Mariamu Magdalene ni Nani Katika Biblia?
Mariamu Magdalene alikuwa mfuasi na msaidizi wa kipekee wa Yesu Kristo wakati wa huduma yake duniani.
Anatajwa katika injili zote nne katika Biblia (Mathayo, Marko, Luka na Yohana) na alikuwa mmoja wa wanawake kadhaa ambao sio tu walikuwa wanafunzi wa Yesu, bali pia walimsaidia kifedha katika huduma yake (Luka 8:1-3).
Kujitoa kwake kwa dhati kwa Yesu kuko wazi kwa sababu alikuwa pamoja naye wakati wa huduma yake, wakati wa kusulubiwa kwake (wakati wengi wa wafuasi wake wengine walipokuwa wamejificha), na baada ya kufufuka kwake.
Mariamu lilikuwa jina la kawaida sana kati ya Wayahudi wakati wa Yesu, hivyo siyo jambo la kushangaza kwamba kati ya wafuasi wengi wa Yesu, kulikuwa na Mariamu kadhaa. Mariamu Magdalene mara nyingi haeleweki vizuri na hata kutambuliwa vibaya kama wanawake wengine wenye jina la Mariamu katika Agano Jipya.
Ili kuelewa vizuri Mariamu Magdalene alikuwa nani kwa kweli,Tutaangalia:
- Maisha yake kabla ya Yesu
- Maisha yake pamoja na Yesu
- Mambo yanayochanganya kumhusu
- Tunaweza kujifunza nini kutoka kwake
Tuanze na kile tunaweza kujifunza kutoka kwa Biblia kumhusu kabla Yesu hajaja katika maisha yake.
Maisha ya Mariamu Magdalene kabla ya Yesu
Hakuna mengi yanayosemwa katika Maandiko kuhusu maisha ya awali ya Mariamu Magdalena, lakini kama jina lake la mwisho linavyopendekeza, alitokea Magdala, kijiji cha uvuvi kwenye pwani ya magharibi ya Ziwa Galilaya.1
Inaaminika kuwa alikuwa tajiri kwa kuwa alisaidia huduma ya Yesu kwa kutumia rasilimali zake mwenyewe (Luka 8:2-3), ingawa chanzo cha utajiri huo hakijatajwa.
Maisha na huduma nyingi za Yesu zilifanyika katika eneo la Galilaya na maeneo yanayo zunguka, ambayo yalijumuisha Magdala. Kwa hivyo, inaeleweka kwamba Mariamu Magdalene angekutana na Yesu Mwenyewe wakati fulani wakati wa huduma yake.
Biblia inasema kuwa Mariamu Magdalene alikuwa amepagawa na pepo saba (Luka 8:2). Saba! Yesu aliwaponya watu wengi waliopagawa na mapepo wakati wa huduma yake, lakini Biblia inarekodi mtu mmoja tu mwingine ambaye alikuwa na mapepo zaidi ya Mariamu Magdalene (Marko 5:1-13; Luka 8:26-33).
Watu waliokuwa wamepagawa na pepo katika Biblia walionyesha tabia mbalimbali. Baadhi walikuwa bubu (Marko 9:17), wengine walikuwa na kifafa (Mathayo 17:15), wengine walikuwa na ulemavu wa kimwili (Luka 13:10-11).Wakati mwingine, mtu aliyepagawa na pepo wabaya alisababisha fujo na tishio kwa wengine na kwa wao wenyewe (Marko 5:2-5). Wakati mwingine walifukuzwa kutoka kwenye jamii na kutengwa na familia na marafiki zao.2
Tunaweza kujaribu kufikiria alivyokuwa, kama inavyoonyeshwa katika kipindi cha The Chosen, lakini Biblia haitaji tabia yoyote maalum ambayo Mariamu Magdalene aliionyesha alipokuwa amepagawa na pepo. Kwahiyo yawezekana alitendewa kama watu wengine waliopagawa na pepo walivyotendewa kipindi chake.
Lakini mara tu Mariamu Magdalene anapoponywa, tunamuona akirejewa na ufahamu, ana akili zake zote, na anakuwa sehemu ya jamii kama mfuasi wa Yesu.
Ni uponyaji huu wa ajabu ambao unabaki kama msingi wa maisha yote ya Mariamu kama mfuasi mwaminifu wa Kristo.
Maisha ya Mariamu Magdalene akiwa na Yesu

Katika Luka 7, sura katika Luka kabla ya Maramu Magdalene kutajwa kwa mara ya kwanza, Yesu anatoa mfano kwa Mafarisayo mmoja aliyeitwa Simoni ili kuonyesha uhusiano kati ya msamaha na upendo.
