Yesu Kristo alipokuwa akihudumu duniani, wanafunzi wake kumi na wawili walikuwa baadhi ya watu Wake wa karibu. Watatu kati ya hao 12 walitajwa kuwa “kikundi chake cha ndani.”
Mmoja wao alikuwa Yakobo, mwana wa Zebedayo. Alikuwa kaka mkubwa wa Yohana, mwanafunzi mwingine.
Yakobo alikuwa mvuvi hadi alipoitwa kuwa mmoja wa wanafunzi wa karibu wa Yesu. Baada ya Yesu kupaa mbinguni, alitekeleza jukumu muhimu katika kanisa la awali kabla ya kuwa mtume wa kwanza kuuawa kwa ajili ya imani.
Ingawa unaweza kumjua mtume huyu kwa jina, kuna zaidi kuhusu hadithi yake kuliko unavyoweza kudhani. Hivyo basi, hebu tuangalie:
Historia ya Yakobo
Hakuna orodha ndefu ya mambo yaliyothibitishwa kuhusu Yakobo mwana wa Zebedayo, lakini tunajua pia aliitwa Yakobo Mkubwa. (Hii ilikuwa labda kumtofautisha na mwanafunzi mwingine aitwaye Yakobo ambaye aliitwa Yakobo Mdogo).1
Yakobo aliishi mahali fulani karibu na Bahari ya Galilaya, labda Kapernaumu au Bethsaida, kwa kuwa Yesu alimkuta “mbali kidogo” na Simoni Petro na Andrea (Marko 1:19).
Alikuwa na ndugu aitwaye Yohana, ambaye pia alikuwa mwanafunzi wa Yesu. Biblia inatuambia kwamba baba yao alikuwa Zebedayo (Marko 1:19), na tunaweza kudhani kwamba mama yao alikuwa Salome kwa kulinganisha Mathayo 27:56 na Marko 15:40.
Yakobo, Yohana, na baba yao wote walifanya kazi pamoja kama wavuvi katika Bahari ya Galilaya, pamoja na watumishi wao wa kuajiriwa (Marko 1:20).
Wakati Yakobo kadhaa wametajwa katika Agano Jipya, wao ni watu tofauti tofauti. Yesu alikuwa na ndugu aitwaye Yakobo (hilo sio la kuchanganya!), na ndugu huyu huenda ndiye aliyeandika kitabu cha Yakobo.2 Huenda pia alikuwa kiongozi wa kanisa la Yerusalemu (Matendo 15:13).
Yesu alikuwa na mwanafunzi mwingine aitwaye Yakobo, ambaye mara nyingi huitwa Yakobo mwana wa Alfayo au Yakobo Mdogo.
Lakini hebu tuelekeze fikra zetu kwa Yakobo Mkubwa, nduguye Yohana.
Kisa chake na Yesu kiilianza Yesu alipokuwa akihubiri Nazareti. Yesu alikuwa amewaita Petro na Andrea kuwa wanafunzi Wake. Kisha, akaona wengine wachache:
“….akaona ndugu wengine wawili, Yakobo wa Zebedayo, na Yohana nduguye, ambao walikuwamo chomboni pamoja na Zebedayo baba yao, wakizitengeneza nyavu zao; akawaita. Mara wakakiacha chombo na baba yao, wakamfuata” (Mathayo 4:21-22, UV050).
Maelezo ya Marko yanaongeza kwamba walimwacha baba yao pamoja na watumishi walioajiriwa ili baba yao asilazimike kuendeleza biashara ya familia peke yake (Marko 1:20).
Kitabu cha Luka kinasimulia hadithi tofauti kidogo, kikionyesha kwamba huenda Yakobo na Yohana hawakuwa wanafunzi wa kudumu hadi baadaye kidogo. Luka 5 inasema Petro, Andrea, Yakobo, na Yohana walikuwa washirika katika uvuvi, lakini hawakuwa wamepata kitu baada ya usiku mzima. Yesu aliwaambia washushe tena nyavu zao (Luka 5:4).
