Je, Kila Kitu Alichosema Ellen White Kilikuwa na Uvuvio wa Kiungu?

Kanisa la Waadventista Wasabato linaamini kwamba ujumbe mwingi wa Ellen White ulikuwa ufunuo kutoka kwa Mungu. Lakini hiyo haimaanishi kwamba kila kitu alichowahi kusema kilikuwa cha kinabii, au kilipaswa kuchukuliwa kama maagizo ya moja kwa moja kutoka kwa Mungu.

Hata hivyo, wengi wetu bado tunajiuliza jinsi tunavyoweza kutofautisha kati ya maoni yake binafsi na mawazo yaliyovuviwa, au maneno aliyosema alipokuwa katika maono kutoka kwa Roho Mtakatifu.

Basi hebu tuchambue jinsi ya kutambua asili ya ujumbe na nukuu zake nyingi zilizoandikwa.

Tutaeleza:

Lakini hebu tuanze kwa kufafanua maana ya kuongozwa na Mungu kwa karama ya unabii. Tutaangalia hasa jinsi hiyo inavyoweza kutumika kwa mambo tofauti ambayo manabii wanasema, kwa nyakati tofauti.

Maana ya kuwa mjumbe wa Mungu

A man walking with a Bible in his hand

Photo by Ben White on Unsplash

Sio kila kitu ambacho Ellen White alisema au kuandika kilitolewa kwake na Mungu moja kwa moja.

Watu wanaosema vinginevyo kuhusu Ellen White—au nabii yeyote wa kweli—hawajaelewa jinsi ufunuo wa kiungu unavyotolewa. Mawazo haya huwafanya watu waamini kwamba kila kitu ambacho nabii anasema ni amri ya kiungu.

Lakini wazo hili halina msingi katika Biblia.

Ellen White mwenyewe alilishughulikia swala hili wakati mshiriki mwenzake wa kanisa alipomwandikia barua, akimwambia kuwa alikuwa amefundishwa kuamini kwamba kila kitu alichosema au kuandika kilikuwa kimevuviwa na Mungu.

Alijibu:

“Ndugu yangu, umejifunza maandishi yangu kwa bidii, na hujawahi kuona kwamba nimewahi kudai mambo kama hayo. Wala hutakuta kwamba waanzilishi wa kazi yetu wamewahi kudai mambo kama hayo.”1

Ingawa Ellen White alilifafanua swala hili, bado kuna watu wengi wanaojiuliza kama huu ndio uhalisia.

Hata hivyo, je, haingekuwa na maana zaidi kwa Mungu kuhakikisha kwamba kila kitu ambacho manabii Wake walisema kilitoka moja kwa moja Kwake, hadi kwenye uchaguzi wa neno moja moja? Je, hilo lisingesaidia kupunguza mkanganyiko ambao wasomaji wanakutana nao wanapojaribu kutofautisha kati ya ujumbe uliovuviwa na usio vuviwa?

Jibu la swali hili lina sehemu mbili.

Sio kila kitu nabii anachosema kimeongozwa na Roho kwa sababu:

  • Manabii ni watu wenye uhuru wa kuchagua.
  • Manabii wanaweza kupewa maneno maalum ya kusema, lakini mara nyingi wanaongozwa na mawazo ambayo wanaagizwa kuyashiriki na wengine (hii inaitwa “uvuvio wa mawazo”).

Sababu ya kwanza kwa nini kila neno analosema nabii sio la kiungu ni kwa sababu Mungu alimpa kila mwanadamu nia na uchaguzi huru.

Hata katika wadhifa wa kiroho unaotambuliwa kama nabii, hawa wanadamu bado wana uhuru wa kusema mawazo yao wenyewe na kueleza hisia zao binafsi.

Angalia tu jinsi Yonah alivyoongea kuhusu Ninawi katika Agano la Kale, ingawa alijua kwamba Mungu alitaka kuwaokoa watu hao (Yona 4:1-10). Au jinsi Yohana Mbatizaji alivyokataa kumbatiza Yesu katika Agano Jipya kwa sababu alijihisi hastahili (Mathayo 3:14).

Kwa kifupi—Maandiko yanaeleza kwamba manabii bado ni watu. Wao ni watu binafsi wanaowajibika kufanya maamuzi yao wenyewe.

