato yenyewe. Ni mambo gani unaweza kufanya ili kufuata lengo lake?
Jinsi ya kutumia Sabato
Unaweza kufanya mambo mengi ili kufurahia Sabato kikamilifu!
Kama tulivyoona mapema, Sabato inahusu mahusiano. Hivyo unaweza kuanza na shughuli za familia ili kufurahia muda pamoja ambao kawaida haupatikani.
Jambo lingine unaloweza kufanya ni kutembelea watu ambao kawaida huonani nao, iwe ni ziara ya uso kwa uso au simu au simu kwa njia ya video. Wanaweza kuwa wazee katika familia, marafiki, majirani, au mtu mwingine.
Sabato pia inahusu kuendeleza uhusiano wetu na Mungu. Hivyo unaweza kutumia sehemu ya Sabato kusoma na kujifunza Maandiko, kutafakari juu yake, na kuomba.
Na Sabato ni wakati mzuri wa kufanya mambo ambayo mara nyingi huwezi kufanya. Unaweza kutumia muda nje, kufanya mradi wa kupumzika, au kupata mazoezi.
Kama ungependa mawazo maalum ya jinsi ya kutumia Sabato, hakikisha unapitia ukurasa wetu kuhusu shughuli za Sabato!
Pata Pumziko lako la Sabato
Kuendelea kutunza Sabato ni lengo zuri la kuwa nalo, lengo moja ambalo linakuja na faida nyingi za kiroho na kimwili.
Ingawa inaweza kuhitaji umakini sana na uvumilivu ili kuweza kuweka muda katika ratiba yako, kuna mambo halisi unaweza kufanya ili kuupa kipaumbele muda huu wa pekee pamoja na Mungu
Juu ya yote, tambua kuwa kwa namna yoyote unayofanya kwa jambo hili, omba mwongozo katika hatua kubwa unazopiga. Uwe tayari kuitikia msukumo wa Roho Mtakatifu. Mungu yupo kwa ajili yako. Anatuhakikishia
“Usiogope wala usifadhaike, kwa kuwa BWANA, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako” (Yoshua 1:9, NKJV).
Na atakuwa pamoja nasi tunapoanza safari hii mpya ya kutunza Sabato.
Unataka kujifunza zaidi kuhusu siku hii?
Je, unataka kupata jamii karibu yako inayotunza Sabato?
Mistari ya Biblia Kuhusu Kushika Sabato
- Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya, akapumzika siku ya saba kutoka kazi yake yote aliyoifanya. akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya. Mungu akaibariki siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba na kuifanya” (Mwanzo 2:2-3, NKJV).
- Amri ya nne kati ya Amri Kumi: “Ikumbuke siku ya Sabato, uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni Sabato ya BWANA, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. Maana, kwa siku sita BWANA alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo BWANA akaibarikia siku ya Sabato, akaitakasa” (Kutoka 20:8-11, NKJV). Tazama pia Kumbukumbu la Torati 5:12-14 kwa aya inayofanana.
- Akawaambia, Sabato ilifanywa kwa ajili ya mwanadamu, si mwanadamu kwa ajili ya Sabato” (Marko 2:27, NKJV).
- “Kama ukigeuza mguu wako usihalifu Sabato, usifanye anasa yako siku ya utakatifu wangu; ukuiita Sabato siku ya furaha, na siku takatifu ya BWANA yenye heshima; ukiitukuza, kwa kutokuzifanya njia zako mwenyewe, wala kuyatafuta yakupendezayo, wala kusema maneno yako mwenyewe; ndipo utakapojifurahisha katika BWANA; nami nitakupandisha mahali pa nchi palipoinuka; nitakulisha urithi wa Yakobo baba yako; kwa maana kinywa cha BWANA kimenena hayo” (Isaya 58:13-14, NKJV).
- “Akawaambia, Ni nani miongoni mwenu, ikiwa Ng’ombe wake au punda wake ametumbukia kisimani, asiyemwopoa mara hiyo siku ya Sabato?” (Luka 14:5, NKJV).
