Maombi ndiyo njia kuu ambayo kwayo tunadumisha uhusiano wetu na Mungu. Ni njia yetu ya mawasiliano, na Yeye anasikia kwa namna ya ajabu kila neno linalotoka moyoni mwetu.
Lakini maombi pia yanabaki kuwa ya ajabu na ya kufikirika. Kwa hiyo, kama unatafuta njia za kujumuisha maombi katika ratiba yako ya kila siku, au kama unatafuta kitu cha kuboresha maisha yako ya maombi, hakuna mahali pazuri pa kuangalia kuliko Maandiko!
Tunaweza kupata mifano ya aina nyingi za maombi, yaliyoombwa na watu wa aina mbalimbali katika hali tofauti tofauti. Pia kuna mbinu chache tunazoweza kuiga katika maisha yetu ya maombi.
Tutaangalia:
- Mifano 15 ya maombi katika Biblia
- Mifano miwili ya maombi katika Biblia unayoweza kutumia
- Rasilimali za kukusaidia kuwa na maisha hai ya maombi
Hebu tuanze kwa kuangalia namna mbalimbali za watu walivyosali katika Maandiko.
Mifano 15 ya maombi katika Biblia
Maombi tutakayoangalia yanatoka kwa watu wa hadhi tofauti, tabia, mitazamo, na hali za kihisia. Tutasoma maombi kutoka kwa wafalme na manabii, na pia kutoka kwa watu wa kawaida. Na pia yale ya Yesu Kristo alipokuwa akiishi kama mwanadamu miongoni mwetu.
1. Ombi la shukrani la Hana (1 Samweli 2:1–10)

Photo by Heather Mount on Unsplash
Hana alikuwa hajapata mtoto kwa miaka mingi. Na kutokana na imani za kishirikina za watu wa wakati huo, hilo lilimsababisha kudhihakiwa mara kwa mara.
Kisha tunapata kumbukumbu ya ombi lake la dhati na lenye hisia kali katika 1 Samweli 1:9-18. Alimwomba Mungu kwa bidii ampe mtoto, na Mungu akampa mwana.
Ni katika shukrani yake ndipo anafurika katika ombi la shukrani, akimsifu Mungu kwa kumjibu.
Sisi pia tunashuhudia miujiza katika maisha yetu. Huenda isiwe mafanikio makubwa kama ya Hana, lakini miujiza midogo tunayoweza kuitafuta kila siku inaweza kuwa na maana sawa.
Na hii inaweza kuwa nafasi yetu ya kumshukuru Mungu kwa maombi.
2. Ombi la Ibrahimu kwa ajili ya Lutu (Mwanzo 18:22-33)
Kwa sababu ya mambo mabaya na hatari yaliyokuwa yakitokea katika miji ya Sodoma na Gomora, Ibrahimu alijua kwamba Mungu alikuwa na mpango wa kuiangamiza. Lakini mpwa wake Lutu alikuwa akiishi Sodoma.
Hivyo Ibrahimu akaanza kujadiliana kwa niaba ya Lutu, akiomba kwa Mungu kuihurumia miji hii ya waovu endapo bado kulikuwa na watu waadilifu ndani yake.
Hatimaye, maombi yake kwa Bwana yalizaa matunda, na Lutu akapewa nafasi ya kutoroka pamoja na familia yake kabla ya janga kutokea.
Inaweza kuonekana kama wazo la ajabu “kujadiliana” na Mungu. Lakini wazo hapa ni maombezi. Tunaweza kuomba kwa ajili ya usalama na wokovu wa wengine, hata kama wao wenyewe hawaombi mambo hayo. Mungu anaweza kufanya mambo mengi ya ajabu kwa sababu ya maombi yetu ya maombezi (mradi kile tunachomwomba Mungu hakivunji uhuru wa kuchagua wa mtu).
3. Maombezi ya Yesu kwa ajili ya Petro (Luka 22:31-34)
Mtazamo mwingine wa maombezi unamhusisha Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Alijitwika jukumu la kumuombea mmoja wa wanafunzi Wake aliyekuwa katika hatari ya kuanguka majaribuni.
Sisi pia tunaweza kuwaombea wale walio karibu nasi wanaohitaji hekima ya kuongoza maisha yao. Na tunahimizwa kuwaombea wale ambao tunawajibika kwa ajili yao, kama vile watoto wetu, wafanyakazi wetu, au yeyote atakayekuwa chini ya uangalizi wetu.