Walipofanya hivyo, walipata samaki wengi sana hata nyavu zao zikaanza kukatika (Luka 5:6)!
Yesu aliwaambia,
“Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu” (Luka 5:10, UV050).
Au, kama Marko 1:17 inavyosema,
“Yesu akawaambia, Njoni mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu” (UV050).
Walipokuwa nchi kavu, wanafunzi waliziacha nyavu zao za uvuvi na kumfuata Yesu.
Yakobo kama mwanafunzi
Kama wanafunzi wote wa Yesu, na kama sisi sote, Yakobo alikuwa na sifa nzuri na pia sifa zenye changamoto. Lakini bila kujali sifa zake, alianza uhusiano thabiti na usiotetereka na Mwokozi wake. Alionekana kuwa mmoja wa wanafunzi wa karibu zaidi na Yesu, pamoja na Yohana na Petro.
Tabia ya Yakobo
Sehemu za Agano Jipya zinazozungumzia kuhusu Yakobo na ndugu yake Yohana zinawaelezea kama watu jasiri, wenye uthubutu, na wakati mwingine wenye hasira ya haraka.
Kwa sababu hii, Yesu aliwapa wale ndugu wawili jina la utani “Wana wa Ngurumo,” au “Boanerge” kwa Kiaramu (Marko 3:17).
Tunaweza kuona tabia hii ya Yakobo katika hadithi moja kwenye Luka, wakati Yesu na wanafunzi Wake walikuwa wakisafiri kwenda Yerusalemu. Walituma wajumbe mbele yao kwenye kijiji cha Wasamaria, lakini Wasamaria walikataa kumpokea Yesu kwa sababu alikuwa anaenda Yerusalemu, mji wa Wayahudi. Wasamaria na Wayahudi walikuwa na uhasama wa muda mrefu.
Jibu hili liliwakasirisha Yakobo na Yohana. Wakamwambia Yesu,
“Bwana, wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize; [kama Eliya naye alivyofanya]?” (Luka 9:54, UV050).
Hasira yao ilikuwa imewashinda kabisa. Yesu aliwakemea kwa kufikiri namna hii:
“Akawageukia, akawakanya. [Akasema, Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo.] Kwa maana Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa” (Luka 9:55-56, UV050).
Hawa Wasamaria walikuwa watu ambao Yesu alikuja kuwahudumia.
Wakati mwingine, ndugu hawa walikuwa na uhakika sana wa nafasi yao ya heshima kiasi kwamba walimwomba mama yao amwombe Yesu kama Yakobo angeweza kuketi upande mmoja wa Yesu na Yohana upande mwingine katika ufalme wa Yesu ujao (Mathayo 20:20-21).
(Kulingana na simulizi ya Marko, ndugu hao wenyewe ndio wanaouliza.)
Kuketi karibu na mfalme kulikuwa karibu na cheo cha juu zaidi baada ya mfalme mwenyewe.
Yesu akajibu,
“Yesu akawaambia, Hamjui mnaloliomba. Mwaweza kunywea kikombe ninyweacho mimi, au kubatizwa ubatizo nibatizwao mimi?” (Marko 10:38, UV050)
Ndugu hao kwa upumbavu walisema wanaweza, ingawa hawakuwa na wazo lolote la maana halisi ya kunywa kikombe cha mateso na kifo cha Yesu.
Yesu akasema,
“Hakika mtakinywea kikombe changu; lakini kuketi mkono wangu wa kuume na mkono wangu wa kushoto, sina amri kuwapa, bali watapewa waliowekewa tayari na Baba yangu” (Mathayo 20:23, UV050).
Yakobo na Yohana huenda walidhani hili lilikuwa jambo la ajabu. Lakini wangeelewa maana ya kweli na kamili ya hili Yesu alipo kufa na kufufuka tena.
Lakini kabla hatujafika hapo, hebu tuangalie nafasi ya Yakobo miongoni mwa wanafunzi wengine.
