Yesu ndiye kiini na msingi wa Ukristo. Na kama Waadventista wa Sabato, tunathibitisha kwamba Yeye ni Mwana pekee wa Mungu na Mwokozi wa wanadamu, ambaye anatupenda kwa upendo usiopimika na alikufa msalabani kubeba matokeo ya dhambi zetu.
Ina maana tu, kwamba mtu ambaye anatupenda vya kutosha hata kufa kwa ajili yetu anastahili muda wa kumjua, ambao unatuleta kwenye lengo la makala hii.
Chapisho hili ni muhtasari wa msingi wa maisha Yake, utume, na utambulisho.
Tutachunguza:
- Yesu ni nani
- Maana ya jina lake
- Sifa za tabia yake
- Unabii unaomhusu
- Huduma yake duniani
- Jinsi alivyo badilisha maisha ya watu
- Kifo na ufufuo wake
- Jinsi Anavyoendelea kuwa muhimu kwetu leo
Hebu tuchambue na tujifunze zaidi ili kujua Yesu ni nani.
Yesu ni nani, kulingana na Biblia?

Photo by Aaron Burden on Unsplash
Yesu Kristo ni Mungu kamili kama mshirika wa Utatu wa Mungu. Alifanyika mwanadamu alipozaliwa na Mariamu Akitimiza unabii wa Kiyahudi kuhusu Masihi, au mwokozi wa watu (Mwanzo 3:15). Alikuja kwenye dunia ili kuishi na kufa ili aweze kutuokoa kutoka katika dhambi na ubinafsi ulioanza na Adamu na Hawa katika Bustani ya Edeni.
Kama madhehebu mengine mengi ya Kikristo, Waadventista wa Sabato wanaamini kuwa kuna Mungu mmoja tu ambaye yupo katika Utatu yaani Mungu Baba, Mungu Mwana, na Mungu Roho Mtakatifu.
Yesu, kama Mwana wa Mungu, alikuja duniani hapa kutuonyesha Mungu ni nani, kutuonyesha mfano, na kusulubiwa ili tuweze kuwa na tumaini kwa ajili ya siku zijazo (Yohana 1:1, 14; 1 Wakorintho 8:6). Tunapata kisa cha Yesu akishuka duniani katika Injili za Agano Jipya.
Wakati Yesu alipokuwa duniani, aliishi maisha yasiyo na dhambi ya huduma (1 Petro 2:22). Na maisha haya yasiyo na dhambi aliyaishi kama mwanadamu, au kama Wafilipi inavyotuambia, katika “mfano wa wanadamu” (Wafilipi 2:7, NKJV).
Katika kiini cha Yesu, tunamuona mwana mnyenyekevu wa Mungu anayetupenda bila kikomo na anataka kutuponya kutokana na ugonjwa unaosababishwa na dhambi.
Kwa kweli, tunaona utume huu katika maana yenyewe ya jina lake.
Jina Yesu lina maana gani?
Kulingana na Maandiko, jina Yesu linamaanisha, “Atakayewaokoa watu wake na dhambi zao” (Mathayo 1:21, NKJV). Maana ya jina lake inatuambia kusudi la maisha yake, ambalo lilikuwa kufa kwa ajili yetu na kutuokoa kutoka kwa matokeo na nguvu ya dhambi katika maisha yetu.
Katika Biblia, majina ni muhimu sana kwa sababu yanatuambia kuhusu sifa na tabia za mtu.
Kwa mfano, katika Mwanzo 17, Mungu alibadilisha jina la Abramu (lenye maana “baba aliyeinuliwa”) kuwa Abrahamu (“baba wa mataifa”), ambalo lilimaanisha na kuthibitisha ahadi ya Mungu ya kumfanya “baba wa mataifa mengi” (Mwanzo 17:5, NKJV).
Vivyo, majina mengi ya Yesu yanaakisi sifa zake. Hapa kuna baadhi yake:
- Mwenyezi (Ufunuo 1:8)
- Mkate wa Uzima (Yohana 6:35)
- Mwokozi (Warumi 11:26)
- Imanueli au “Mungu pamoja nasi” (Mathayo 1:23)
- Mchungaji Mwema (Yohana 10:11)
- Mfalme wa Wayahudi (Mathayo 2:1–2)
- Mwana-Kondoo wa Mungu (Yohana 1:29)
- Nuru ya Ulimwengu (Yohana 8:12)
- Bwana wa Wote (Matendo 10:36)
- Masihi (Yohana 4:25–26)
- Mfalme wa Amani (Isaya 9:6)
- Rabi (Yohana 1:38)
- Mwokozi (Luka 2:11)
- Mungu (Isaya 40:3)
- Mwana wa Mungu na Mwana wa Adamu (Mathayo 26:63–64)
- Kristo (Mathayo 16:16)
Fikiria hivi:
Mtu ambaye ni mwaminifu, wa kweli, mtiifu, na mwenye kutegemewa huenda akaitwa “mwaminifu,” kama vile mtu ambaye ni mwaminifu, mkweli, mwenye upendo, na mwenye huruma anavyoweza kuitwa “rafiki”.