4. Sala ya Yehoshafati ya kuomba ukombozi kutoka kwa maadui (2 Mambo ya Nyakati 20:1-29)
Wakati mataifa matatu ya adui yalipopanga kuishambulia Yuda, mfalme Yehoshafati aliwakusanya watu wake na kuomba msaada. Kama mwitikio, Mungu aliwashughulikia maadui zake na hawakuhitaji hata kupigana vita.
Wewe pia unaweza kumwomba Mungu wakati unapohisi umenaswa au unakabiliana na dunia ukiwa peke yako. Mungu atapigana upande wako (Warumi 8:31).
5. Sala ya Yona katika dhiki (Yona 2:1-10)
Yona aliamua kukimbia wito wa Mungu na akaishia baharini akiwa njiani kuelekea Tarshishi. Lakini dhoruba kubwa ikaja juu ya meli yake na hatimaye, akatupwa baharini. Na samaki mkubwa akammeza.
Ni hali ya ajabu na ya kukata tamaa! Lakini akiwa ndani ya tumbo la samaki, aliomba kwa bidii kwa Mungu, na Mungu akamsikia. Samaki akamtapika kwenye ufukwe.
Sisi pia tunaweza kumwita Mungu katika nyakati zetu ngumu. Hata kama tuko kwenye matatizo kwa sababu ya maamuzi yetu mabaya, kama ilivyokuwa kwa Yona. Mungu wetu mwenye uweza ni mwenye rehema, msaada, na upendo pia. Anaweza kutuokoa katika hali ngumu na kutupa nafasi nyingine ya kuishi kwa ajili Yake.
“Ni huruma za BWANA kwamba hatuangamii, Kwa kuwa rehema zake hazikomi” (Maombolezo 3:22, SUV).
6. Sala ya toba ya Daudi (Zaburi 51:1-11; 32:1-5)

Photo by Jametlene Reskp on Unsplash
Mfalme Daudi alikuwa amelala na mke wa mtu mwingine na akapanga kwa mafanikio kumuua mume wake. Kisha Mungu akamtuma nabii ili amkumbushe matendo haya ya kuchukiza.
Akiwa amezidiwa na utambuzi na msukumo wa dhamira, alitubu haraka. Alimsihi Mungu kwa rehema, akitambua uzito kamili wa dhambi zake.
Anamsihi Mungu, akisema “Ee Mungu, uniumbie moyo safi, Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu, Usinitenge na uso wako, Wala roho yako mtakatifu usiniondolee” (Zaburi 51:10-11, SUV).
Ingawa alikuwa amekosea, pia alikuwa na uhakika kwamba Mungu Angemsamehe. Na kama mtu aliyepata msamaha wa Mungu, anaishia kusema:
“Kwa maana Wewe, Bwana, U mwema, Umekuwa tayari kusamehe, Na mwingi wa fadhili, Kwa watu wote wakuitao” (Zaburi 86:5, SUV).
Wewe pia unaweza kumjia Mungu kwa sala ukiwa na mzigo wa hatia na aibu, hata kama ni mkubwa kiasi gani. Unaweza kumuomba msamaha na urejeshwaji wa nafsi yako.
7. Sala ya Petro na Yohana ya kuomba ujasiri (Matendo 4:23-31)
Baada ya kifo na ufufuo wa Yesu, mitume walipewa agizo la kueneza injili duniani kote. Na walipofanya hivyo, walikumbana pia na mateso makubwa kutoka kwa serikali dhalimu au viongozi wa kidini waliompinga Yesu.
Lakini hilo halikuwazuia. Petro, Yohana, na mitume wengine walitumia kila nafasi waliyoipata kuomba nguvu walizohitaji, na daima walimshukuru Mungu kwa jinsi alivyowasaidia.
Petro na Yohana walimtukuza Mungu kwa maneno mazuri na yenye nguvu, na baada ya kuomba pamoja na waumini wenzao, “mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri” (Matendo 4:31, SUV).
Inaweza kuwa jambo la kutia moyo sana kusoma sala hii unapojisikia mpweke, umekata tamaa, au huna msaada. Inatukumbusha kwamba Mungu yuko upande wetu, na kwamba tunahimizwa pia kumkaribisha Roho Mtakatifu ndani yetu.
8. Sala ya Ezra ya kuomba ulinzi (Ezra 8:21-22)
Waisraeli walikuwa wamepata ruhusa na rasilimali za kurudi Yerusalemu mwishoni mwa utumwa wa Babeli. Na walihitaji kuwa salama waliposafiri kupitia maeneo ya kigeni wakiwa na mali nyingi.