Watu wengine wanaona ubinafsi huu kama kikwazo cha kufuata mapenzi ya Mungu. Lakini Mungu anathamini ubinafsi na bado anaweza kutumia watu binafsi kuendeleza mpango Wake.

Kwa kweli, ubinafsi wa manabii wa Mungu (na wafuasi kwa ujumla) ni njia ya Mungu ya kuwafikia wengine kwa njia zinazofaa na zinazoweza kueleweka.

Hii ni kwa sababu ufunuo wa kiungu sio swala la manabii kuandika kile ambacho Mungu aliwaamuru neno kwa neno (isipokuwa katika matukio machache), bali ni kufikisha dhana ambazo Mungu anawapa kwa kutumia maneno yao wenyewe.

Na ingawa manabii wanajitahidi kutochakachua ujumbe waliopokea, wana uhuru wa kuandika kwa namna itakayosaidia wasomaji wao kuelewa vizuri kile ambacho Mungu anataka kuwaambia.

Baadhi ya hayo yanaweza kujumuisha aina ya lugha wanayoitumia, mafumbo au misemo wanayoweza kutumia, au mtindo wa uandishi wa nabii huyo binafsi.

Hivi ndivyo uvuvio wa mawazo unavyofafanuliwa.2

Kuhusu sehemu ya Roho Mtakatifu katika mchakato huu, Yeye huwapa manabii ujumbe na kuwasaidia kuona mambo kwa mtazamo wa kimbingu. Roho Mtakatifu anaweza kufanya hivi kupitia maono, ndoto, matendo au maneno ya watu wengine, Biblia, au kwa kuweka hisia za kiungu au msukumo katika akili ya nabii.

Manabii pia wanaweza kutumia uzoefu wao na Roho Mtakatifu kutoa ushauri wa kitaaluma unaotegemea Biblia, na kufanya maamuzi yenye ufahamu.

Hii ina maana kwamba hata kama nabii anatoa ushauri bila maagizo mahususi kutoka kwa Roho Mtakatifu, kuna uwezekano kwamba ushauri wao (ikiwa unafaa) bado utakuwa na manufaa kwako.

Kwa kweli, hisia hii inaonyeshwa na mtume Paulo katika 1 Wakorintho 7:25, anapoanza ujumbe kwa kusema, “Kwa habari za wanawali sina amri ya Bwana, lakini natoa shauri langu, mimi niliyejaliwa kwa rehema za Bwana kuwa mwaminifu” (SUV).

Hata hivyo, bado ni muhimu kutofautisha kati ya hekima ya kimungu na hekima ya kibinadamu ili tuweze kuelewa vyema jinsi ya kuitumia katika maisha yetu.

Kutofautisha kati ya ujumbe mtakatifu na ujumbe wa kawaida

Ellen G. White writing

“Courtesy of the Ellen G. White Estate, Inc.”

Ingawa Ellen White alikuwa na jukumu la kushiriki ujumbe ambao Mungu alimpa, kulikuwa na nyakati ambapo alitoa maoni kuhusu mambo ya kawaida ya maisha au kujibu maswala ambayo hayakuhusiana moja kwa moja na dini au mambo ya kiroho.

Ingawa alikuwa na karama ya unabii, bado alikuwa mtu wa kawaida. Alikuwa na sababu zake binafsi za kuandika na kuzungumza—iwe ni kuandika orodha ya manunuzi au kuandika barua kwa familia—kama vile mtu mwingine yeyote angefanya.

Lakini hata katika nyakati za Ellen White, kulikuwa na watu walioshindwa kuelewa jinsi uvuvio wa kiungu unavyofanya kazi. Walidhani kwamba kila kitu alichosema kilipaswa kuwa ujumbe wa moja kwa moja kutoka kwa Mungu.

Ellen White alizungumzia wazo hili kwa kueleza tofauti kati ya mambo matakatifu (dhana ya kidini iliyoongozwa na Mungu), na yale ya kawaida (maoni ya kila siku):

“Kuna nyakati ambapo mambo ya kawaida lazima yasemwe, mawazo ya kawaida lazima yajaze akili, barua za kawaida lazima ziandikwe na taarifa kutolewa ambayo imepitishwa kutoka kwa mmoja hadi mwingine kati ya wafanyakazi. Maneno kama haya, taarifa kama hizi, hazijatolewa chini ya uvuvio maalum wa Roho wa Mungu.