Mmoja wa rafiki wa karibu wa Yesu
Kwa kuwa Yakobo alikuwa sehemu ya “kikundi cha ndani” cha Yesu, wakati mwingine alipata kushuhudia mambo ambayo wanafunzi wengine hawakuyashuhudia. Hapa kuna visa vichache kuonyesha hili.
Kuponywa kwa binti ya Yairo

Photo by cottonbro studio from Pexels
Hadithi hii imeandikwa katika akaunti zote za Injili isipokuwa ya Yohana.3 Mkuu wa Wayahudi aitwaye Yairo alimwendea Yesu, akimsihi aje amponye binti yake aliyekuwa karibu kufa. Yesu alichukua wanafunzi wake wote kwenda nyumbani kwa huyo mtu, lakini ni Petro, Yakobo, na Yohana tu ndio walioruhusiwa kuingia ndani ya nyumba pamoja na Yesu (Marko 5:37).
Wakati Yesu alipofika, yule msichana alikuwa amekufa na waombolezaji walikuwa wamefika, hivyo Yesu ilibidi awatoe waombolezaji wote nje. Kisha, mbele ya macho ya wazazi wa yule msichana, alimfufua tena.
Hivyo Yakobo alikuwa shahidi wa kufufuliwa kwa binti ya Yairo, mojawapo ya miujiza ya pekee sana ya Yesu, na aliona mwenyewe nguvu ya upendo ya Yesu.
Kubadilika Sura4
Yesu aliwachukua Petro, Yakobo, na Yohana juu ya mlima, ambapo Alibadilika sura—uso wake na mavazi yake meupe yalimetameta (Mathayo 17:2). Kisha Eliya na Musa walitokea na kuzungumza na Yesu.
Wakati Petro alijaribu kujibu hali ile (Mathayo 17:4), Yakobo na Yohana walikuwa kimya kabisa. Inawezekana kwamba Yakobo alikuwa ameshangaa, akijaribu kuelewa kuonekana kwa nabii na baba wa imani maarufu.
Na aliposikia sauti kutoka mbinguni, ikimtangaza Yesu kama Mwana wa Mungu wa kweli, Yakobo hatimaye alizidiwa na tukio hili la kimiujiza. Akaanguka chini na kufunika uso wake kwa hofu pamoja na wanafunzi wengine (Mathayo 17:6).
Lakini Yesu alimthibitisha alipokuwa akipitia ishara hizi zenye nguvu (Mathayo 17:7).
Tunaweza tu kufikiria jinsi tukio hili lilivyoweza kuimarisha imani ya Yakobo kwa Yesu kama Mwana wa Mungu.
Bustani ya Gethsemane
Yakobo na wale wanafunzi wengine wawili pia waliandamana na Yesu katika Bustani ya Gethsemane, usiku ule alipokamatwa.5 Lakini mwitikio wao kwa fursa hii haukuwa wa kuridhisha.
Mara tatu tofauti Yesu aliwaomba Yakobo, Yohana, na Petro wakae macho na kuomba wakati Yeye alienda mbele kidogo kuomba peke yake. Wakati huo wote, Yesu alipitia maumivu makali ya kiroho bustanini alipokuwa akiomba kuhusu hatima yake inayokuja msalabani (Luka 22:44).
Na mara tatu, wale waliokuwa karibu zaidi na Yesu, ambao walipaswa kuwa marafiki zake wa karibu, walilala usingizi.
Muda mfupi baadaye, Yuda, mwanafunzi mwingine wa Yesu, alikuja kumsaliti, akiwa ameleta kundi la askari kumkamata.
Ingawa Yakobo alikuwa na mtazamo wa ndani wa huduma ya Yesu, bado alikuwa na mengi ya kujifunza. Ilimchukua kuona Yesu akisulubiwa ili kumsaidia kuelewa kusudi lake la kweli na huduma yake.