Hivyo Ezra aliwaongoza kufunga na kuomba ulinzi kwa ajili ya safari yao, na Mungu aliwapa safari salama.
Kutokana na hili, tunaona kwamba zile sala tunazozifanya kila mara kabla au wakati wa kusafiri ni muhimu. Daima ni wazo jema kuomba ulinzi—kwa ajili yetu wenyewe, marafiki zetu, familia zetu, na wale tunaokutana nao njiani.
9.Sala za Nehemia na Esta za kuomba kibali na msaada (Nehemia 2:1-4; Esta 4:1-17)
Nehemia alihitaji ruhusa na rasilimali ili kujenga upya kuta za Yerusalemu zilizokuwa zimeharibiwa. Na Esta alihitaji kubatilisha amri ya mauti iliyokuwa imepangwa kuangamiza familia na kabila lake lote huko Uajemi.
Lakini ili kupata haya yote, walihitaji msaada kutoka kwa wafalme wa Uajemi. Na wafalme hawa hawakuwa na tabia ya kueleweka—kosa dogo tu mbele ya mfalme lingeweza kuwa na madhara makubwa.
Hivyo wakaomba. Wakaomba kibali kutoka kwa wafalme hawa wasiotabirika… na Mungu akajibu sala zao.
10. Sala ya Danieli ya kuelewa ukweli wa kiroho (Danieli 10:1-21)

Photo by Kelly Sikkema on Unsplash
Danieli alihitaji kuelewa unabii aliokuwa amepewa kuhusu watu wake na nyakati za mwisho. Hivyo alifunga na kuomba kwa siku 21, na Mungu akamtumia malaika kumpa taarifa zilizomsaidia kuelewa.
Kwa hiyo kama kuna sehemu yoyote ya Maandiko usiyoielewa, muulize Mungu kuhusu hilo. Ameahidi kwamba Roho Wake Mtakatifu “ Atawaongoza awatie kwenye kweli yote” (Yohana 16:13, SUV).
Majibu hayawezi kuja kila mara kupitia malaika kama ilivyokuwa kwa Danieli, lakini uwezekano ni mkubwa. Unaweza kuongozwa kupata hekima zaidi kupitia rafiki, hubiri kanisani, utafiti wa ziada, au hata ufunuo unaokujia wakati usiotarajiwa.
11. Sala ya Yesu ya kuomba nguvu na kujisalimisha katika Gethsemane (Mathayo 26:36-46)
Wakati Yesu alipokuwa karibu kusulubiwa, aliogopa njia iliyokuwa mbele Yake. Uzito wa dhambi aliokuwa akienda kubeba kwa ajili ya wanadamu wote, na maumivu na aibu aliyopaswa kuvumilia.
Hivyo akaomba nguvu ili apitie hayo ikiwa ni mapenzi ya Baba Yake, na njia pekee ya kuuokoa.
Na tunasoma kwamba Mungu alimtumia malaika kumtia nguvu.
Tunapoomba kwa jina la Yesu, tunaweza kuwa na uhakika kwamba anatuelewa kwa sababu amepita njia hii kabla yetu. Yesu alipitia kila aina ya uzoefu wa kibinadamu ambao tumepitia (Waebrania 4:15).
Akiwa Mwana wa Mungu mwenyewe, Yesu aliomba kwa Baba Yake alipohisi uzito wa dunia ukimlemea, na Mungu alihakikisha anapata nguvu kwa ajili ya utume Wake.
Sisi pia tunaweza kuomba kwa ajili ya nguvu ya Roho Mtakatifu kushinda majaribu, na nguvu ya kuvumilia tunapojikuta katika hali ngumu zaidi.
12. Sala ya Eliya wakati wa kukata tamaa (1 Wafalme 19:4-10)
Eliya alikuwa ametoka tu kwenye pambano la ajabu na waabudu sanamu wa Israeli.
Kisha malkia Yezebeli akamtishia kumuua kwa sababu aliwashinda manabii wake wote wa Baali.
Hivyo alikimbia kuokoa maisha yake, na huzuni kuu ikamshukia. Alijisikia mpweke na aliyekata tamaa. Na katika kufadhaika kwake, akaomba. Hata alimwambia Mungu kwamba anataka kufa.
Lakini Mungu alimtunza kwa upole, akampa chakula chake, na akajifunua mwenyewe kwa Eliya, hadi hatimaye akapata moyo wa kuendelea.