Vivyo hivyo, majina ya Yesu yanafunua kwamba Yeye ni mwalimu wetu, kiongozi, mtoaji, na mwokozi. Na yanatupa taswira ya jinsi alivyo.
Hebu sasa tuanglie baadhi ya sifa hizo.
Baadhi ya sifa za Yesu zilizo funuliwa katika Biblia?

Photo by Megan Watson on Unsplash
Biblia inatuambia kwamba Mungu—na Yesu—ni upendo. Sifa nyingine zote zake ni matokeo ya sifa hiyo kuu. Yeye ni:
- Mwenye kusamehe
- Mnyenyekevu
- Mwenye haki
- Mvumilivu
- Mwenye huruma
- Mpole
- Mwenye furaha
Na hizo ni mwanzo tu! Sifa za Yesu ni nyingi sana hatuwezi kuzihesabu.
Lakini hebu tuangalie jinsi sifa hizi zilivyojitokeza katika maisha yake. Ukifanya hivyo, utaona ukizidi kumpenda.
Upendo
Biblia inatuambia kwamba Mungu ni upendo (1 Yohana 4:8)—sio tu kwamba Anapenda. Kila sehemu yake ni upendo usio na ubinafsi, unaowalenga wengine (1 Wakorintho 13), na sifa zote nyingine alizonazo ni matokeo ya upendo huo.
Yesu alikuja kuonyesha upande huu wa Mungu (Yohana 3:16). Ingawa hakuwa na dhambi, alishuka duniani kama binadamu kutuhudumia na hatimaye akateswa msalabani kwa ajili ya dhambi zetu. Yeye ni mfano bora wa upendo na jinsi tunavyopaswa kupenda wale wanaotuzunguka.
Jambo la kushangaza pia ni kwamba Yesu anatupenda na kutujali sana hivi kwamba anatupa heshima ya kuitwa rafiki zake (Yohana 15:13).
Mwenye kusamehe
Yohana anatuambia kwamba “Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote” (1 Yohana 1:9, NKJV).
Yesu ana moyo wa kusamehe kwa kila mmoja wetu, hawezi kushikilia dhambi na makosa yetu dhidi yetu. Hachukui hesabu ya makosa yetu, wala kutufukuza kwa kuchukizwa.
Badala yake, Yeye huvutwa kwa wale wanaopambana na kutenda dhambi.
Hata alipokuwa amesulubiwa, akiwafia watu hao hao waliokuwa wanamkejeli, aliomba kwa Baba yake “uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo” (Luka 23:34, NKJV).
Mnyenyekevu

Photo by Davis Arenas
Yesu aliposhuka duniani, hakuja kama mfalme halisi ili aketi kwenye kiti cha enzi na kutawala ulimwengu, ingawa hivyo ndivyo watu na viongozi wa kidini walivyotarajia. Badala yake, alidhihirisha ufalme wa Mungu, ambao unahusu unyenyekevu na upendo usio na ubinafsi.
Biblia inasema,
“Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa maisha yake iwe fidia ya wengi” (Marko 10:45, NKJV).
Tunaona mfano wa hili katika Yohana 13 alipoosha miguu michafu ya wanafunzi wake. Kama mwalimu wao na Mwokozi, alistahili wao wamwoshe miguu yake, lakini hilo halikumzuia. Hakuna cheo kilichokuwa cha chini au cha aibu kwake.
Utumishi na unyenyekevu vilikuwa sehemu kubwa ya mtindo wa maisha ya Yesu na jinsi alivyo kama mfalme wa kweli.
Mwenye haki
Pamoja na kuwa hapa duniani, Yesu alisimama kwa ajili ya haki kwa wale ambao kawaida walikuwa wanapuuzwa au kuteswa. Hatimaye, upendo haukai kimya na kuruhusu wengine kuumizwa na kutendewa vibaya.
Tunaona hili likionyeshwa katika hadithi ya mwanamke aliyekamatwa katika uzinzi (Yohana 8). Wakati viongozi wa kidini walitaka kumpiga mawe, Yesu kwa unyenyekevu alisimamia haki. Aliinama chini, akaandika katika mavumbi, kisha akawaambia waandishi na Mafarisayo, “Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza kumtupia jiwe” (Yohana 8:7, NKJV).
Ingawa Biblia haijatuambia Yesu aliandika nini katika mavumbi, ni kwa uwezekano mkubwa kwamba Aliandika dhambi za waandishi na Mafarisayo, kuwasaidia kuona kwamba hawakuwa watu wasio na hatia katika majaribio yao ya kumhukumu mwanamke.