Katika mfano huo, watu wawili wanasamehewa deni ambalo hakuna hata mmoja wao angeweza kulipa. Deni moja ni dinari 500 – zaidi ya mshahara wa mwaka mmoja kwa mfanyakazi wa kawaida.3 Deni lingine, dinari 50, lilikuwa dogo zaidi, lakini halikuweza kulipwa hata hivyo.
Yesu anamuuliza Simoni swali muhimu: “Katika hao wawili ni yupi atakayempenda zaidi? Simoni akajibu akasema, Nadhani ni yule ambaye alimsamehe nyingi. Akamwambia, Umeamua haki” (Luka 7:42-43, NKJV).
Ujumbe hapa uko wazi – msamaha huamsha na kuongeza upendo, na unaposamehewa mengi, unampenda yule aliyekusamehe zaidi.
Biblia haijasema kwa muda gani Maria Magdalene aliteseka kutokana na pepo wabaya, lakini kupagawa na mapepo mengi kwa muda wowote ni jambo lisilowezekana kufikirika. Uponyaji wake lazima ulizua furaha isiyokuwa na kifani, shukrani, na hata shauku ya kumfahamu mtu huyu aliyeitwa Yesu.
Je, Mariamu Magdalene alimimina upendo kiasi gani kwa Yesu baada ya yeye kumponya kutoka kwa mapepo saba?
Jukumu la Mariamu Magdalene katika huduma ya Yesu
Baada ya kuponywa, Mariamu Magdalene alionyesha upendo na ibada yake kwa Yesu kwa vipaumbele vyake – pesa zake, muda wake, na maisha yake ya kila siku. Aliyasikiliza mafundisho Yake na kujifunza Torati pamoja na wafuasi wengine wa Kristo. Alikuwa mwanafunzi kwa kila maana ya neno hilo, jambo ambalo lilikuwa nadra kwa wanawake wakati huo.4
Kukubali pesa za Maria Magdalene kulikuwa na hatari kidogo kwa Yesu. Ingawa kwa ujumla ilikuwa inakubalika, maadui wa Yesu wangeweza kumkosoa kwa urahisi kwa kuwa na wanawake wanaomuunga mkono.5
Lakini uwezekano wa kupata upinzani kamwe haukumsumbua Yesu. Na haukumkatisha tamaa Maria Magdalene kumfuata.
Hata alishikamana Naye wakati wanafunzi wengine walipojificha wakati wa kusulubiwa kwa Yesu.
Uwepo wa Mariamu Magdalene msalabani, kwenye mazishi na ufufuo wa Yesu

Photo by Pixabay
Mathayo, Marko, Luka, na Yohana wote wanarekodi kwamba Mariamu Magdalene alikuwepo wakati wa kusulubiwa kwa Yesu, maziko yake, na kaburini baada ya kufufuka kwake.
Yesu alikuwa ametabiri kukamatwa kwake, kifo chake, na kufufuka kwake mara kadhaa kwa wanafunzi kumi na wawili kabla ya kukamatwa kwake. Na cha kusikitisha, wakati umati ulipofika kumkamata, wanafunzi wote walirudi nyuma na kujificha kwa sababu walihofia kwamba wangeweza pia kukamatwa na kuuawa kwa kumfuata Yesu (Mathayo 26:56). Petro hata alikana kumjua Yesu alipoulizwa kuhusu uhusiano wake naye (Luka 22:54-62).
Wafuasi wa Yesu walijua kwamba ilikuwa hatari kuwa na uhusiano naye. Katika huduma yake yote, Yesu alilazimika kusimamia msimamo wake kwamba yeye alikuwa Mwana wa Mungu na kwamba alikuwa na mamlaka ya kufanya huduma yake. Hivyo tunaweza tu kufikiria jinsi ilivyokuwa wakati wanafunzi wake wa karibu kumwacha alipowahitaji zaidi.
Mariamu Magdalene, hata hivyo, hakumwacha Yesu wakati alipomhitaji zaidi. Kwa kweli, yeye—pamoja na Mariamu mama wa Yakobo na Salome—walimfuata hadi msalabani ili kumhudumia kipekee kabisa (Marko 15:40-41).
Lakini Yesu alipokufa msalabani huku askari Warumi wakimfedhehesha, Mariamu Magdalene hakuweza kufanya chochote ila kutazama (Yohana 19:24-25).