- “Lakini Bwana akajibu akasema, Enyi wanafiki, kila mmoja wenu, je! Hamfungui ng’ombe wake au punda wake siku ya sabato katika zizi, aende naye kumnywesha?” (Luka 13:15, NKJV).
- “Na tazama, yumo mtu mwenye mkono umepooza; wakamwuliza, wakisema, Ni halali kuponya watu siku ya sabato? Wapate kumshitaki. Akawaambia, Ni mtu yupi miongoni mwenu mwenye kondoo mmoja, na yule kondoo ametumbukia shimoni siku ya sabato, asiyemshika akamwopoa? Je! Mtu ni bora kuliko kondoo mara ngapi? Basi ni halali kutenda mema siku ya sabato” (Mathayo 12:10-12, NKJV).
- Uponyaji wa siku ya Sabato kwa mwanamke mwenye ugonjwa kwa miaka 18 (Luka 13:10-17).
- Uponyaji siku ya Sabato kwa mwanamume kwenye birika la Bethesda (Yohana 5:1-18).
- Uponyaji siku ya Sabato kwa kipofu (Yohana 9:1-14).
- “Mtafanya kazi siku sita, lakini siku ya saba ni Sabato ya kustarehe kabisa, kusanyiko takatifu; msifanye kazi ya namna yo yote; ni Sabato kwa BWANA katika makao yenu yote” (Walawi 23:3, NKJV).
- “Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya Sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome” (Luka 4:16, NKJV).
- “Na Paulo, kama ilivyokuwa desturi yake, akaingia mle walimo, akahojiana nao kwa maneno ya maandiko sabato tatu” (Matendo 17:2, NKJV).
- “Na siku ile ilikuwa siku ya Maandalio, na Sabato ikaanza kuingia. Na wale wanawake waliokuja naye toka Galilaya walifuata, wakaliona kaburi, na jinsi mwili wake ulivyowekwa. Wakarudi, wakafanya tayari manukato na marhamu. Na siku ya Sabato walistarehe kama ilivyoamriwa” (Luka 23:54-56, NKJV).
- “Akatoa hoja zake katika sinagogi kila Sabato, akajaribu kuwavuta Wayahudi na Wayunani” (Matendo 18:4, NKJV).
- Nehemia anafundisha upya Israeli jinsi ya kutunza Sabato kwa utakatifu katika Nehemia 13:15-22.
- “Hata siku ya Sabato tukatoka nje ya lango, tukaenda kando ya mto, ambapo tukadhani ya kuwa pana mahali pa kusali; tukaketi, tukasema na wanawake waliokutana pale” (Matendo 16:13, NKJV).
- Christian, Ed, PhD. “‘Sabbath is a Happy Day!’ What does Isaiah 58:13-14 Mean?” Journal of Adventist Theological Society, Andrews University. [↵]
- Finley, Mark. “How to Keep the Sabbath,” HopeLives365, Jan. 23, 2021. [↵]
- Comer, John Mark. The Ruthless Elimination of Hurry, p. 155. [↵]
- DePaul, Kristi. “What Does It Really Take to Build a New Habit?” Harvard Business Review, Feb. 2, 2021. [↵]
- Ibid. [↵]
- Comer, John Mark. The Ruthless Elimination of Hurry, p.147. [↵]
- “What Does It Really Take To Build a New Habit?” [↵]
- “Time Management,” Corporate Finance Institute. [↵]
- Davis, Elizabeth. “Ask An Expert—Working Through Religious Differences in Marriage,” Utah State University, Oct. 12, 2022. [↵]
Majibu Zaidi
Kila kitu unachohitaji kujua kuhusu Shule ya Sabato
Kila kitu unachohitaji kujua kuhusu Shule ya SabatoShule ya Sabato ndio sehemu ya kujifunza Biblia ya programu za kanisa katika makanisa mengi ya Waadventista wa Sabato. Ni wakati wa kujifunza Biblia kuhusu mada au somo fulani. Badala ya kumsikiliza mhubiri, watu...