Kupitia tukio hili, Yesu sio tu kwamba alionyesha haki bali pia alifanya iwe wazi kwamba Mungu, na Mungu pekee, ndiye hakimu.
Mwenye subira
Uvumilivu wa Yesu unang’aa katika jinsi alivyowatendea watu waliokuwa karibu naye wakati wa maisha yake duniani.
Alionyesha uvumilivu hasa kwa wanafunzi wake, ambao walikuwa pamoja naye wakati wa huduma yake ya miaka mitatu na nusu. Wengi wao walikuwa na dhana potofu kuhusu utume wa Yesu na ubaguzi dhidi ya watu wa Mataifa (wasio Wayahudi). Walijifunza pole pole sana!
Na bado, Yesu hakukata tamaa juu yao.
Kwa mfano, mmoja wa wanafunzi wake mwenyewe, Petro, mara nyingi alishindwa katika imani yake, hata alimkana Yesu mara tatu kwa wale waliomuuliza kama ni mwanafunzi wake (Yohana 13:31–38; 18:25–27).
Lakini baada ya kufufuka kwake, Yesu hakumkemea Petro. Hakuonyesha hasira wala kukosa uvumilivu kwa kukana kwa Petro. Zaidi ya yote, Yesu hakumwondoa Petro kama mmoja wa wanafunzi wake. Badala yake, alimsamehe Petro na kumpa kazi: “Lisha kondoo wangu” (Yohana 21:15–17, NKJV).
Mwenye huruma
Yesu daima aliwahurumia wale waliokuwa na mahitaji; Alitamani kupunguza mateso yao.
Tena na tena, miujiza yake ya uponyaji inaonyesha huruma hii. Hata alipokuwa amechoka na alipohitaji kupumzika, huruma yake ilimfanya awasaidie wale waliokuwa wakiteseka na wenye njaa ya ukweli (Marko 6:30–34).
Wakati mmoja, wakati vipofu wawili waliokuwa wamekaa kando ya barabara waliposikia kwamba Yesu angepita. Licha ya makutano kuwataka wanyamaze, vipofu hao wawili walimlilia kwa uhitaji wao:
“Uturehemu, Bwana, Mwana wa Daudi!” (Mathayo 20:31, NKJV).
Tofauti na umati, Yesu hakuyaona haya kama usumbufu. Badala yake, “akawahurumia, akawagusa macho yao; mara wakapata kuona, wakamfuata” (Mathayo 20:34, NKJV).
Mpole
Badala ya maisha ya haraka na ya pupa, Yesu alituonyesha maisha ya amani na upole. Pia anatupa ahadi hii ya upole:
“Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu” (Mathayo 11:29, NKJV).
Mwenye furaha
Mara nyingi tunamfikiria Yesu kama mtu mwenye umakini, na hakika alijua jinsi na wakati wa kuwa na umakini. Lakini ni muhimu pia kukumbuka kwamba Yesu alikuwa na furaha ya Mungu moyoni mwake.
Furaha hii inaonyeshwa kupitia jinsi alivyowakaribisha watoto waje kwake ili awabariki (Marko 10:13–16), jinsi muujiza wake wa kwanza ulivyokuwa katika karamu ya arusi, wakati wa sherehe kubwa (Yohana 2:1-12), na jinsi anatamani furaha kwetu (Yohana 15:11)!
Baada ya kujua zaidi kuhusu tabia ya Yesu, hebu tuone jinsi maisha yake yalivyotimiza unabii wa Biblia.
Unabii kuhusu Yesu
Kuja kwa Mwana wa Mungu kulisubiriwa kwa muda mrefu! Kwa mamia ya miaka, Wayahudi walikuwa wakimtarajia Masihi, ambaye aliahidiwa mwanzoni mwa historia ya dunia hii. Walitegemeza matarajio haya kwenye Agano la Kale, ambalo limejaa unabii kuhusu kutokea na huduma ya Masihi.
Ufuatao ni baadhi ya unabii ambao Yesu alitimiza:
- Aliishi Misri katika miaka yake ya awali (Hosea 11:1)
- Alihubiri kwa mifano (Zaburi 78:2)
- Alifanya miujiza ya uponyaji (Isaya 35:5–6)
- Watawala walipanga njama dhidi yake (Zaburi 31:13)
- Aliteseka na kufa kwa ajili ya dhambi zetu (Isaya 53:1–10)
- Mikono na miguu yake ilichomwa (Zaburi 22:16)
- Alifufuliwa (Zaburi 16:9–11)
Lakini turudi nyuma zaidi:
Mwanzo wa kutajwa kwa Masihi ni ndani ya sura tatu za kwanza za Biblia, muda mfupi baada ya kisa cha Uumbaji. Mwanzo 3:15 ulitabiri kwamba mwanamke angezaa Mwokozi, ambaye angemshinda Shetani na kuwaokoa wanadamu kutokana na udanganyifu wake.