Vivyo hivyo, Mungu anaweza kutoa amani, faraja, na tumaini ambalo hatuwezi kulipata mahali pengine popote (Zaburi 23:4; Wafilipi 4:7). Anaweza kukusaidia kupata ujasiri hata unapojisikia umeishiwa kabisa (Zaburi 56:3, 4; Yohana 14:17).
13. Sala ya mfalme Hezekia aliyelala kitandani akiomba uponyaji (2 Wafalme 20:1-11)
Mfalme Hezekia alikuwa mgonjwa sana, na hata akapewa habari kwamba angekufa hivi karibuni.
Lakini hakutaka kufa, hivyo akaomba uponyaji.
Katika jibu la sala yake, Mungu alimponya na kumpa miaka mingine 15 ya kuishi.
Wewe pia unaweza kuomba uponyaji wa mwili wako, akili, na roho. Hatuwezi kujua ni miaka mingapi tutakuwa nayo ya kuishi, lakini tunaweza kumtumaini Mungu anayeweza kuponya roho zetu kwa njia ambazo hatutarajii.
14. Sala ya sifa ya Sulemani (1 Wafalme 8:22-24)
Baada ya Sulemani kujenga hekalu na wakati wa kuliweka wakfu ulipowadia, alikumbuka uaminifu wa Mungu na akamsifu.
Anaonyesha jinsi alivyotimiza ahadi Zake kwake na kwa baba yake Daudi, na anamshukuru Mungu kwa upendo Wake usio na mwisho.
Inaweza kuwa kichocheo kikubwa cha imani kuchukua muda kutafakari ushindi wa maisha yako na maombi yaliyopata majibu. Wewe pia unaweza kutangaza shukrani zako na utambuzi wa wema wa Mungu kwako.
Mimina kila kitu kilicho moyoni mwako, ukimshukuru Mungu kwa mambo yote mazuri anayofanya. Kama maneno ya Daudi, “Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA” (Zaburi 103:1, SUV).
15. Yeremia anatumia maombi “kumimina” hisia zake kwa Mungu wakati wa kipindi kigumu (Maombolezo 1-5)

Photo from Unsplash
Baada ya kuharibiwa Yerusalemu na Wababeli, na baada ya watu wengi wa taifa lake kuchukuliwa mateka, Yeremia alimwomba Mungu akieleza masikitiko yake. Imeandikwa kama kitabu kizima katika Biblia, kitabu cha Maombolezo.
Alimweleza Mungu kuhusu aibu, hali ya kukosa makazi, na hata kukata tamaa kwa watu wake. Alionyesha mashaka yake, hofu, na hasira, na alitafuta faraja ya Mungu na kutumaini urejeshwaji wa baadaye.
Vivyo hivyo, sisi pia tunaweza kumkimbilia kwa Mungu tunapokabiliwa na maafa makubwa. Ikiwa tunavunjika moyo na hali tulizo nazo, au hata kama tunakasirika na kutamani Mungu angejibu maombi yetu kwa njia tofauti, Anakaribisha uaminifu huu na maelezo haya. Inatupa nafasi ya kukua na kujifunza. Na hilo huanza daima na kuwa wazi kweli kweli.
Kisha, ndani Yake, tunaweza kupata faraja, tumaini, na nguvu ya kuendelea mbele.
Na ingawa tunaweza kuomba aina hizi za maombi kila moja peke yake katika hali tofauti, mara nyingi aina hizi tofauti huungana katika ombi moja na kutengeneza sala moja.
Hata ile sala ambayo Yesu aliwafundisha wanafunzi Wake ilikuwa sala moja, iliyojumuisha aina nyingi za sala hizi.
Ifuatayo, tutaangalia mifano ya sala inayopatikana katika Biblia ambayo inaweza kukusaidia kusali aina hiyo ya sala “kamili”.
Mifano 2 ya sala katika Biblia
Kuna mifano miwili ya sala katika Biblia ambayo unaweza kutumia:
- Sala ya Bwana
- Mfano wa KKKK
Hebu tuangalie kila moja yao.
1. Sala ya Bwana
Mfano huu ulifundishwa na Yesu Mwenyewe kwa wanafunzi Wake. Wakati mmoja walipomwona akisali, “mmoja katika wanafunzi wake alimwambia, Bwana, tufundishe sisi kusali” (Luka 11:1, SUV).
Hivyo, Yesu aliwafundisha sala ya Bwana itumike kama mfano.
