Karibu katika kila Kanisa la Waadventista wa Sabato, mahubiri ndiyo kitovu cha ibada kuu—kama ilivyo kwa madhehebu mengi ya Kikristo ya Kiprotestanti. Ni wakati wa mafundisho ya Kibiblia kutoka kwa mchungaji, ambaye hushiriki alichojifunza katika Biblia na kujiandaa kwa juma zima.
Kwa kupitia visa vinavyovutia, mifano, na ufafanuzi wa Biblia, mahubiri hulenga kusaidia kuwaleta waumini katika safari ya kina na Mungu (Warumi 10:17).
Tujifunze zaidi kuhusu jinsi mahubiri yanavyofanya kazi.
Tutachambua hili kwa kujibu baadhi ya maswali ya kawaida:
- Ni nini kinachofanya hubiri kuwa hubiri?
- Zipi ni aina tofauti za mahubiri?
- Mahubiri ya Waadventista yanahusu nini?
- Wapi ninaweza kusikiliza mahubiri ya Waadventista?
Mwishoni, utatambua jinsi sehemu hii ya ibada ya Waadventista inavyolingana na uzoefu mzima.
Ni nini kinachofanya hubiri kuwa hubiri?

Photo by Mitchell Leach on Unsplash
Mahubiri ni hotuba ya kidini inayotolewa mara nyingi wakati wa ibada kuu ya kanisa kwa waumini wote. Mahubiri kawaida hufanywa na mchungaji, ingawa ni jambo la kawaida kwa wazee wa kanisa au viongozi wengine kuyatoa. Mara kwa mara waumini au hata vijana hupata nafasi ya kuhubiri kwa familia ya kanisa yao.
Sehemu hii ya ibada inaweza kudumu kati ya dakika 20-40, kwa wastani.
Dakika hizo 40 zinalenga kuzungumza moja kwa moja na mioyo ya watu, kutupa ufahamu unaofanya maneno ya Biblia yaweze kutusaidia katika maisha yetu ya kila siku. Hatupaswi kumzingatia mzungumzaji—bali ujumbe kutoka kwa Mungu ambao mhubiri anautoa. Kisha wasikilizaji wanahimizwa kutafakari kuhusu mapenzi ya Mungu kwao, na kusoma Maandiko wenyewe.
Jinsi gani mhubiri anafikia lengo hili?
Badala ya kutoa habari nyingi, mhubiri hujikita katika hoja kuu. Akitoa matumizi ya kivitendo kutoka hoja hii na, mwishoni, kuwaalika wasikilizaji kuchukua hatua katika maisha yao ya kila siku.
Ikiwa unahitaji mfano wa hubiri katika Biblia, unaweza kutazama kinachoitwa “Hubiri la mlimani,” wakati Yesu alipohubiri kwa maelfu ya watu kuhusu jinsi ya kutumia Neno la Mungu katika maisha yao. Imeandikwa katika Mathayo sura ya 5-7.
Lakini sio mahubiri yote yanafanana na hili. Kuna mitindo na aina tofauti.
Ni zipi aina tofauti za mahubiri?
Mahubiri mengi yanaweza kugawanywa katika makundi matatu makuu: yaliyojengwa kwenye mada, ya ufafanuzi wa aya, na ya kibiografia.
Mahubiri yaliyojengwa kwenye mada
Mahubiri yaliyojengwa kwenye mada huchunguza mada kutoka kwenye Biblia, yakileta aya za Maandiko kutoka Agano la Kale na Agano Jipya ili kupata muhtasari kamili. Yanaweza kujengwa katika mafundisho (k.m. Kurudi kwa Pili, wokovu, mbingu) au mambo mengine ya kiroho (k.m. imani, maombi, kujua mapenzi ya Mungu).
Mara nyingi, mhubiri anaweza kuzingatia jinsi Biblia inavyotumia neno au kauli fulani. Ziko mada za mahubiri ya aina hii zisizo na kikomo.