Baadaye, Mungu alimwahidi Ibrahimu kwamba Mwokozi angekuja kutoka uzao wa Ibrahimu, Isaka, na Yakobo (Mwanzo 12:3; Hesabu 24:17), jambo lililotimia kama ilivyoelezwa katika Uzao wa Yesu katika Mathayo 1:1–16.
Nabii Isaya alitabiri kwamba Yesu angezaliwa na bikira:
“Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara hii. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Immanueli” (Isaya 7:14, NKJV).
Na hata mahali kamili pa kuzaliwa kwa Yesu palitabiriwa katika Maandiko. Bethlehemu ilikuwa mji mdogo, duni, lakini ukawa mahali pa kuzaliwa kwa Masihi:
“Bali wewe, Bethlehemu Efratha, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele” (Mika 5:2, NKJV).
Manabii wa Agano la Kale walielezea maisha ya Masihi kwa undani mkubwa. Na Yesu alitimiza kila unabii kwa usahihi kamili.
Lakini ingawa kuzaliwa kwake na maisha yake yalitimiza unabii wa Agano la Kale, Yesu aliishi kwa njia ambayo watu wengi hawakutarajia. Walitarajia angekuja duniani kama mtawala. Kuketi kwenye kiti cha enzi na kuvaa taji, kama vile mfalme wa kawaida. Na kuwashinda Warumi—wakandamizaji wa Wayahudi.
Hii ilisababisha baadhi ya watu kuwa na huzuni kubwa na kuchanganyikiwa kidogo wakati Yesu alipojitokeza akiwa amevaa joho la unyenyekevu, akiwa amevaa viatu vya kawaida bila nia ya kudai kiti cha enzi cha mfalme wa wakati huo kuwa chake mwenyewe.
Tutaona baadaye jinsi maisha yake yalivyoonekana kwa uhalisia.
Huduma ya Yesu duniani

Photo by FRANK MERIÑO
Maisha ya Yesu kwa ujumla yalihusu huduma kwa wengine. Lengo lake lilikuwa kuweza kuhusiana nasi ili aweze kutusaidia. Alikumbana na majaribu kila siku kama sisi. Tofauti pekee ni kwamba alishinda kila jaribu kupitia uhusiano wake na Baba yake Mungu, kutuwekea mfano kamili wa jinsi tunavyoweza kushinda pia (1 Petro 2:22).
Injili nne, Mathayo, Marko, Luka, na Yohana, hutuonyesha jinsi Mwokozi wetu alivyo chukua kila upande wa maisha ya kibinadamu—misukosuko yake, maumivu yake, majaribu yake (Waebrania 4:15).
Alijua ilimaanisha nini kufanya kazi kwa bidii siku baada ya siku ili kukidhi mahitaji, kuwa na mvutano ndani ya mahusiano ya familia, na kuhisi kutokueleweka na kutendewa vibaya.
Alipitia mapambano ya mara kwa mara kati ya wema na uovu ambayo tunapaswa kupitia kila siku.
Na alilazimika kumchagua Mungu kila siku.
Mtume Paulo asema kwamba kwa sababu Yesu “Na kwa kuwa mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wao wanaojaribiwa” (Waebrania 2:18, NKJV).
Wakati wote huo, lengo lake lilikuwa kwa wale waliokuwa karibu naye.
Alihudumia mahitaji ya kimwili na ya kimaisha ya watu kisha akashughulikia mahitaji yao ya kiroho. Alituachia mfano kamili wa jinsi ya kuwatumikia wale wanaotuzunguka.
Kristo hakujali umaarufu, utajiri, au hadhi, bali badala yake alimtendea kila mtu aliyekuja kama rafiki aliyestahili kujaliwa, kukubalika, na ufahamu.
Kwa Yesu, mahusiano mazuri—kwa Mungu na kwa wanadamu—yalikuwa muhimu kuliko starehe na raha zote za kidunia.
Na kwa kuwatanguliza wengine na kufuata mapenzi ya Baba yake, aliweza kubadilisha maisha.
Jinsi gani Yesu alibadilisha maisha ya watu?
Yesu aliwabadilisha watu kupitia jinsi alivyowashughulikia. Alitambua thamani yao, alikutana na mahitaji yao, na kisha aliwaita wamfuate.