Haikukusudiwa tu kurudiwa, bali kufunua vipengele vya sala kamili.
Katika kujibu ombi la wanafunzi, Yesu alisema…
“Basi ninyi salini hivi;
Baba yetu uliye mbinguni,
Jina lako litukuzwe,
Ufalme wako uje,
Mapenzi yako yatimizwe,
hapa duniani kama huko mbinguni.
Utupe leo riziki yetu.
Utusamehe deni zetu,
kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu.
Na usitutie majaribuni,
lakini utuokoe na yule mwovu.
[Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele.
Amina.] ” (Mathayo 6:9-13, SUV).
Hebu tuchambue na tuangalie kila sehemu ya sala hii:
Mwite Mungu “Baba”
Jina hilo la upendo, “Baba yetu,” linamaanisha kwamba tunamtambua Mungu kama yule aliyetuumba. Zaidi ya hayo, inamaanisha kwamba tunatambua sisi ni wanafamilia ya kifalme ya Mungu mbinguni. Sisi ni watoto wa Mungu Aliye Juu Sana na anafurahia kututimizia mahitaji yetu.
Baba yetu aliye mbinguni ndiye Mungu wa kweli pekee; miungu mingine yote ni sanamu. Yeye peke yake ndiye Muumba wa ulimwengu (Yeremia 10:10,11).
Pia ana rasilimali zote za ulimwengu mikononi mwake. Tunaweza kumuomba kwa ujasiri, kumkiri, na kumtegemea kabisa kama mtoto anavyo mwamini baba yake wa duniani.
Tambua kwamba Mungu ametukuka sana

Photo by Jeremy Perkins on Unsplash
Yeye ni Baba yetu mpendwa lakini pia Yuko “mbinguni” (Mathayo 6:9, SUV). Yeye ameinuliwa zaidi kuliko baba zetu wa duniani. Hii inamaanisha kwamba humchukulii Mungu kama kiumbe wa kawaida kwa kuwa “kwa maana, Mungu yuko mbinguni, na wewe upo chini” (Mhubiri 5:2, SUV).
Onyesha heshima kwa jina Lake takatifu
Kwa kusema “jina lako litukuzwe,” inamaanisha kwamba tunamheshimu na hatupaswi “kulitaja jina la BWANA Mungu wetu bure.” Hatupaswi kuchukulia majina Yake kwa wepesi kwa kuwa “jina Lake ni takatifu na la kuogopwa” (Mathayo 6:9; Kutoka 20:7; Zaburi 111:9, SUV).
Tunapaswa “kusimama kwa hofu mbele Zake” (Zaburi 33:8, SUV).
Pia inamaanisha kwamba tunatambua kuwa jina la Bwana linawakilisha tabia Yake.
“….BWANA, BWANA, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli; mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi” (Kutoka 34:6-7, SUV).
Eleza shauku yako kwa ajili ya ufalme Wake ujao
Kuomba “Ufalme wako uje” ni kukiri kwamba tunataka ufalme wa Mungu ukue na ustawi (Mathayo 6:9, SUV). Na kwamba tunataka ushawishi Wake usambae duniani kote.
Inaonyesha kwamba uko katika umoja na mbingu, ukitazamia uzima wa milele pamoja na Mungu mwisho wa ufalme huu wa duniani.
Na kwamba unahitaji msaada wa Mungu katika maisha yako ya kila siku ili kuishi kanuni za Ufalme Wake hata tukiwa bado duniani. Kanuni zilizoonyeshwa katika sheria Yake ya upendo na uongozi wa utumishi.
Kuchagua kujisalimisha kwa mapenzi ya Mungu
Yesu aliendelea kusema, “Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni” (Mathayo 6:10, SUV).
Hii inamaanisha tunajisalimisha kwa mapenzi ya Mungu kwa kutii mapenzi yake. Kisha, kama mtunga Zaburi, tutasema, “Kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu; Naam, sheria yako imo moyoni mwangu” (Zaburi 40:8, SUV).
Sheria hii ya Mungu ina asili yake mbinguni. Mbinguni, “malaika hufanya maagizo yake” (Zaburi 103:20, SUV).
Na Mungu alitupa amri hizo hizo kupitia Musa katika Mlima Sinai. Aliiandika kwenye mbao za mawe na kuiweka katika sanduku la agano (Kutoka 40:20).
Katika maono, Yohana aliona hekalu la Mungu likifunguliwa mbinguni na “sanduku la agano lake likaonekana ndani ya hekalu lake” (Ufunuo 11:19, SUV).