Mahubiri ya ufafanuzi wa aya
Mahubiri ya ufafanuzi wa aya hujikita katika sehemu maalum ya Biblia. Lengo ni kuchambua kwa undani maana yake, kuelezea, na kushiriki maelezo kuhusu muktadha wake. Mhubiri anaweza kutoa muktadha wa kitamaduni na kihistoria wa kifungu au kutazama maana za msingi za maneno. Lengo ni kuleta dhana kuu ambayo maandiko yanazungumzia.
Mahubiri ya ufafanuzi wa aya yanaweza kuhusu kisa au ufafanuzi.
Mahubiri ya masimulizi yanazingatia visa katika Biblia, kama vile Yesu kuwalisha watu 5,000.
Mahubiri ya ufafanuzi yanazingatia kanuni za kiimani zaidi. Mfano wa hili ni kifungu kutoka kwenye barua ya Paulo kwa Wagalatia, ambapo anaeleza dhana kuhusu wokovu badala ya kusimulia hadithi.
Mahubiri ya kibiografia
Mahubiri ya kibiografia hupitia kisa cha mhusika fulani katika Biblia, yakilenga masomo tunayoweza kujifunza kutoka kwake. Yanaweza kuhusu mada, yakihusisha maandiko kutoka sehemu nyingi katika Biblia, au ya ufafanuzi wa aya, yakilenga sehemu muhimu ya mhusika huyo.
Mahubiri ya Kiadventista yanahusu nini?

Photo by Martin Schmidli on Unsplash
Kama yalivyo mahubiri mengi ya Kikristo, mahubiri ya Kiadventista yana mada tofauti tofauti lakini hupata msingi wake uko katika masomo ya Biblia. Wahubiri huchukua kwa uzito ushauri katika 2 Timotheo 4:2 wa “lihubiri neno” (NKJV).
Badala ya kuwa na mahubiri ya moto na kiberiti au ya kuwapamba watu, mahubiri ya Kiadventista hujitahidi kushughulikia mada zenye umuhimu na za kivitendo kutoka katika Biblia. Yanaweza pia kuwa na mambo ya kiunabii na hisia ya dharura.
Kanuni hizi zinatoka kwa Yesu Mwenyewe.
Yesu aliongea ukweli kwa wasikilizaji wake, akionyesha jinsi ulivyohusiana na maisha yao ya kila siku. Mara nyingi alitumia mifano kutoka kwenye vitu au shughuli za kawaida ili kuendana na watu (mshumaa, kondoo aliyepotea, sarafu iliyopotea).
Lakini zaidi ya yote, Alinukuu Maandiko Matakatifu na kuyafanya yaweze kueleweka mioyoni mwa watu, akiwaita wafanye maamuzi. Unabii na umuhimu wa kuwa tayari ulikuwa msingi wa ujumbe wake.1
Vivyo hivyo, viongozi katika kanisa la Agano Jipya walihubiri Neno la Mungu (Matendo 4:31; 5:42; 8:4). Walirejelea unabii na visa vya Agano la Kale kuelekeza kwa Yesu (Matendo 13:6–41).
Kisha, Roho Mtakatifu alitumia ujumbe huo kuishawishi mioyo ya watu na kuwaongoza kwa Mungu (Matendo 2:37).
Mahubiri ya Kiadventista yanafuata mfano wa Yesu na viongozi wa kanisa la Agano Jipya kwa kuwawezesha wasikilizaji kumtafuta Mungu.
Ni nini kinachofanya mahubiri ya Kiadventista kutofautiana na mahubiri mengine?
Kama ilivyo kwa wachungaji Wakristo wa madhehebu mengine, wachungaji wa Kiadventista wanataka kusaidia wasikilizaji wao kujifunza zaidi kuhusu Biblia na kusogea karibu na Mungu. Wanatafuta kumfanya Yesu kuwa kitovu cha ujumbe wao. Lakini mahubiri ya Kiadventista yana tofauti kadhaa pia, hasa katika njia yao ya kujifunza Biblia na mada zao msingi.