Hapa kuna baadhi ya namna alivyofanya katika Biblia:
- Alifanya miujiza ya kubariki na kusaidia watu
- Aliwaokoa watu kutoka katika dhambi zao
- Aliwaondolea mizigo ya vikwazo vya kidini na kuonyesha jinsi ya kushika sheria
- Aliotuonyesha upendo unavyoonekana
Alifanya miujiza ili kubariki na kuwasaidia watu
Katika Injili nne, Yesu alifanya miujiza mingi—kutuliza dhoruba kali hadi kufufua watu kutoka kwa wafu.
Katika kila kisa, miujiza haikuwa kwa ajili Yake mwenyewe. Alikataa kufanya miujiza ili kukidhi mahitaji yake mwenyewe au kujithibitisha (Mathayo 4:3–4). Badala yake, alifanya miujiza hiyo ili kuleta uponyaji na kusisitiza kweli za kiroho.
Yohana mwanafunzi anasema kwamba kazi za Yesu zilikuwa nyingi sana hivi kwamba “ambayo yakiandikwa moja moja, nadhani hata ulimwengu usingetosha kwa vile vitabu vitakavyo andikwa” (Yohana 21:25, NKJV).
Kwa hivyo, orodha ya baadhi ya miujiza itatosha:
- Aliugeuza maji kuwa divai (Yohana 2:1–11).
- Aliutuliza dhoruba baharini (Marko 4:35–41).
- Aliwalisha watu 5,000 kwa mikate mitano na samaki wawili (Yohana 6:1–14).
- Alitembea juu ya maji (Mathayo 14:22–33).
- Aliwaponya waliokuwa na ukoma (Marko 1:40–45).
- Alimponya na kumsamehe mwenye kupooza (Luka 5:17–26).
- Alimponya kipofu huko Bethsaida (Marko 8:22–26).
- Aliwafukuza pepo wachafu kutoka kwa mtu (Luka 4:31–37).
- Aliwaponya wanaume wawili waliokuwa na pepo (Mathayo 8:28–34).
- Alimfufua binti ya Yairo kutoka kwa wafu (Luka 8:40–56).
- Alimfufua Lazaro kutoka kwa wafu (Yohana 11:1–44).
Na ingawa miujiza ya Yesu ilikuwa muhimu, haielezi kabisa jinsi Yesu alivyo badilisha maisha ya watu. Utagundua zaidi baadaye.
Aliwaweka watu huru kutoka kwa dhambi zao

Photo by Pixabay
Yesu alibadilisha maisha kwa kuwapa watu msamaha na uhuru kutoka dhambini. Yesu hakuwaponya kimwili tu; Alitoa uponyaji wa kiroho kutoka katika ugonjwa wa dhambi. Alifanya hivi kwa kuondoa hatia na hukumu na kuonyesha kwamba inawezekana kushinda.
Msamaha ambao Yesu alitoa ulikuwa (na bado ni) mapinduzi, hasa kwa watu na utamaduni ambao walikuwa wakitoa dhabihu za wanyama kwa ajili ya msamaha na walikuwa wamepoteza lengo la dhabihu hizo.
Unaweza kufikiria kutoa dhabihu kisha ugundue kwamba Mungu anayesamehe dhambi anatembea kati yenu?
Lilikuwa jambo la kimapinduzi sana kiasi kwamba Yesu alipotangaza kwa mtu kwamba dhambi zao zilisamehewa, waandishi na Mafarisayo walipiga kelele: “Ni nani huyu anayesema maneno ya kukufuru? N’nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?” (Luka 5:21, NKJV).
Hawakujua walikuwa wakizungumza na Mungu Mwenyewe.
Yesu aliwabadilisha watu kwa kusamehe dhambi zao, lakini pia aliwabadilisha kwa kuwapa uhuru kutoka katika dhambi zao.
Tafakari tena kisa cha mwanamke aliyenaswa katika uzinzi.
Waandishi na Mafarisayo waliomleta mwanamke walidai apate adhabu ya kifo kama ilivyoagizwa katika sheria ya Musa kwa uzinzi (Yohana 8:5).
Lakini Yesu aliijua mioyo ya watu hawa na unafiki wao: “Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza kumtupia jiwe” (Yohana 8:7, NKJV).
Baada ya wanaume hao kuondoka kwa hasira, Yesu akageuka kwa mwanamke:
“Mwanamke, wako wapi wale washitaki wako? Je! Hakuna aliyekuhukumu kuwa na hatia? Akamwambia, Hakuna, Bwana. Yesu akamwambia, Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako; wala usitende dhambi tena” (Yohana 8:10–11, NKJV).
Yesu alimwamuru “enenda zako, wala usitende dhambi tena.” Hakuwa tena chini ya nguvu na hukumu ya dhambi iliyokuwa imemshikilia. Yesu alimpa msamaha na uhuru.
Wakati huo huo, Yesu alitwaa sheria ambayo Mafarisayo walikuwa wameipotosha na kuirekebisha tena.
Aliondoa mizigo ya vizuizi vya kidini na kuonyesha jinsi ya kushika sheria.