 

Maswali huulizwa wakati mwingine ambayo hayahusiani kabisa na mambo ya kidini, na maswali haya lazima yajibiwe. Tunazungumza kuhusu nyumba na mashamba, biashara za kufanywa, na maeneo ya taasisi zetu, faida na hasara zake.

 

Napokea barua zikiuliza ushauri juu ya mambo mengi ya ajabu, nami natoa ushauri kulingana na nuru niliyopewa.”3

Neno “mtakatifu” halimaanishi kwamba maandishi haya yanaheshimiwa au kuabudiwa kuliko Biblia. Inamaanisha tu kwamba ujumbe huo ulikuwa kuhusu mambo muhimu ya kiroho, ambapo Mungu alimpa mawazo ya kujadili na hoja za kutoa.

Kutofautisha kati ya maandishi ya kawaida na maandishi matakatifu ni hatua ya kwanza katika kubaini kama ujumbe wa Ellen White umevuviwa na Roho wa Mungu au la.

Unaweza kufanya hivi kwa kuangalia yaliyomo kwenye kitabu au makala husika.4

Utajua kwamba anazungumza kwa uvuvio wa Mungu…

  • Ikiwa alisema kwamba “alionyeshwa” jambo fulani katika maono
  • Ikiwa alizungumza kuhusu mambo ambayo asingeweza kuyajua au kuyatabiri yeye mwenyewe
  • Alipozungumza kama mwenye mamlaka
  • Alipokemea dhambi (Kumbuka: Hii ni tofauti na ushauri au kujali. Hii ni kuitaja waziwazi dhambi hatari miongoni mwa jamii ya Wakristo).
  • Alipozungumza kwa mamlaka kuhusu mambo ya kiroho

Utajua kwamba labda anashiriki mawazo yake binafsi…

  • Ikiwa alisema waziwazi kwamba anatoa maoni yake binafsi
  • Ikiwa alisema Bwana bado hajamfunulia jambo fulani
  • Alipozungumza kuhusu mambo ya kawaida (burudani, kazi za nyumbani, safari)
  • Alipoandika barua binafsi kuhusu mambo ya kawaida

Hebu tuangalie mifano kadhaa.

Mifano ya jumbe takatifu

A stack of Ellen White's books from her Conflict of the Ages series, which includes The Desire of Ages and The Great Controversy.

Photo by Emmanuel Phaeton on Unsplash

Maandishi mengi ya Ellen White yalivuviwa na Mungu. Hii ni hasa kwa vitabu alivyovichapisha wakati wa uhai wake. Hii inajumuisha Shuhuda kwa Kanisa, Matendo ya Mitume, Tumaini la Vizazi Vyote, Mafundisho ya Kristo kwa Mfano, na Pambano Kuu. Ingawa pia aliandika makala yaliyovuviwa kwenye majarida kama Review and Herald.

Moja ya vitabu vyake maarufu, Tumaini la Vizazi Vyote, kinashiriki ufunuo aliopokea kuhusu huduma ya Yesu alipokuwa duniani.

Vitabu vyake pia vilisaidia watu kuelewa zaidi kuhusu wahusika muhimu wa Biblia, kama vile Paulo, Petro, Danieli, Daudi, Paulo, na hata Roho Mtakatifu na Shetani.

Lakini ingawa aliandika kuhusu mafundisho au watu wa Biblia katika muktadha mbalimbali, si yote yalichukuliwa kuwa yameongozwa moja kwa moja. Wakati mwingine aliandika kuhusu mada za kibiblia katika maandishi yake binafsi, kama vile alipowaandikia watoto wake, marafiki, au watu aliowafahamu akiwapa habari za kawaida au ushauri.

Hii inaonyesha tu kwamba alikuwa akimfikiria Mungu kila mara na kutafuta njia za kumtumikia Mungu kikamilifu na kutumia mafundisho Yake katika maisha yake.

Lakini kwa kuwa kuzungumza kuhusu Biblia sio kigezo pekee cha kuamua kama ujumbe unatoka moja kwa moja kwa Mungu au la, tunapaswa kuangalia viashiria vingine vya maandiko yake matakatifu.

Ellen White mara nyingi alitoa ushauri wa kiungu uliogusa maeneo yafuatayo:

  • Kweli za Biblia: Kila mara Ellen White alipothibitisha kweli za Biblia, alifanya hivyo chini ya uvuvio wa Roho Mtakatifu. Alitumia kwa uangalifu ufahamu aliopokea ili kuthibitisha masomo ya Biblia ya waumini wa kwanza wa Uadventista.