Ingawa mahubiri katika madhehebu mengine pia yanatoa mafundisho kutoka kwa Biblia, wachungaji wa Kiadventista wanaweka lengo maalum ili kuhakikisha kwamba Biblia nzima inajenga ujumbe wao. Badala ya kuchagua aya moja na kuitumia kujenga hoja, wanachunguza kile Biblia nzima inachosema kuhusu mada hiyo.
Pili, mada fulani ni za kawaida kwa mahubiri ya Kiadventista ambazo zinaunganishwa moja kwa moja na imani zao, kama vile:
- Vipengele mbalimbali vya huduma ya Yesu (maisha yake, kifo, ufufuo, na jukumu lake la kikuhani katika patakatifu pa mbinguni)
- Utume wa kiunabii wa kanisa (mwili wa Kristo)
- Ujumbe wa malaika watatu wa Ufunuo 14
- Sabato ya siku ya saba
- Ujio wa hivi karibuni wa Yesu
(Ili kujifunza zaidi kuhusu mada hizi, soma kuhusu utume wa pekee wa Kanisa la Waadventista wa Sabato).
Ni wapi naweza kusikiliza mahubiri ya Waadventista?
Ili kusikiliza mahubiri wewe mwenyewe, tembelea Kanisa lako la Waadventista wa Sabato. Unaweza kupata nyakati zao za ibada kwa kuangalia tovuti yao au ukurasa wao wa Facebook. Ikiwa hauko tayari kwenda kuhudhuria ibada, unaweza kutazama mahubiri yanayoendelea moja kwa moja kwenye tovuti, televisheni, au mitandao.
Mahubiri ya kanisa mtandaoni pia yapo karibu yako kwenye tovuti muhimu na akaunti za YouTube. Angalia hizi:
- HopeLives365
- Mafundisho ya Kustaajabisha
- Mtandao wa Utangazaji wa Malaika Watatu (3ABN)
- Kituo cha Matumaini
- Sauti ya Mstari wa Maandiko
Mahubiri yanatuongoza katika uhusiano wa karibu na Mungu.
Sisi sote tuna nafasi ya kumtafuta Mungu sisi wenyewe kupitia maombi na kusoma Biblia. Lakini Mungu pia hutumia watu wanaojitolea, kama wachungaji na viongozi wa kanisa, kutusaidia kumfahamu vizuri. Kujifunza kwao Biblia kwa bidii na ushawishi wa Roho Mtakatifu hutuletea ufahamu mpya, tumaini, na mtazamo mpya wa upendo wa Mungu.
Mahubiri ni sehemu ya muundo wa ibada ya kanisa inayoruhusu hilo kutokea. Kupitia hayo, tunapata hekima ya kivitendo ya kuishi kulingana na kusudi la Mungu kwa ajili ya maisha yetu.
Je una shauku ya kusikiliza hubiri? Tafuta kanisa la Waadventista karibu yako na uje siku ya Sabato. Tungependa kuabudu pamoja nawe!
Tafuta Kanisa
If you’re interested in finding a local Adventist church near you, you can use the Adventist Locator provided by the General Conference of Seventh-day Adventists.
Makala yanayohusiana
- Find some of Jesus’ sermons in Matthew 5–7, 13, 24, and John 6. [↵]
Majibu Zaidi
Wasimamizi wa Waumini Wana Nafasi Gani Ikilinganshwa na Wachungaji?
Neno “Usimamizi wa kidini” linatokana na neno la Kigiriki laikos, ambalo maana yake ni “wa watu.”
Muundo wa Uongozi wa Kanisa la Waadventista wa Sabato.
Kanisa la Waadventista wa Sabato lina mfumo wa uwakilishi unaounganisha makanisa yake zaidi ya 90,000 ulimwenguni na kuwapa washiriki wake nafasi katika kufanya maamuzi.
Kitabu cha Nyimbo cha Waadventista Wa Sabato
Kitabu cha nyimbo cha Waadventista wa Sabato ni kitabu cha nyimbo kinachotumiwa ulimwenguni kote na makanisa mengi ya Waadventista wakati wa ibada zao.