Watu wa siku hizo walichukua Amri Kumi na kuzitekeleza kwa ukali na kisheria sana kiasi kwamba walikuwa wanazingatia herufi ya sheria bila kuzingatia roho ya sheria.
Mafundisho ya Yesu yaliwaonyesha jinsi ya kurejea kwenye roho ya sheria.
Kwa mfano, katika Fundisho la kwenye Mlimani, moja ya mahubiri maarufu ya Yesu, Alizungumzia jinsi sheria inavyosema usiue na usizini. Lakini Alishusha hadi kwenye ngazi ya moyo kwa kueleza kwamba chuki ni dhambi kama ilivyo mauaji, na tamaa ni dhambi kama uzinzi (Mathayo 5).
Sheria inalenga kuwa njia ya kubadilisha maisha yetu, sio tu sheria za kufuata kama vipofu.
Yesu alifupisha kile sheria inahusu wakati alipoulizwa sheria ipi muhimu zaidi:
“Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii” (Mathayo 22:37–40, NKJV).
Hili lilikuwa la kushangaza kwa Mafarisayo. Walikuwa wakishika sheria, lakini walishindwa kuwapenda wengine, na walishindwa kumpenda Mungu kweli kweli.
Yesu anafanya iwe wazi: upendo uko katika msingi wa sheria ya Mungu. Na kuitii sheria kunahitaji mabadiliko ya moyo. Hii bila shaka ilikuwa mabadiliko ya mtazamo na wazo linalobadilisha maisha.
Akizungumzia upendo…
Yesu alibadilisha maisha kwa kuwaonyesha watu jinsi upendo unavyoonekana
Maisha ya Yesu ni mfano kamili wa upendo. Huduma yake isiyo na ubinafsi, iliyolenga wengine ilikuwa msingi wa kanisa la Kikristo la awali. Na bado inatuhimiza kuwatendea wengine kwa aina hii ya upendo leo.
Vipengele vyote vilivyo tangulia—miujiza yake, uhuru kutoka dhambini, na kufundisha upya sheria—ni mifano ya upendo wake kwetu.
Lakini labda mfano mkubwa na wenye kugusa moyo zaidi wa upendo ni uamuzi wake wa kufa kwa ajili yetu ili tuweze kuponywa kutoka kwa ugonjwa wa dhambi.
Hebu tuchunguze zaidi kuhusu onyesho hili kushangaza la upendo sasa.
Kifo na ufufuo wa Yesu

Photo by Rodolfo Clix
Kifo na ufufuo wa Yesu ndio kiini cha kisa cha wokovu. Ndicho kilele cha maisha ya Yesu na mfano mkubwa wa upendo usio na ubinafsi.
Mambo yaliyopelekea kifo cha Yesu na ufufuo wake wa hatimaye yalikuwa mazito sana.
Wakati wa kuwepo kwake duniani, Yesu alipata wafuasi wengi. Lakini pamoja na hilo kulikuja upinzani mkubwa pia.
Kulikuwa na daima mtu aliyepinga mafundisho yake, kumdhihaki, au kumshitaki kwa uwongo. Yesu alikuwa daima akiteswa na viongozi wa kidini ambao hawakusadiki kuwa yeye ndiye Masihi (Mathayo 9:34).
Baada ya miaka mitatu katika huduma yake, Yuda Iskariote—mmoja wa wanafunzi wake—alimsaliti kwa vipande 30 vya fedha (Mathayo 26:14–16).
Yesu alikamatwa katika Bustani ya Gethsemane na askari wa Kirumi na kufikishwa mahakamani. Mafarisayo walipotosha maneno yake kuhusu kuwa mfalme wa Wayahudi na kumshitaki kwa kufanya uasi dhidi ya utawala wa Kirumi (Marko 14:53–65; Yohana 18:33–37). Sheria ya Kirumi ilisema kuwa uasi dhidi ya mfalme ulipaswa kuadhibiwa kwa kifo.
Kisha akapelekwa mbele ya gavana wa Kirumi, Pontio Pilato, ambaye hakuwa na hakika kwamba Yesu alikuwa anastahili adhabu. Lakini kwa sababu alikuwa anaogopa jinsi watu wangemrejelea, alitaka kuwapa walichokuwa wakiomba—kifo cha Yesu.
Pilato kwa uwazi aliwaambia Wayahudi kwamba hakupata kosa lolote katika Yesu lililostahili kifo. Hata aliosha mikono yake mbele yao, ikimaanisha kwamba hangechukua jukumu la kifo cha Yesu. Kisha, alimsalimisha Yesu kwa watu apigwe na kusulubiwa (Marko 15:16–20).
Baada ya kuongozwa kwenda Kalvari, eneo nje ya Yerusalemu, Mwana wa Mungu aliye hai alisulubiwa.