    Hii ilionekana katika jinsi alivyothibitisha au kukataa maswala ya mafundisho kwa kuyaelekeza kwenye mada inayolingana katika Maandiko, wakati mwingine katika sehemu kadhaa tofauti. Kwa maneno mengine, kila alichosema kuhusu mafundisho kiliunga mkono Biblia na kubaki sambamba na kanuni zake. Na uvuvio huu ndio uliowaongoza Waadventista wa kwanza kufufua mafundisho muhimu ya Biblia kama Sabato na Yesu kama Kuhani wetu Mkuu.

  • Makaripio ya kiroho: Moja ya sehemu ngumu zaidi katika kubeba karama ya unabii ni kuwaonya Wakristo wenzake wanapokuwa wanaelekea kwenye njia hatari au isiyo na matunda. Ellen White wakati mwingine alikuwa anaogopa kutoa makaripio ya kiroho kwa sababu alikuwa na hisia kali juu ya hisia za wengine.5
  • Maelekezo kuhusu afya: Maandishi ya Ellen White kuhusu matengenezo ya afya yalionyesha maarifa ya ajabu kuhusu kanuni za afya. Aliishi katika enzi ya Victoria—kipindi ambacho dawa na vitu vya kawaida vya nyumbani vilikuwa vimejaa vitu vyenye sumu, hata vyenye madhara makubwa. Hata madaktari walioelimika zaidi walikuwa wanapendekeza dawa zenye vitu hatari.6 Hata hivyo, aliweza kutofautisha kati ya kile kilichofaa kwa afya na kile kilicho na madhara kwa uongozi wa Mungu.
  • Ushauri kuhusu taasisi za Kiadventista: Kulikuwa na nyakati nyingi ambapo Konferensi Kuu, chombo cha utawala cha Kanisa la Waadventista, kilikuwa kinashauriana naye kuhusu maswali ya kiutawala. Wakati mmoja, viongozi wa kanisa walikuwa wanamuuliza ni wapi waanzishe shule ya Kiadventista.

    Kanisa lilikuwa tayari limechagua eneo fulani, lakini wapimaji walioulizwa kulikagua walilielezea kama ardhi isiyo na matunda.7 Lakini Ellen White alisisitiza kwamba Mungu alikuwa amechagua ardhi hiyo.8 Viongozi wa kanisa walinunua ardhi hiyo na ikakua na kuwa chuo kilichofanikiwa (Avondale) ambacho bado kipo hadi leo.

  • Unabii: Unabii wote ambao Ellen White alipokea na kuandika ulikuwa umetoka kwa Mungu Mwenyewe. Neno lake linatuambia kwamba karama ya unabii huja tu kupitia Roho Mtakatifu. Tunajua alikuwa na karama ya unabii kwa sababu kulikuwa na mambo mengi aliyoonyeshwa ambayo asingeweza kuyatabiri vinginevyo.

    Kwanza, alionyeshwa madhara hatari ya kutokujizuia ambayo hayakujulikana sana wakati huo.9 Pia alionyeshwa kwamba kujitenga kwa majimbo ya kusini kungepelekea Vita vya wenyewe kwa wenyewe.10

    Alitoa unabii kuhusu mambo mbalimbali mengine, lakini maono yake mashuhuri zaidi yalihusu matukio ya siku za mwisho na dalili za nyakati.11

Bila shaka, tunapaswa kufahamu kwamba sio kila kitu alichoandika kilikusudiwa kuwa ushauri wa kiroho. Kama mtu mwingine yeyote, alikuwa na maisha nje ya huduma—bado alikuwa na sababu zake binafsi za kuandika na kuzungumza.

Mifano ya ujumbe wa kawaida

A letter, like many of the letters Ellen White wrote throughout her lifetime.

Image by Margarita Kochneva from Pixabay

Wakati maandishi mengi ya Ellen White yalitokana na roho ya unabii, kulikuwa na sababu nyingine pia zilizomfanya aandike. Kulikuwa na nyakati fulani ambapo alitoa ushauri wake binafsi kulingana na uzoefu wake, alivyojifunza, au mambo aliyoyaona.