Hivyo, tunapoomba kwamba mapenzi ya Mungu yatimizwe duniani kama yalivyo mbinguni, tunasema kwamba tuko tayari kutii amri za Mungu.
Tunaonyesha kwamba tunachukia dhambi na tunataka kuishi maisha ya haki na kuwasaidia wengine waishi vivyo hivyo kwa kuwashirikisha injili. Kwa kufanya hivi, tunachangia kuanzishwa kwa ufalme wa haki.
Wasilisha mahitaji yako ya kila siku

Photo by Jack Sharp on Unsplash
Kisha tunaweza kumwomba Mungu “utupe leo riziki yetu” (Mathayo 6:11, SUV).
Yesu aliwafundisha wanafunzi kumweka Mungu wa kwanza kabla ya mahitaji yao. Nusu ya kwanza ya sala inalenga kwa Mungu kama Baba yetu, jina Lake, ufalme Wake, na mapenzi Yake. Unapompa Mungu kipaumbele katika maisha yako, ndipo unaweza kumuomba kwa ujasiri mahitaji yako binafsi.
Aliwafundisha akisema, “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa” (Mathayo 6:33, SUV).
Na kwa kusema kwamba tunaomba “Utupe leo riziki yetu” badala ya “chakula changu cha kila siku,” inamaanisha kwamba tunapaswa pia kuwaombea wengine mahitaji yao, sio yetu tu. Na tunapobarikiwa, tunapaswa kupanua baraka zetu ili kuwabariki wengine pia.
Pia, Anatuomba tuzingatie mahitaji yetu ya kila siku. Ni bora kuzingatia kile kilicho mbele yetu, bila kuwa na wasiwasi kuhusu mambo ya mbali ya baadaye. Siku ya sasa ndiyo kazi yetu ya sasa, na tunahakikisha kumuomba Mungu atuongoze katika hilo.
Mungu anajua kwamba misongo na wasiwasi wa kidunia vinaweza kutuzidi. Hivyo anatuhimiza tuombe mara kwa mara na tuwasiliane naye hata katika mahitaji yetu ya msingi ya kila siku. Kufanya hivi husaidia kulinda akili zetu dhidi ya mambo yanayosababisha msongo.
Omba kwa ajili ya mahitaji yako ya kiroho (kukiri/toba)
Kwa kumuomba Mungu “Utusamehe deni zetu” (Mathayo 6:12, SUV), Anamaanisha deni la dhambi zetu. Tunajua hatuko wakamilifu, na tunajua tunahitaji msamaha. Na Mungu anatupatia msamaha huo na kutusaidia kukabiliana na mapambano yetu.
Na kama vile tunaomba msamaha Wake wa upendo, Anaonyesha kwamba tunapaswa pia kuwasamehe wengine—“kama sisi tunavyowasamehe wadeni wetu” (Mathayo 6:12, SUV).
Kanuni hii ni muhimu sana kiasi kwamba Yesu alituonya akisema, “Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu” (Mathayo 6:15, SUV).
Omba uongozi na nguvu za Mungu kushinda majaribu
Tunapaswa kumwomba Mungu atusaidie tusishindwe na majaribu yanayotupata (Mathayo 6:13).
Baada ya kuwasilisha mbele za Mungu mahitaji yako ya kimwili na kiroho, Anakupa ruhusa ya kumwomba “Awalinde ninyi msijikwae” (Yuda 24, SUV Msisitizo umeongezwa). Ni sawa kumwomba Mungu msaada kwa jambo lolote!
Jaribu sio dhambi bali ni ushawishi wa Shetani kutuongoza kwenye dhambi (Yakobo 1:13; Mathayo 4:1).
Habari njema ni kwamba “Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili” (1 Wakorintho 10:13, SUV).
Ukimwomba akuongoze, utasikia sauti yake ikisema, “Njia ni hii, ifuateni” (Isaya 30:21, SUV).
Omba ukombolewe
Tunapojikuta tumejaribiwa, tunaweza kuomba, “utuokoe na yule mwovu” (Mathayo 6:13, SUV).
Haijalishi Shetani amekushikilia kwa nguvu au kwa muda gani katika dhambi yoyote, Yesu ni mkombozi mwenye nguvu. Isaya anasema kwamba “Hata jeshi la wafungwa wake aliye hodari watapokonywa mikononi mwake, na mateka yake aliye jabari wataokoka” (Isaya 49:25, SUV).