Katika karne ya kwanza, kusulubiwa ilikuwa ni kifo chenye maumivu makali na cha kudhalilisha zaidi kinachoweza kufikiriwa. Kilitumika kuua wahalifu, watumwa, na maadui wa serikali ya Kirumi.
Hivyo Yesu alikufa kifo cha mhalifu.
Lakini haikuwa msalaba uliomwua Yesu. Yesu alikufa kutokana na uzito wa dhambi za ulimwengu na maumivu ya kutengwa na Baba yake (Marko 15:34, 2 Wakorintho 5:21, Isaya 53). Kwa kweli, ilikuwa ni nadra kwa watu waliotundikwa msalabani kufa haraka kama Yesu alivyofanya.1
Muda mfupi ambao Yesu alikuwa msalabani, ulimwengu wote na mbingu zote zilimlilia. Anga likawa giza kabisa, nchi ikatetemeka, na pazia la hekalu likapasuka kutoka juu hadi chini (Mathayo 27:45, 51–53).
Baada ya kuzikwa Ijumaa usiku, Ali pumzika kaburini siku ya Sabato na, kama ilivyotabiriwa, akafufuka siku ya tatu (Zaburi 16:9–11).
Baadhi ya wanawake walikwenda kuupaka marhamu mwili wa Yesu siku ya Jumapili asubuhi baada ya kifo chake. Lakini walikuta kaburi likiwa wazi, na malaika wa Bwana akatangaza, “Msiogope ninyi; kwa maana najua ya kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulubiwa. Hayupo hapa; kwani amefufuka kama alivyosema” (Mathayo 28:5–6, NKJV).
Wanawake walikimbia kuwaeleza wafuasi wengine wa Yesu kuhusu ufufuo wake lakini wakakutana na Yesu njiani. Aliwaagiza akisema, “Msiogope; enendeni, mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona” (Mathayo 28:10, NKJV).
Yesu alijitokeza kwa wanafunzi wake mara kadhaa kwa kipindi cha siku 40. Hatimaye, siku yake ya mwisho duniani, walimshuhudia akiondoka kwenda mbinguni (Matendo 1:9–11).
Wakati huo, Yesu aliwaahidi wanafunzi wake (na sisi) kwamba atamtuma Roho Mtakatifu kuwaongoza, kuwafariji, na kuwapa nguvu ya kuishi maisha ya haki na kuwa mashahidi wake kwa watu wengine (Matendo 1:8–9)—utekelezaji wa ahadi hii ulianza Siku ya Pentekoste (Matendo 2).
Na Yesu alipokuwa akipaa mbinguni, malaika alizungumza na wanafunzi wake waliokuwa wakimtazama na kuwapa ahadi ya kurudi kwake. Alisema:
“Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni” (Matendo 1:11, NKJV).
Kutokana na hili, tuna tumaini na uhakika kwamba Yesu atarudi tena kutuchukua kwenda mbinguni, ambayo ni matokeo mazuri ya kumpokea kama Mwokozi.
Jukumu la Yesu katika mpango wa wokovu

Photo by Sam Carter on Unsplash
Kifo cha Yesu msalabani kililipia gharama ya dhambi ya mwanadamu. Kilitimiza haki iliyohitajika kwa kukiuka sheria ya Mungu. Kwa maneno mengine, kifo chake kilikuwa sadaka ya kafara kwa wokovu wa mwanadamu (Mathayo 20:28).
Hili lilidhihirishwa katika huduma ya patakatifu pa Agano la Kale ambapo Mungu aliamuru kwamba kondoo alipaswa kuchinjwa kwa ajili ya dhambi.
Watu walipofanya dhambi, walilazimika kuleta kondoo mkamilifu, asiye na mawaa, ambaye angechukua dhambi zao. Kondoo huyu aliitwa kondoo wa kafara.
Yesu alipoanza huduma yake, Yohana Mbatizaji alimwita “Mwana-Kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu” (Yohana 1:29, NKJV).
Hivyo, Yesu alipokufa msalabani kwa ajili yetu, alikuwa ile sadaka ya mwanakondoo. Alikuwa hana dhambi na kamili katika vipengele vyote vya tabia yake. Na ingawa hakulazimika, alithibitisha upendo wake kwa binadamu kwa kutoa maisha yake kwa ajili yetu. Kifo chake hutupa uzima wa milele na kutufanya tuweze kupatanishwa na Mungu.
Biblia inasema wazi kwamba “mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu” (Warumi 6:23, NKJV).
Kupitia Kristo, tunaweza kuwa na umilele pamoja naye, badala ya kifo cha milele.