Hapa kuna maeneo kadhaa ambapo inawezekana aliongozwa na ufahamu wake binafsi:

  • Barua binafsi kuhusu mambo ya kawaida: Ellen White aliandika barua nyingi kwa marafiki na familia yake. Alipokuwa akisafiri kwa ajili ya Kanisa, alikuwa akiwatumia wanawe barua akieleza yote aliyoyaona katika safari yake.12 Walipokuwa watu wazima, aliendelea kuwaandikia kuhusu mambo mbalimbali. Wakati mmoja alimwandikia mwanawe, Edson, kuhusu hali ya afya ya James White na maisha yake ya kila siku.13
  • Hoja binafsi: Wakati Ellen White alipoongea kuhusu maswala ya maisha ya kila siku, alitumia akili yake ya kawaida. Wakati mmoja mwanawe Willie alimuuliza kama alikuwa na ushauri kuhusu eneo jipya la shule. Na katika jibu lake, Ellen White hakutaja kupokea ufunuo kutoka kwa Mungu au kuonyeshwa eneo maalum. Badala yake, alimpa jibu la jumla akitumia hoja zake binafsi. Alimwambia atafute kile kitakachoonekana bora kwake, lakini hasa aangalie eneo lenye kijito cha maji.14
  • Mazungumzo ya kawaida: Kama watu wengine wote, Ellen White alitumia muda wake kuzungumza kuhusu mambo ya kila siku. Alikuwa na mambo aliyoyapenda nje ya maisha yake ya kiroho ikiwa ni pamoja na familia yake, bustani yake, kushona, kupanda farasi, na mengine mengi! Ingawa neno la Mungu lilikuwa moja ya mambo aliyopenda sana kuyazungumzia, pia alipenda kuzungumza na marafiki na kujadili mambo ya kawaida. Alijulikana pia kwa ucheshi wake!15

Ni muhimu kujua tofauti kati ya maandishi matakatifu na ya kawaida ya Ellen White, kwa sababu wapo baadhi ya watu ambao watashikilia kimakosa ushauri aliotoa katika maandiko yake ya kawaida kana kwamba ni amri kutoka kwa Mungu.

Wakati huo huo, ni muhimu kutochukulia jambo alilosema Ellen White kama “maoni yake tu,” kwa sababu tu ni kitu kinachopingana na mapendeleo yetu binafsi. Hata hivyo, Biblia inaonya tusidharau maneno ya manabii wa kweli (1 Wathesalonike 5:20-21).

Ndiyo maana ni muhimu kuelewa muktadha wa maandiko ya Ellen White na kuyalinganisha na Biblia sisi wenyewe. Hivyo ndivyo angependa tufanye!

Kwa njia hiyo tunaweza kubaini ni ushauri upi ulitokana na uzoefu wake binafsi, ni upi uliotolewa kwa mahali au wakati maalum, na ni ushauri upi wa kiungu tunaoweza kuendelea nao hadi wakati wa sasa.

Na mradi tu unajisomea mwenyewe, unalinganisha na neno la Mungu, na kumuomba Yesu Kristo akuongoze, huna haja ya kuwa na wasiwasi kuhusu kushindwa kuelewa ujumbe wake.

Roger W. Coon, aliyekuwa mkurugenzi msaidizi wa Taasisi ya Ellen G. White, aliwahi kusema:

“Akili ya kawaida na iliyotakaswa vinapaswa kuwa viongozi wetu katika kutofautisha kati ya makundi haya mawili [maandishi matakatifu na ya kawaida].”16

Ikiwa unatafuta kujifunza maandiko ya Ellen White mwenyewe, Taasisi ya Ellen G. White imehifadhi na kuweka kidijitali kazi zake zote. Unaweza kuzitafuta kwenye egwwritings.org.

Ikiwa ungependa kujifunza zaidi kuhusu manabii wa kibiblia kwa ujumla, angalia Kile Kinachomfanya Mtu awe Nabii na Manabii wa Biblia.

Chagua Masomo ya Biblia Mtandaoni

Unataka kuendelea kujifunza? Pata habari zaidi kuhusu Yesu, mwanadamu, mpango wa wokovu, na jinsi Mungu anavyokupenda kiasi cha kutosha kujitolea kila kitu, ili tu kukupatia nafasi ya kumchagua.

Wakati mwingine inaweza kuwa ngumu kujua pa kuanzia, ndio maana tunatoa chaguo za masomo ya Biblia mtandaoni bure, rahisi kutumia, unaweza kufanya wakati wowote, mahali popote, na kwa kasi yako mwenyewe.