Bwana wetu ana “mamlaka yote mbinguni na duniani,” na ukimwita, “Nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua” (Mathayo 28:18; Yeremia 3:33, SUV).
Tambua ukuu, nguvu, na mamlaka ya Mungu
Hatimaye, tunapaswa kutambua ukuu Wake. Kwa kufanya hivi, tunaonyesha kwamba tunaamini Yeye hafungwi na chochote mbinguni na duniani, na kwamba tuna uhakika Atajibu maombi yetu (Mathayo 6:13).
2. Mfano wa maombi wa KKKK
Mfano huu haujanukuliwa moja kwa moja katika Biblia lakini unafuata mfano wa sala ya Bwana kwa njia ambayo inaweza kuwa rahisi kwetu kuelewa. K.K.K.K ni kifupi cha:
Kusifu
Kuungama
Kushukuru
Kuomba mahitaji
Hebu tuangalie kila kipengele kati ya hivi kwa undani.
Kusifu

Image by Daniel Reche from Pixabay
Kama ilivyo katika mfano wa sala ya Bwana, mfano wa maombi wa KKKK unaanza kwa kuchukua muda kutafakari kwa makusudi ukuu wa Mungu. Kumsifu mtu au kitu ni kukitazama kwa upendo, na kuthamini sifa zote nzuri. Ni kuabudu kitu au mtu kwa upendo na heshima ya kina.
Tunapoanza maombi yetu, tunaonyesha upendo wetu kwa Mungu ambaye kwa upendo alituumba kila mmoja wetu. Hii ni nafasi yetu ya kila siku “Mpeni BWANA utukufu wa jina lake” (Zaburi 29:2, SUV).
Mungu ni Muumba wetu, Mkombozi wetu, Mtoaji wetu, na Mtegemezi wetu. Tena, hii inaonyesha kwamba tunamjua tunayemwabudu.
Kuungama
Sisi sote “kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;” Na “Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu” (Warumi 3:21; 1 Yohana 1:8, SUV).
Sote tunakutana na changamoto kila siku, na Mungu ndiye Mtu mkamilifu wa kutusaidia nazo. Na ili tuweze kushinda jambo fulani, kwanza tunapaswa kulikubali.
Tunapotambua kwamba tunapambana na udhaifu fulani tulio nao, au kichocheo, au ikiwa tumeudhika, tumekasirika au kuumizwa, tunaweza kumwaga yote hayo. Hiyo inamruhusu Mungu kuingia na kutuongoza hata katika hali ngumu zaidi.
Tunayo ahadi nzuri kwamba Mungu “ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote” (1 Yohana 1:9, SUV).
Shukrani
Mara tu tunapoungama dhambi zetu, tunaweza kumshukuru Mungu kwa furaha kwa maombi yaliyopata majibu huko nyuma. Mshukuru kwa upendo wake usiobadilika, kwa uangalizi wake wa kila siku, na kwa jinsi anavyo kutimiza mahitaji yako.
Kukuza roho ya shukrani sio tu kwamba ni sahihi kwa kuzingatia Mungu alivyo, bali pia hutusaidia kukua. Na kadri tunavyotumia muda mwingi kufikiria baraka tulizopewa na Mungu, inaweza kuboresha mtazamo wetu wa jumla pia.
Kwa hiyo, “Tuje mbele zake kwa shukrani” (Zaburi 95:2, SUV).
Maombi ya Mahitaji
Kuomba kwa unyenyekevu kunamaanisha kuwasilisha mahitaji yetu mbele za Baba yetu wa mbinguni. Haijalishi hitaji lako ni kubwa au la haraka kiasi gani—liwasilishe tu kwa Mungu.
Paulo anatuambia kwamba “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu” (Wafilipi 4:6, 7, SUV).
Kufuata mifano hii kunatupa mpangilio tunaposali na hutupatia dira unapoanza safari yako kuelekea maisha ya maombi yenye nguvu zaidi.
Rasilimali za kukusaidia kuwa na maisha ya maombi yenye uhai
Maombi hutuwezesha kuungana na Mungu wetu mwenye nguvu zote na mwenye upendo.
Ili kuanza kuboresha maisha yako ya maombi, unaweza kuanza kwa kuangalia sala za mfano—zilizoandikwa au za video.
Kisha pata vitabu vya ibada za kila siku au mwongozo wa maombi wenye aya za Biblia itakayokuongoza wakati wa maombi. Inaweza kuwa vitabu, mtandaoni, au kama programu tumishi. Na unaweza hata kuweka kumbukumbu za maombi.