Na matukio machache ambayo wanafunzi walikuwa nayo na Yesu kabla Yeye hajapaa tena mbinguni yaliimarisha dhamira ya kweli ya Yesu katika akili ya Yakobo, na kuchochea shauku yake ya kuwa shahidi Wake.
Basi hebu tuangalie maisha ya Yakobo baada ya wakati wa Yesu duniani kuisha.
Maisha ya Yakobo baada ya Yesu kupaa mbinguni

Photo by Ricardo Cruz on Unsplash
Jambo pekee ambalo Biblia inatuambia kuhusu maisha ya Yakobo baada ya kupaa kwa Yesu ni kwamba alikuwa mwanafunzi wa kwanza—baada ya Yuda Iskariote—kufa.
Yeye pia ndiye mtume pekee ambaye Biblia inarekodi kifo chake. Matendo 12:1-2 inatupa mwanga mfupi:
“Panapo majira yale yale Herode mfalme akanyosha mikono yake kuwatenda mabaya baadhi ya watu wa kanisa. Akamwua Yakobo, ndugu yake Yohana, kwa upanga” (UV050).
Herode huyu alikuwa Mfalme Herode Agripa, na wasomi wengi wanaamini Yakobo aliuawa mwaka wa 44 MK huko Yerusalemu.6 Hadithi za Kihispania zinapendekeza kwamba mwili wake ulipelekwa Santiago de Compostela, ambapo kaburi lake likawa alama muhimu ya Ukristo katika Enzi za Kati.7
Mwanahistoria wa Kanisa la Kikristo Eusebius wa Caesarea, aliyeishi katika karne ya tatu na ya nne MK, aliongeza kisa hiki kuhusu kifo cha Yakobo:
“Inaonekana kwamba askari aliyemleta [Yakobo] mahakamani aliguswa sana alipoona ushuhuda wake kiasi kwamba alikiri kuwa yeye pia ni Mkristo. Hivyo wote wawili wakachukuliwa pamoja, na njiani akamwomba Yakobo amsamehe. Yakobo alifikiria kwa muda, kisha akasema ‘Nakutakia amani,’ akambusu. Hivyo wote wawili walikatwa kichwa kwa wakati mmoja.”8
Hakuna uthibitisho wowote kutoka kwenye Maandiko kwamba hili lilitokea kweli, lakini tunajua kwamba Yakobo alifanya kazi ya kueneza Injili kwa takriban miaka 10 hadi kifo chake. Vinginevyo Herode asinge mlenga yeye badala ya mitume wengine muhimu kama Petro au Yohana.
Hadithi maarufu inasema kwamba alifanya kazi kama mwinjilisti, akiieneza Injili nchini Hispania kabla ya kufa kwake.9 Lakini hakuna ushahidi wowote wa jitihada hii isipokuwa maandishi yaliyoandikwa mamia ya miaka baadaye, Breviary of the Apostles.10 Na haiwezekani kwamba Yakobo angefanya yote haya na kurudi Yerusalemu kuuawa mwaka wa 44 MK.
Paulo pia alisema katika Warumi kwamba hakutaka kuhubiri “hapo ambapo jina la Kristo limekwisha kutajwa” (Warumi 15:20, UV050) na anazungumzia kwenda Hispania katika aya chache zinazofuata (Warumi 15:24). Kama Yakobo tayari alikuwa ameanzisha kanisa huko, Paulo huenda asingesema kwamba Kristo hakutajwa huko.
Lakini ingawa maisha ya Yakobo yalikuwa mafupi ukilinganisha na mitume wengine, bado tunaweza kujifunza mengi kutoka kwake.
Mafunzo kutoka kwenye maisha ya Yakobo

Photo by Joshua Earle on Unsplash
Yakobo ni mtume ambaye wengi wetu tunaweza kujilinganisha naye. Aliwahi kuwa na hisia kali, haraka, na mwenye kiburi. Lakini pia alimruhusu Yesu ambadilishe na kumfanya awe bora zaidi.