Baada ya kifo chake, Mariamu Magdalene alifuata kwa karibu usiku huo wakati mwili wa Yesu ulipokuwa unatayarishwa na kuwekwa katika kaburi (Mathayo 27:59-61). Hata baada ya kifo, hakutaka kuondoka karibu yake.
Mapema sana asubuhi siku inayofuata, yeye na wengine wawili walikwenda kuupaka mwili wa Yesu manukato, lakini walikuta kaburi tupu. Jiwe lilikuwa limeondolewa kwenye mlango wa kaburi na hakukuwa na walinzi!
Kabla Yesu hajawatokea wanafunzi wake, Alimtokea Mariamu Magdalene (Marko 16:9). Yeye alikuwa mtu wa kwanza kushuhudia ufufuo wa Yesu. Kulingana na Injili ya Yohana, alimdhania kuwa ni mtunza bustani, lakini baada ya Yesu kumwita jina lake, “Mariamu,” mara moja alitambua kuwa ni Yeye (Yohana 20:14-16).
Bila kujali hali, Maria Magdalene alikuwa mtiifu kwa Yesu. Alikuwa tayari kusimama upande wake hata wengine wasipofanya hivyo, na Yesu alijua angeweza kumwamini kuwashuhudia wanafunzi wengine kwamba alikuwa amefufuka kutoka kwa wafu (Yohana 20:17-18).
Lakini ikiwa hivi ndivyo Biblia inavyosema kuhusu Mariamu Magdalene, ni mawazo gani mengine yaliyopo kuhusu utambulisho?
Dhana Potofu kuhusu Mariamu Magdalene
Kuna dhana kadhaa zisizo sahihi kuhusu utambulisho wa Mariamu Magdalene.
Kutokana na uvumi na mawazo mbalimbali kutoka kwenye sanaa na fasihi, mara nyingi huchanganywa kuwa kahaba na amekuwa akichanganywa na “mwanamke mwenye dhambi” ambaye alimimina mafuta kichwani mwa Yesu na kuosha miguu ya Yesu kwa machozi yake (Luka 7:37-38).6 Hata hivyo, Biblia haisemi kwamba mambo haya yana uhusiano wowote na Mariamu Magdalene.
Kwa kuwa jina Mariamu lilikuwa la kawaida, mara nyingine Mariamu Magdalene huchanganywa na Mariamu mama ya Yesu na mke wa Yusufu au Mariamu wa Bethania, dada ya Lazaro na Martha. Lazaro, Martha, na Mariamu walitoka Bethania, ambayo ilikuwa kijiji katika Yudea, maili mbili kutoka Yerusalemu (Yohana 11:1,18).
Lakini tunajua kwamba Mariamu Magdalene alitoka Magdala, kijiji katika Galilaya.
Pia kuna uvumi unaosambazwa katika riwaya maarufu ya The Da Vinci Code kwamba alikuwa ameolewa na Yesu na hata walikuwa na mtoto pamoja.
Lakini hakuna ushahidi wowote wa Kibiblia kuhusu shuhuda hizi potofu kuhusu Mariamu Magdalene. Badala yake, tunaweza kujifunza mengi kutokana na yale Biblia inayosema kumhusu, ingawa sio mengi.
Tunachoweza kujifunza kutoka kwa Mariamu Magdalene
Mariamu Magdalene alikuwa mwanamke wa kipekee ambaye alipokea zawadi ya uponyaji na akamfuata Yesu kama matokeo yake. Alikuwa jasiri, mwanafunzi mwenye bidii, na alimsaidia kifedha na kihisia.
Ingawa wanawake wengine pia walimfuata Yesu, jina lake ndilo linalotajwa zaidi miongoni mwa wanawake hawa katika Biblia, na tunaweza kujifunza mengi kutokana na maisha yake na mfano wake.
Tuna Mwokozi
Moja ya somo muhimu ambalo maisha ya Mariamu Magdalene yanatuonyesha ni kwamba tunaye Mwokozi binafsi.
Haijalishi ni jambo gani lililotokea katika siku za nyuma, Yesu daima yuko tayari na anatamani kukuponya na kukubadilisha.
Siku zako zilizopita hazitakiwi kuwa utambulisho wako. Pamoja na Mungu, utambulisho wako ni mpya katika Kristo (2 Wakorintho 5:17). Kuna heshima kubwa katika hilo!
Kukutana Yesu hutuongoza kwenye uhusiano wa kujitolea
Tunaweza pia kujifunza kutoka kwa Mariamu Magdalene kwamba kujitolea kikamilifu kwa Yesu Kristo ndio mwitikio sahihi kwa uponyaji wake.