Unaweza kuanza kwa kuwa na sala ya asubuhi tu. Kisha unaweza kuongeza sala ya jioni ili kupitia yote yaliyotokea uliyoyaombea asubuhi.
angalia Maombi—Ni nini na kwa nini ni muhimu?
Chagua Masomo ya Biblia Mtandaoni
Unataka kuendelea kujifunza? Pata habari zaidi kuhusu Yesu, mwanadamu, mpango wa wokovu, na jinsi Mungu anavyokupenda kiasi cha kutosha kujitolea kila kitu, ili tu kukupatia nafasi ya kumchagua.
Wakati mwingine inaweza kuwa ngumu kujua pa kuanzia, ndio maana tunatoa chaguo za masomo ya Biblia mtandaoni bure, rahisi kutumia, unaweza kufanya wakati wowote, mahali popote, na kwa kasi yako mwenyewe.
Shule hii ya Biblia mtandaoni itakuelekeza kupitia mada kuu za Maandiko, ikivunja dhana ngumu za Biblia katika vipande vidogo, ambavyo vinaweza kukusaidia kupata majibu ya maswali magumu zaidi ya maisha.
Makala Zinazohusiana
Majibu Zaidi
Biblia Inasemaje Kuhusu Kutatua Migogoro
Ukikabiliana na mgogoro mgumu? Jifunze mahali mgogoro ulipoanzia na kanuni za Biblia unazoweza kuzitumia kukusaidia kutatua mgogoro.
Kanuni za Kibiblia kwa Mahusiano Yenye Afya
Mahusiano ya maisha yetu yanaweza kutofautiana kutoka furaha hadi matatizo, rahisi hadi ngumu, furaha hadi kuchosha…
Je, Maombi Yanafanya Kazi? Ikiwa Ndio, Maombi Yanajibiwaje?
Maombi ni jinsi wanadamu wanavyoifikia nguvu kubwa kuliko wao. Kwa Wakristo, ni jinsi tunavyowasiliana na Mungu.
Tunda la Roho Mtakatifu katika Biblia Ni Nini?
Tunapokuza uhusiano wetu na Yesu, Roho Mtakatifu hutupa tabia ambazo hutusaidia katika shughuli zetu za kila siku na mwingiliano wetu.
Sifa za Heri ni Nini (Na Maana Yake)?
Sifa za heri zinazopatikana mwanzoni mwa Mahubiri ya Yesu kwenye Mlima katika Injili ya Mathayo, ni tamko la ufalme wa Yesu.
Jinsi Biblia Inavyotafsiri Upendo
Neno “upendo” linatumika katika namna ya kihisia sana, ya muda mfupi, na isiyo na maana. Hapa tunaangalia maelezo yote ya Biblia kuhusu upendo wa kweli, ambao ni mkubwa na wa kina zaidi.
Ngazi ya Fadhila ya Petro, Ni nini na Inafanyaje Kazi?
Ngazi ya fadhila ya Petro ni msemo unaohusiana na tabia nane zinazopaswa kuendelezwa wakati mtu anakua katika uhusiano wao na Yesu Kristo.
Silaha Zote za Mungu Kama Ilivyoelezwa Katika Waefeso 6
Katika Waefeso 6, Mtume Paulo alikuwa akisaidia watu kuelewa maana ya kujilinda katika vita vya kiroho (Waefeso 6:10-18).
Je, Ni Kawaida Wakristo Kuwa na Mashaka?
Ndio, ni kawaida kabisa kwa Wakristo kupitia vipindi vya mashaka katika maisha yao ya kiroho. Kila mtu ameshawahi kuwa na mashaka wakati mmoja au mwingine, hata wachungaji, wanatheolojia, na watu muhimu katika Biblia.
Kile Mfano wa Yesu Kinatufundisha Kuhusu Maombi na Kufunga
Kufunga na kuomba vilikuwa sehemu muhimu ya huduma ya Yesu Duniani. Hebu tujifunze jinsi mfano wa Yesu unavyoweza kutufundisha jinsi ya kuwa na uhusiano wa karibu zaidi na Mungu. Kufunga na kuomba vilichukua sehemu kubwa ya huduma ya Yesu Duniani.
Aya za Biblia Wakati Unapojisikia Kukata Tamaa
Maisha kamwe sio rahisi, lakini mara kwa mara mambo huwa magumu zaidi, yenye maumivu, au yanayo vunja moyo.