Yakobo alimtumikia Mungu kwa moyo wake wote
Yakobo alikuwa na bidii na shauku nyingi—ndiyo maana akapewa jina la utani Mwana wa Ngurumo. Katika siku zake za mwanzo kama mwanafunzi, alikuwa na mtazamo finyu kuhusu huduma ya Yesu ingawa alikuwa amejitoa sana kwa Yesu.
Baadaye, alipoelewa kusudi la kweli la Yesu duniani na kile Alichotimiza katika kifo chake, Yakobo alijitoa upya kama mtume—lakini safari hii, akieneza ukweli wa Yesu kwa wote waliomzunguka.
Kama wafuasi wa Yesu, tunaweza kutumia upendo wetu kwake kuongoza mahusiano yetu na wengine. Tunaweza kumshiriki Yesu kwa wale waliotuzunguka kupitia matendo yetu, jinsi tunavyowatendea watu, na kile tunachosema.
Imani yake inatia moyo
Bidii ya Yakobo ilikuwa imeelekezwa vibaya kidogo mwanzoni alipokuwa mwanafunzi. Lakini moyo wake ulikuwa mahali sahihi, na wakati ulipofika wa kuchagua upande, Yakobo alimchagua Yesu.
Aligeuza shauku hii kuwa nguvu isiyoweza kushindwa, akieneza Injili kwa wale waliokuwa Yerusalemu na pengine maeneo ya jirani. Sasa alielewa kusudi la kweli la Yesu, na alikuwa na imani ndani Yake inayolingana na hilo.
Alikuwa hata tayari kuhatarisha maisha yake kwa ajili ya Yesu. Mfalme Herode Agripa I alikuwa amemlenga Yakobo, na siku moja akamjia. Imani ya Yakobo ilisimama imara, hata alipokuwa akitishiwa kwa upanga (Matendo 12:2).
Na alikufa kwa ajili ya imani yake.
Hili linaweza kuwa msukumo kwetu. Haijalishi nini kinatupata, mwishowe, ni imani yetu ndiyo muhimu zaidi. Tunajua kwamba Yesu atakuwa akitusubiri kutukaribisha Atakaporudi.
Daima kuna mengi ya kujifunza

Photo by Sincerely Media on Unsplash
Ingawa alikuwa mmoja wa mitume wa karibu zaidi na Yesu, Yakobo hakuwa mtu mkamilifu au aliyekomaa. Alidhani yeye ni bora kuliko wengine na anastahili nafasi maalum karibu na Yesu. Bado alihitaji kujifunza kwamba njia bora ya kumtumikia Yesu ni kwa kuwatumikia wengine.
Huu ndio mfano ambao Yesu aliweka duniani, na Yakobo alilazimika kufanya makosa kadhaa kabla ya kujifunza ukweli huu.
Kwa kuwa sisi ni wanadamu, tutafanya makosa katika maisha yetu na hata katika uhusiano wetu na Yesu. Lakini bado tunaweza kujifunza, na bado tunaweza kukua, haijalishi tuna umri gani tayari. Daima kutakuwa na fursa za kuwahudumia wengine, kama vile Yakobo alivyojifunza.
Yakobo aliishi maisha ya kusisimua, maisha yaliyohusisha uvuvi na kusafiri kote Yudea akiwa mwanafunzi wa Yesu. Alishuhudia mambo ambayo sio mitume wote 12 walipata fursa ya kuyaona, na akawa mtumishi mwaminifu wa Mungu.
Angekuwa mfia dini, kama Yesu alivyotabiri (Mathayo 20:23). Ingawa Yakobo hakujua kuwa Yesu alimaanisha hivyo Alipomwambia, alikua katika imani na msimamo hata hivyo. Hakuishi maisha marefu, lakini alikua mtumishi wa Mungu anayetia moyo. Na hilo ni mojawapo ya mambo muhimu zaidi kuhusu milki yake ya kiutume.