Wakati mwingine tunapopokea zawadi, tunaweza kutojua jinsi ya kueleza shukrani zetu. Mara nyingine maneno yetu au matendo yetu yanaweza kuonekana kuwa madogo ikilinganishwa na yale yaliyo fanywa kwa ajili yetu.
Katika huduma ya Yesu, alitoa mwaliko wa “nifuate” kwa wengi. Kwa wanafunzi (Marko 1:17-18), waandishi (Mathayo 8:19-22), “kijana tajiri” (Mathayo 19:21), na kwa watu wote (Luka 9:23), Anatoa mwaliko huo huo wa “nifuate”.
Wakati Mariamu Magdalene alipoponywa kutoka kwa pepo saba, alipata uzoefu wa tabia halisi ya Mungu. Alikuja kwake binafsi kwa upendo na huruma. Na akajibu mwaliko wake wa: “Mtu akinitumikia, na anifuataye” (Yohana 12:26).
Kujitoa kwa Kristo ni onyesho la imani na upendo kwake

Image by RDNE Stock project
Lakini kufuata Yesu kunamaanisha nini hata?
Kwa Mariamu Magdalene, ilimaanisha shukrani, umakini, kipaumbele, na utumishi. Alimpa Yesu muda wake, umakini wake, na rasilimali zake. Aliamini kwamba Atamfundisha Biblia, jambo ambalo halikutokea sana kwa wanawake katika siku za Mariamu.
Huenda hata alikuwa miongoni mwa wanawake katika chumba cha juu pamoja na wanafunzi walipokuwa wakisali na kusubiri kupokea Roho Mtakatifu, jambo ambalo linamaanisha kwamba angekuwa mmoja wa waumini wa kanisa la awali, ingawa Biblia haijamtaja kwa jina lake moja kwa moja. Tunajua hakika, hata hivyo, kwamba alimfuata Yesu na kumtunza wakati alipohitaji sana.
Kwa yeyote kati yetu, kumfuata Yesu kunaweza kuonekana kama kujifunza Biblia ili kujua zaidi kumhusu, au kutoa michango kanisani au kwa mtu mhitaji, kujitolea katika kituo cha jamii yako, au kuwa tayari kumsaidia yeyote anayehitaji faraja. Inaweza kuonekana kama kumsaidia mpendwa au mgeni anayekabiliana na hali ngumu. Au inaweza kuwa jambo rahisi kama kukubaliana kwenda popote Mungu anapoongoza, bila kujali kama ilikuwa sehemu ya mipango yako au la.
Labda Mariamu hakupanga maisha yake iwe kama yalivyokuwa. Lakini baada ya kukutana na Yesu, alikumbatia kwa moyo wote lengo jipya la maisha yake.
Hivyo basi, bila kujali wakati au mahali tulipo, kumfuata Yesu kunamaanisha kujisalimisha kwake. Na kukaribisha ujasiri, amani, kusudi, na changamoto zinazoambatana na wito huo.
Tunaweza kufanya uamuzi wa kuishi maisha yetu kwa ajili ya Kristo kama vile Mariamu Magdalene alivyofanya. Tunaweza kumpa muda wetu, rasilimali zetu, akili zetu, na mioyo yetu kikamilifu kwake kama tendo la imani na upendo.
Hivyo, ingawa kuna mengi ya uwongo na visa kuhusu utambulisho wa Mariamu Magdalene, tunajua kwa uhakika kuhusu yeye kama ilivyoelezwa wazi katika Biblia: kama jibu la kuponywa na Yesu, alimfuata, alimsaidia katika huduma yake, akajifunza kutoka kwake, na alikuwa mwaminifu kwake wakati Alipomhitaji zaidi.
Ungependa kujifunza kuhusu wafuasi wengine wa Yesu? Angalia,
- Grudem, Wayne and Thomas R. Schreiner. “Notes on Luke,” in The ESV Study Bible, English Standard Version, Crossway, 2008, p. 1967. [↵]
- Keener, Craig S. “Notes on Luke.” NIV Cultural Backgrounds Study Bible, 1763. [↵]
- Ibid., 1760. [↵]
- Keener, Craig. “Luke,” in NIV Cultural Background Study Bible, edited by John H. Walton and Craig S. Keener, Zondervan, 2016, p. 1761. [↵]
- Ibid.. [↵]
- Beavis, Mary Ann, PhD, “Who is Mary Magdalene?” The Center for Christian Ethics at Baylor University (2013). [↵]
Majibu Zaidi
No Results Found
The page you requested could not be found. Try refining your search, or use the navigation above to locate the post.