Kile Yesu anaweza kuwa kwa ajili yetu leo

Photo by Ben White on Unsplash
Kipawa cha wokovu cha Yesu kinaweza kupokelewa na kufurahiwa na yeyote. Ukikipokea kwa imani, unaweza kukua katika uhusiano wako naye na kupata uzoefu wako kuimarishwa kila siku.
Na ili kutusaidia kuishi maisha ya haki, Yeye ni kielelezo kamili na mpatanishi wetu mbinguni.
Yesu ndiye njia pekee ya wokovu kwa mwanadamu. Na Anataka ujue yote aliyokuwa nayo akilini aliposhuka kuishi katika dunia hii ya dhambi kutupa tumaini na kesho angavu.
Yesu pia anataka umjue yeye kama rafiki yako mwaminifu. Anatusikia tunapomwomba, hutuongoza katika matatizo yetu, na kufurahi pamoja nasi katika ushindi wetu. Yeye habadiliki kamwe. Yeye ndiye yule aliyekuwepo, yupo, na atabaki kuwa Mungu wetu milele (Waebrania 13:8).
Kwa Waadventista Wa Sabato, Yesu ni muhimu katika imani yetu. Na tunaamini kwamba Neno la Mungu ndipo mahali kamili pa kumjua na kujenga uhusiano naye.
Unataka kujifunza zaidi kuhusu Yesu na jinsi anavyotaka uishi milele?
Chagua Masomo ya Biblia Mtandaoni
Unataka kuendelea kujifunza? Pata habari zaidi kuhusu Yesu, mwanadamu, mpango wa wokovu, na jinsi Mungu anavyokupenda kiasi cha kutosha kujitolea kila kitu, ili tu kukupatia nafasi ya kumchagua.
Wakati mwingine inaweza kuwa ngumu kujua pa kuanzia, ndio maana tunatoa chaguo za masomo ya Biblia mtandaoni bure, rahisi kutumia, unaweza kufanya wakati wowote, mahali popote, na kwa kasi yako mwenyewe.
Shule hii ya Biblia mtandaoni itakuelekeza kupitia mada kuu za Maandiko, ikivunja dhana ngumu za Biblia katika vipande vidogo, ambavyo vinaweza kukusaidia kupata majibu ya maswali magumu zaidi ya maisha.
Kurasa zinazohusiana
- “The History and Pathology of Crucifixion,” South African Medical Journal. [↵]
Majibu Zaidi
Yesu na Yohana Mbaptisti: Uhusiano Wao na Huduma
Yohana Mbatizaji na Yesu walikuwa ndugu wa damu, marafiki, na wafanyakazi wa karibu katika huduma. Jifunze umuhimu wa kudumu wa uhusiano wao.
Biblia Ina Maana Gani Inaposema Yesu ni Mwana wa Mungu?
Biblia inapomwita Yesu Mwana wa Mungu inarejelea uungu wake. Jifunze ni nini kinachofanya hili kuwa muhimu na kinahusianaje na wokovu.
Kwa nini Ukoo wa Yesu Kristo ni muhimu sana?
Je, umewahi kufuatilia ukoo wako nyuma ya vizazi kadhaa? Je, umewahi jaribu kujua kama mababu zako walifanya jambo lolote maarufu (au la kusikitisha)?
“Mwana wa Adamu” ni nani katika Biblia?
Kwa kujiita Mwenyewe Mwana wa Adamu, Yesu alithibitisha jukumu lake kama mwokozi wa wanadamu. Jifunze jambo jingine jina hili linachosema kuhusu Yesu.
Kwa Nini Yesu Alikuwa na Wanafunzi na Walikuwa Akina Nani?
Wakati wa huduma ya Yesu duniani, Aliwachagua baadhi ya watu ili kusaidiana naye na kuendeleza kazi Yake. Walifahamika wakati huo kama “wanafunzi” Wake.
Je, Tunaweza Kumpata Yesu Kristo Katika Agano la Kale?
Je, Tunaweza Kumpata Yesu Kristo Katika Agano la Kale?Ndio, unaweza kushangaa kujua kwamba kuna mamia ya aya katika Agano la Kale kuhusu Yesu. Ingawa hazimtaji Yesu kwa jina, zinataja majina mengine tunayoyahusisha naye kama Masihi, Mwana wa Mungu, na Mwana wa Adamu....
Ni Lini Yesu Atarudi Tena?
Biblia inasema kwamba hakuna mtu anayeweza kujua, hata malaika (Mathayo 24:36)! Ndio maana Biblia inatushauri tusijaribu kuweka tarehe ya kurudi kwake. Kwa sasa, tunahimizwa kuwa tayari.
Baada ya Yesu kupaa: Alichofanya katika Agano Jipya
Tunapata kumjua Yesu, Mwana wa Mungu na Masihi wetu, kwanza kwa kusoma habari za Injili kuhusu huduma yake duniani.