Una hamu ya kujua kuhusu wanafunzi wengine? Soma kuhusu wao kwenye ukurasa wetu mkuu kuhusu wanafunzi.
Kurasa Zinazohusiana
- “James,” ATS Bible Dictionary, Bible Hub. [↵]
- “Introduction,” Holy Bible, English Standard Version, Crossway, 2007. [↵]
- Matthew 9:18-26; Mark 5:21-43; Luke 8:40-56. [↵]
- Matthew 17:1-8; Mark 9:2-8; Luke 9:28-36. [↵]
- Matthew 26:37-46; Mark 14:33-42. [↵]
- Nelson. [↵]
- “St.James,” Britannica. [↵]
- Nelson.[↵]
- Ibid. [↵]
- Ibid. [↵]
Majibu Zaidi
Nani Walikuwa Waamuzi wa Israeli Katika Agano la Kale?
Nani Walikuwa Waamuzi wa Israeli Katika Agano la Kale?Nyakati za misukosuko zinahitaji wanaume na wanawake wa vitendo. Waisraeli, waliokuwa wamekalia nchi ya Ahadi hivi karibuni, walijikuta katika nyakati hizo. Mataifa ya adui yaliposhambulia na kuwatesa makabila ya...
Mathayo Alikuwa Nani Katika Biblia?
Mathayo Alikuwa Nani Katika Biblia?Katika kitabu cha kwanza cha Agano Jipya, tunapata simulizi la Injili kutoka kwa Mathayo. Alikuwa mtoza ushuru Myahudi kutoka Kapernaumu katika karne ya kwanza MK, na huenda alichukiwa na Wayahudi wenzake kwa kuchagua kazi hiyo....
Wafalme 42 (na Malkia 1) wa Israeli na Yuda katika Biblia
Umewahi kujiuliza ni akina nani wote waliokuwa wafalme wa Israeli na Yuda katika Biblia? Wafahamu wote 42 (pamoja na malkia 1) na ujifunze masomo ya kina na yasiyotarajiwa kutoka kwenye hadithi zao.
Tunaweza Kujifunza Nini Kutoka Katika Maisha ya Yoshua
Yoshua alikuwa kiongozi maarufu katika Agano la Kale la Biblia.
Maisha ya Simoni Petro, Mtume wa Yesu
Simoni Petro alikuwa mvuvi wa kawaida ambaye alikuwa mmoja wa wanafunzi maarufu zaidi wa Yesu Kristo.
Yohana ni Nani, Mwanafunzi “aliyependwa na Yesu”?
Biblia inasemaje kuhusu mtume Yohana? Anajulikana kwa jambo gani leo? Jifunze zaidi kuhusu maisha, huduma, na urithi wa Yohana hapa.
Kujifunza Kuhusu Marko – Mwandishi wa Injili na Mfuasi wa Yesu
Kujifunza Kuhusu Marko - Mwandishi wa Injili na Mfuasi wa YesuMarko (ambaye jina lake kamili lilikuwa Yohana Marko) alikuwa na majukumu mengi katika Agano Jipya: alikuwa mfuasi wa awali wa Yesu Kristo, alisafiri katika Bahari ya Kati kama mhubiri wa Kikristo, na...
Luka Mwinjilisti Alikuwa Nani katika Biblia?
Luka alikuwa nani katika Biblia? Alijulikana kwa jambo gani na ni mchango gani alioutoa kwa kanisa la awali? Pata maelezo hapa.
Mfalme Daudi: Alikuwaje Mtu Ambaye Aliupendeza Moyo wa Mungu?
Vita, umwagaji damu, mauaji, uzinzi—maovu haya yote yalifunika maisha ya mtu wa Agano la Kale aliyeitwa Daudi.
Mariamu Magdalene ni Nani Katika Biblia?
Mariamu Magdalene alikuwa mfuasi na msaidizi wa kipekee wa Yesu Kristo wakati wa huduma yake duniani.