Shule hii ya Biblia mtandaoni itakuelekeza kupitia mada kuu za Maandiko, ikivunja dhana ngumu za Biblia katika vipande vidogo, ambavyo vinaweza kukusaidia kupata majibu ya maswali magumu zaidi ya maisha.

Kurasa Zinazohusiana

  1. White, Ellen G., The Review and Herald, August 30, 1906 []
  2. Douglass, E. Herbert, Messenger of the Lord, pp. 16-17 []
  3. Ibid., p. 37 []
  4. Ibid., p. 174 []
  5. Ibid., p.157 []
  6. https://www.mentalfloss.com/article/550867/dubious-victorian-cures-first-merck-manual-diagnosis-and-therapy[]
  7. Douglass, p. 190 []
  8. Ibid. []
  9. Ibid., p. 365 []
  10. Ibid., p. 158 []
  11. Ibid. []
  12. White, Ellen G., I’d Like to Ask Sister White, p. 105 []
  13. White, Ellen G., Letters and Manuscripts, vol. 8., Letter 201, (1903) []
  14. White, Ellen G., Letters and Manuscripts, vol. 9., Letter 144, (1894) []
  15. Douglass, p. 94 []
  16. Coon, W., Roger, “Distinguishing Between the Sacred and the Common,”https://mail.google.com/mail/u/0/?tab=rm#search/tim/KtbxLxgNNvWTNRXdtpCsXCwdsqhKGJtvlq?projector=1&messagePartId=0.1. []

Je, Una swali kuhusu Waadventista? Uliza hapa!

Pata majibu kwa maswali yako kuhusu Waadventista Wasabato

Majibu Zaidi

Ellen G. White Alitoa Ushauri Gani kuhusu muziki?

Ellen G. White Alitoa Ushauri Gani kuhusu muziki?

Ellen G. White Alitoa Ushauri Gani kuhusu muziki?Katika kiini chake, muziki ni mkusanyiko wa sauti, muinuko wa sauti na mapigo ambayo huleta wimbo. Pia ni zaidi ya hayo. Kama aina yoyote ya sanaa, inaweza kuwa nzuri sana au mbaya sana, yenye kusisimua au yenye...

Kuelewa Maisha na Huduma ya Ellen G. White

Kuelewa Maisha na Huduma ya Ellen G. White

Jifunze Ellen G. White ni nani hasa na jukumu alilokuwa nalo katika kuongoza Kanisa la Waadventista Wa Sabato mapema kupitia huduma yake na maandishi yaliyoongozwa na Roho Mtakatifu.

Sabato katika Maisha na Mafundisho ya Ellen White

Sabato katika Maisha na Mafundisho ya Ellen White

Sabato katika Maisha na Mafundisho ya Ellen WhiteSabato ni mada muhimu katika Kanisa la Waadventista wa Sabato. Sio jambo la kushangaza, basi, kwamba Ellen G. White, mwanzilishi mwenza wa kanisa, alisoma mafundisho ya Biblia kuhusu Sabato na akaandika kiasi kikubwa...

Urithi wa Kudumu wa Ellen G. White

Urithi wa Kudumu wa Ellen G. White

Urithi wa Kudumu wa Ellen G. WhiteEllen G. White ni jina linalojulikana sana miongoni mwa Waadventista wa Sabato, lakini pia aliathiri sehemu nyingi za historia, mbali na kuwa mwanzilishi wa Kanisa la Waadventista wa Sabato. Ndiyo maana Jarida la Smithsonian...

Wafahamu Watoto wa Ellen White

Wafahamu Watoto wa Ellen White

Ellen White, ambaye ni mmoja wa waanzilishi maarufu zaidi wa Kanisa la Waadventista wa Sabato, alikuwa na watoto wanne na mumewe, James: Henry Nichols, James Edson, William Clarence, na John Herbert.

Jinsi Ellen White Alivyochangia Ujumbe wa Afya wa Waadventista

Jinsi Ellen White Alivyochangia Ujumbe wa Afya wa Waadventista

Jinsi Ellen White Alivyochangia Ujumbe wa Afya wa WaadventistaWaadventista wa Sabato wanajulikana kwa kusisitiza maisha yenye afya bora. Na Ellen G. White alikuwa na ushawishi mkubwa katika maendeleo ya kipaumbele hiki na utekelezaji wake miongoni mwa Waadventista....